Wasira 'kufa' na waliotafuna fedha za TASAF

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
270
KATIKA kuhakikisha fedha za mfuko wa maendeleo ya jamii zinafanya kazi zilizokusudiwa kwa ajili ya ustawi wa nchi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uhusiano wa Jamii na Uratibu, Steven Wasira ameagiza apewe orodha ya halmashauri zote zenye rekodi mbaya ya kutafuna fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Amesisitiza pia kuwa, hatakuwa na huruma kwa watendaji wa halmashauri ambazo orodha yao itafika mikononi mwake. Wasira alitoa agizo hilo jana wakati alipotembelea ofisi za makao makuu ya mfuko huo Dar es Salaam na kuzungumza na wakuu wa idara wa mfuko huo.

Alisema, anatambua ukubwa wa tatizo la wizi wa fedha za miradi unaofanywa na halmashauri nchini na kuongeza kuwa atahakikisha kuwa hakuna fedha za miradi ya Tasaf zitakazoendelea kutafunwa.

Aliiagiza TASAF kuhakikisha kuwa inamkabidhi ripoti haraka iwezekanavyo ambayo itagusia majina halisi ya halmashauri ambazo zimekuwa zikifuja fedha hizo pamoja na idadi ya fedha walizokula.

Alisema, ulaji huo wa fedha za miradi unaongeza umasikini kwa wananchi kwa kuwa malengo yaliyokusudiwa kufanyika yanakuwa hayajafikiwa.

Alisema kuwa akiwa kama waziri mwenye dhamana ya mahusiano atahakikisha kuwa suala hilo analifikisha kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Mkuchika ili hatua za kinidhamu zichukuliwe.

“Ni kwamba nina hasira sana na hawa watu wa halmashauri wanaoiba fedha za miradi ya Tasaf na nitahakikisha kuwa nafikisha suala hili kwa Waziri Mkuchika au hata kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kama ikiwezekana,” alisema Wasira.

Pia aliushauri mfuko huo kuwa na utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii ambayo wameifadhili ili kupima utekelezaji wa miradi hiyo.

Pia alitoa mwito kwa wanasiasa kuhamasisha wananchi kuchangia fedha za miradi ya Tasaf badala ya kutoa hoja za upotoshaji.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga alisema kuwa baadhi ya wilaya zilizokula fedha za miradi wameshaziandikia barua kudai kurudishiwa fedha hizo.

Alisema, Tasaf itafuatilia suala hilo kiundani na kumpatia taarifa kamili waziri ili hatua zaidi zichukuliwe.

“Nina imani kuwa baada ya halmashauri kupata taarifa kamili kutoka kwetu zinazowataka kutoa ufafanuzi, basi hatua za haraka watachukua na kuturudishia hizo fedha,” alisema Mwamanga.
 
Back
Top Bottom