Wasabato Masalia waendeleza vituko Dar

Ngongo

JF-Expert Member
Sep 20, 2008
18,917
31,157
Kundi la watu wanaojiita wa madhehebu ya Wasabato Masalia waliopiga kambi Dar es Salaam, wameendelea kuishi katika mazingira magumu hali iliyosababisha mmojawao kupoteza maisha.

Sambamba na kuishi katika mazingira magumu na machafu, Wasabato Masalia hao wapatao 30 walio katika kambi ya Tabata Sanene, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wamesema licha ya kufukuzwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere bado wana mpango wa kwenda tena kwa lengo la kusafiri nje ya nchi kuhubiri Neno la Mungu.

Wakielezea maisha wanayoishi, majirani wa eneo hilo walisema wiki tatu zilizopita, walishuhudia mwanaume wa kundi hilo aliyeumwa na nyoka katika kichaka wanamoishi na majirani wakataka kutoa msaada wa kwenda kumtibu, lakini wenzake wanaojiita Wainjilisti walikataa wakidai angetibiwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.

“Yule kijana aliumwa na nyoka na akabadilika rangi mwishowe akafariki dunia na wenzake (Wasabato Masalia) wakamzika kwenye mwembe jirani na walipo na sasa hivi kuna mwanamke anaumwa amevimba sana miguu na tunamsikia analia sana, lakini wenzake hawataki apelekwe hospitalini wanamficha,” alisema Paulina Maro anayeishi jirani na kambi hiyo.

Hata hivyo, mmoja wa waumini hao, Fanuel Saasita, aliliambia gazeti hili kuwa hakuna mtu aliyefariki dunia eneo hilo na wao hawatakufa kwani Mungu anawalinda na kuongeza: “Aliyekufa ni kijana wa miaka 30 ambaye alifia katika gereza la Keko na walimzika huko huko, na hapa hakuna aliyekufa”.

Mbali na hilo, Saasita alidai kuwa Mungu ameshawaeleza waendelee na mpango wao wa kwenda Uwanja wa Ndege wa Julius kupanda ndege bila hati za kusafiria wala tikiti na kwenda nchi mbalimbali kutangaza onyo maalumu kutoka kwa Mungu.

“Tunachosubiri sasa ni amri kutoka kwa Mungu kutuambia leo nendeni na ndipo tutakapokwenda huko, Mungu hutuambia kwa njia ya njozi nasi tutatekeleza, tunakwenda kuieleza Dunia, kuwa utawala wa serikali unapaswa kushirikiana na utawala wa dini kukuza uchumi wa Dunia na Jumapili ni siku ya mapumziko na si kuchanganya na kazi,” alisema.

Majirani wa eneo hilo walisema watu hao hawana usumbufu isipokuwa wanawakera kwa kujisaidia hovyo katika maeneo yao, hasa katika bustani za mchicha na kusababisha watu wengi kuacha kununua mboga hiyo katika eneo hilo.

Gazeti hili liliwashuhudia zaidi ya Wasabato Masalia 15 waliokuwa eneo hilo huku wengi wao wakiwa na ugonjwa wa ngozi, wakati wenzao wengine wakiwa wamekwenda kutafuta chakula na fedha na kuwaona wakipika chakula, wakichota maji ya kunywa na kwa matumizi yao kutoka kwenye dimbwi la maji yasiyo salama.

Katika eneo hilo walilopo kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, wameweka karatasi ndogo ya nailoni wanakohifadhi vyakula huku wenyewe wakilala ardhini, hali wanayoieleza kuwa wamepangiwa na Mungu na kuridhika nayo na kuongeza kuwa wakati wowote watahamia eneo lingine watakaloelekezwa pia na Mungu.

Ingawa wenyewe walidai kuwa fedha na chakula wanapelekewa na Mungu, majirani walisema mara kwa mara wamekuwa wakienda katika maduka barabarani kuomba msaada wa fedha na chakula.

Akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema kwa sasa hawezi kuwakamata kwa sababu hawajafanya kosa la jinai na kuahidi suala lao kuliwasilisha katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ilala, ili watu wa Ustawi wa Jamii waweze kuwapa elimu na kuwarejesha maeneo walikotoka.

Wengi wao wanatokea Kyela, Mbeya na Musoma, Mara. Hata hivyo, alisema watakapokwenda kuweka kambi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, atawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria. Wasabato Masalia walianza kuweka kambi katika maeneo manne tofauti, matatu eneo la Tabata Sanene na Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere tangu mwaka jana.

Waliwahi kukamatwa na kuwekwa rumande kwa siku 40 kwa tuhuma za kuvamia eneo la mtu. Hata hivyo, waliachiwa baada ya aliyewashitaki kuwasamehe. Wamekuwa wakihama maeneo kutokana na kupigwa na wananchi wa maeneo husika kwa uchafuzi wa mazingira.

Source:Habari leo
 
Yaani shetani mbaya sana, Mungu wetu ni wa utaratibu, huyo ni Mungu gani wanaye mtumikia asiye taka taratibu zifuatwe?

Nadhani serikali inapaswa kuwasaidia pia kwa kuwapeleka hospitali wapimwe akili! Nina wasi wasi huenda ni kundi fulani la wagonjwa wa akili walijikusanya na kujipachika utume haramu!
 
Shetani mbaya sana. Ikumbukwe kuwa shetani pia husema kwa sauti - na inawezekana anasema na kiongozi waliyemwamini -na sauti anazosikia wanasema ni Mungu. Hata vichaa wanasikia sauti - NI MUHIMU SERIKALI IINGILIE KATI - HIVI UNAWEZA KUMWONA MTU ANAJIUA HALAFU UMWACHE USIINGILIE? MKUU WA KITENGO HICHO CHA POLISI INABIDI AMKAMATE KIONGOZI WAO - AHOJIWE - ILI KUNUSURU MAISHA YA HAO WENGINE -
 
Kama watu wanakufa basi serikali ni lazima iingilie wasambaratishwe wafanye hata kazi za ukulima

Kuna maswali ninayojiuliza na natamani vyombo husika vijiulize maana majibu yote wanayo.

Moja, kwa sheria ya nguvu kazi ilifutwa? Sheria hiyo ilikuwa inaipa nguvu serikali kuwakamata waio na kazi na kuwapeleka vijijini. Kama bado ipo basi itumike

Mbili, sheria ya uzururaji pia inaweza kutumika kuwakamata na kuwafungulia mashitaka ya uzururaji ingawa kamanda wa polisi anadai hawajafanya jinai ya kukamatwa!

Tatu, vyombo vya misaada kibinadamu kama msalaba mwekundu viwasaidie kuwapatia chakula ili waweze kuishi.

Vinginevyo aibu nyingine inalinyemelea taifa pale watu hao watakapokufa kwa magonjwa na ukosefu wa chakula
 
Viongozi wetu ni porojo kwa kwenda mbele,au hili nalo linataka wafadhiri wachangie kuwatoa pale? Huyo aliyekufa watoto wake kamwachia nani kama si bibi kizee fulani huko kwao? kesho tunaanza kuchangia yatima wanaotokana na uzembe huu wa mchana kweupe.
 
Kandoro na jopo lake la ulinzi na usalama wa mkoa wapo likizo?
Hawa masalia ya wasabato wa TZ hawana utaratibu,Watu wasio na utaratibu ni kero kwa wakazi wengine kwa hiyo watafutiwe mapema tiba ya kuwatoa porini,aidha kwa hiari au lazima na kuwarudisha makwao.
 
Hawa wanasumbuliwa na njaa,serikali iwashughulikie kikamilifu kabla hawajasababisha matatizo.
 
Back
Top Bottom