Watawala mmemsikia Obama?
Ansbert Ngurumo
Ansbert Ngurumo
KASI ya wananchi kuishutumu na kuituhumu Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa, hasa mashambulizi yanayomlenga yeye moja kwa moja, imewapa fursa watawala wa sasa kupumua.
Walau wanajua kuwa sasa tumerudi kule walikoanzia, kule walikotaka tuelekeze nguvu zetu tangu mwaka 2006, kule tulikokataa kujielekeza kwa makusudi, maana naamini kuwa, kama tungemwandama Rais Mkapa vilivyo kuanzia mwaka 2006, yangeibuka mengi makubwa ya awamu ya tatu, ambayo yangeficha makubwa ya awamu ya nne.
Hii ingewasaidia wenzetu kupeta kwa muda na ingewafanya wananchi waone kwamba Rais Mkapa alivurunda na Rais Jakaya Kikwete anasawazisha.
Kisiasa udhaifu wa serikali ya Mkapa ulikuwa mtaji tosha kwa serikali ya Kikwete kama angekuwa makini na jasiri wa vitendo. Lakini hawakuwa na bahati hiyo.
Miaka mitatu ya kuichokonoa serikali ya Kikwete imewafanya baadhi ya wananchi sasa waanze kusema kuwa licha ya makosa ya Mkapa na mawaziri wake, licha ya ubabe na hata matumizi mabaya ya madaraka anayotuhumiwa kufanya, serikali yake ilikuwa makini, ilichapa kazi na ilikuwa na nidhamu.
Tutatofautiana katika kujadili umakini, uchapa kazi na nidhamu hiyo, lakini ulinganifu unaofanywa unatokana na udhaifu mkubwa wa kimaamuzi na kiutendaji ulioonekana katika miaka mitatu ya awamu ya nne na unaonyesha tofauti ya wazi ya uwezo wa kiuongozi katika awamu mbili hizi.
Ndiyo maana wapo watu wanaojitokeza kumtetea Rais Mkapa sasa, si kwa kukubali makosa yake, bali kwa hoja (ambazo mimi nimeziita dhaifu) kuwa serikali yake ilifanya makubwa na mazuri mengi (ingawa wanajua kuwa haikuwa hisani bali wajibu).
Wengine wanamtetea wakidhani kwamba haya yanayotokea sasa dhidi ya Rais Mkapa ni mkakati wa makusudi wa watawala wa sasa ili wapate upenyo lakini wao si wema wala waadilifu zaidi.
Miaka mitatu tu imeonyesha kasi mpya waliyokuwa nayo katika kujisimika kwenye ulaji na kulinda masilahi yao na wapambe wao. Bahati mbaya upepo umewageuka.
Kama si Watanzania kushtuka na kuanza kuwarushia mawe mapema, hawa wangekuwa hawasemeki wala hawashikiki.
Kwa kujua mbinu ya awali ya watawala wa sasa, watetezi wa Rais Mkapa wanadhani kwamba mtu wao anaandamwa na watetezi wa serikali hii.
Kuna ukweli kidogo katika hoja hii, lakini msukumo wa sasa wa tuhuma dhidi ya Rais Mkapa umeshavuka mbinu za watawala wa sasa, ni jitihada za wananchi kuirejesha serikali katika misingi tuliyopewa na waasisi wa taifa hili kuhusu dhamana ya uongozi na utumishi wa umma, na kwa baadhi yetu, kauli zetu na maandishi yetu ni msaada na ushauri tunaompatia Rais Jakaya Kikwete ili asijitumbukize katika ulevi wa madaraka, na ulinzi wa masilahi binafsi na ya wapambe wake.
Ni onyo kwake kwamba miaka mitano au 10 ikulu si mingi sana. Aongoze au atawale nchi akijua kuwa muda wake unakaribia kwisha na akiutumia vibaya, historia ya utumishi wake itamwandama hadi popote atakapokuwa kama mstaafu.
Naamini hadi sasa amegundua kuwa Watanzania wamebadilika, na mtu pekee wa kuwarudisha nyuma ni yule atakayerudi kwenye misingi.
Jambo moja lisilomfurahisha ni kwamba wananchi wametambua hulka yake ya kweli, uwezo na udhaifu wake mapema kuliko alivyotarajia katika miaka mitatu iliyopita, wananchi wamepata fursa ya kutafsiri kwa vitendo maana halisi ya kauli mbiu ya ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya ambayo siku hizi imefichwa kabatini.
Wameunganisha unasaba wa kimasilahi na kimadaraka kati ya vigogo wa sasa na wa awamu zilizopita. Wamebaki watu wachache ambao bado wanaamini kwamba Serikali ya Awamu ya Nne ina tofauti yoyote ya kimsingi na iliyopita.
Labda wanatazama sura, majina na vyeo vya watu. Lakini sisi tunaotazama katiba, sera na sheria tunaona kwamba awamu ya nne ni kizazi kile kile cha nyoka yule yule aliyetungata miaka kadhaa iliyopita, tofauti ni kwamba huyu kajivua ngozi, imeota nyingine.
Na nilipokuwa natafakari tukio kubwa la kisiasa wiki hii nilijikuta natazama mafunzo kadhaa yaliyotolewa na Rais Barack Obama wa Marekani kwa dunia nzima, hasa kwa wanasiasa wenzake katika siku chache zilizopita. Nitajadili machache yenye uhusiano na maisha yetu ya kisiasa.
Hata Wamarekani wenyewe wanakiri kwamba miaka miwili iliyopita, haikufikiriwa kwamba umefika wakati wa taifa hilo kumchagua rais mweusi.
Dhana hii ya kipuuzi iliendelea hata wakati wa kampeni lakini uwezo binafsi wa Obama na mikakati makini ya timu yake ya kampeni, viliweza kushinda ugonjwa huu wa ubaguzi.
Leo hii, ingawa ubaguzi haujaisha, Wamarekani wamebadilika kiasi na dunia imepata fundisho.
Watawala wetu bado wanatulazimisha kuendeleza kasumba ya wakati haujafika kuwa na rais mwanamke; wakati haujafika kuwa na mgombe binafsi; wakati haujafika CCM kuondolewa madarakani, eti kwa sababu wengine hawana uzoefu huku wengine wanaleta hoja za kikabila na kidini.
Obama ametufundisha kwamba tulilofikiria haliwezekani jana, linawezekana leo iwapo wananchi watalitaka.
Kikwazo cha Obama hakikuwa rangi tu, bali hata umri na uzoefu wake katika masuala ya uongozi kitaifa. Anapolinganishwa na wagombea wote waliokuwa wanawania urais kutoka vyama vyote, Obama ndiye alikuwa kijana zaidi na mwenye uzoefu mdogo zaidi wa siasa za wakubwa serikalini.
Hoja hizi zilirudiwarudiwa sana wakati wa kampeni, lakini alizishinda kwa hoja. Wamarekani hawakusikiliza hoja za kipropaganda za wapinzani wa Obama.
Na kwa kuwa yeye hakuogopa midahalo na alikuwa tayari kujadili lolote hata pale alipodhihakiwa, wananchi walichunguza mantiki ya hoja zake, wakapima dhamira yake, wakagundua uwezo wake, na wakatazama mahitaji mapya ya wakati huu wakaamini kwamba anafaa.
Funzo la tatu ni jinsi alivyoingia ofisini na kuanza kutekeleza ahadi zake siku ya kwanza. Na ameanza na baadhi ya masuala magumu ya kisera, ambayo wapinzani wake waliwahi kusema kwamba hayawezekani, bali ni kauli za kutafutia kura.
Kabla hajakaa ofisini na kulewa madaraka, ameamua kuchukua hatua kurekebisha mambo kadhaa ya kisera ndani na nje.
Tutampima baadaye kama ameweza au ameshindwa, lakini ameonyesha kwamba heshima ya mwanasiasa itatokana zaidi na ujasiri wa vitendo kuliko kauli na ahadi tupu na kwamba baadhi ya hatua inabidi zichukuliwe mapema.
Obama haombi Wamarekani wampe muda. Ameshapewa muda na ameanza kazi. Anafanya kile anachokiamini, alichowaambia wananchi wakati anaomba kura.
Hatuhitaji kuwasimanga viongozi wetu kwa kumtumia kiongozi wa taifa jingine. Lakini tunaamini nao wameona na wamejifunza, hata kama wamechelewa. Kiongozi anapoomba ridhaa ya watu, akawaahidi kutekeleza jambo fulani, wanapomuamini na kumchagua halafu akashindwa kulitekeleza, au akaliahirisha bila maelezo ya kina, anakuwa amewasaliti.
Sote tunajua kinachowatafuna watawala wetu sasa. Walituahidi kutekeleza mambo mengi kwa kasi ambayo hawakuwa nayo. Tazama masuala yanayowasumbua leo. Ni ya kisera. Wameendelea kusimamia sera za zamani, wameshindwa kuandaa misingi mipya ya kutatua matatizo yanayotusumbua katika mfumo wa elimu, afya, muungano, masuala ya uongozi na utumishi, mawasiliano na mengine.
Wamebaki kujivunia utekelezaji wa miradiya serikali kama ujenzi wa barabara, uchimbaji wa visima na ujenzi wa madarasa kwenye sekondari za kata.
Kwa mtazamo wangu, mabadiliko makubwa katika nchi hayawezi kutokea bila mabadiliko ya kisera na kikatiba. Hapa ndipo watawala walipaswa kujikita tangu siku ya kwanza.
Najua wapo wanaodhani kwamba miaka hii mitano itatumika kujifunza, na kwamba kama watapata tena miaka mitano ijayo ndiyo miaka ya kazi.
Hii ni kejeli kwa watawala waliojinadi kwa uzoefu (wana zaidi ya miaka 30 serikalini) na waliojiandaa kwa zaidi ya miaka 10. Ndiyo maana nasema kwamba Rais Obama ametoa funzo, kwamba wakati mwingine uzoefu tunaozungumzia si wa manufaa, bali ni uzoefu wa kukaa na kuongoza katika mifumo ya kifisadi. Haupaswi kupewa nafasi.
Lakini Rais Obama ametukumbusha jambo la ziada katika siku yake ya kwanza ofisini kwa kauli na vitendo. Amesisitiza kurejea katika misingi ya uwazi, ukweli na uwajibikaji katika utumishi wa umma ili wananchi waweze kuiamini tena serikali. Siku ya kwanza kabisa, aliwaambia watumishi wa umma wanaofanya kazi ikulu kwamba utumishi wa umma si fursa ya kujinufaisha binafsi au kuwanufaisha rafiki zetu na wapambe wetu na wala si fursa ya kutukuza itikadi za kisiasa.
Amewakumbusha kwamba utumishi wa umma ni dhamana na fursa adhimu kwa ajili ya kulinda na kutetea masilahi ya wananchi wote.
Hakuhitaji siku mbili au nne za kuwapeleka kwenye hoteli za kifahari kuwafunda katika suala wanalolijua vema, bali aliweka wazi msimamo na mwelekeo wa utawala wake, na kwamba ni jukumu lao wote kuifanya serikali iaminike mbele ya macho ya umma kwa kuondoa usiri usio wa lazima.
Watanzania si wageni wa kauli za namna hii. Ndivyo tulivyolelewa wakati wa kujenga misingi ya taifa, lakini ufisadi umetafuna tunu hizi taratibu hadi zimetoweka kadiri miaka illivyopita na viongozi kubadilika badilika.
Kama watawala wetu wangeendelea kusimamia misingi hii, sina shaka baadhi ya tuhuma zinazowakumba vigogo leo zisingekuwapo na kama zingekuwapo zisingekuwa nyingi hivi na zisingekuwa za viwango vikubwa kiasi hiki.
Wala tusingekuwa na jamii ya watu wachache ambao wanaona fahari katika kutetea ufisadi wa watawala, kwa kigezo kuwa yapo mazuri machache waliyotenda. Lakini tumefika hapa tulipo kwa sababu, kama nilivyowahi kusema kuwa tumekosa uongozi makini.
Najua kauli hii haiwapendezi walio madarakani kwa sababu wao wanajiona makini, kwa sababu wanasahau au hawajui kwamba viwango vya utambuzi na uelewa wa Watanzania vimepanda na vimekuzwa na udhaifu wa watawala ambao wana akili kama ya Rais mstaafu wa Marekani George W. Bush.
Mnamo Mei mwaka jana, rais huyo mstaafu aliwaambia waandishi wa Kiisraeli, jijini Washington, kwamba: Nitakuwa nimeshasahaulika kabisa kabla mtu yeyote makini hajagundua kilichotokea katika ikulu hii.
Anajua alichokuwa anamaanisha. Ndivyo watawala wetu wanavyoendesha nchi zetu; ndivyo wanavyotufikiria. Ndivyo wanavyochukulia nafasi walizonazo. Na ndiyo maana wanaendekeza ulaji na kulindana.
Wanaamini kwamba kwa muda mrefu ujao, ni wao tu na watoto wao watakaokuwa wanashikilia nafasi za juu za uongozi wa nchi na kwamba kwa yoyote yatakayoharibika sasa, watalindana hadi hapo atakapotokea kiongozi makini wa kugundua uchafu uliotendeka ikulu, wakati huo wao walishatoweka kabisa.
Bahati mbaya kwao, tumeanza kugundua uchafu huo hata kabla hawajatoka ikulu, na wengine kabla hawajatoweka kabisa. Ndiyo maana tunapiga kelele. Tunataka kurudi kwenye misingi.