Waraka wa Bernard Membe kwa Askofu Mwamakula: Sitishiki, sitakaa kimya na kamwe sitaabudu mtu wala miungu wengine

RWANDES

Senior Member
Joined
Jun 12, 2019
Messages
161
Points
250

RWANDES

Senior Member
Joined Jun 12, 2019
161 250
“Niguse ninuke”

"Baba Askofu Emmaus Mwamakula!

Tumsifu Yesu Kristo!

Napenda nikushukuru sana kwa ujumbe mzito na wenye tija katika Taifa. Nikiri kwamba nami nimekuwa nakufuatilia sana kwa maoni na ushauri mbalimbali ambao umekuwa ukiutoa kwenye mitandao. Endelea kufanya hivyo! Nikiri pia kuwa nimekuwa nafuatiliwa, nazushiwa shutuma za hatari kama vile za uhaini, usaliti, ufisadi, uhujumu, kufanya kampeni ya Urais nk.

Nikuhakikishie hakuna hata chembe ya ukweli kuhusu yote hayo na ndiyo maana huoni na hutaona hatua za kisheria zikichukuliwa dhidi yangu. Labda wanichukulie hatua zingine! Nimepata vitisho mbalimbali kutoka kwenye Chama changu, makundi mbalimbali ya wachawi na Serikali vya kunifukuza, kuniloga, kunitupa Gerezani kana kwamba mimi ni mhalifu. Baba Askofu, kwa kuwa moyo wangu ni safi, na kwa kuwa sijatenda kosa lolote, SITISHIKI , SITAKAA KIMYA na KAMWE SITAABUDU MTU WALA MIUNGU WENGINE.

Ninakushukuru sana kwa ushauri na maneno ya busara uliyonipatia. Tusipotokea wachache wa kuyasema na kuyakemea mabaya Baba Askofu, nchi hii itaingia kwenye matatizo makubwa zaidi ya haya tunayoyaona! Serikali ya Awamu ya tano imepewa ridhaa ya Uongozi na sisi wenyewe. Lakini leo sisi tunaonekana ni maadui wa Serikali na hakuna jema lililofanywa na awamu zilizopita. Ninawasikitikia washauri wanafiki na waoga wanaokaa kimya au kumshauri vibaya Rais wetu. Wanafiki wanaomlinganisha Rais wetu na Yesu na wanaomwomba Mungu amshukuru Rais wetu kwa yote anayoyafanya. Pamoja na makosa yote yaliyofanywa na Awamu zilizopita, Serikali na Viongozi hao walijitahidi kuheshimu Katiba, Uhuru, Sheria na Haki za binadamu. Huo ndiyo msingi wa Uongozi Bora Duniani.

Baba Askofu, usichoke kutushauri na kutupa moyo wa kuyatenda yale ambayo yatampendeza Mungu. Unifikishie salaam zangu kwa Maaskofu wote! Ubarikiwe sana Baba Askofu Mkuu Emmaus Bandikile Mwamakula na tuzidi kuombeana.

Bernard K. Membe. Mstaafu!"

NB: Waraka huo hapo juu kutoka kwa Mheshimiwa Membe (pichani), umenifikia leo kupitia nami nimeona niuweke hapa hasa ikizingatiwa kuwa ujumbe wangu wa awali kwake niliuweka hapa pia.

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani (World Fellowship of Moravian Revival Churches)

-------

****UJUMBE WA ASKOFU MWAMAKULA ULIOJIBIWA NA BERNARD MEMBE****

UJUMBE MAHSUSI KWA MHESHIMIWA BERNARD MEMBE.

Mheshimiwa Bernard Membe!

Pokea salaam za upendo kutoka kwangu mimi niliye mdogo sana miongoni mwa Maaskofu wa Kanisa la Mungu hapa duniani nisimamaye katika zamu yangu sasa! Nimekuwa nikifuatilia kwa makini na kusikia mengi juu yako katika siku za hivi karibuni. Ninatambua kuwa wewe ni mwanasiasa na siasa ni uwanja wa hoja.

Hata hivyo, kwa mazingira yalivyo tumeshuhudia kauli nyingi kukuzunguka wewe ambazo wakati mwingine zinatia hofu na mashaka. Kauli zinazoashiria kuwa siasa za Tanzania zimeanza kuonyesha dalili za watu kuanza kukosa kuvumiliana hasa pale watu wengine wanapoonyesha muono tofauti wa mambo.

Ninapenda nikuhakikishie kuwa pamoja na ukimya wao, Maaskofu walio wengi katika Nchi hii wanafuatilia kwa karibu sana mambo yanayohusu nchi hii ambayo Mungu amewaweka kuwa watumishi na mawakili wa siri zake. Pengine utatiwa moyo kusikia kuwa mimi pamoja na Maaskofu, Wachungaji, na watu wengine wengi usiowajua tunakuombea na kulitaja jina lako mbele za Mungu wetu.

Tunapenda ifahamike kuwa kukuombea kwetu hakutufanyi sisi kuwa lazima tukubaliane na muono wako wa mambo kuhusiana na siasa za Nchi hii, la hasha! Bali tunakuombea kutokana na ukweli kuwa kwa mazingira yaliyopo sasa baadhi yetu tunahisi kuwa unaweza kujikuta unaishi katika maisha ya hofu na wasiwasi mkubwa.

Tunamuomba Mungu ili akupe utulivu moyoni na pia akupe ulinzi dhidi ya watu ambao wanaweza kutaka kukudhuru kutokana na wao kutokupenda misimamo na mitazamo yako. Kwa kuwa na washindani wako na wao pia watausoma ujumbe huu, tunawasihi sana wasije wakaingia katika mtego wa kugusa uhai wako. Lakini pia, na wewe uepuke kuingia katika mtego wa kutaka kuwadhuru washindani wako. Mungu wetu atahusika na mtu ye yote anayejipanga kumwaga damu ya mtu mwingine iwe yeye mwenyewe au kuwatumia watu wengine.

Tunapenda wanasiasa wote wafahamu kuwa Mungu anapotoa kibali kwa mtu, kibari hicho hakiwezi kuondolewa na mtu au mamlaka ye yote ya kidunia. Kupambana na mtu aliyepata kibali kwa Mungu ni sawa na kupambana na Mungu mwenyewe. Tunapenda ifahamike kuwa kama wapo watu ambao Mungu amewapa kibali, wewe ukipambana nao utakuwa unajisumbua bure. Lakini pia, kama wewe utakuwa umepata kibali kutoka kwa Mungu, basi wale watakaoinuka kupambana na wewe na wao watakuwa wanafukuza upepo!

Tunakemea mambo yote ya kutishana na kunyamazishana na hata kutaka kupotezana miongoni mwa wanasiasa iwe ni katika Vyama vya Upinzani au ndani ya Chama Tawala. Kiongozi ye yote atakayeasisi au kushiriki katika vikao au mikakati ya kutaka kumuua mtu mwingine kwa sababu za kisiasa na mambo mengine nje ya mfumo na mchakato wa ki-Mahakama atakuwa anajitoa mwenyewe katika kibari cha Mungu kwa kuwa damu ya mtu haiwezi kumwagika bure pasipo kupiga kelele!

Ninaomba ukipata nafasi uweze kutafakari kwa kina Zaburi 35.

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula -
Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani
 

Oumuamua

JF-Expert Member
Joined
Dec 26, 2018
Messages
293
Points
1,000

Oumuamua

JF-Expert Member
Joined Dec 26, 2018
293 1,000
"Tusipotokea wachache wa kuyasema na kuyakemea mabaya Baba Askofu, nchi hii itaingia kwenye matatizo makubwa zaidi ya haya tunayoyaona!"

"Lakini leo sisi tunaonekana ni maadui wa Serikali na hakuna jema lililofanywa na awamu zilizopita"

"Pamoja na makosa yote yaliyofanywa na Awamu zilizopita, Serikali na Viongozi hao walijitahidi kuheshimu Katiba, Uhuru, Sheria na Haki za binadamu. Huo ndiyo msingi wa Uongozi Bora Duniani".

Kama haya kweli ni maneno ya Membe, basi amemaliza! Need we say more?
 

Bams

JF-Expert Member
Joined
Oct 19, 2010
Messages
6,951
Points
2,000

Bams

JF-Expert Member
Joined Oct 19, 2010
6,951 2,000
Kwanza nimsifu Askofu kwa kusimama kwenye ukweli kwa ujasiri. Watu wa Mungu hawastahili kuwa waoga maana aliyetuumba hakutuumba hivyo. Alitupatia roho ya ujasiri ipendayo kweli. Ibilisi ametutia uoga na unafiki sisi na viongozi wetu wa dini, serikali na makundi mbalimbali.

Namshukuru Mungu pia kwa kumjalia Bernard roho ya ujasiri. Ujasiri wa kuunena ukweli. Kwa hali ya sasa ambapo wengi wamepigwa ganzi na sindano ya uoga, inahitaji msaada wa Mungu kuunena ukweli. Wengi tumebakia kuwa majasiri wa mtandaoni. Hata huku pia tumeyaficha majina yetu kwa uoga. Naomba siku moja Roho wa Mungu atujilie, sote tuamue kuyaweka majina yetu dhahiri, ikiwezekana na namba zetu na mahali tuishipo. Ili kama kuna shetani aliyewahi kuushinda ukweli atukamate wote tunaounena ukweli (ukiacha wanaotusi).

Kwa upande mwingine hekima iwaingie watawala ili watambue hawabebi chochote katika miili yao zaidi ya kile Mungu aliwaumba nacho:

1) hawatuzidi wengine katika ubinadamu

2) hawakupewa akili kutuzidi sisi sote

3) hawakupewa roho nyingi zaidi ya wengine

4) wamepewa madaraka yanayoweza kuwafanya wabarikiwe au walaanike kutokana na kiburi cha mamlaka au unyenyekevu utokanao na hekima ya Mungu

Wakipata hekima, watayafanya haya:

1) watakuwa watumishi wa vitendo badala ya kuwa watawala wanafiki wanaonena tofauti na wanayotenda

2) watakubali hekima za wazee wetu kuwa ukubwa ni jalala, watayapokea mema na mabaya dhidi yao lakini wao watatenda mema hata dhidi ya wale wawaneneao mabaya kwa husda

3) watatmbua kuwa hawakuletwa duniani wala hawakupewa mamlaka kwaajili ya kutesa, kuteka, kupoteza watu au kuua bali walistahili kusimama katika hekima ya utawala yaani kuwa kama jabali lenye kutoa kivuli kwenye jangwa (kukiwa na joto kali la jua, watu wajikinge nalo), na pia wawe kama kijito kitiririshacho maji katika ardhi kame (watu wakifuate hicho kijito ili kupata tulizo la kiu)

4) hawatahangaika na kisasi wala kuwakomoa watu kwa kuwatengenezea kesi za utakatishaji fedha au uhujumu uchumi pasipo haki wala hawatapora mali za watu kwa sababu tu wana mamlaka

5) hawatawakomoa wapinzani wao kwa kuwafilisi bali watakuwa wanyenyekevu na wenye hamu kuwasikiliza wapinzani wao ili wayasikie mapungufu yao

6) hawatafanya teuzi za upendeleo wala utumbuaji wa kisasi bali kila jambo kwa kweli ya Mungu

7) Hawatajificha katika jina la Mungu katika kuuficha uovu wao bali wataenda mbele za Mungu kumwomba awajalie roho ya kutenda haki, kuondoa chuki na upendeleo, kuyaishi wanayoyatamka na kuongoza kwa kweli yake na wala siyo kwa hadaa.

8) hawatatenda kwaajili ya kutafuta sifa, wala hawatataka kuwatweza watawala na watendaji waliotangulia bali kwa unyenyekevu watasawazisha ambapo hapakuwa sawasawa maana na wao ya kwao yatasawazishwa na wengine

9) watatamani kusikia mapungufu yao kuliko kusifiwa kwa unafiki

10) watatambua kuwa ukiwa mtawala, wengi wanafiki watakuimbia sifa usiku na mchana, lakini ukiwa na hekima utawasikiliza zaidi wenye mawazo tofauti kuliko wanaokusifia tu.
 

Kitwa-Mulomoni

JF-Expert Member
Joined
Oct 25, 2016
Messages
858
Points
1,000

Kitwa-Mulomoni

JF-Expert Member
Joined Oct 25, 2016
858 1,000
Aisee maneno ya waraka huu yanamuhitaji mtuu jasiri kuyasema hasa wakati huu na aliyeyasema ni jasiri
Mtenda hutendwa! Membe ana hali ngumu mpaka anapiga magoti kana kwamba ni mtakatifu. Si aongee na wanao mpa kashi kashi sisi personal matters zinatuhusu nini!
 

Bams

JF-Expert Member
Joined
Oct 19, 2010
Messages
6,951
Points
2,000

Bams

JF-Expert Member
Joined Oct 19, 2010
6,951 2,000
Upuuzi na uomgo , eti kampeni na ufisadi.
Hivi huyu siyo yule wa mabilion ya Gaddafi, siyo yule wa clip za kupindua serikali?
Shetani hana tone la aibu.
Hayo mabilioni ya Libya, una kielelezo chochote? Naamini siyo kweli.

Kama ingekuwa ni kweli, yaani kwa utawala huu na jinsi unavyomchukia Membe, angekuwa wa kwanza kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Kwa sababu hakuna lolote mpaka sasa dhidi yake, itakuwa ni kweli kuwa anasingiziwa.
 

uvugizi

JF-Expert Member
Joined
Oct 13, 2012
Messages
1,153
Points
1,500

uvugizi

JF-Expert Member
Joined Oct 13, 2012
1,153 1,500
baba askofu Emmaus Mwamakula! .....usiingie kunako mtego ..... Mtu akishasema nimetokewa na Yesu, usimuamini haraka haraka utakuwa umenasa kwenye mtego wa ibilisi, maana jicho litamuangalia yeye kwa kila kitu hata akibolonga bolonga mambo, tayari mawazo ni ametokewa na Yesu kwa hiyo kila kitu kiko sawa...........
 

Bams

JF-Expert Member
Joined
Oct 19, 2010
Messages
6,951
Points
2,000

Bams

JF-Expert Member
Joined Oct 19, 2010
6,951 2,000
KAMWE SITAABUDU MTU WALA MIUNGU WENGINE.

***akimaanisha kamwe hataenda jumba jeupe kupiga magoti kuomba msamaha**
Hiyo ni kauli thabiti. Ni sawa na ile ya shahidi wa uganda aliyeifia dini ya Kikristo. Alipewa vitisho, aliona wenzake wakiuawa, na yeye akielekea kwenye njia ya kifo lakini bado kwa ujasiri mkubwa alinena:

INANIPASA KUMHESHIMU MUNGU ZAIDI KULIKO MWANADAMU

Kama raia wema kwa Taifa letu na watu tunaomtii Mungu, pale viongozi wetu wanapokengeuka na kutoheshimu katiba yetu, SISI TUNASTAHILI KUSIMAMA KATIKA UKWELI WA KUHESHIMU NA KULINDA KATIBA. Yatupasa kunena kwa ujasiri:

TUNASTAHILI KUILINDA, KUHESHIMU NA KUIFUATA KATIBA kuliko kauli ya mtawala iendayo kinyume na katiba yetu. Na kauli yetu iwe thabiti hasa, na mtawala mwenye kutenda kinyume na katiba aweze kufahamu kuwa hana nafasi ya kuongoza Taifa letu.
 

Forum statistics

Threads 1,353,165
Members 518,272
Posts 33,073,148
Top