Wataka Sheria ya Habari ishughulikie unyanyasaji wa waandishi wanawake, Serikali yatoa tamko...

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,267
5,366
Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk. Rose Reuben ameshauri maboresho ya Sheria za Habari kuingizwa suala la kushughulikia unyanyasaji wa waandishi wa habari wanawake ili kukabiliana na changamoto hiyo katika vyombo vya habari.

Dk. Rose amesema hayo kwenye mkutano wa wadau wa habari na serikali ulioandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania, MISA-TAN na TAMWA kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Kusaidia vyombo vya habari, IMS, wakilenga pamoja na mambo mengine kujadili mapitio ya Sheria za Habari.

Alisema waandishi wa habari wanawake wameendelea kupungua katika vyombo vya habari kutokana na changamoto mbalimbali kubwa likiwa ni unyanyasaji wa kijinsia.

Alishauri vyombo vya habari kuwa na sera ya usawa wa jinsia ili kusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea katika vyombo hivyo.

Sidha, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Gerson Msigwa amesema suala la unyanyasaji waandishi wa habari wanawake linashughulikiwa na ofisi yake na kuahidi kuweka dawati maalum la jinsia kukabiliana na changamoto hiyo.

"Unyanyasaji wa kijinsia haukubaliki ni kinyume cha sheria za nchi, tutaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kuboresha sheria mbalimbali zinazokwaza uhuru wa habari," alisema Msigwa.

Aliwapongeza waandishi wa habari wa Tanzania ambao licha ya wengi wao kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kutolipwa au kukosa mishahara, bado hawajarudi nyuma katika kutimiza majukumu yao ya kuhabarisha umma.

"Niwaahidi tu hakuna jambo litakwama ndani ya Serikali ya awamu ya sita, labda tuamue wenyewe (wanahabari) kuanzisha chokochoko zenye nia ovyo na kuharibu hali ya hewa," alisisitiza Msigwa.

Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe, alisema vyombo vya habari nchini bado vinakabiliwa na changamoto ya unyanyasaji dhidi ya wanawake, sheria kandamizi na ukosefu wa maslahi bora kwa wanahabari.

Naye Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Salome Kitomari alisema pamoja na mambo mengine, mkutano huo wa pili licha ya kulenga kushauriana na serikali na wadau wengine masuala hayo ya kisheria yamelenga pia kujadili usalama wa waandishi wa habari katika vyombo vya habari.

Mengine ni kuangalia sera na sheria zinazominya uhuru wa vyombo vya habari na mazingira ya Tanzania, masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na rushwa ya ngono katika vyombo vya habari na kupata mrejesho wa mapendekezo ya uwakilishi wa timu maalum ya majadiliano itakayoshughulikia marekebisho ya sheria za habari kama alivyoagiza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye.

Makamu Mwenyekiti wa MISA TAN, Wakili James Marenga alisema bado kuna upungufu kadhaa katika Sheria za Habari nchini ikiwamo kugeuzwa makosa ya wanahabari ya kitaaluma kuwa makosa ya jinai na vifungu kadhaa vinavyokinzana na lbara ya 18 ya Katiba ya nchi.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom