Wasaudi si wa kuwaongoza Waislamu

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,238
Na Ahmed Rajab

SAYYID Aydarus bin Abdullah bin Sumayt, au Habib Aydarus kama wengi walivyozoea kumwita, alikuwa mcha Mungu wa kupigiwa mfano. Akipendwa mno na wenyeji wenzake wa mji wa Tarim, huko Hadhramawt, kusini mwa Yemen.

Bwana huyu alikuwa na unyenyekevu uliomfanya asiweze kumtweza hata nzi. Pamoja na kuwaongoza watu katika mambo ya dini alikuwa pia tabibu.

Hakuna aliyemwendea kwake, si mwenyeji si mgeni, aliyemfukuza au aliyemuondosha njiani. Na hakuna aliyeikanyaga Tarim asiende nyumbani kwake ubavuni mwa Masjid al-Mihdhar, moja ya misikiti mikubwa na ya kale mjini humo. Kwa miaka mingi alikuwa imamu wa msikiti huo, unaosemekana kujengwa na Sayyid Omar al-Muhdhar Abdulrahman Saggaf, aliyeishi Tarim katika karne ya 15..

Watu wakimuendea Habib Aydarus kumtaka ama awaombee dua ili wapate matilaba yao au awatibu.

Kama ilivyokuwa ada yake alfajiri ya Ijumaa ya Machi 2, mwaka huu, alisali sala ya jamaa katika msikiti wa al-Mihdhar kisha akarudi nyumbani kwake. Baada ya muda, mlango uligongwa. Ulipofunguliwa alidhihiri kijana aliyemtaka amsomee aya za Qur’an kwa sababu alisema alikuwa mgonjwa.

Habib Aydarus alimkaribisha ndani lakini alimwambia asubiri kidogo amalize kusali sala ya sunna ya dhuha. Akaingia chumba kingine na akaanza kusali.

Yule jamaa alimfuata akampiga risasi. Habib Aydarus, aliyekuwa na umri wa miaka 82, alikata roho akiwa juu ya msala, mauti yake yakishuhudiwa na mkewe.

Utajiuliza ni Mwislamu wa aina gani atayethubutu kumuua hivyo Mwislamu mwenzake, tena aliye juu ya msala akielekea Makkah akiwa ndani ya sala?

Hadi sasa aliyemuua hajapatikana. Hata hivyo, kuna kundi la Waislamu waliokuwa na sababu mbili kuu za kumuua.

Sababu ya kwanza, ni kwamba alikuwa sufi na, kwa hivyo, wakimzulia mambo kama wanavyozuliwa masufi wengine kwamba wanaingiza mambo ya uzushi (ya bidi‘a) na ya kumshirikisha Mungu katika Uislamu.

Sababu ya pili ni kwamba kwa vile alikuwa tabibu aliyepata umaarufu kwa kuwatibu wagonjwa, wakimsingizia kwamba eti alikuwa mchawi na, kwa hivyo, akenda kinyume na Uislamu.

Hizo ni hoja zinazopendwa kutolewa na Waislamu wafuatao mafundisho ya Kiwahhabi yenye chimbuko lake Saudi Arabia.

Wanawashutumu masufi kuwa wanamshirikisha Mungu ilhali ni wao wenye kumshirikisha Mungu kwa namna “wanavyowaabudu” watawala wa Saudi Arabia, kana kwamba watawala hao si binadamu wasiofanya kosa.

Kwa hakika, kutokana na vitendo vya hivi karibuni vya mwana wa mfalme Mohammed Bin Salman, ambaye ndiye mrithi wa mfalme, huu ni wakati muwafaka wa kuitafakari dhima ya Saudi Arabia, tukiwa na maana ya watawala wake katika ulimwengu wa Kiislamu.

Kuna sababu kadhaa zinazowanyima watawala hao sifa za kuwa viongozi wa Waislamu, hasa wa madhehebu ya Sunni. Nitazitaja chache tu. Ya kwanza ni kwamba hii aila au ukoo wa al-Saud, uliojipachika ufalme baada ya kuua na kuiita nchi iliyoiteka kwa jina lake ni ukoo uliofurutu ada katika maovu mengi na unaoonekana dhahir ukenda kinyume na maslahi ya Waislamu.

Pili, ufalme wao si halali. Wamejipachika baada ya kuibuka washindi katika vita vya kikabila katika maeneo ya Nejd na Hijaz ya Uarabuni. Ukoo huu umetokea eneo la Nejd, lililo sehemu za kati za nchi ijulikanayo leo kama Saudi Arabia. Huko pia ndiko alikozaliwa mwanzilishi wa itikadi ya Kiwahhabi, Mohamed bin Abdulwahab (1703-1792).

Lakini, hata ingalikuwa ufalme huo ulipatikana kwa ridhaa ya watawaliwa, taasisi ya ufalme haimo katika uislamu.

Tatu ni kwamba tangu mwanzo wake, ukoo huo umekuwa ukitawala kimabavu ukishirikiana na mashekhe wao wa kiwahhabi.

Ma al Saud wana utajiri mkubwa, usiosemeka, wanaoutumia kwa ubadhirifu. Utajiri wenyewe wameupata kwa njia za haramu, za wizi wa mali ya taifa. Wanajiona kwamba wao ndio wenye haki ya kuimiliki Saudi Arabia nzima na utajiri wake wote.

Wana haki ya kufanya watakacho katika taifa la matajiri wachache na maelfu kwa maelfu ya mafukara.

Tangu miaka ya mwanzo ya 1960, watawala hao wamekuwa wakiutumia utajiri wa Saudi Arabia kwa kuisambaza itikadi ya kiwahhabi kwingineko duniani, ikiwa pamoja na Afrika. Wamefanya hivyo ili kuzivunja nguvu itikadi za kimaendeleo zisizojikita juu ya dini. Waliziona itikadi hizo kuwa ni zenye kuhatarisha tawala za kifalme za Mashariki ya Kati.

Moja ya itikadi walizokuwa wakizipiga vita ni ile ya uananchi wa Kiarabu iliyokuwa ikipigiwa debe na waliompindua Mfalme Farouk nchini Misri 1952, wakiongozwa na Gamal Abdel Nasser.

Itikadi nyingine waliyotaka kuishinda ni ile ya uBa ‘ath, iliyoanzishwa na wasomi wa Syria kina Michel Aflaq, Salahal Din al Bitar na Zaki al Arsuzi. Itikadi hiyo pia ilijikita juu ya Uarabu. Ndiyo iliyokuwa ikifuatwa Iraq enzi za Saddam Hussein na Syria (ilipokuwa chini ya Rais Hafez al Assad na sasa ikiwa chini ya mwanawe Bashar).

Na tangu apinduliwe mfalme wa Iran, Shah Mohammad Reza Pahlavi Februari 1979 na vuguvugu la Kiislamu, Saudi Arabia imezidi kuingiwa na kiwewe na imeshiriki katika njama za kuuangusha utawala wa kiislamu nchini Iran. Wameitumia itikadi yao ya kiwahhabi kuwakufurisha mashi‘a na kuleta fitna na mgawanyiko katika umma wa Kiislamu. Kuwagawanya Waislamu sio sifa ya kiongozi wa Waislamu. Hiyo ni sifa ya adui wa Waislamu.

Watawala hao wamekuwa wakiwatumia mashekhe kama Abdulrahman asSudais na Abdulaziz al Rays kuwatetea. Mashekhe hao ambao ni maimamu wa msikiti mkuu wa Makkah wamekuwa wakiwatetea katika khutba zao za Ijumaa.

Wamekuwa wakihoji kwamba ni wajib wa Waislamu wote kumuunga mkono na kumtii mfalme wa Saudi Arabia. Inasikitisha kuwasikia mashekhe hao wakihubiri hivyo huku wakitambua kwamba watawala hao hawana uadilifu wa kustahiki kutiiwa na Waislamu si wa ulimwengu mzima na wala si wa huko kwao.

Mashekhe hao na wana wenzao katika nchi zetu za Afrika ya Mashariki wameshindwa kuwakemea watawala wa Saudi Arabia kwa walivyomuua kinyama mwandishi Jamal Khashoggi. Wameshindwa kutanabahisha kwamba Shari‘a ya Kiislamu inaharamisha kabisa kitendo cha “muthla” yaani cha kuikatakata maiti kama ilivyokatwa ya Khashoggi. Hata wafiwa wa mtu aliyeuliwa na maiti yake kukatwakatwa hawaruhusiwi kumsamehe aliyefanya unyama huo.

Wamekaa kimya waislamu wenzao wenye asili ya Palestina wanavyonyimwa viza, kwa sababu za kisiasa, za kuingia Saudi Arabia kufanya ibada za hijja au umra.

Badala ya kuujenga na kuupa nguvu Uislamu, watawala wa Saudia kwa vitendo vyao wamekuwa wakiuvunja nguvu Uislamu.

Wameliharibu jina la Uislamu ulimwenguni na ndani ya nchi yao wamezibomoa kabisa turathi za Kiislamu zilizo karibu na msikiti mkuu wa Makkah na msikiti wa Mtume Muhammad huko Madinah.

Mohammed Bin Salman ameanzisha vita Yemen; matokeo yake ni kuuawa kwa maelfu ya wanawake na watoto. Asitosheke akaigeukia Qatar na kuipiga pande kwa sababu nchi hiyo haikukubali kukaliwa kichwani naye Bin Salman. Kuna tetesi kwamba alifika hadi hata ya kujaribu kuivamia kijeshi Qatar.

Halafu kuna kadhia ya Saad Hariri, waziri mkuu wa Lebanon, aliyetekwa Riyadh, Saudi Arabia, na akaamrishwa na Bin Salman ajiuzulu.

Ndani ya nchi kuna hali ya woga mkubwa.

Kamatakamata ilianza kwa nguvu tangu Juni, 2017 alipoteuliwa Bin Salman awe mrithi wa Mfalme. Maelfu ya watu wametumbukizwa jela kwa sababu wana fikra zenye kupingana na zake.

Miongoni mwa hao wafungwa wa fikra ni wanaharakati, mashekhe, makadhi, maimamu wa zamani wa msikiti mkuu wa Makkah na mahakimu. Wengi wa hao waliokamatwa haijulikani wamefungwa jela gani. Kwa mujibu wa taarifa, mashekhe na wanazuoni 60, maprofesa 50 na zaidi ya mawakili 10 wametiwa korokoroni.

Wanaharakati wanaozidi 20 nao pia wako ndani kwa kutetea haki za binadamu. Kadhalika, wanahabari 25 na waandishi 40 wamekamatwa pamoja na watu wasiopungua 60 wenye shahada za juu za uzamivu (PhD).

Watu hao mashuhuri na mahashumu si wahalifu wa sheria. Wanazipinga tu baadhi ya hatua za Bin Salman. Kati yao ni Sheikh Bandar bin Aziz Bilal, Sheikh Saleh al-Talib na Sheikh Salman al-Awdah ambaye mshtaki wa serikali ametaka apewe hukumu ya kifo.

Kuna mmoja, mchumi Essam al-Zamil, aliyefungwa jela bila ya mashtaka tangu Septemba mwaka jana kwa sababu alijaribu kuishauri serikali isiliuze shirika lake la mafuta la Aramco, kama alivyotaka kufanya Bin Salman.

Mwaka huu wanaharakati wengi wa haki za wanawake walijikuta nao wametumbukizwa gerezani.

Wengine wamekamatwa kwa sababu wamekuwa wakipendekeza kuwa mfumo wa ufalme wa nchi hiyo ubadilishwe na uwe wa ufalme wa kikatiba. Si kwamba wanataka ufalme uondoshwe kabisa ila wanataka urekebishwe ili uruhusu chaguzi za kidemokrasia.

Baadhi ya wafungwa wameteswa na wamefariki gerezani. Kati yao ni Sheikh Suleiman Daweesh. Wengine kama Sheikh Nimr al Nimr, shekhe wa kishi‘a, walifunguliwa mashitaki ya uwongo na wakahukumiwa kifo.

Mashekhe wenzao wenye kuwatetea watawala hawakuwatetea. Al Rayes, kwa mfano, amethubutu kuhoji kwenye mhadhara kwamba hata ikiwa mtawala wa Saudia “ataonekana anazini hadharani kwenye televisheni kwa nusu saa kila siku, bado unatakiwa uwafanye watu wamuunge mkono mtawala huyo, na sio uwachochee wawe dhidi yake.”

Muumini yeyote atajua kwamba huu ni uzandiki wa kujipendekeza kwa watawala wa Saudi Arabia wasiostahiki kutawala kwao wala kuwaongoza Waislamu duniani kote.
 
Nakubali kabisa kuwa Saudi Arabia haitakiwi kuongoza umma ya Kiislam. Ukweli ni kwamba utawala huu ni adui mkubwa wa Islam na wanadhoefisha Uislam. Utawala huu umebandikzwa na Marekani na washirika wenzake, na hawana nia njema na Waislamu. Nchi za Kiislamu zimejaliwa utajiri mkubwa lakini yote inaishia Marekani na Ulaya! Wanapoteza mabillioni ya dolla kwenye starehe na anasa za kupindukia, lakini hawajitokezi kutoa msaada kwa waislamu kama marohingya huko Burma au wauighur huko China! Sasa wanastahili vipi kuongoza Uislamu?!!!
 
Kinachowalinda watawala wa Saudia ni utajiri wao wa mafuta, biashara ya mabilioni ya dola ya silaha kutoka Marekani na nchi za magharibi hivyo hata wafanye unyama watavumiliwa tu.
 
Yaani mashehe huwa mnanifurahisha sana yakiwabumia wa kwanza kumlaumu Ni USA hivi mnataka USA awe analiwasha chakula mdomoni?

Mbona marekani ndiye anayeongoza kuzalisha duniani? Jaribu kusoma usiwe unaamini kila unachoambiwa
Nakubali kabisa kuwa Saudi Arabia haitakiwi kuongoza umma ya Kiislam. Ukweli ni kwamba utawala huu ni adui mkubwa wa Islam na wanadhoefisha Uislam. Utawala huu umebandikzwa na Marekani na washirika wenzake, na hawana nia njema na Waislamu. Nchi za Kiislamu zimejaliwa utajiri mkubwa lakini yote inaishia Marekani na Ulaya! Wanapoteza mabillioni ya dolla kwenye starehe na anasa za kupindukia, lakini hawajitokezi kutoa msaada kwa waislamu kama marohingya huko Burma au wauighur huko China! Sasa wanastahili vipi kuongoza Uislamu?!!!
 
Inaonesha mwandisha umeandika makala yako kwa chuki bila hoja za kisheria zinazothibitisha unachokizungumza


Makala ndefu lakini umejaza tuhuma badala ya ushahidi wa like uachokisema pia uitakiwa ufahamu kwanza uisilamu kisha uje kuandika makala vuzuri

Ktik mambo uiyiyagusa unasema serikali ya saudia inatumia Mali za Saudi kueneza uwahaby hapo ninaswali kidogo

UWAHABY MAANA YAKE NINI ?
 
Muandishi wahii makala ni ktk watu waongo tena wanaopenda kuwazulia watu uongo
Kwani kwamujibu wa sheria za uisilamu kiongozi akiwa muovu na uovuawake ikilawa haumtoi katika uisilamu hapaswi kutiiwa ?


Ungekuwa unafahamu viongozi waovu waluopita na walikuwa wanatiiwa inasikitisha sana madudu ulivyo uliyajaza na mwida mwingi uliyotumia kuyaandika loo! Huku ni kuizungumza dini bila misingi ya kisharia na kutumia hukumu ya kijahil kwa kuwa hukumu viongozi wanaokosea

Ilitosha ukatafuta watu wakufundishe juu ya viongozi unatakiwa kuishinao vpi

Yaani miamala ya kiongozi na wewe maana wajaza tuhuma na chuki ndaniyake kwa hoja za uongo kabisa

Hayo ndiyo madhala ya kuto kukaadarasani badala yake watu mnajisomesha kwa mitandao ya kijamii kupotea kulioje
 
Nakubali kabisa kuwa Saudi Arabia haitakiwi kuongoza umma ya Kiislam. Ukweli ni kwamba utawala huu ni adui mkubwa wa Islam na wanadhoefisha Uislam.
Makka wao ndio waitunza wangetaka kuudhoofisha uislamu si wangepiga marufuku waislamu kwenda kuhiji makka
 
KWANI NANI KASEMA UFALME WA SAUDIA NI VIONGOZI WA WAISLAM HASA WASUNNI? Ni bahati tu qibla na misikiti mitakatifu ipo kwao lakini si viongozi wa waislamu wasunni. Wasunni hawana centralized leadership structure, kila nchi, kila mji unaruhusiwa kufanya mambo yake!
 
Inaonesha mwandisha umeandika makala yako kwa chuki bila hoja za kisheria zinazothibitisha unachokizungumza


Makala ndefu lakini umejaza tuhuma badala ya ushahidi wa like uachokisema pia uitakiwa ufahamu kwanza uisilamu kisha uje kuandika makala vuzuri

Ktik mambo uiyiyagusa unasema serikali ya saudia inatumia Mali za Saudi kueneza uwahaby hapo ninaswali kidogo

UWAHABY MAANA YAKE NINI ?
Mwandishi anaonekana ni Mshia au ameathiriwa na fikra za Kishia. Haoni baadhi ya nchi za kiarabu/kiislamu zilivyoparanganyika kwa kuwatoa watawala kwa nguvu? Mafunzo sahihi ya Uislamu ni kuwa watawala wanapokuwa waovu mnatakiwa mfanye subira juu ya uovu huo na mrejee kwa Allah ukweli wa kurejea, kinyume cha hivyo ndio tunaona leo fikra za kigaidi zinavyosumbua ulimwengu. Kila mtu leo ni shahidi jinsi gani ugaidi ulivyowaathiri watu duniani hasahasa Waislamu wenyewe. Mwisho naomba watu tuusome uislamu sahihi, na huwezi kupata kuujua isipokuwa kupitia kwa SALAF SWAALIH
 
Back
Top Bottom