Watanzania asilimia 28 wanaogopa benki

radika

JF-Expert Member
Jul 15, 2014
20,438
32,248
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianzishwa mwaka 1966

Mbeya. Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Tawi la Mbeya, Jovent Rushaka amesema asilimia 28 ya Watanzania ni maskini wenye kipato kisichotabirika kutokana na kuogopa benki, wakiamini zipo kwa ajili ya matajiri.

Rushaka alisema hayo wakati wa ufunguzi wa sherehe za maadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa BoT.

Alisema watu hao hawajiamini na hawana hata wazo la kutafuta huduma za fedha, kwa kujiona kuwa benki siyo kwa ajili yao.

Rushaka alisema asilimia 42 ya Watanzania hawajajumuishwa kwenye mfumo rasmi taasisi mbalimbali za benki.

Hata hivyo, Rushaka alisema asilimia 28 kati ya 42 ni maskini zaidi na kwamba, hawawezi hata kuuliza huduma.

Mkurugenzi huyo alisema benki na taasisi za fedha kwa sasa zinafanya juhudi kubwa kuwatafuta wateja mijini na vijijini, lakini zinashidwa kuwapata wengi kwa sababu hawana vitambulisho vya Taifa.

“Vitambulisho vya Taifa kutowafikia watu wengi ni changamoto mojawapo, kwani kama wangekuwa navyo ingerahisisha kuwatambua na kuwa wateja kwenye taasisi rasmi za fedha,’’ alisema Rushaka.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo, mkazi wa Forest jijini hapa, Joyce Mwansasu alisema watu wengi hawajiamini hivyo hawathubutu hata kusogelea benki kutokana na umaskini wao.

Mwansasu alisema wengi wanashindwa kujiunga na benki kwa sababu ya vipato duni walivyo navyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyirembe Munasa alizitaka benki na taasisi mbalimbali za fedha kujipanga ili kupunguza kiwango cha umaskini kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu.

“Nashauri benki na taasisi za fedha kwa sasa zielekeze nguvu kuwakopesha watu wa vijijini na kwa riba nafuu, ili kupunguza umaskini,’’ alisema.

Alisema kukua uchumi wa Taifa ambao hauwiani na kipato cha watu wa chini, kunakuwa na tatizo kwani wananchi hawaelewi chanzo chake.

Alitaka wachumi kukuna vichwa kuhakikisha kunakuwa na uwiano kati ya ukuaji wa Taifa na maisha ya wananchi. Pia, aliipongeza BoT kwa kazi ambazo imefanya tangu kuanzishwa.
 
Back
Top Bottom