Washauri wa rais wanapogeuka maswahiba wa Machiaveli…

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,047
Washauri wa rais wanapogeuka maswahiba wa Machiaveli…

Deusdedit Jovin Februari 20, 2008
Raia Mwema

SAKATA la umeme hewa unaotengenezwa na kampuni ya Richmond ni mfano hai kuonyesha dosari kubwa iliyo katika “sheria ya maadili ya Umachiaveli” ambayo baadhi ya watu katika Serikali ya CCM wamekuwa wakiitumia kama mizani ya kupimia ubora wa maamuzi yao na pia ubora wa sheria za bunge badala ya kutumia sheria ya maadili asilia ambayo ni mizani huru zaidi.

Ukweli ni kwamba pamoja na kuwa taifa lilijikuta katika mazingira magumu ya ukosefu wa umeme bado nia njema ya serikali katika kuingia mkataba na kampuni hii haiwezi kufuta kabisa dosari kubwa iliyo katika mbinu zilizotumika kuikabidhi majukumu kampuni hii. Utetezi wa rai hii unafuata kwa kuzingatia nadharia thabiti kuhusu anatomia ya matendo ya binadamu (theory of human action).

Ukifanya utafiti katika familia, koo, makabila, mbari na katika mataifa mbalimbali duniani utagundua kwamba baadhi ya matendo kama vile ya ngono, kuchukua mali za majirani, kusema kauli zisizo za kweli na yanayosababisha kifo cha binadamu, yanakatazwa.

Na kwa upande mwingine, utagundua kwamba katika mazingira fulani fulani baadhi ya matendo ya ngono, baadhi ya matendo ya kuchukua mali za majirani, baadhi ya matendo ya kusema kauli zisizo za kweli, na baadhi ya matendo yanayosababisha kifo cha binadamu, yanaruhusiwa.

Pia kuna matendo ambayo hayakatazwi wala kuruhusiwa, kwa maana kwamba ni hiari ya mtendaji kuyafanya au kuyaacha. Na kwa ujumla, utagundua kwamba matendo yote ya binadamu huweza kugawanywa katika makabila matatu bila kubaki: matendo adilifu (moral acts), matendo ya kihalifu (immoral acts) na matendo yasiyofungamana na upande wowote kimaadili (morally neutral acts). Kimaadili, haya ndiyo makabila matatu ya matendo ya binadamu.

Hivyo, basi, kwa msingi wa ukweli huu, swali lifuatalo linajitokeza: Kwa kuzingatia kwamba matendo ya binadamu yanacho kiwiliwili chenye sehemu tatu kuu - mbinu, lengo na mazingira—ukiwa na matendo matatu, moja likiwa ni tendo adilifu, jingine tendo la kihalifu, na la tatu likawa ni tendo lisilofungamana na upande wowote kimaadili, unawezaje kusema kwamba tendo hili liwekwe katika kikapu cha matendo adilifu, lingine liwekwe katika kikapu cha matendo ya kihalifu, na la tatu liwekwe katika kikapu baki?

Jibu kwa swali hili ni rahisi pia. Kwa kawaida ukichanganya maji moto na maji baridi unapata, siyo maji moto wala maji baridi, bali maji vuguvugu. Ukichanganya rangi nyeupe na rangi nyeusi unapata, siyo rangi nyeusi wala rangi nyeupe, bali rangi ya kahawia.

Vivyo hivyo, ukichanganya mbinu yenye dosari na lengo zuri, unapata siyo kitendo adilifu, bali kitendo chenye waa la uhalifu kwa sababu uzuri wa lengo hauwezi kufuta kabisa dosari iliyo katika mbinu. Kwa mfano ukiiba dawa hospitali kwa lengo la kuokoa uhai wa mtoto wako mwenye malalria hiki ni kitendo kibaya kimaadili kwa sababu uzuri ulio katika lengo la kuokoa uhai hauwezi kufuta kabisa ubaya ulio katika tendo la kuiba.

Ukichanganya mbinu nzuri na lengo lenye dosari, unapata siyo kitendo adilifu, bali kitendo chenye waa la uhalifu kwa sababu uzuri wa mbinu hauwezi kufuta kabisa dosari iliyo katika lengo. Kwa mfano ukitoa msaada kwa watoto yatima kwa lengo la kutafuta umaarufu kupitia luninga hicho ni kitendo kibaya kimaadili.

Na kwa ujumla, kama ukielezwa kwamba mtu fulani ameamua kufanya tendo kadha wa kadha, tendo hilo likiwa linahusisha mbinu ambayo hapa tuiite “x”, matokeo aliyolenga kuyafanikisha mtendaji ambayo hapa tuyaite “y” , na mazingira yanayomzunguka mtekelezaji ambayo hapa tuyaite “z”, basi, tendo hili litahesabiwa ni zuri kimaadili ikiwa tu katika pembe tatu ya “xyz” hakuna kona yenye dosari hata kidogo. Dosari katika kona moja tu katika pembe tatu hii inatosha kulifanya tendo zima kuitwa tendo la kihalifu.

Hata hivyo, maelezo haya yanazalisha swali jingine. Tunawezaje kuitambua dosari iliyo katika mbinu, au katika lengo au katika mazingira? Jibu kwa swali hili ni kwamba, haki za binadamu lazima ziheshimiwe na watu wote, siku zote na katika sehemu zote.

Hivyo, ikiwa lengo linahujumu haki linakuwa na dosari. Mfano ni kutoa msaada kwa watoto yatima kwa lengo la kutafuta umaarufu. Ikiwa mazingira ya tendo yanahujumu haki yanakuwa na dosari. Mfano ni kufanya tendo la ndoa kanisani wakati wa ibada.

Na ikiwa mbinu inahujumu haki inakuwa na dosari pia. Mifano hapa ni kuiba dawa hospitali kwa lengo la kuokoa uhai wa mtoto, kumbaka mtu ili aseme ukweli, kudanganya kwa lengo la kupata habari muhimu kwa ajili ya usalama wa taifa, na kadhalika.

Hivyo basi, hata kama matokeo hayajadhamiriwa na mtendaji, kama matokeo hayo ni sehemu ya mbinu iliyochaguliwa na mtendaji kwa ajili ya kufanikisha jambo alilolidhamiria yeye bado matokeo ambayo hayajadhamiriwa lazima yawe ni sehemu ya uchanganuzi wa kimaadili kutokana na mantiki kwamba tendo la binadamu katika ujumla wake linahusisha mbinu, lengo na mazingira ya tendo.

Jambo hili litaeleweka zaidi ikiwa itaeleweka kwamba katika kila tendo la binadamu kuna matokeo ya aina mbili. Kwa upande mmoja, kuna matokeotamati yaliyodhamiriwa na mtendaji (finis operantis) pale anapotumia mbinu fulani kwa ajili ya kukidhi haja yake. Na kwa upande mwingine, kuna matokeotamati ambayo lazima yaambatane na mbinu iliyotumiwa na mtendaji, bila kujali kama mtendaji anayataka matokeo haya au la (finis operis).

Katika makala hii, kwa kuwa neno “telosia” ni kisawe cha neno “matokeotamati”, basi matokeotamati yaliyodhamiriwa na mtendaji yataitwa “telosia ya mtendaji”. Kadhalika, matokeotamati yasiyodhamiriwa na mtendaji lakini ambayo lazima yajitokeze kwa sababu ya mbinu iliyochaguliwa na mtendaji yataitwa “telosia ya tendo”.

Katika aya zifuatazo natoa mifano kadhaa kuonyesha tofauti kati ya “telosia ya tendo” kwa upande mmoja na “telosia ya mtendaji” kwa upande mwingine, na hatimaye kuonyesha kwamba mara zote telosia ya mtendaji haiwezi kufuta telosia ya tendo.

Kama Juma akitengeneza saa kwa lengo la kuiuza na hivyo kujipatia mkate wake wa kila siku hapa kuna telosia za aina mbili. Telosia ya mtendaji ni kutafuta mkate wa kila siku. Na telosia ya tendo la kutengeneza saa ni kuzalisha mashine inayohesabu wakati. Telosia ya mtendaji haiwezi kufuta telosia ya tendo hili kamwe. Hii ndiyo sababu inasemwa kwamba ubora wa matokeo hutegemea mbinu zilizotumika.

Kama James atashiriki kwenye shindano la kula chakula (eating contest) ili aweze kujipatia zawadi hapa kuna telosia za aina mbili. Telosia ya mtendaji ni kutafuta zawadi. Na telosia ya tendo la kula chakula ni kuujenga mwili. Telosia ya mtendaji haiwezi kufuta telosia ya tendo hili kamwe. Hii ndiyo sababu inasemwa kwamba ubora wa matokeo hutegemea mbinu zilizotumika.

Kama daktari ataukata mguu wa Naka kwa lengo la kuzuia ugonjwa ulio mguuni kuenea mwili mzima hapa kuna telosia za aina mbili. Telosia ya mtendaji ni kuzuia ugonjwa usienee mwili mzima. Na telosia ya tendo la kukata mguu ni kusababisha kilema. Telosia ya mtendaji haiwezi kufuta telosia ya tendo hili kamwe. Hii ndiyo sababu inasemwa kwamba ubora wa matokeo hutegemea mbinu zilizotumika.

Kadhalika, kama serikali ikiingia mkataba wa kifisadi na kampuni ya Richmondi kwa nia njema ya kutatua tatizo la umeme lililoikumba nchi hapa kuna telosia za aina mbili. Telosia ya mtendaji (serikali) ni kutatua tatizo la umeme. Na telosia ya tendo la kuingia mkataba wa kifisadi ni kusababisha hasara ya mabilioni kwa taifa. Telosia ya mtendaji haiwezi kufuta telosia ya tendo hili kamwe. Hii ndiyo sababu inasemwa kwamba ubora wa matokeo hutegemea mbinu zilizotumika.

Kwa kuhitimisha basi, niseme kwamba, mpaka hapa ni wazi kuwa, tofauti na anavyofundisha Niccolo Machiavelli, malengo yanayostawisha baadhi ya haki hayawezi kuhalalisha mbinu zozote ili kuyafanikisha hata kama mbinu hizo zitabomoa haki baki (constructive ends can never justify destructive means).

Hivyo, ni wazi kwamba maadili ya Ki-machiaveli ndiyo yanaelekeza kwamba ni halali kwa Azimio la Zanzibar kufuta kipengele cha maadili ya uongozi kilichomo katika Azimio la Arusha hii ikiwa ni mbinu ya kufanikisha lengo la kuwawezesha viongozi kujishughulisha na biashara.

Ni wazi kwamba maadili ya K-imachiaveli ndiyo yanaelekeza kwamba ni halali kwa maafisa wa chama na serikali kuanzisha makampuni kama mbinu ya kufanikisha lengo la kuiba mabilioni ya pesa kutoka Benki Kuu ya Tanzania.

Ni wazi kwamba maadili ya Ki-machiaveli ndiyo yanaelekeza kwamba ni halali kwa Afisa Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania kuwaajiri watoto wa vigogo waliosomea sayansi ya upishi katika idara ya kompyuta ili kwa njia hiyo waweze kupata mishahara mikubwa inayowawezesha kuishi maisha bora kama waliyoyazoea nyumbani kwao.

Ni wazi kwamba maadili ya Ki-machiaveli ndiyo yanaelekeza kwamba ni halali kwa Waziri wa Fedha kuidhinisha malipo makubwa hata kama ni makubwa kiasi cha kuwafanya Watanzania wakose huduma za afya kwa lengo la kununua rada ya taifa.

Ni wazi kwamba maadili ya Ki-machiaveli ndiyo yanaelekeza kwamba ni halali kwa Waziri wa Fedha kuidhinisha malipo makubwa hata kama ni makubwa kiasi cha kuwafanya Watanzania kukosa huduma za kielimu kwa lengo la kununua ndege inayompatia usafiri wa uhakika rais.

Ni wazi kwamba maadili ya Ki-machiaveli ndiyo yanaelekeza kwamba ni halali kwa mkuu wa nchi kumteua mtu anayeongea lugha ya kimchumi katika nafasi ya Uwaziri wa timu ya wachezaji wanaoongea lugha ya kisheria kwa lengo la kuzuia mgawanyiko katika chama tawala.

Ni wazi kwamba maadili ya Ki-machiaveli ndiyo yanaelekeza kwamba ni halali kwa mkuu wa nchi kuunda serikali kubwa kadiri inavyowezekana kwa lengo la kulipa fadhila kwa wote waliomwezesha kuingia ikulu wakati wa uchaguzi.

Ni wazi kwamba maadili ya Ki-machiaveli ndiyo yanaelekeza kwamba ni halali kwa serikali kuwanyima mikopo baadhi ya wanafunzi waliosajiliwa katika taasisi za elimu ya juu kwa lengo kulipa ruzuku ipatayo milioni 1000 za walipa kodi kila mwezi kwa vyama vya siasa hata kama tangu tupate uhuru miaka 46 iliyopita bado hatuna hata wahitimu wa vyuo vikuu wapatao laki moja na nusu!

Na ni wazi kwamba maadili ya Ki-machiaveli ndiyo yanaelekeza kwamba ni halali kwa bunge kumnyofoa koromeo au roho mbunge anayeibana mbavu serikali ili kwa lengo la kulinda heshima ya bunge hilo.

Na kwa ujumla, ni wazi kwamba nia njema ya serikali katika kuleta kampuni ya Richmond haiwezi kuhalalisha mbinu za kifisadi zilizotumika kuileta kampuni hii.

Ni kwa sababu hii maadili ya U-machiavelli hayawezi kutumika kama mizani ya kupima ubora wa sheria za bunge kama ambavyo hayawezi kutumika kuratibu maamuzi na matendo ya serikali! Kulazimisha hilo ni sawa na kujenga kwa mkono wa kushoto na kisha kubomoa kwa mkono wa kulia.
 
Back
Top Bottom