Wasanii wataka mgao wa mirabaha uwe wa haki na kwa mujibu wa sheria

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,001
9,866
Wasanii wataka mgao wa mirabaha uwe wa haki na kwa mujibu wa sheria
Ugawaji wa mirahaba wa hivi karibuni haukujumuisha vikundi vingi vya wasanii na haukufuata matakwa ya kisheria
19 Februari 2022, Dar es Salaam: Mtandao wa Sekta ya Ubunifu Tanzania Ujulikanao kama “The Creative Industry Network Tanzania(CINT), kwa kushirikiana na Twaweza, wanatoa wito kwa serikali na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA kuangalia upya utaratibu wao wa kugawa mirabaha kwa wasanii.

Tarehe 28 Januari 2022, Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kiligawa mirabaha yenye thamani ya Tsh 312,290,259 kwa wasanii 1,123 kwa kazi za wasanii wa muziki 5,924 zilizokusanywa kuanzia mwezi Julai hadi Novemba 2021. Mirabaha hiyo ilitolewa na vituo saba vya redio.

Hata hivyo, ugawaji wa mirabaha hiyo ulikiuka utashi na matakwa ya sheria kwenye maeneo kadhaa muhimu. CINT inaitaka serikali kutekeleza jukumu lake kama mdhibiti na COSOTA kama chombo cha usimamizi wa makusanyo na hivyo kuwa mgawaji/msambazaji, na wote wawili wapitie haraka mchakato wa ugawaji wa mirabaha ili kusaidia tasnia ya ubunifu nchini Tanzania isonge mbele.

Masuala yaliyoangaliwa na CINT ni pamoja na:

Ugawaji wa mirabaha iliyokusanywa kati ya mwezi Januari 2019 na Juni 2022
: Mirabaha iligawiwa kwa mara ya mwisho na COSOTA mwezi Agosti 2019 ikichukua kipindi cha hadi mwisho wa 2018. Hata hivyo, COSOTA inatakiwa kugawa mrabaha angalau mara moja kwa mwaka. Kwenye tangazo la ugawaji wa mrabaha lililotolewa mwezi Januari 2022, halikutaja kiasi cha mirabaha iliyokusanywa kati ya mwaka 2019 na 2021, na mirabaha hii bado haijagawanywa kama sheria inavyotaka.

Mirabaha ililipwa kwa wanamuziki tu: Hadi muda huu mirabaha imetolewa kwa wanamuziki pekee, mara mbili, mwezi Agosti 2019 na hivi karibuni tu mwezi Januari 2022. Hata hivyo, COSOTA inafanya kazi kwa ajili ya wasanii wote na watunzi/wabunifu wa kazi zenye hakimiliki zikiwemo filamu, program (maunzilaini), sanaa za uchongaji, usanifu, waandishi na makundi mengine. Utaratibu huu siyo mzuri na hautendi haki kwa wasanii wengine wote wasio wanamuziki na inaleta mgawanyiko ndani ya sekta

Mirabaha iligawiwa kwa baadhi tu ya wanamuziki: Sheria ya Hakimiliki na Ushirikishaji inaitaka COSOTA kugawa mirabaha kwa kuzingatia leja ya kumbukumbu. Leja hizi zinapaswa kukusanywa kutoka nchini nzima kwa watumiaji mbalimbali wa kazi za ubunifu. Hata hivyo, COSOTA ilitangaza kuwa wametumia kumbukumbu za redio kwa baadhi tu ya wanamuziki kama sampuli ya kugawa mirabaha. Huu ni ubaguzi, kinyume na matakwa ya sheria, na haueleweki kwasababu hakuna njia ya kujua COSOTA iliamua kwa kutumia kanuni au vigezo gani kuhusu mirabaha gani igawiwe na nani apewe nini.

Kukosekana kwa uwazi COSOTA: Haieleweki kwa wadau ni wapi COSOTA huwasilisha taarifa za hesabu zake. Hakuna uwazi katika ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha. Hii ina maana kwamba watunzi wa kazi zilizo na hakimiliki hawana namna ya kuelewa ni kwa namna gani COSOTA anakusanya na kugawa fedha kwa niaba yao. Hii inasababisha wadau kupoteza Imani na COSOTA, na inaweza kuleta migogoro ndani ya sekta.

Kuchangia mfuko mkuu wa sanaa na utamaduni: Kwenye tangazo lao kuhusu mgawanyo wa mirabaha, COSOTA iliutangazia umma kuwa mrabaha uliokuwa umepokelewa kutoka Afrika Kusini, ambao ni kiasi kidogo, umepelekwa kwenye mfuko mkuu wa sanaa na utamaduni. Uamuzi huu ni ukiukaji wa sheria ambayo inasema wazi kwamba, mrabaha kutoka nje ya nchi unapaswa kulipwa moja kwa moja kwa watayarishaji wa maudhui husika. Aidha, sheria inasema kuwa asilimia ya mirabaha inayopokelewa inaweza kupelekwa kwenye mfuko mkuu kwa ajili ya wasanii na ustawi wao. Mfuko mkuu wa sanaa na utamaduni hadi sasa bado haujaanza kufanya kazi na hauna wanachama. Kwahiyo, kupeleka mrabaha kwenye mfuko huu kunakiuka matakwa ya sheria.

Hadi sasa Hakuna Bodi ya Uongozi ya COSOTA: Tangu 2008, COSOTA haijawahi kuwa na Bodi ya Uongozi. Hii ina maana kuwa kuna maamuzi kadhaa yanayochukuliwa na menejimenti ambayo yanakiuka sheria. Kwa mfano, ugawaji wa mrabaha unatakiwa kutanguliwa na mkutano mkuu, jambo ambalo halikufanyika.

Kutokana na ukiukwaji huu wa Sheria ya Hakimiliki na Ushirikishaji kupitia ugawaji wa mirabaha wa hivi karibuni, na kwa kutambua mchango mkubwa wa wasanii na wabunifu wote kwenye maendeleo ya nchi yetu kiuchumi na kisiasa, Mtandao wa Sekta ya Ubunifu Tanzania(CINT), unaitaka COSOTA kufanya yafuatayo:

Isitishe ugawaji wa mirabaha unaoendelea ili kutoa fursa ya kupitia upya na kuhakiki uhalali wa wanufaika kulingana na sheria na kanuni zilizopo kisha irudie zoezi la kugawa mirabaha kulingana na sheria punde itakapojiridhisha imefanya marekebisho na uhakiki wa vipengele vyote vyenye mapungufu.

Iitishe mkutano mkuu wa wanachama ili kuwezesha kufanya maamuzi kulingana na katiba ya chama pamoja na kupitia mahesabu ya chama.

Itangaze mchakato wa kupata wajumbe wa bodi.

Imtaarifu Waziri mwenye dhamana juu ya wajibu wake kisheria wa kuchagua mwenyekiti wa bodi ya COSOTA.

Itoe ufafanuzi juu ya ugawaji wa mirabaha uliofanywa mwezi Agosti 2019 na kupendekeza namna ya kumaliza utata unaotokana na ugawaji huo.

Robert Mwampembwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Tasnia ya Ubunifu Tanzania, alisema “Tumekuwa tukiishauri Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kutatua changamoto za ugawaji wa mirabaha na uongozi wa COSOTA kwa miaka kadhaa. Ni wazi kwamba wabunifu wanachangia kwa kiasi kikubwa amani na mshikamano nchini kwetu, vile vile ukuaji wa uchumi. Wanahitaji kulelewa na kuheshimiwa haki zao. Tunaiomba Serikali ishirikiane nasi kutatua matatizo haya kwa manufaa na maendeleo ya wabunifu wote wa Tanzania.”

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema “Twaweza inafanya kazi ya kupaza sauti za wananchi ili wawe sehemu ya maamuzi yanayohusu maisha yao. Kama mfano huu wa ugawaji wa mrabaha unavyotuonesha, sauti za wasanii na wabunifu hazizingatiwi sana wakati maamuzi kuhusu sekta yao yanafanywa. Tunatumai kuwa wito huu wa pamoja wa kupitia upya mchakato wa ugawaji wa mrabaha ili kuuweka wazi zaidi na utende haki, utasikilizwa.”
 

Attachments

  • Mirabaha PDF.pdf
    180.4 KB · Views: 18
Back
Top Bottom