Waraka wa Elimu namba 06 wa Mwaka 2022 kuhusu Usimamizi wa Maadili kwa wanafunzi wa Shule za Awali, Msingi na Sekondari

Sildenafil Citrate

JF-Expert Member
Jan 29, 2021
572
2,548
Mataifa mbalimbali duniani yamekuwa yakifanya jitihada za kuhakikisha kwamba kila Taifa linalinda na kukuza utamaduni na maadili yake kwa lengo la kudumisha amani, mshikamano, umoja na maendeleo katika nchi husika.

Hata hivyo, kutokana na maendeleo makubwa ya Sayansi na Teknolojia yaliyopelekea kuwepo kwa utandawazi na haja ya kuwa na Raia wa Dunia (Global Citizens), jitihada zaidi zinahitajika ili kuhakikisha kuwa utandawazi hausababishi mmomonyoko wa utamaduni na maadili yetu ambayo ni nguzo muhimu katika kulinda utaifa wetu.

Ni muhimu kutambua kwamba, muktadha wa malezi ya watoto katika zama za utandawazi ni tofauti na muktadha wa malezi ya watoto kabla ya utandawazi. Katika muktadha wa utandawazi, watoto na jamii kwa ujumla wanaona, kusoma, kusikia, kushika, kunusa, kuhisi na kujifunza mambo mengi kutoka vyanzo mbalimbali vya habari ambavyo kimsingi vinafanya kazi sawa na ile ya mwalimu na mzazi/mlezi.

Mifano michache ya vyanzo vya taarifa vinavyofanya kazi ya kufundisha na kutoa malezi katika mfumo rasmi au usio rasmi ni kama ifuatavyo-
  1. Video (nyumbani, taasisi na vibanda-umiza);
  2. Kompyuta (michezo ya kompyuta, face book, twitter, Instagram, barua pepe, na mtandao);
  3. Simu;
  4. Redio;
  5. Katuni, vinyago na vikaragosi;
  6. Mabango mbalimbali;
  7. Vitabu, magazeti, majarida na vipeperushi:
  8. Mavazi, tabia na mitindo mbalimbali ya maisha ya watu kutoka ndani na nje ya nchi:
  9. Watu maarufu (Wasanii na Wanamichezo);
  10. Makundirika; na
  11. Kumbi za starehe.
Vyanzo hivyo vya taarifa na vinginevyo, vinahitaji umakini na utayari wa jamii katika kuweka mazingira ambayo yatahakikisha kuwa vyanzo husika vya taarifa havisababishi athari hasi kwa tabia na maadili ya watoto wetu na jamii kwa ujumla.

Vinginevyo, upo uwezekano mkubwa wa mmomonyoko wa maadili na utamaduni wetu katika jamii zetu.

Aidha, katika muktadha huo wa utandawazi, imebainika kuwa kumekuwa na jitihada kubwa kutoka kwa wadau wa elimu nchini kusisitiza matokeo bora kitaaluma na kuacha au kuweka jitihada ndogo katika ujenzi wa maadili na tabia za wanafunzi. Hali hii, kwa kiasi kikubwa, inaweza kutoa mwanya kwa watoto wetu kujenga tabia zisizokubalika na kusababisha mmomonyoko wa tamaduni na maadili yetu.

Kwa sababu hiyo, iko haja ya kufanya jitihada za makusudi ili kuhakikisha kuwa wadau wa elimu kote nchini wanasisitiza matokeo bora kitaaluma kwa upande mmoja na kimaadili kwa upande mwingine.

Maadili ni jumla ya mambo yote mazuri aliyonayo mtoto, mwanafunzi au mtu mzima yanayomfanya kukubalika katika jamii yake. Maadili humfanya mtu kutambua mambo mema na mabaya katika kufanya maamuzi au kutenda ili kutunza amani na umoja katika jamii husika maadili. Taaluma bila maadili haiwezi kuwa na matokeo chanya katika jamii zetu.

Tafiti mbalimbali kuhusu makuzi na maendeleo ya mtoto zimeonesha kwamba, kwa kiwango kikubwa, tabia na maadili aliyonayo mtu mzima ni matokeo ya malezi aliyopata wakati wa miaka minane ya awali katika maisha yake. Katika kipindi hicho, mtoto hujenga misingi imara ya tabia na mielekeo inayodumu katika maisha yake yote.

Kwa kutambua ukweli huo, ni muhimu walimu na wazazi/walezi kwa pamoja wakaweka kipaumbele katika kutoa malezi bora kwa watoto wadogo.

Kwa ujumla, Shule za Awali na Msingi nchini zinatoa fursa kwa Taifa letu kujenga misingi imara ya tabia na maadili yanayokubalika katika jamii zetu na hivyo kuleta ustawi na maendeleo endelevu.

Ili kulinda na kujenga maadili ya watoto wetu, Waraka huu unaelekeza yafuatayo:
  1. Shule zote zianzishe au kuimarisha Kamati za Maadili/Nidhamu shuleni kwa usimamizi wa karibu wa Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule ili zifanye kazi zake za ujenzi wa tabia na maadili mema kwa wanafunzi kwa ufanisi;
  2. Maafisa Elimu Kata washirikiane na viongozi wa vijiji/mitaa/vitongoji kuhakikisha kwamba mazingira wanamoishi na kukulia watoto hayana vyanzo vya taarifa zinazoharibu maadili ya wanafunzi. Mfano wa vyanzo hivyo ni uwepo wa vibanda-umiza vinavyoruhusu watoto kuingia na kutazama au kusikiliza mambo yaliyo kinyume na maadili yetu
  3. Kila shule iimarishe huduma za Ushauri na Unasihi na kuhakikisha kwamba Walimu wa Malezi na Unasihi wanafanva vikao na wanafunzi ili kuiadili
  4. Kila shule iwe na Sanduku la Maoni ili wanafunzi watoe taarifa na maoni yatakayowezesha kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya ujenzi wa tabia njema na maadili miongoni mwa wanafunzi;
  5. Kuhakikisha kwamba Klabu za Masomo hasa zile za masomo yenye maudhui ya uraia na maadili kwa shule za msingi na sekondari zinajadili masuala mtambuka hususan maadili kama ajenda ya kudumu;
  6. Kuanzisha au kuboresha utendaji wa SKAUTI kama chombo muhimu katika ujenzi wa maadili miongoni mwa wanafunzi;
  7. Vikao vyote vya walimu, wazazi/walezi na Kamati/Bodi za Shule zinajadili suala changamoto mbalimbali kuhusu nidhamu a maadili ya wanafunzi;
  8. Wathibiti Ubora wa Shule wazingatie kipengele cha namna shule inavyoshughulikia maadili ya wanafunzi katika kazi zao za kuthibiti ubora;
  9. Shule zote ziongeze umakini katika kuandaa taarifa za maendeleo ya wanafunzi kwa kuzingatia suala la maadili ya mwanafunzi husika;
  10. Kuimarisha Mabaraza na Madawati ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto ili kuhakikisha kwamba suala la maadili linajadiliwa katika vikao vyote kama ajenda ya kudumu; na
  11. Shule zote za Awali, Msingi na Sekondari ziweke msisitizo katika ufundishaji wa Somo la Dini ili kuweka msingi imara wa maadili kwa wanafunzi.

Waraka huu unaanza kutumika rasmi tarehe 10 Oktoba, 2022.
 

Attachments

  • WARAKA WA ELIMU NA_06 WA MWAKA 2022.pdf
    1.3 MB · Views: 119
Hii ni kwa walimu hawahawa walioelemewa na idadi ya mwanafunzi; na maisha yamewapiga 3 - 0?
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom