Warioba na sheria zinazobagua watu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Warioba na sheria zinazobagua watu

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by BAK, Aug 27, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Aug 27, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,754
  Likes Received: 82,730
  Trophy Points: 280
  Warioba na sheria zinazobagua watu

  Mwandishi Wetu Agosti 27, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema matukio ya kifisadi ya hivi karibuni yamezua hisia kwamba Tanzania inaongozwa kwa sheria mbili; za walala hoi na vigogo.

  Akifungua warsha kuhusu Uimarishaji wa Uwajibikaji wa Umma katika nchi za Afrika Mashariki iliyofanyika Arusha wiki iliyopita, Jaji Warioba, akimkariri rafiki yake mmoja, alisema kwamba mtu wa kawaida akifanya kosa, polisi haraka huchangamka kumchunguza na kumfikisha mahakamani.

  Lakini, alisema kwa mujibu wa rafiki yake huyo, kigogo anapofanya kosa, itaundwa tume kuchunguza kosa lake na ripoti ya uchunguzi huo haitawezesha mtuhumiwa huyo kigogo kufikishwa mahakamani.

  Akisimulia yaliyojitokeza kati yake na rafiki yake huyo alisema: “Hivi karibuni nilibishana na rafiki yangu mmoja mwanaharakati. Aling’ang’ania kusema kwamba katika nchi hii kuna sheria mbili. Kuna sheria kwa ajili ya watu wa kawaida na sheria nyingine kwa ajili ya wakubwa.

  “Kwa maoni yake, mtu wa kawaida anapofanya kosa, polisi watachunguza na kumfikisha mahakamani. Lakini ofisa wa ngazi ya juu akifanya kosa, tume itaundwa na ripoti ya tume hiyo kwa kawaida haisababishi ofisa huyo kupelekwa mahakamani,” alisema.

  Jaji Warioba alisema ya kuwa rafiki yake aliyesema kuwa maoni yake hayo ndiyo mtizamo wa kundi kubwa la Watanzania wa kawaida, anaamini kuwa uongozi hufanyia usanii mwingi ripoti za tume hizo kiasi kwamba hakuna kinachofanyika ambacho kinapunguza maumivu ya wananchi. Alisisitiza kuwa ripoti hizo na usanii wa uongozi unaweza kufananishwa na filamu yenye makali tele lakini bado inabaki kuwa ya burudani.

  “Kwa sasa Tanzania kuna usanii mwingi kuhusu ufisadi,” alisema akizungumzia sakata la ufisadi wa kampuni hewa ya Richmond lililosababisha Waziri Mkuu na mawaziri wawili kujiuzulu na kuundwa kwa tume ya kuchunguza wizi uliotokea kwenye Benki Kuu ya Tanzania katika Akaunti ya Madeni ya Nje.

  Alisema nyingi ya sakata zilizojitokeza ambazo zimesababisha kuundwa kwa tume, zinahofiwa kuhusiana na Uchaguzi Mkuu na kwa sababu hiyo wananchi wa kawaida hawana imani na uongozi katika kupiga vita ufisadi.

  “Ingawa takrima imeelezwa na Mahakama Kuu kuwa ni kinyume cha sheria, Serikali haijabadilisha sheria. Katika hotuba yake bungeni Desemba 2005, Rais alisema takrima ni tatizo na kuahidi kulishughulikia, sasa ni miaka mitatu kuna ukimya na inaonekana tutafika uchaguzi wa 2010 bado kukiwapo na takrima,” alisema.

  Jaji Warioba ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Rushwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1995, alisema ya kuwa kuwapo kwa rushwa katika uongozi wa juu kumesababisha kukithiri kwa uozo huo katika ngazi ya chini.

  “Maofisa wa ngazi ya chini hudai rushwa kwa sababu wanajua kwamba uongozi wa juu hauna uadilifu wa kukemea jambo hilo.

  Jaji Warioba alisema kuna umuhimu wa kupiga vita aina zote za rushwa badala ya hali iliyoko sasa ya kutolea macho rushwa kubwa kubwa tu kwa vile kuna shikinizo la kufanya hivyo kutoka kwa wafadhili.

  Akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi, Jaji Warioba alisema kuwa Rushwa ni jinamizi katika Afrika Mashariki. “Juhudi zinazofanywa sasa hazifanyi kazi vizuri kulidhibiti hivyo kunahitajika mbinu mpya,” alisema.
   
Loading...