Wasiojulikana wanaojulikana....Pasco Mayalla.Miaka kama miwili iliyopita kasi za kikundi cha "Wasiojulikana" ilikuwa ya juu ajabu. Kulikuwa na tetesi nyingi kuhusu nani hasa walikuwa nyuma ya hiki kikundi, na mengi sana yalisemwa.
Kwa wengi ilikuwa ni vigumu kuamini kuwa kikundi cha "Wasiojulikana" kilikuwa hakina uhusiano na serikali kwa lojiki kwamba wale waliotekwa au kuuwawa walikuwa (victims) na "Wasiojulikana" ni wale tu walioonekana kuikosoa serikali au viongozi wa serikali, na hata Rais Magufuli. Kwa maneno mengine, ilionwa wazi kwamba uwepo wa kikundi cha "Wasiojulikana" ulikuwa kwa manufaa ya serikali iliyopo madarakani.
Na pia watu walihoji uwezo wa kifedha na ujipangaji wa kikosi hiki, ambao ni wazi haukuwa wa kikundi kisicho na mafunzo au kuwa na chanzo kikubwa cha fedha. Kwa mfano, gari aina ya Nissan Patrol mpya inayosemekana kutumika katika tukio mojawapo la "Wasijulikana" linasemakana kuchomwa moto ili kupoteza ushahidi.
Na ajabu ni kwamba mara zote matukio ya "Wasiojulikana" yalipotokea, Polisi walionekana kujiumauma katika kutoa majibu au kufanya upelelezi. Hadi leo hii, hakuna kesi hata moja inayohusu "Wasiojulikana" ambapo wahusika walikamatwa na kuhukumiwa.
Lakini sasa kikundi hiki cha "Wasiojulikana" ni kama kimepunguza kasi yake. Sintadiriki kusema kimefutwa au kukoma kuwapo. Je, ni kwa kuwa watu wameelewa kwamba katika awamu hii ukiikosoa serikali au watawala "utapotezewa" na "Wasiojulikana" ambao ni wazi wanafanya "uhalifu" kwa namna ya kuinufaisha serikali iliyopo madarakani dhidi ya kukosolewa na kutuhumiwa, huku serikali hiyo ikikana kuwafahamu au kuhusika nao. Inawezekana kuna mtu au watu wenye busara waliongea neno la hekima na "Wasiojulikana" wakawekwa gavana, kwa kuwa kuna wakati walifanya vitendo vyao kwa namna ya kuelekea kuwa kama enzi za "State Research Bureau" ya enzi ya Idd Amin wa Uganda, kikosi cha intelijensia kilichoteka na kuua yeyote aliyemkosoa Idd Amin na serikali yake.
Je, kuna siku ukweli kuhusu "Wasiojulikana" utajulikana?