Warioba: Wananchi wasizibwe midomo; Ni katika mjadala wa Muswada wa Katiba mpya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Warioba: Wananchi wasizibwe midomo; Ni katika mjadala wa Muswada wa Katiba mpya

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by nngu007, Apr 8, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Apr 8, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  *Ni katika mjadala wa Muswada wa Katiba mpya
  *Ataka kila kitu kijadiliwe kupata kwa uwazi
  *CCT yasema rais amepora madaraka ya wananchi


  PAMOJA na kuzuka kwa zogo kubwa lililosababisha mkutano wa utoaji maoni ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba kuvunjika, muswada huo umeendelea kukosolewa kwa kiasi kikubwa, huku serikali ikiambiwa isizibe watu midomo, kuhoji au kuzungumza baadhi ya masuala 'kwani hayo yanayozuiliwa kuhojiwa ndiyo katiba yenyewe'.

  Imeelezwa kuwa itakuwa si sahihi kuwazuia Watanzania kuhoji baadhi ya masuala ya msingi hata kama tayari yapo katika katiba ya sasa, kwani ni bora yakajadiliwa kwa kina ili yajulikane kama yanakidhi mahitaji ya watu kujitawala au la.

  Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na mmoja wa viongozi waandamizi wastaafu nchini, Jaji Joseph Warioba, wakati akitoa maoni yake katika kuboresha muswada wa sheria ya marekebisho ya katiba, akisisitiza kuwa masuala yaliyoko sehemu ya 3, kifungu cha 9(2), yajadiliwe bila zuio lolote.

  Kifungu hicho cha muswada, kinataja mambo 8 ambayo ni marufuku watu kuyahoji au kuyazungumzia wakati tume ya kukusanya maoni ya watu juu ya katiba mpya itakapokuwa ikitekeleza majukumu yake.

  Masuala hayo yanayoitwa kuwa ya 'heshima na utukufu', hivyo hayapaswi kuguswa kwa maslahi ya taifa, yameainishwa katika muswada kama ifuatavyo; Kuwepo kwa Muungano wa Tanzania na Zanzibar, kuwepo kwa mihimili mitatu ya dola (bunge, serikali na mahakama), nafasi ya urais, mshikamano wa kitaifa na amani ya nchi.

  Mengine ni; kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuwepo kwa mfumo wa uchaguzi wa kidemokrasia, haki za binadamu, dhana ya utu wa mtu, usawa mbele ya sheria na mfumo unaoweka utaratibu wa kufuata sheria, dhana ya Serikali ya Tanzania kutokuwa na dini na uhuru wa mahakama.

  "Haya mambo yanayoitwa matakatifu na hivyo hayaguswi ndiyo katiba yenyewe, ndiyo mambo ya muhimu katika katiba huwezi kuyaondoa watu wasiyazungumze...lazima watu wayazungumze hata kama tayari yako katika katiba ya sasa. Msiwazuie watu kusema, kama ni muungano tuwaruhusu waseme.

  "Watu wasikilizwe, wengine hawafurahishwi na muundo wa muungano ulivyo sasa, wengine watataka serikali moja, wengine serikali tatu, kama wakiweza kuwashawishi watu wengi wasikilizeni, hata kama watasema hatutaki kuwa na rais waache waseme, wanataka kuzungumzia Serikali ya Mapinduzi waacheni, huu ni wakati wa masuala haya kujadiliwa, maana ndiyo yanayozungumzwa sana sasa, ndiyo katiba haya.

  Jaji Warioba ambaye mbali ya kuwahi kuwa jaji wa mahakama kuu pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, alisema kuwa kifungu hicho kifanyiwe marekebisho kisiwazuie Watanzania kujadili mwafaka wa kitaifa juu ya mstakabali wa taifa lao.

  Jaji Warioba pia alionekana kushangazwa na vyama vya siasa na asasi zingine za kiraia kuzuiwa kuelimisha wananchi kwa kufanya kampeni wakati wa upigaji kura ya maoni ya 'ndiyo' au 'hapana' ili kupitisha sheria ya kuanza kutumika katiba mpya, badala yake shughuli hiyo kusimamiwa na tume ya uchaguzi.

  Huku akionya Watanzania kuacha ushabiki katika suala la utungaji wa katiba mpya, Jaji Warioba alisema "sasa mimi najiuliza hii tume itakwenda kufanya kampeni juu ya nini, tume iliyohusika katika mchakato wa katiba kweli inaweza kwenda kuwaambia wananchi wapige kura ya ndiyo au hapana. Waachwe watu wafanye kampeni.

  "Kama ni vyama vya siasa au watu waacheni wapige kampeni. Lakini natoa angalizo hili si jambo la ushabiki, huu ni mwafaka wa kitaifa. Tusifanye ushabiki, tutafute mantiki," alisema Jaji Warioba, huku akishangiliwa baada ya mwanzoni kuonja zomea zomea, alipoonekana akisifia baadhi ya vipengele katika muswada huo.

  "Pia hapa imeelezwa kuwa baada ya bunge la katiba kupitisha rasmu ya katiba, rais atatia saini, sasa kwa kawaida bunge la katiba likishapitisha kitu hakuna tena assent ya rais. Halafu baada ya rais kutia saini mnataka iende kwa wananchi, sasa sheria inapitishwa halafu inakwenda kwa wananchi, je, wakiikataa itakuwaje."

  Jaji Warioba alishauri kuchaguliwa kwa njia mojawapo kati ya bunge la katiba au mkutano jumuiko la kitaifa la katiba, huku pia akitoa angalizo juu ya kura ya maoni kuangalia namna ya kuratibu kura za pande mbili za muungano.

  Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye alikuwa mchangiaji wa tatu baada ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe, alisema kuwa ni vyema serikali ikaweka wazi juu ya jina la muswada huo, kwani wananchi wanazungumzia utungwaji wa katiba mpya, si marekebisho ya katiba.

  Alisema kuwa ni vyema muswada huo ukabeba dhana sahihi kwa ajili ya mabadiliko ya katiba kwani kinyume chake, kitasababisha hata vifungu vya muswada huo kuwa vibovu, huku akitoa angalizo kuwa si sahihi muswada huo kutoa mamlaka makubwa kwa rais, kwani mamlaka ya kuongoza nchi yanapaswa kutoka kwa wananchi.

  Alisema kuwa katiba inazaa taasisi zote, ikiwemo ya urais, hivyo Watanzania wanapaswa kuzungumzia masuala yote, bila kuzuiwa, huku akitaka baadhi ya maneno yaliyomo katika muswada huo yafafanuliwe vizuri ili yasitumike kuminya haki za Watanzania katika tafsiri zake.

  "Hiki kifungu cha 9(2) kinachosema mambo yasiyogusika, si kwamba Watanzania hawataki muungano, anayesema kuwa hataki muungano huyo ana matatizo yake, lakini Watanzania wanachotaka ni kuzungumzia aina gani ya muungano, wanahoji madaraka ya Tanganyika yako wapi, maana kumekuwa hakuna clarity katika suala la muungano.

  "Si kwamba hawataki rais awepo, wanahitaji kujadili urais wa namna gani, maana hapa kuna suala limechakachuliwa, tumechukua mfumo wa Marekani na Uingereza, sasa wanataka kujua tuko upande upi, tusianze kuweka limit (vizuizi) katika kujadili katiba, maana hapa tunatengeneza nchi yetu si nchi ya mtu mmoja.

  Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa kama mchakato wa uandikaji wa katiba mpya utaanza vibaya, nchi inaweza kuingia katika matatizo makubwa ya kisiasa, hivyo ni vyema mchakato huo ukapata uhalali wa kisiasa kutoka kwa wananchi, badala ya mamlaka makubwa kuachiwa rais.

  Akisisitiza suala la matumizi ya lugha ya Kiswahili na jina la muswada huo kubadilishwa, kutoka kusomeka marekebisho ya katiba, bali uandikwe Muswada wa Utungaji wa Katiba mpya, Prof. Lipumba alisema kuwa wananchi hawana imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia mchakato wa kura ya maoni kwani inaweza kuzichakachua.

  "Karibu kila kitu kinatokana na rais hapa, mapendekezo yatokane na wananchi, si rais. Tukianza hivyo itakuwa mwanzo mbovu, ili mchakato huu upate uhalali ni bora utokane na wananchi, msimpatie rais mzigo mkubwa kiasi kwamba mambo yakiharibika aonekane yeye ndiyo kaharibu. Katika kura ya maoni hatuna imani kabisa na tume ya uchaguzi.

  "Hatuna imani nayo kabisa maana tume hii mwaka jana katika uchaguzi mkuu ilituchakachua kweli kweli, sasa hawa hawa tena wanapewa kazi ya kusimamia kura za maoni, matokeo yatakuwa tayari yanajulikana, tunataka tume inayoaminiwa na watu. Kuwepo na nia thabiti, maana tukianza vibaya tutaingia katika matatizo makubwa ya kisiasa," alisema Prof. Lipumba.

  Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia alisema kuwa muswada huo haujatungwa kwa nia njema, akitaka umma upatiwe nafasi kubwa ya kuamua namna ya kujitawala, si mamlaka hayo kuwekwa mikononi mwa rais kwa kuamua mchakato mzima utakavyokwenda, huku naye akisisitiza suala la jina la muswada huo libadilishwe, usomeke kuwa ni 'katiba mpya'.

  "Hatutaki damu imwagike lakini serikali inaweza kuchochea vurugu, hatutaki katiba ya CCM, tunataka katiba ya wananchi, rais hapa anapewa madaraka yote. Pia lazima tuwe makini hapa maana tuna complex state maana tuna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tofauti na nchi kama Kenya ambao wana simple state, maana ni Jamhuri ya Kenya," alisema Bw. Mbatia.

  Zamu hiyo ya wawakilishi wa makundi mbalimbali iliendelea mpaka kufikia kwa Chama cha APP- Maendeleo na Chama cha Walemavu nchini, ambaye alitaka kundi hilo kuzingatiwa na kupewa umuhimu mkubwa unaostahili katika mchakato mzima mpaka kupatikana kwa katiba mpya, akitoa angalizo kuwa kwa sasa muswada umewaweka pembeni na kuwasahau.

  Ilipofika zamu ya mwakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Naibu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda, Bw. Tambwe Hizza, ambaye mara muda mfupi baada ya kuwasilisha hoja yake, yalianza kusikika makofi yasiyokoma yakipigwa na baadhi ya wahudhuriaji, ikiwa ni dalili ya kuzomea, huku yeye akipuuza kwa kusema "Mwenyekiti hayo tulishayazoea, yaache."

  Katika hoja yake ambayo ilikuwa ikikatishwa mara kwa mara kutokana na zomea zomea hiyo, hatimaye ilizua mtafaruku wa kambi mbili zinazopingana na kusababisha mkutano huo kuahirishwa kwa muda, Bw. Hizza alisema kuwa iwapo mchakato wa katiba mpya hautafuata sheria zilizopo na katiba iliyopo, nchi haitapata katiba mpya, badala yake itaambulia vurugu.

  Alisema kuwa si sahihi wananchi kutaka kumnyang'anya rais mamlaka yake katika mkutano kama huo wa utoaji maoni ya muswada, kwani mamlaka aliyonayo yamewekwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi, akisema kuwa ibara ya 98 ya katiba ya sasa, inaruhusu katiba kubadilishwa au kufutwa kabisa.

  Zomea zomea, zilizoanza kwa makofi yasiyo na mwisho, hatimaye kupigwa miguu chini na kibwagizo cha 'atokeeee atoke, aondokeeee aondoke, ilizidi na kumlazimisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Bi. Pindi Chana kuahirisha mkutano kwa ajili ya chakula, kisha uanze baadaye.

  Hata hivyo aliporudi baada ya kusimama kwa mkutano huo takribani saa mbili, Bi. Chana alisema haiwezekani kuendelea, bali mkutano huo wa kuchukua maoni utaendelea leo kwa watoaji kuwasilisha kwa maandishi na wengine wataruhusiwa kuzungumza.

  Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu alisema kuwa zomea zomea hiyo ni suala la aibu, kwani kila mtu anayo haki ya kutoa maoni yake na wengine wanapaswa kusikiliza hata kama hawataki au hawaungi mkono maoni hayo. Aliongeza kuwa hali hiyo ikiendelea muswada utapitishwa bungeni bila wananchi kutumia fursa hiyo ya kuujadili na kuuboresha.

  CCT yaonya rais kupora madaraka ya wananchi

  Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imeonya serikali kuwa kitendo cha rais kuteua tume kukusanya maoni ya katiba mpya ni kuwapokonya wananchi haki zao kwamba lengo la kazi hiyo haitafikiwa.

  Pia imesema serikali isithubutu kuharakisha suala hilo kulenga Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kuongeza kuwa iwapo watanzania hawatapata muda wa kutosha kutoa maoni yao kwa uhuru itakuwa haijakidhi matakwa ya watanzania.

  Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Makamu wa kwanza wa Mwenyekiti wa CCT, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dkt. Valentino Mokiwa, jumuiya hiyo imesema mwenye mamlaka ya kuteua tume hiyo ni bunge kwa niaba ya wananchi na si rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala.

  "Ipo hatari ya kukasimu mamlaka haya kwa Mheshimiwa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Tawala kuteua Tume ya kusimamia mchakato huu ikiwemo sekretarieti yake.

  "Ni sharti wananchi wenyewe wawezeshwe kutoa maoni yao moja kwa moja au kwa njia ya wawakilishi wa makundi yote ya kijamii, alisema Askofu Mokiwa katika taarifa hiyo na kuongeza.

  "Utaratibu huu unamfanya Rais awe wa mwanzo na mwisho (Alpha na Omega) na kuondoa ushiriki wazi wa wananchi katika kusimamia na kuamua mstakabali wa nchi yao. Ni vyema mamlaka haya yakakasimiwa na wawakilishi wa wananchi kupitia bunge na vyama vya siasa," alisema Askofu Mokiwa katika taarifa hiyo.

  Alisema Watanzania wanahitaji katiba mpya ili kukidhi matakwa yao ambayo hayajawai kufikiwa na marekebisho yaliyokuwa yakifanyika katika katiba ya sasa, chini ya mfumo huo bila kuleta faida.

  Katika barua hiyo iliyoelekezwa kwa Waziri wa Katiba na Sheria Bi. Celina Kombani yeye kichwa cha habari, tahadhari kutoka CCT juu ya muswada wa mapendekezo ya kutungwa kwa sheria ya mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2011, CCT iliikumbusha serikali kuwa wananchi ndio wenye maamuzi ya mwisho juu ya nchi yao na si rais.

  "Tunakuomba utumie weledi na hekima yako kuhakikisha kwamba rai yetu inapewa nafasi na umuhimu katika jambo hili, ili kuleta umoja, usawa, amani na utangamano pamoja na maendeleo ya nchi yetu yatakayotokana na katiba iliyoandaliwa na wananchi wenyewe," alisema.

  CCT ilisema katiba ijayo inatarajiwa kukidhi haja ya kizazi cha leo, kesho na kijacho na si kama marekebisho yaliyopita ambayo hayakukidhi haja ya Watanzania.

  "Muswada unafifisha na kudhoofisha ari na matarajio yao, mabadiliko yamekuwa yakifanyika kila mara lakini bado lengo la kupata katiba mpya halijakidhiwa," alisema Askofu Dkt. Mokiwa.
   
Loading...