Wataalam: Ni muhimu kuwepo sheria madhubuti ya kuongoza Teknohama

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125

tech.jpg

Mkuu wa Kitivo cha Sheria wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Eleuter Mushi, akiwasilisha mada wakati wa semina ya siku moja ya masuala ya sheria na teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama).(PICHA: MPIGAPICHA WETU)


Wataalam kutoka Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Stockholm cha nchini Sweden, wamesema kunahitajika kuwepo na sheria maalum itakayosimamia teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama) ili kuchochea shughuli za maendeleo na kulinda haki miliki nchini.

Mkuu wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu Mzumbe, Dk. Eleuter Mushi, aliyasema hayo wakati wa semina ya siku moja ya masuala ya sheria na Teknohama jana jijini Dar es Salaam jana.
Chuo Kikuu Mzumbe kupitia kitivo chake cha sheria kilishirikiana na taasisi ya Chuo Kikuu cha Stokholm ya nchini Sweden ijulikanayo kama Swedish Law & Informatics Research Institute (IRI) kuendesha semina hiyo.

“Tunahitaji kuwa na sheria maalum ambayo itasaidia kusimamia, kuongoza, kudhibiti na kuleta mafanikio katika eneo hili muhimu ambalo linakua kwa kasi kubwa duniani, hivyo bila kuwa na sheria ni kurudisha nyuma shughuli za maendeleo,” alisema Dk. Mushi.

Alisema Chuo Kikuu Mzumbe kimejipanga na kimeanza kushirikiana na Chuo Kikuu cha Stockholm kupitia IRI kubadilishana mawazo, kupata uzoefu na kusomesha wahadhiri wake katika chuo hicho.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuchota ujuzi ili kutoa mchango kwa taifa kwa kuwa suala hilo ni la msingi na halitakiwi kubaki nyuma katika kipindi hiki ambapo maendeleo yanategemea Teknohama kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa, alisema semina hiyo imesaidia kubadilishana mawazo kuangalia jinsi ya kutatua changamoto ziletwazo na maendeleo ya teknolojia katika kutekeleza sera na sheria mbalimbali nchini.

“Changamoto hizi zinatakiwa kujadiliwa na mtu mmoja mmoja na taasisi ili kusaidia juhudi za serikali katika eneo hili,” alisema.
Mkurugenzi wa IRI, Profesa Cecilia Magnusson, alisisitiza umuhimu wa kuwa na sheria madhubuti zitakazosimamia Teknohama akisema kwamba hilo ni eneo linalohusisha maendeleo katika kila nyanja ya maisha kwa sasa.

“Hatuna budi kulishughulikia suala hili sasa kama tunataka maendeleo ya kweli,” alisema. Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Faustin Kamuzora, alisema semina hiyo imefanyika katika wakati mwafaka kwa kuwa hakuna sheria maalum inayosimamia eneo hilo la Teknohama nchini na hiyo ni hatari kwa kuwa eneo hilo linahusika na shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananachi.

Naye Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania, Patricia Boshe, akitoa mfano alisema kukosekana sheria madhubuti zinazoendana na upya wa teknolojia katika eneo la Teknohama nchini ni hatari hasa inapotokea uhalifu kupitia mtandao.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ubena John, ambaye anachukua masomo ya Shahada ya Uzamivu katika maeneo ya sheria na Teknohama Chuo Kikuu cha Stockholm, Sweden alisema sheria hiyo ikiwepo itasaidia kuleta maendeleo na kulinda haki miliki.




CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom