Watanzania na safari ya utumwani | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Watanzania na safari ya utumwani

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Yona F. Maro, Jan 6, 2009.

 1. Yona F. Maro

  Yona F. Maro R I P

  #1
  Jan 6, 2009
  Joined: Nov 2, 2006
  Messages: 4,237
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 0
  Zamani niliiona jamii ya Tanzania kama inafanana na jamii ya wana wa Israeli chini ya uongozi wa Nabii na Mtume Musa, katika zoezi lake la kutoka utumwani na kuiendea nchi ya ahadi ambayo Mungu wao aliwaahidi kuyafaidi mema ya nchi ile na kula maziwa na asali kama wangefanikiwa kufika bila kumkorofisha mkombozi wao mkuu.
  Lakini kwa bahati mbaya kwakuwa waliiasi kanuni ya uhuru na ile sheria ya ukombozi, wakaishia kutangatanga jangwani kwa muda wa miaka arobaini hadi waasi wote walipokuwa wamekufa, hiyo ilikuwa ndiyo adhabu halali kutoka kwa Mungu wao ili kulipa gharama za maasi yao, vinginevyo walistahili kuuawa kwa kutoweshwa mara moja, maana mtu ambaye uhuru umemshinda ana thamani gani maishani mwake kisha ana umuhimu gani wa kuendelea kuishi?
  Zamani nilikuwa na njozi za kuiona jamii ya Tanzania kwamba inatangatanga kwenye jangwa la umasikini, kwani baada ya uhuru jamii yetu bado ingali inatafuta njia ya kuifikia neema ambayo katika uhalisi wa mambo ni kuifikia nchi mpya ya Tanzania mpya iliyojaa maziwa na asali ambayo ndaniyake hakuna matabaka ya kudhalilisha na wala kutukanisha utu wa mwanadamu yaani tabaka la waheshimiwa na wadharauliwa daima, tabaka la watawala na watawaliwa, tabaka la waonezi na wanaoishi kwa kuonewa daima, tabaka la wenye haki na wasio na haki.
  Sikutarajia kwamba katika Tanzania mpya yaani Tanzania huru baada ya kumwondoa mkoloni kutakuwako na tabaka la wanaocheka na kufurahia maisha kisha tabaka jingine la watu wanaolia na kusaga meno maishani mwao huku hawajui ni kosa gani walilolifanya hadi yawapate hayo yaliyowapata.
  Sikutarajia kwamba siku moja nitashuhudia ndani ya nchi huru umasikini wa watu ukigeuzwa na ukifanywa kuwa sawa na kosa la jinai ambalo adhabu yake kwa mkosaji ni mateso. Badala yake mimi niliuona umasikini wa walio wengi kuwa sawa na jangwa na kwahiyo siku moja watu wanaweza kuvuka jangwa la umasikini na kuifikia neema, kumbe loo! Nilikuwa naota ndoto. Sasa ndoto zangu zimebadilika, naota Tanzania ikigeuka kama vile mcheza gwaride aliyepewa amri ya nyuma geuka, na mara tu baada ya kugeuka nchi inaendelea na mwendo kasi ule ule, lakini sasa inayo safari mpya ya kuelekea kule ilikotoka yaani utumwani.
  Enzi za Nabii Musa walikuwepo viongozi wa maasi, hao ndio waliowadanganya ndugu zao kwa ushawishi wa nguvu na propaganda za uwongo eti ni heri kurudi Misri, na kuishi tena chini ya utawala wa Firauni, naam kuishi bila uhuru alimradi tu wao kama wanadamu waweze kufaidi makulaji ya mikate ya shairi, nyama za nguruwe, michuzi mizito iliyoungwa kwa vitunguu swaumu, na minofu ya samaki, na matikiti maji.
  Katika uhalisi wa mambo si watu wote katika jamii ile waliokuwa walafi na waroho kwa kiwango hicho, bali waliponzwa na viongozi wachumia tumbo, viongozi ambao walipenda ukubwa lakini hawakuwa wamechaguliwa na Mungu. Hao viongozi vipofu, waliojitahidi kukuza hadaa zao hadi umma wote ukadanganyika ni wale ambao kabla ya Nabii Musa kuwatoa wana wa Israeli nje ya Misri, wao walikuwa manokoa na wenye madaraka makubwa dhidi ya ndugu zao, na zaidi ya yote walikuwa ni viongozi wala makombo, wakifaidi mabaki yaangukayo kutoka meza ya Firauni, ndiyo maana walihubiri bila aibu wakisema Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani? (Kama Farao alivyokuwa akitufanyia Misri!) Hapa msisitizo ni wangu maana maandiko hayamtaji Farao. Sasa inasikitisha, inahuzunisha, na inatisha Tanzania kupata viongozi wa kuirudisha nchi kwenye miongo iliyopita ya utumwa na ukoloni. Yanaweza kuweko maneno mapya ya kupumbaza akili za watu, na kuwaliwaza kama vile, Ubinafsishaji, utandawazi na soko huria, lakini madhara yake, na matunda yake bado ni yale yale ya utumwa na ukoloni.
  Hakuna apandaye miiba na mbigili kisha akavuna tini na zabibu, apandacho mtu ndicho atakachovuna, yeye apandaye haba ni lazima atavuna haba, na mti mwema hujulikana kwa matunda yake. Kwa ajili hiyo hatuhitaji Nabii afufuke, au Mtume ashuke tena toka mbinguni na kutuhubiria mabaya au mema ya sera za utandawazi, bali matunda ya sera hizi ni mahubiri tosha ya kumfanya yeyote mwenye akili timamu, na yeye mwenye masikio na asikie ujumbe utolewao na sera hizi.
  Matunda mema siku zote hayahitaji mtetezi wa kuhubiri kwa nguvu ili watu waamini kwamba ni mema bali siku zote mema yanajiuza na kujidhihirisha kuwa ni mema, sasa huyo anayeutetea utandawazi ana lengo gani hapa? Ana ujumbe gani kwa wale waliopoteza ajira zao? Anawaambia nini wale waliokatizwa kwenye kazi zao na hawajalipwa bado mafao yao? Anawaeleza nini wahanga wa tatizo la rushwa na uonezi wa vyombo vya dola kwa wanyonge?
  Alimradi yeye binafsi utandawazi unamshibisha, unamnenepesha na kumfanya aongezeke mara mbili ya alivyokuwa zamani., basi kwake utandawazi ndiyo ukombozi baada ya kutoka kwenye ukoloni na kwenye ujamaa? Inakuwaje wale wale wakoloni ambao miaka ya sitini sauti ya Mwafrika iliwaambia ondokeni mtuachie nchi yetu, rudini kwenu Ulaya kwenye nchi yenu leo hii wawe na kauli juu ya kila neno linalohusu uendeshaji wa nchi yetu? Mbona uhuru wa mwananchi unauzwa kwa bei poa!
  Hivi sasa Watanzania watakuwa na tofauti gani na wale watu waliosema ni aheri kurudi Misri? Baada ya kushindwa kuifikia Tanzania yenye neema, ni wazi kwamba tumeanza safari mpya ya kuurudia utumwa na ukoloni. Zamani tulikuwa koloni la mkoloni mmoja tu aliyeitwa Muingereza, lakini sasa tuko chini ya himaya ya wakoloni wengi waitwao madola makubwa na nchi tajiri, kwani kila nchi iliyo tajiri ina kauli juu yetu. Zamani baba zetu walifungwa minyororo na kusafirishwa kwa majahazi ya upepo hadi nchi za mbali ili kwenda kuwafanyia kazi wanadamu wengine, leo hii watawala wetu wanafunga safari za kwenda majuu, na kupokea maelekezo jinsi ya kuendesha maisha yetu.
  Unapowadia wakati wa uchaguzi huenda mbio mbio vijijini kutafuta kura za wananchi, baada ya uchaguzi mkataba wao na wapiga kura hukoma, na mara hiyo huanza mbio mpya, yaani mbio zingine za kwenda majuu kupokea mashinikizo ya aina aina kuhusu uendeshaji wa nchi wanayodai kuitawala. Ni ajabu ya kutisha kwamba nchi baada ya miaka 40 ya uhuru wake inakodisha menejimenti toka taifa jingine ili kuboresha huduma za shirika lake la umeme kana kwamba hakuna wananchi wenye uwezo.
  Na kama huo ndio mtindo kwamba taasisi ikidorora basi waletwe wenye uwezo kutoka nje ya nchi itakuwaje hapo itakapodhihirika kwamba Bunge la nchi nalo limedorora halikidhi haja ya kuwepo kwalo, je, itabidi tulete wabunge wenye uwezo kutoka nchi zingine hususan Afrika Kusini ili waje waliboreshe?
  Je, itakuwaje hapo itakapodhihirika wazi kwamba jeshi la polisi limeshindwa kazi? Ina maana itatulazimu kuleta polisi toka Afrika Kusini kama tulivyofanya kwenye suala la TANESCO! Iwe itakavyokuwa mantiki ya ubinafsishaji kwa maana ya kukabidhi mashirika ya umma kwa watu binafsi na hasa kwa wageni, haina uhalali wowote kwani Mtanzania huyo aliyeshindwa kuendesha mashirika ya umma ndiye huyo huyo aliyeshindwa kuendesha mashirika ya uma ndiye huyohuyo aliyeshindwa kwenye maeneo mengine, ameshindwa kwenye FAT na TFF , ameshindwa kwenye elimu shule zake za msingi ni vichekesho, vyuo vyake vya elimu ya juu ni matatizo, ameshindwa kwenye sheria, mahakama zake zimeoza kwa rushwa na jeshi lake la polisi limetiwa ulemavu hadi ujambazi unageuka kuwa tatizo sugu. Ameshindwa kwenye afya hadi hospitali zake zinageuka mahala pa watu kufia ama kuhifadhi maiti za waliogongwa mitaani. Ameshindwa kwenye kilimo hadi wakulima wake wanahaha kutafuta masoko ya bidhaa zao pasipo mafanikio, hivyo umasikini umewanasa kama wavu unasavyo samaki.
  Ni Mtanzania huyo huyo ambaye ameshindwa kutawala kwa haki na kuisababishia nchi ukiwa, kwa ajili hiyo kuangalia ubinafsishaji kwenye eneo moja tu la mashirika ya umma na kukazania ubinafsishaji wake, kana kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya ukombozi wa nchi, ni kujidanganya kwani wanaokazania hilo wana ajenda yao ya siri sawa kabisa na wale waliosema heri turudi Misri!
   
 2. T

  Tikerra JF-Expert Member

  #2
  Jan 10, 2009
  Joined: Sep 3, 2008
  Messages: 1,704
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 0
  Hongera sana Shy kwa thread hii.Lakini kwa mtazamo wangu mimi tayari tuko utumwani!
   
 3. Ngongo

  Ngongo JF-Expert Member

  #3
  Jan 10, 2009
  Joined: Sep 20, 2008
  Messages: 12,155
  Likes Received: 3,632
  Trophy Points: 280

  Mkuu Tikerra tuko pamoja.
  Watanzania tayari ni watumwa katika nchi yao.Rasilimali zetu kama madini wamekabidhiwa wageni sisi tumebaki kupiga kelele bila kuchukua hatua.
  Ukiangalia kwa makini sifa na vigezo vyote vya utumwa tayari tunavyo au tunakaria kuwanavyo.
   
Loading...