Yoyo Zhou
Member
- Jun 16, 2020
- 72
- 110
Tunafahamu kuwa kuchagua au kuchaguliwa ni haki na ni demokrasia ya kila mtu hasa endapo umetimiza umri wa kuchagua ama vigezo vya kuchaguliwa. Ndio maana hivi karibuni tumekuwa tukishuhudia wimbi kubwa la wasanii wakitangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao. Wimbi hili kwa sasa limezua maswali mengi sana, wengi wakishuku uwezo wa kuongoza wa wasanii hawa wanaotaka kuhama kwenye sanaa na kuingia upande wa siasa. Uongozi sasa umegeuzwa kama mchezo wa watoto ambapo kila atakaye anajiunga na kucheza. Kwa ninavyofahamu kiongozi ili uitwe kiongozi basi ni lazima kutakuwa na vigezo vyake vinavyokutambulisha kuwa wewe ni kiongozi, halikadhalika kwa msanii pia kutakuwa na vigezo vyake. Lakini kinachotia hofu ni kwamba baadhi ya wasanii wanatumia umaarufu wao waliopata kwenye usanii na kuamua kujitosa kwenye siasa. Uongozi sio lele mama, uongozi unahitaji weledi na uwezo mkubwa, lakini pia unahitaji mtu kujitoa kwa kuweka mbele maslahi ya watu waliokutuma na kukuchagua kuliko maslahi yako binafsi.
Kwa Tanzania nafasi inayoonekana kukodolewa macho na wasanii wengi ni ya ubunge. Tumesikia majina makubwa ya wasanii kama vile Rajab Abdul Kahali au maarufu kama Harmonize ambaye aliweka wazi nia yake ya kutaka kugombea ubunge kwenye jimbo la nyumbani kwao alikozaliwa huko Tandahimba Mtwara. Ingawa kwa upande mmoja ndoto ya Harmonize ilichochewa na rais Magufuli alipomwambia ajitokeze kugombea kwenye jimbo lake, lakini kabla ya kuamua kuingia mzimamzima kwanza alipaswa kujipima na kujiuliza je, kweli ninafaa kuliongoza jimbo? Wengine ni Hamisi Mwinjuma almaarufu kama Mwana FA, mtoto wa mwanasiasa mkongwe Steven Wasira ambaye anaitwa Wabiro Noel Wasira maarufu kwa jina la Wakazi, msanii wa kike anayeitwa Zuwena Mohammed anayejulikana zaidi kama Shilole, na Steven Mlengele maarufu kama Steve Nyerere, ambaye ni muigizaji na ameshaueleza umma kuwa jimbo la Iringa mjini safari hii ndilo atakalokwenda kuwania.
Huu si uchaguzi wa kwanza kushuhudia wasanii au hata wanamichezo wakitupia jicho lao kwenye siasa, mfano mzuri ni aliyekuwa mchezaji maarufu wa Liberia ambaye baadaye akaingia kwenye ulingo wa siasa, George Manneh Oppong Weah. Ni rais wa 25 nchini Liberia lakini ukiangalia huko nyuma kabla ya kuingia madarakani alipata pingamizi kubwa kwa kuonekana kwamba hana uwezo wala uzoefu wa kuendesha nchi.
Kwa suala hili la uzoefu na uwezo wa kuongoza, watu huwa wanataka viongozi wenye akili tendaji na masikio sikivu yatakayoweza kusikia vilio vya wananchi wenye shida mbalimbali. Na sio viongozi ambao wanaingia madarakani kutokana na shinikizo la mashabiki wao au kusifiwa kidogo tu kuwa wana uwezo wa kuongoza pasi na kujitathmini kwanza kujua kama kweli wanaweza kuongoza jahazi bila kulipeleka mrama.
Kama hayo hayatoshi juzijuzi tu tumesikia tena msanii nguli nchini Marekani Kanye West akitangaza kupitia twitter kwamba kwenye uchaguzi wa rais wa Novemba 3 mwaka huu naye pia atawania. Kanye anasema anawania kwasababu “Mungu amemfumbua macho na kumwambia kwamba sasa ndio wakati wenyewe”
Ni kweli dini ni muhimu kwa muumini yeyote yule, lakini hapa tunazungumzia kuongoza taifa. Mana kipindi ugonjwa wa corona ulipoibuka baadhi ya viongozi wa dini pia walisema wameoteshwa na Mungu usingizini dawa ya corona, cha ajabu hakuna hata mmoja wao aliyetoa dawa hiyo, na kibaya zaidi miongoni mwa haohao waliosema wameoteshwa dawa, sasa wameshatangulia mbele ya haki kwa ugonjwa wa COVID-19. Kwa hiyo kabla ya kufanya jambo lolote ni lazima kwanza tungekaa na kutafakari.