WASU: Nadharia tata katika zama tata; tulijikwaa wapi? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

WASU: Nadharia tata katika zama tata; tulijikwaa wapi?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MAKOLE, Jul 26, 2012.

 1. MAKOLE

  MAKOLE JF-Expert Member

  #1
  Jul 26, 2012
  Joined: Feb 5, 2012
  Messages: 601
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 35
  Kipindi kabla ya nchi yetu haijaonyesha nia ya kuelekea katika mifumo ya kiliberali, ilikuwa tunafundishwa
  shuleni nadharia hii ya W.A.S.U. wakubwa walitufundisha na ilikuwa ni lazima ukariri na utambue kama mwanafunzi kuwa ili tuendelee tunahitaji W.A.S.U, hii ni finyanzo (kifupisho) cha maneno W=Watu, A=Ardhi, S=Siasa Safi, U=Uongozi Bora.

  Ili nchi yetu iendelee ilihitaji mambo haya. Mwalimu Nyerere yawezekana aliikopa nadharia hii kutoka pahala Fulani, sina hakika na jambo hili lakini kwa vyovyote ilivyo, bado alikuwa sahihi na jambo hili, ingawa pia yawezekana haikuwa sahihi kwa mazingira ya wakati huo katika nchi yetu na nadharia pia haiwezi kuwa faafu kwa wakati huu kwa sababu ya mwendokasi wa mabadiliko ya kimfumo ya kidunia.

  Ni kweli kuwa ili nchi yoyote iendelee ilihitaji sana Watu, wenye uwezo wa kufanya kazi katika Ardhi yenye rutuba, wenye uwezo wa kuongozwa na siasa safi zenye kujenga uongozi bora. Yawezekana mwalimu alisahau baadhi ya mambo ya msingi hapa, lakini hata hivyo hapaswi kulaumiwa kwa sababu nilizotangulia kuzieleza hapo juu-mfumo haukuruhusu jambo hili. Lakini hebu tuangalie nyuma; tukitaka kuiendeleza nadharia hii kutokana na mazingira yetu tufanyeje?

  Tunafahamu kwa yakini kuwa nchi yetu imehama, tena hata hatujui tuko upande upi. Hatupo katika mfumo wa kiliberali, wala kwenye mfumo wa ujamaa. Wapo wanaosema kwamba tunapiga ngoma ya ujamaa ila tunacheza Kibepari. Tulikurupuka, lakini yawezekana pia hatungeweza kusubiri kwani mwendokasi wa mabadiliko ni mkubwa sana.

  Kimsingi, na kwa maoni yangu nafikiri kwamba kulingana na jamii yetu hapa ilipo, ili tuendelee tunahitaji mambo yafuatayo:-

  1 Watu wenye uwezo:

  Nafikiri sana kuwa alichokuwa amekosea mwalimu katika nadharia ya awali ni kuwa ili tuendelee tunahitaji Watu. Je, ukiwa na watu tu inatosha kukufanya uendelee? Cha maana hapa ilikuwa ni kuwa na Watu wenye uwezo kiuchumi na Kifikra kuweza kuwa na ujasiri wa kuthubutu.

  2
  Ardhi:-

  Ardhi ni rasilimali ya msingi katika maend eleo ya mwanadamu. Nchi zote zilizoendelea zinaithamini sana ardhi yao kama nyenzo msingi wa maendeleo. Haijalishi kuwa ardhi hiyo ina rutuba ama haina, kinacho tiliwa maanani ni nini kinapatikana ndani ya ardhi hiyo. Nchi za jangwani hawakuhitaji ardhi yenye rutuba, wao wanaangalia kiasi cha mafuta ardhini. Hiyo rutuba wao sio muhimu. Na pamoja kuwa ardhi ya jangwa lakini hawakuweza kuigawa hovyo kwa tama na inda kwa wawekezaji kwa sera za ubinafsishaji ama ugenishaji. Hapa kwetu tunavyo vyote, Ardhi yenye rutuba ya kutosha na madini, mbuga na misitu lakini haitusaidii sana. Yawezekana mwalimu aliliona hili mapema na akasema tu ardhi yenye rutuba akikwepa masuala ya uchimbaji madini kwani hatukuwa tayari na uwezo huo.

  3
  Siasa zenye utashi:

  Kwa sasa kulingana na mfumo wa vyama vingi tunahitaji siasa safi kama mwalimu alivyotufundisha. Lakini ni zipi siasa safi? Ni hizi zenye kukaribisha ugenishaji? Ni hizi siasa za majitaka tunazoshuhudia leo? Nadhani tunahitaji Siasa zenye Utashi. Siasa zenye kuvumiliana na kujaliana. Hii ni pamoja na kufanya siasa zenye mantiki na kujali upamoja na uwajibikaji. Sio siasa za kujuana tunazozishuhudia leo hii katika Tanzania.

  4 Uongozi wenye kujali raia wake:

  Katika mafunzo ya mwalimu, alizungumzia Uongozi bora; Lakini uongozi bora kwa nani? Kiongozi awajibike kwa nani? Hapa kwetu Tanzania Katika zama hizi kiongozi anawajibika kwa wenye mitaji, hasa wawekezaji wa kutoka nje. Hawawajali tena watu wao, Ni wakati sasa nadharia iseme wazi kuwa ili tuendelee tunahitaji uongozi unaowajali raia wake, uongozi usiokumbatia mfumo Fisadi wenye kuendekeza libeneke la rushwa, viongozi *Malaya( *kwa maana wasio na aibu) wanaoshuhudiw a leo ambapo viongozi wanafanya ubadhirifu mchana wa jua kali.

  Mwalimu aliishia hapo kulingana na zama zile. Kwa sasa tunahitaji kufika mbali zaidi, kwa maoni yangu; yapo mambo ya msingi yanayotakiwa kuendeleza nadharia ya mwalimu. Haya ni kama yafuatayo:-

  5 Taarifa sahihi:

  Katika zama hizi, ili taifa na watu wake liendelee yapasa wananchi wapate taarifa stahili na sahihi kulingana na wakati. “information is power” na wamepata kunena kuwa tajiri kwa sasa si Yule anaemiliki pesa tena, lakini ni Yule anayemiliki taarifa. Mwenye pesa kwa sasa anaweza akahaha kumtafuta mwenye taarifa ili anunue. Ukitaka kufahamu vizuri angalia biashara ya udalali ilivyo. Dalali anamiliki taarifa Fulani sahihi, lakini mwenye pesa atahaha kumtafuta dalali ili apate huduma. Watu wanahitaji taarifa sahihi na za mara kwa mara ili waende sambamba na mabadiliko ya kimfumo.

  6
  Elimu yenye sauti:


  Naam,watu hawahitaji elimu, bali elimu yenye sauti. Elimu yenye sauti ni ile ambayo haiyumbi. Elimu yenye kumuandaa msomi anayeweza kupambana na changamoto za kidunia, msomi ambaye uwezo wake wa kufikiri na kumbambanua mambo hauna mashaka. Sio wasomi ambao hawana historia, hawaandaliwi. Mfumo wetu wa sasa unamkurupusha msomi. Unamuibua samaki ambaye hajatarajiwa kuvuliwa. Kama mwanafunzi alikuwa na talanta za masomo ya sayansi mfumo wetu utamuua kwa sababu hapana shule zinazomuandaa kukuza na kuendeleza talanta yake, kama mwanafunzi alikuwa mzuri katika talanta za uongozi mfumo unamlazimisha akasomee ualimu kwa vile wazazi wake hawataweza kumsomesha elimu ya juu kwa kukosa mkopo. Kwa wale waliowahi kuangalia sinema ya kihindi inayoitwa “3 ******” Wajinga watatu watanielewa zaidi.

  7 Mtaji na maarifa ya kuuendeleza:

  Hii ni nyenzo ya mwisho kwa maoni yangu ambayo aghalabu, watu Taifa linalohitaji maendeleo linahitaji kuwapa watu wake. Mwalimu yawezekana alifungwa na mfumo wa kijamaa ambao hauruhusu watu kumiliki mtaji, bali serikali. Lakini kwa zama hizi, si tu watu wanamiliki au kumilikishwa mitaji, bali wanapaswa wawe na maarifa ya namna ya kuendeleza mitaji. Imetokea hapa kwetu kumetolewa mabilioni ya bwana Fulani, wamepewa watu masikini bila kuwapa elimu na maarifa ya namna ya kuiendeleza hiyo mitaji- KWISHA, kwani hawakuwezeshwa maarifa. Hili ni jambo la kawaida sana kwani hata mtu akipewa Tsh Milioni thelathini, kama hana maarifa ya kuziendeleza ataishia pabaya; mfano mzuri ni wastaafu wetu na namna wanavyoadhirika.

  Naomba kuwasilisha nikitarajia kupata mikinzano chanya na jengefu kutoka kwenu wadau wa JF.

  kwa sasa tunawahitaji viongozi kama hawa:

  1.
  mwalimu.jpg


  2 viongozi wakiwemo wabunge wakiagana kuelekea Bungeni Dodoma enzi za mwalimu
  bunge.jpg
   
Loading...