Wasifu kwa minajili ya kutunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi kwa Rais Samia Suluhu

Billal Saadat

Senior Member
Nov 30, 2022
169
356
D9DF5D11-EC46-4814-A595-04F4CC1D4807.jpeg


Mheshimiwa Mkuu wa Chuo

Kwa heshima na taadhima, pia kwa unyenyekevu mkubwa,ninaomba niwasilishe taarifa kumhusu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kwa minajili ya kuifahamisha hadhira hii kwa nini mwisho wa maelezo haya nitakuomba umtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi (Doctor of Letters - Honoris Causa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Taarifa Binafsi

Kabla sijaelezea masuala mbalimbali kuhusu mchango wake kwa taifa la Tanzania, uniruhusu nieleze kwa kifupi taarifabinafsi kuhusu yeye ni nani.

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ni Rais mwanamke wa kwanza wa nchi yetu. Kwa kipindi hiki, barani Afrika kuna wanawake viongozi wa nchi wawili tu ambao ni Rais Sahle-Work Zewde wa Ethiopia pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan. Hata hivyo Rais Sahle-Work Zewde wa Ethiopia ni Rais ambaye si Mtendaji kiserikali. Ni Mkuu wa Nchi tu nasiyo Mkuu wa Serikali. Ni “Ceremonial President”. Lakini,Rais Samia Suluhu Hassan ni Rais Mtendaji, (Excutive President) mwanamke pekee katika bara la Afrika kwa kipindi hiki. Yaani ni Mkuu wa Nchi na Mkuu wa Serikali (Head of State and Head of Government).

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alizaliwa mnamo tarehe 27 Januari 1960 huko Makunduchi Zanzibar. Elimu yake ya msingi aliipata katika shule za Chwaka, Ziwani na Mahonda na baadaye kujiunga na shule ya sekondari ya Ng’ambo na pia Lumumba huko Zanzibar.

Baadaye, kiu yake ya elimu ilimsukuma hadi Chuo cha Mzumbe wakati huo kikiwa bado ni “Institute of Development Management“ ambapo alifuzu na kupata Advanced Diploma katika masuala ya Utawala wa Umma (Public Administration).

Mwaka 1994, alijipatia Postgraduate Diploma katikamasuala ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza. Mwaka 2015 alipata degree ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii katika Uchumi ya Chuo Kikuu Huria Tanzania kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.

Ajira

Historia ya ajira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaanzia Wizara ya Mipango na Maendeleo, Zanzibar,ambapo aliajiriwa kuanzia mwaka 1977 hadi 1987. Kati ya 1992 hadi 1994, alifanya kazi kama Meneja wa Miradi kwenye Shirika la Chakula Duniani (World Food Programme). Pia alijishughulisha na miradi mbalimbali kuhusiana na masuala yahusuyo jinsia.

Siasa

Safari ya Rais Samia Suluhu Hassan katika medani ya siasa ilianzia katika Umoja wa Vijana wa Chama cha Afro-Shiraz na baadaye katika Umoja wa Vijana CCM baada ya kuunganishwa kwa Umoja wa Vijana wa ASP na Umoja wa Vijana wa TANU. Hii ilifuatia kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi baada ya kuunganishwa kwa ASP na TANU mwaka 1977. Katika Chama ameshika nyadhifa mbalimbali katika ngazi ya Tawi, Wilaya, Mkoa na Taifa. Mwaka 2002 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na baadaye Mjumbe wa Kamati Kuu. Amekuwa Mjumbe wa vikao hivyo viwili vya juu vya uongozi na uamuzi vya Chama tangu wakati huo mpaka sasa.

Mnamo mwaka 2000, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,aliingia katika ulingo wa siasa za kitaifa kwa kugombea na kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia Viti Maalum. Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa Waziri katika Baraza la Mawaziri chini ya uongozi waMheshimiwa Amani Abeid Karume, aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wakati ule.Aliwahi kuwa Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake na Watoto (2000/2005) na baadaye (2005/2010) akawa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji.

Mwaka 2010, aligombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge akiwakilisha Jimbo la Makunduchi katika Bunge la Jamhuriya Muungano wa Tanzania. Mwaka huo huo aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano, nafasi aliyoitumikia hadi 2015.

Mwaka 2014 aliteuliwa kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba lililokuwa na lengo la kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika nafasi hiyo alijizolea sifa kubwa kutoka kwa Wajumbe wa Bunge hilo na Watanzania wengi kuwa aliongoza mchakato huo, uliokuwa na mivutano mikali kisiasa na changamoto nyingi, kwa umahiri mkubwa sana. Kipaji chake cha uongozi kilijipambanua na kuonekana.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliteuliwa na Chama cha Mapinduzi kuwa Mgombea Mwenza wa Mgombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli (ambaye sasa ni marehemu). Walishinda uchaguzi huo na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akawa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Makamu wa Raiswa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwaka 2020 aliteuliwa tena kuwa Mgombea Mwenza pamoja na Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Walishinda tena na kwa mara nyingine akawa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwaka 2021 tarehe 17 Machi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wa Awamu ya Tano, aliaga dunia. Roho yake ipumzike kwa amani.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano waTanzania, inapotokea Rais wa nchi kufariki, Makamu wa Rais anakuwa Rais kwa kipindi kilichosalia hadi uchaguzi mkuu unaofuata. Kwa hivyo basi Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 19 Machi 2021.

Mnamo tarehe 30 Machi 2021, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pia alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. Hapa pia aliweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kushika wadhifa wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, kikiwa ni Chama Tawala, tangu kuasisiwa kwake mwaka 1977 kufuatia kuunganishwa wa Chama cha TANU cha Tanzania Bara na Chama cha ASP cha Zanzibar.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo

Uongozi

Kabla ya kumuongelea Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhusiana na mchango wake katika masuala ya uongozi, naomba ruhusa niseme jambo.

Watu wengi huwa hawafamu kuwa kila wakati wa uchaguzi mkuu na kuingia kwa awamu mpya ya uongozi kitaifa, moyo wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam huwa unadunda kwa kasi zaidi ya kawaida. Kwa nini inakuwa hivyo?

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimepewa jukumu kubwa na Watanzania la kunoa bongo za vijana wa Taifa hili ili wanapohitimu waweze kutoa mchango muhimu wa kitaalam na kitaaluma katika kuleta maendeleo ya nchi katika sekta walizozisomea. Katika miaka yake 61 tangu kuasisiwa kwake, Chuo Kikuu hiki kimeifanya kazi hiyo kwa dhati na kwa umahiri mkubwa na mafanikio makubwa. Chuo hiki kinajivunia sana mchango mkubwa kitaalam na kitaaluma unaotolewa na wahitimu wake katika tasnia zote za maendeleo ya nchi yetu.

Hata hivyo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinafahamu fika kuwa uwezekano wa wahitimu wake kutoa mchango wenye tija kunategemea sana mazingira ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni yaliyojengwa katika jamii. Mazingira haya yanaweza kuwa wezeshi au la. Chuo Kikuu kinaelewa pia kuwa ujengwaji wa mazingira hayo wezeshi au la,unategemea kwa kiasi kikubwa sana uongozi wa kitaifa ulioko madarakani.

Ndiyo maana moyo wa Chuo Kikuu huwa unadunda kwa kasi kila uongozi wa kitaifa unapobadilika. Hofu inakuwa je katika uongozi huu mpya, wahitimu wetu wataweza kupata fursa za kutimiza wajibu wao kulitumikia Taifa lao? Je kazi kubwa iliyofanyika na Chuo Kikuu kunoa bongo za wahitimu wake itazaa matunda ndani ya jamii au itapotea bure?

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo

Kwa hivyo basi, kama ilivyokuwa kwa awamu zilizotangulia, moyo wa Chuo Kikuu ulienda kasi ile tarehe 19 Machi 2021,ulipoingia Uongozi mpya wa Awamu ya Sita, ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo, haikuchukua muda, kwa Chuo Kikuu kugundua kuwa hapakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi na uongozi mpya huu na mapigo ya moyo yakaanza kukaa sawa.

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hakuchelewa kuonesha Watanzania kuwa uongozi wake ulikuwa wa kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na kuleta utengamano na matumaini mapya kwa Taifa la Tanzania.

Katika hotuba aliyoitoa baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 19 Machi 2021,Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alisema;

“Nawasihi Watanzania kusimama pamoja na kushikamana…kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa…kuonyeshana upendo, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu na uzalendo wetu…Huu ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini…..tuweke nguvu zetu kwa pamoja kujenga Tanzania mpya….”

Katika mahojiano yake na BBC akihojiwa na Salim Kikeke, mwezi Agosti 2021, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassanpia aliwapa ujumbe mzito wale waliotilia shaka kuwepo kwa Rais mwanamke akasema;

“Some people don’t believe that women can be better presidents and we are here to show them”

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi minanetu lakini tayari amefanya mambo makubwa kwa maendeleo ya Tanzania. Waswahili husema “siku njema huonekana asubuhi.”

Uongozi Kiuchumi

Uongozi wake kwa upande wa uchumi, umejikita katikakuinua uchumi wa Taifa hili. Rais Samia ameweka juhudi kubwa katika kujenga mahusiano mema ya kiuchumi nchini, kimataifa na kikanda. Juhudi zake zimewezesha upatikanaji wa mabilioni ya fedha za misaada, mikopo na uwekezaji katika miradi mikubwa kama vile ile ya kuimarisha miundombinu, pamoja na barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari pamoja na ile ya shule, vyuo vikuu na vituo vya afya.Uwekezaji katika uchimbaji madini, viwanda, sekta binafsi na huduma nyingine za kijamii pia umeimarika.

Kuhudhuria kwake Expo-2020 huko Dubai, ambayo kutokana na Uviko-19 ilibidi ifanyike mwaka 2022, kulifungua fursa nyingi za biashara na uuzaji wa bidhaa za Tanzania nchi za nje. Kuridhia kwa serikali yake makubaliano ya African Continental Free Trade Area (AFCFTA) ambako kumefungua soko la walaji wapatao bilioni 1.2 katika ukanda wa Afrika.

Kutokana na juhudi zake za kujenga mahusiano mema na nchi jirani, uuzaji nje wa bidhaa za Tanzania katika soko la Afrika Mashariki umeongezeka kwa asilimia thelathini, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa katika historia ya nchi yetu.Mikataba ya miradi mikubwa imesainiwa kama vile ile ya usafirishaji wa gesi asilia kutoka Dar es salaam kwenda Mombasa, Kenya na bomba la mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga.

Chini ya uongozi wake, juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuinua sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania. Bajeti ya kilimo imeongozeka kwa kiwango kikubwa hadi kufikia shilingi bilioni 954 mwaka wa fedha 2022/2023. Ruzuku ya serikali imewezesha kushuka kwa bei ya mbolea kwa asilimia 50. Rais Samia Suluhu Hassan pia ameweka juhudi binafsi katika kuwatafutia wakulima masoko ya mazao yao nchi za nje, kama vile alivyowapatia soko laparachichi huko China katika ziara yake nchini humo hivi karibuni.

Rais Samia Suluhu Hassan pia ameweka juhudi kubwa katikakuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji na sekta binafsinchini ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje na kukuza sekta binafsi. Hii ni pamoja na kupunguza vikwazo katika upatikanaji vibali na leseni za biashara na kurekebisha kodi mbalimbali.

Katika hatua ya kipekee kabisa, mwaka 2022, Rais Samia alishiriki katika filamu (Ducumentary) ya “Tanzania: TheRoyal Tour” kwa madhumuni ya kutangaza kimataifa vivutio vya utalii nchini Tanzania. Filamu hii iliyoongozwa na mwandishi wa habari na mtengeneza filamu mashuhuri duniani, Peter Greenberg, ilizinduliwa rasmi kimataifa, katikaukumbi maarufu wa Paramount Theatre huko Los Angeles Marekani na baadaye katika miji kadhaa nchini Tanzania.“Tanzania: The Royal Tour” ambayo imeoneshwa katika nchi mbalimbali, imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watalii wanaoitembelea Tanzania ambalo linakadiriwa kufikia asilimia 34 kufikia mwezi Juni 2022.

Uongozi kisiasa

Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha nia kubwa ya kupanua ushiriki wa vyama vya siasa katika siasa za nchi hii. Katika kipindi kifupi cha utawala wake ameweza kupunguza, kwa kiasi kikubwa, sintofahamu za kisiasa nchini na kuashiria matumaini mapya ya amani na ushirikiano. Katika azma yake ya kujenga demokrasia na umoja nchini, amechukua hatua za makusudi kujaribu kuleta maridhiano kati ya vyama vya siasa. Mwaka 2022 aliunda “Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa”. Nakatika hotuba zake mara kwa mara, amekuwa anatilia mkazo umuhimu wa kuzingatia, umoja, mshikamano, amani, haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na uwajibikaji.

Uongozi katika kuzingatia haki za binadamu

Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa vitendo imani yake katika umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu katikauongozi. Hili limejitokeza hasa katika jitihada zake za kuimarisha usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali na kukemea unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.

Mara tu baada ya kuapishwa kuwa Rais na alipoanza kuunda safu yake ya uongozi, aliwatambua wanawake wenye uwezo na kuwateua kujaza nafasi mbalimbali za uongozi. Kwa mara ya pili Tanzania ikapata Spika wa Bunge mwanamke hivyo kufanya mihimili mikuu ya nchi, miwili kati ya mitatu,kuongozwa na wanawake. Kwa mara ya kwanza pia akateuaKatibu wa Bunge Mwanamke.

Idadi ya wanawake katika Baraza la Mawaziri ikaongezeka kutoka wanne wa awali hadi tisa. Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Waziri wa Ulinzi Mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi. Akiamini kuwa wanawake wana uwezo mkubwa kiutendaji, aliwapa Mawaziri wanawake katika Baraza lake, wizara nyingine nyeti kama vile wizara zinazoshughulika na Ardhi, Afya, Mambo ya Nje, Viwanda, Utalii na Mali Asili, Utawala Bora na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Pia Rais Samia Suluhu aliteua Maafisa Tawala wa Mikoa (RAS) wanawake 12 kati ya 26, ambayo ni asilimia 46%. Akateua majaji wapya wanawake 13 kati ya 28. Pia akahakikisha kuwa katika uteuzi wake wa Mabalozi, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Wilaya, wanawake wanafikia asilimia 30%. Idadi ya viongozi wanawake wa Taasisi na Mashirika ya Umma pia imeongezeka kutokana na juhudi binafsi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Azma yake, ambayo ameisema katika majukwaa mbalimbali kitaifa na kimataifa, ni kufikia lengo la Umoja wa Mataifa la uwiano wa 50/50 katika uongozi kati ya wanawake na wanaume.

Rais Samia Suluhu Hassan, katika azma yake hiyo hiyo ya kuleta usawa wa kijinsia, aliwezesha kupitishwa kwa sheria inayoruhusu watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa bado masomoni waruhusiwe kuendelea na shule baada ya kujifungua. Hii ni baada ya kuona kuwa takribani wasichana 8,000 walikuwa wanaacha shule kila mwaka kwa sababu ya ujauzito. Sheria hiyo hiyo pia imeruhusu watoto wote, wa kike na wa kiume, ambao kwa sababu nyingine, wameacha shule, warejee kuendelea na masomo. Wengi wa watoto hawa hasa wale wa kiume, huacha shule kutokana na umasikini unaowasukuma wakatafute vibarua ili kupata fedha za kujikimu wao na familia zao.

Pia Rais Samia ameweka nguvu nyingi katika kuhakikisha watoto wa Tanzania wanakwenda shule. Katika kipindi cha uongozi wake pamekuwepo na upanuzi mkubwa wa miundo mbinu ya shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu kupitia fedha za miradi mbalimbali ukiwemo ule wa COVID-19 uliofadhiliwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na ule wa HEET, mkopo wa Benki ya Dunia.

Katika azma yake ya kuzingatia haki za binadamu, uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pia umeweka juhudi za kustawisha uhuru wa mawazo na kujieleza katika nyanja mbalimbali za mawasiliano. Katika yale majadiliano na Salim Kikeke wa BBC Augosti 2021, niliyotaja awali, akiongea kuhusu mitandao ya jamii alisema alikuwa anaifuatilia mitandao ya jamii kwa sababu kwa mawazo yake;

“It helps us to know what people are thinking. If we ban (social media), we won’t have that freedom”.

Tuzo

Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, tayari mashirika na watu mbalimbali duniani wameona na kutambua mchango wake muhimu katika kuleta maendeleo, jambo lililopelekea yeye kupewa tuzo kadhaa ambazo ni pamoja na zifuatazo;

2022- AFRIMMA - Transitional Leadership Award – US- Dallas, Texas. Tuzo hii ni kutambua mchango wake katika kuleta maendeleo ya tasnia ya sanaa na utamaduni. Maraiswengine wa nchi za Afrika ambao wamewahi kupata tuzo hii ni pamoja na Sereste Khama Ian Khama wa Botswana- (2015) na Olusegun Obasanjo wa Nigeria (2017).

2022 – 100 Most Influential People in the World – The American Time Magazine. Kama Tuzo inavyojieleza, Rais Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kuwa kati ya watu 100 mashuhuri duniani.

2022- African Road Builders Ndiaye Trophy – Accra Ghana. Hapa alitambuliwa kwa uongozi wake na uwekezaji mkubwa wa serikali yake katika kuendeleza miundombinu ya usafirishaji wa barabara na reli nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo

Natumaini wewe na hadhira hii mbele yako, mtakubaliana na mimi kuwa kweli Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais huyu mwanamke, katika kipindi kifupi sana cha uongozi wake, ameudhihirishia ulimwengu kuwa ni Rais, Kiongozi bora, makini na mahiri ambaye ameweza kuutumikia umma wa Tanzania kwa viwango vya juu kabisa.

Uniruhusu nimnukuu tena yale maneno yake kwenye mahojiano na BBC;

“Some people don’t believe that women can be better Presidents and we are here to show them”

Kwa hakika, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amewaonesha Watanzania, na ameuonesha ulimwengu uwezo wake mkubwa wa uongozi. Na bado – KAZI INAENDELEA.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo

Kwa heshima na taadhima namhudhurisha kwako, mbele ya hadhira hii, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ili umtunukie Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi, yaani Doctor of Letters- Honoris Causa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Asanteni.
 
Binafisi mimi katika wasifu huu sioni hoja ambazo zinajustfy hadi kutunukiwa PhD hii ya heshima ni wazi weledi na misingi ya taasisi kama hii ya elimu ya juu havipo tena zaidi ya kufuata matakwa binafisi ya watu na wanasiasa, it have been reached a period where the country is rotten in every where.
 
Binafisi mimi katika wasifu huu sioni hoja ambazo zinajustfy hadi kutunukiwa PhD hii ya heshima ni wazi weledi na misingi ya taasisi kama hii ya elimu ya juu havipo tena zaidi ya kufuata matakwa binafisi ya watu na wanasiasa, it have been reached a period where the country is rotten in every where
Ikiwa musukuma kapewa kwanini inakuwa nongwa Bi Tozo 🧕
 
Wanasiasa dhaifu wanajitahidi kujivika majohonya kisomi bila kuwa na sifa stahiki. Wapo walionunua udaktari, Phd fake, wanajulikana. Kikwete alimuhonga Kubaki jina la barabara ya old bagamoyo ili yeye apewe udaktari.
 
Binafisi mimi katika wasifu huu sioni hoja ambazo zinajustfy hadi kutunukiwa PhD hii ya heshima ni wazi weledi na misingi ya taasisi kama hii ya elimu ya juu havipo tena zaidi ya kufuata matakwa binafisi ya watu na wanasiasa, it have been reached a period where the country is rotten in every where
Exactly
 
Huku Afrika kwenye katiba mbovu kama yetu, unaweza kuagiza utangazwe mshindi wa urais kwa kura uzitakazo. Hizo shahada mbalimbali unapaga ww mwenyewe utakavyo. Ukitaka hata cheo cha kijeshi unapewa. Ndio mambo ya shithole country.
 
Kuna mambo ya ovyo sana barani afrika. especially Tanzania.

Kuna mambo lukuki udsm, wanatakiwa kufanya siyo kupiga porojo za kisiasa.

Udsm jengeni ubora wa taasisi yenu iwe imara siyo kupambana na kutunuku watu PhD za fasihi ambazo hazitusaidii kabisa kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Katka Dunia ya sasa, Ma professor wa udsm kuweni wabunifu kuleta chachu kwenye secta ya elimu elimu siyo siasa.
 
Kuna mambo ya ovyo sana barani afrika. especially Tanzania. Kuna mambo lukuki udsm, wanatakiwa kufanya siyo kupiga porojo za kisiasa.
Udsm jengeni ubora wa taasisi yenu iwe imara siyo kupambana na kutunuku watu PhD za fasihi ambazo hazitusaidii kabisa kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia..... Katka Dunia ya sasa
Ma professor wa udsm kuweni wabunifu kuleta chachu kwenye secta ya elimu elimu siyo siasa

Neno sahihi ni Sekta ya Elimu.

Kutunukiwa shahada ya heshima hakupunguzi na hakuondoi sifa ya chuo. I see you more kwenye upande wa chuki binafsi kuliko hoja.
 
Wanasiasa dhaifu wanajitahidi kujivika majohonya kisomi bila kuwa na sifa stahiki. Wapo walionunua udaktari, Phd fake, wanajulikana. Kikwete alimuonya Kubaki jina la barabara ya old bagamoyo ili yeye apewe udaktari.

Hapa umeandika kama mwananfunzi wa darasa la nne…!
 
"Suala la kupewa tuzo hii nimelipokea kwa unyenyekevu mkubwa lakini nilijiuliza maswali kadhaa, sababu huko nyuma nilijaribu kuitafuta shahada hii lakini muda haukunipa nafasi, na nikajitazama sikuona kwamba nina sifa za kupewa shahada hii, lakini baada ya kusikiliza kwa makini maelezo marefu juu ya wasifu wangu, nimepata mwanga wa sababu zilizosukuma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kunitunuku shahada hii" Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Mhe.Dkt.@samia_suluhu_hassan

Chanzo: ITV

=======

Wenye Akili Kubwa (akina GENTAMYCINE) tunajua kuwa Mkakati huu Uliosukwa vyema ni wa Kukuandaa kwa (2025 Presidential Race) ili katika Karatasi ya Kura Jina lako liwe limeogezewa thamani kwa kuanza na Dk / Dkt (PhD Holder) ili Wapiga Kura wajue kuwa Mgombea nae ni Academician kama aliyeondoka mazima (your Former Boss) na Usidharaulike kama ambavyo mara zote unahisi hivyo.

Hongera kwa Doctorate yako hii ila Wengine kwa Akili Kubwa tulizobarikiwa na Mwenyezi Mungu tunaona hizi Bachelor Degrees zetu tu zinatutosha kwani hatukuenda Vyuo Vikuu kutafuta Vyeti tu vya Kitaaluma bali tulienda Kujengwa vyema Kiakili, Kifikra na Kimkakati ili tuje kuwa Msaada mkubwa wa Kimawazo (Kiushauri) kwa nyie wenye PhD's za Vikao na Msisitizo ili wanaowapeni (wanaowatunuku) nao waje Kufaidika kwa Fursa mbalimbali kwa kuwepo Kwenu Madarakani hivi.
 
Huyo rais wako wshagundua Nini?

nonsense.
Kitendo cha kuwa rais hata kama ni kwa bahati mbaya tayari ni ugunduzi tosha

We huoni katika watu karibia milion 60 rais ni yeye tu, kaugundua urais
 
Back
Top Bottom