Wataka Rais asitenganishwe na Baraza lake la Mawaziri

Keil

JF-Expert Member
Jul 2, 2007
2,214
801
Wataka Rais asitenganishwe na Baraza lake la Mawaziri

* Ni kuhusu umaarufu wake kuzidi wa mawaziri wake

* Profesa Safari asema haiyo haikubaliki kisheria

* Dk Lwaitama:Kinachotakiwa ni JK kusafisha baraza

* Chiligati matatani kwa kukataa ripoti ya redet


Na Waandishi Wetu

RIPOTI ya Utafiti wa Taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia (Redet) iliyoonyesha imani ya wananchi kwa Serikali ya Awamu ya Nne imeibua hoja mpya kuwa ni jambo lisilokubalika kisheria kwa Rais Jakaya Kikwete kutenganishwa na baraza lake la mawaziri.

Hoja hizo zimekuja kufuatia matokeo ya utafiti huo kuonyesha kuwa Watanzania wanaoridhika sana na utendaji wa Rais Jakaya Kikwete ni asilimia 44.4 wakati wale wanaoridhika sana na Baraza la Mawaziri ni asilimia 20, huku bunge likiwa na asilimia 21.8, jambo linaloonyesha kuwa Rais amelizidi baraza lake kwa utendaji kazi.

Vyanzo mbalimbali vilivyozungumza na Mwananchi Jumapili baada ya matokeo ya utafiti huo kutangazwa, vimesema kuwa haiwezekani Rais akalizidi baraza lake la mawaziri kwa utendaji kwani wale ndio watu wake wa karibu na wanaomshauri kiongozi wao.

Chanzo kimoja cha habari kilichopo karibu na serikali kimesema kwamba kwa kuwa Rais ndiye mwenyekiti wa baraza la mawaziri, ndiye anasimamia maamuzi yote yanayofanywa na baraza hilo, haiwezekani yeye akawa mtendaji mzuri na baraza lake likawa la ovyo.

"Hii inaweza kumaanisha kwamba Rais wetu anafanya kazi peke yake, au shughuli zake zimekuwa zinatangazwa kuliko za baraza lake la mawaziri. Hii si sahihi na haikubaliki," Kilisema chanzo hicho bila kutaka kutajwa jina gazetini.

Akizungumzia suala hilo Mwanasheria Mwandamizi, Profesa Abdallah Saffari, amesema si sahihi utafiti kuonyesha kuwa, Watanzania bado wana imani na Rais Jakaya Kikwete katika utendaji kazi, lakini wamepoteza imani hiyo kwa Baraza lake la Mawaziri.

Alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya utawala, makubaliano ya uwajibikaji wa pamoja na mfumo wa utawala bora unaofuatwa na serikali, Rais na baraza lake la mawaziri, hawawezi kutenganishwa na matokeo yoyote ya utendaji kazi serikalini.

Profesa Saffari alisema mfumo huo unaanzia kwa waziri ambaye anawajibika kwa kila kitu kibaya au kizuri kinachotendwa na watu walio chini yake.

"Na ndio maana Mwinyi (Ali Hassan, Rais Mstaafu) aliwahi kujiuzulu Uwaziri wa Mambo ya Ndani katika miaka ya 1980 kwa makosa yaliyotendwa na watu wa chini yake," alisema Profesa Saffari na kuongeza:

"Pia kuna collective responsibility (uwajibikaji wa pamoja). Nyumbani baba ni kiongozi, hivyo makosa yanayotendwa na mtoto, baba lazima atawajibika."

Alisema vivyo hivyo katika mfumo wa utawala bora unaofuatwa na serikali, Rais anawajibika moja kwa moja kwa vitendo vyovyote vya Baraza lake la Mawaziri.

"Ndio maana Mwalimu Nyerere alaiwahi kumfukuza kazi mkuu wa mkoa kutokana na kutamka maneno yaliyo kinyume na Baraza la Mawaziri," alisema Profesa Saffari.

Vile vile Profesa Saffari aliukosoa utafiti wa Redet kuwa sampuli wanazotumia katika kufanya utafiti huo, zimekuwa hazioani na sheria.

"Hili tumelizoea. Lakini sampling (sampuli) lazima ioane na sheria, maana uongo sasa umezidi," alisema Profesa Saffari.

Mapema, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisema si jambo la heri kwa umaarufu wa rais kuzidi ule wa serikali yake.

Alisema utendaji wa rais unatokana na ushauri unaotolewa kwake na Baraza la Mawaziri na hivyo inapotokea rais akaonekana kukubalika kuliko ilivyo kwa mawaziri wake, hizo ni dalili za kuwapo kwa tatizo kubwa katika mfumo wa utawala.

Kwa upande wake, Dk Azaveli Lwaitama wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema yeye haoni kama kuna tatizo, kwani hata utendaji wa Rais Kikwete umeshuka kutoka asilimia 67 hadi asilimia 44.4, isipokuwa tu ule wa mawaziri umeporomoka zaidi.

Alisema maana ya maoni hayo ya wananchi ni kwamba wananchi walioonyesha imani kwa Rais Kikwete wana matumaini naye kwamba akichukua hatua na kuwadhibiti mawaziri, au kupangua baraza lake utendaji wa serikali unaweza kuwaridhisha.

"Unajua utafiti huo ulifanyika Oktoba wakati kuna viguvugu la Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma Kaskazini), ambapo mawaziri wote walikuwemo wakati anasimamishwa ubunge?na Waziri Mkuu kama kiongozi mkuu wa shughuli za serikali alibariki, hiyo inaweza kuwaondolewa sifa kwa wananchi," alisema.

Dk Lwaitama alisema Rais Kikwete anaweza kuonekana kwamba hayuko pamoja na mawaziri wake, kwani hata baada ya Kabwe kusimamishwa yeye ameunda tume ya kuchunguza mikataba ya madini na kumuingiza, hivyo kuwepo uwezekano kuwa utafiti mwingine ukifanyika sasa anaweza kuongeza namba ya wanaomuunga mkono.

Mmoja wa wasomaji wa Mwananchi Jumapili ambao wamekuwa wanachangia suala hilo kwa njia ya mtandao na simu, Sabasi Bakari amesema anashangazwa na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chiligati na kumtaka atambue kuwa tathmini imefanywa kwa uongozi wa CCM ambayo umri wake si wa miaka miwili na kuwa muda huo ni sawa na asilimia 40 ya miaka mitano anayokaa rais madarakani.

Wakati msomaji mwingine, Ben Stephen, alisema umefika wakati CCM inatakiwa iwe na viongozi wanaokubali kujifunza na kujisahihisha pale inapobidi, mwingine ambaye hakujitambulisha alisema kauli hiyo ya Chiligati inaonyesha kama vile hayupo Tanzania au haelewi chochote kuhusu CCM.

"Kinachosikitisha hapa ni kuona mtu anayepinga maoni ambayo tunaamini yanotoa mwanga na ishara fulani, kuyapinga ni sawa na kutuambia hawako tayari kukosolewa lakini pia hawatafanya chochote cha maana," alisema.

Ripoti hiyo ya redet imekuwa mjadala wa takriban wiki nzima sasa ambapo kila mmoja anazungumzia lake, lakini mzigo mzito unaelekezwa kwa Katibu wa Uenezi Itikadi na Uenezi wa Chama Chama Mapinduzi (CCM), John Chiligati kwa kauli yake kuwa ni mapema mno kutoa tathmini hiyo kwani hakuna serikali yeyote duniani inayoweza kufanya miujiza katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wake.

Source: Mwananchi
 
Chilligati asikwepe wajibu, kwani chama kinachotawala tangu uhuru ni nani kama si ccm hiyohiyo kwa mda wa miaka 46.Awamu ya nne haiwezi kujitoa lawama kwa kuyumbisha uchumi wa nchi
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom