Waraka kwa Rais Samia Suluhu Hassan: Kilio cha wafanyakazi kwenye hifadhi ya jamii

SUBE2021

JF-Expert Member
Aug 5, 2011
348
101

Waraka kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kwanza kabisa kwa vile ni mara yangu ya kwanza kuandiaka toka Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Ushike hatamu za Uongozi wa nchi yetu, nachukua nafasi hii kukupongeza sit u kwa kuwa Rais wa nchi yetu lakini kwa namna ambavyo umeanza vizuri sana kwa kuogeza kiwango cha Furaha Kwetu. Ninakusalimia kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kukuahidi kwamba kazi inaendelea na ninakuombea Mungu akujalie ili utufikishe mbali na hasa kwa maono uliyo nayo Juu ya Taifa letu.

Hoja inayonifanya kuandika leo na kutoa maoni ni juu ya Hifadhi ya Jamii kwa wafanyakazi wa Tanzania. Kwanza kabisa kuna mashaka ya namna gani dhana ya hifadhi ya Jamii inaeleweka kwa wadau wote na hasa wafanyakazi ambao ni wawezeshaji na wachangiaji kwani hata malengo ambayo yamefinywa na kuwekwa kwenye sharia hayatongani na wafanyakazi bali watunga sharia na sera. Nasema hivi kwa sababu ni kawaida kukuta mstaafu mchangiaji analalamika kwa dhiki na karaha anazopitia ili kuweza kuyafikia /kuyapata mafao yake ambayo kimsingi yeye ni mchangiaji akishirikiana na mwajiri, au mwajiri peke yake anapokubali kubeba mzigo wote kutokana na manufaa anayoyapata kutoa kwa mwajiriwa. Ukiyatathimini madhira haya huoni kama yanaendana na dhana inayotambulika ya kidunia ambayo kwa tafsri isiyo rasmi imesema; Hifadhi ya Jamii ni ni Ulinzi au Uhifadhi ambao Jamii humpatia mtu au watu ili waweze kumudu gharama za afya, kulinda kipato wakati mtumishi amekosa ajira au amefikia umri wa kustaafu, wakati wa ugonjwa, madhira yasababishayo ulemavu, ajali mahala pa kazi, mtumishi kujifungua na wakati mtumishi amefariki dunia.

Tunatambua nchi yetu inasera ya hifadhi ya Jamii na kumekuwa na sharia mbalimbali zilizotungwa kwa nyakati tofauti kusimamia jambo hili ambalo limepitia historia kubwa. Tumekuwa na mifuko mingi ya hifadhi ya Jamii ambayo ilianzishwa kujibu matakwa ya sekta mbalimbali ambazo kuna kipindi zililazimika pia kuwekewa Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii. Baadaye serikali baada ya kupokea ushauri na kuangalia gharama za uendeshaji iliamua kuunganisha mifuko na kutengeneza miwili tu yaani ule wa watumishi wa serikali na ule wa watumishi wa sekta binafsi pamoja na kufuta mamlaka ya uthibiti wa hifadhi ya Jamii. Jambo hili kwa maelekezo hata kwa kuangalia lilikuwa kabisa na nia njema ya kupunguza gharama za uendeshaji ili kuondoa mzigo huo ambao ulikuwa unatumia rasilimali fedha kubwa ya mifuko hii kugharamia uendeshaji. Kama mfanyakazi nadhani hata watumishi wengine wenzangu jambo hili tunaliafiki kwani lililenga kulinda na kuokoa fedha zetu ambazo tunachangia kwenye mifuko.

Aidha Wakati wa Mchakato wa kuyafanya Mabadiliko haya ya kisheria kulikuwa na ushirikiswaji wa kiasi kwa wadau. Nasema wa kiasi kwa sababu ukienda kwa wadau wenyewe kulikuwa na uelewa hafifu juu ya Mabadiliko yenyewe na watu kutofahamu nini kinaendelea. Japokuwa inaaminika hakuna mwanya unaruhusu mtu kutojua sharia lakini kuna changamoto ya mfumo wa kupata maoni ya wadau wakati wa uaandaji wa sharia mablimbali zikiwemo hizi za hifadhi ya Jamii pamoja na muda unaotolewa na ikizingatiwa hata mijadali ya wawakilishi wetu kwa siku za Karibuni haionekani au kusikilizwa Mubashara na hivyo kuchukua muda wa walengwa kujua au kufuatilia mambo yanayoendelea.

Mabadiliko haya ndiyo yalizaa mwana maarufu aitwaye KIKOKOTOO ambacho kilitokana na Mabadiliko ya sharia na kanuni za Hifadhi ya Jamii. Kwanamna kilivyowekwa kikokotoo kipya hakijibu dhana halisi ya maana ya hifadhi ya Jamii. Pamoja na kwamba mchakato wenyewe kama nilivyosema ulikuwa ni shirikishi kwa kiasi lakini mara baada ya kuanza kutumika kwa kikokotoo kipya Julai 2019, kulizuka taharuki kubwa hadi kupelekea Mheshimiwa rais wa wakati huo hayati John Joseph Pombe Magufuli kuamua kukipeleka likizo. Ni kikokotoo ambacho kiliacha hisia za kunyonywa kwa wafanyakazi wa kundi Fulani hasa baada ya kulinganishwa na namna malipo yalivyokuwa yanapatikana kwa Kikokotoo cha Zamani. Aidha ukiipitia sharia ya PSSSF Namba 2 ya 2018, unagundua imetenganisha makundi mawili; moja ni kundi la watu waliolindwa kisheria namna ya kukokotoa mafao yao huku kundi la pili likiwa lile ambalo KIKOKOTOO chao kinatokana na Kanuni za Waziri mwenye dhamana

Mheshimiwa rais, tunategemea tunapoelekea sherehe za Mei Mosi mwaka huu, utusaidie kuliangalia jambo hili kwa undani wake. Tuangalie Kikokotoo na namna ya kutengeneza mafao yote yaliyoainishwa ili yatoe faraja hata kwa mtumishi anayefanya kazi kuendelea kufanya kwa bidii. Ifikie pahala tuone kama ilivyo kwa kundi la watumishi ambao wametajwa kwenye Kifungu cha 40 cha sharia ya PSSSF, basi iwe hivyo kwa mwalimu, kwa nesi, kwa Llinzi, kwa Daktari, Mtunza kumbukumbu na wengine wote na ikiwezekana itamkwe kwenye sharia mama badala ya kutegemea kanuni.

Upande wa pili ulio na shida ni juu ya kuondolewa kwa FAO la Kujito kwenye mifuko kwa wachangiaji wenye mikataba ya muda mfupi. Hapa napo kuna mkanganyiko mkubwa sana. Kabla ya Kuunganishwa kwa mifuko, tulikuwa nayo mifuko mingi ya hifadhi ya Jamii ambayo mingi ilikuwa na fao la kujitoa kwenye sharia zake na wanachama walikuwa wanajiunga kwa kuvutiwa na hili. Mtumishi anafanya kazi miaka miwili na ikiisha na mkataba unaisha alikuwa na uwezo wa kwenda kuchukua fedha ake alizochangia ili zimsaidie kuishi, kujishughulisha kwa kujiajiri na pengine kutengeneza ajira kwa wengine na kulipa kodi. Ghafla sharia zilizokuja zikafuta jambo hili na kutaka mtu akikosa ajira asubiri mpaka afikie umri wa kustaafu na katikati limewekwa FAO la kukosa Ajira ambalo ni Kichomi na Mkanganyiko Mkubwa. Linalipwa kwa miezi kadhaa na ni asilimia kidogo ambayo haina suluhisho linaloeleweka kwa mfanyakazi huyu aliyemaliza mkataba wa mradi wake.

Mheshimiwa Rais, Pia ikumbukwe kuwa sambamba na hili, watu wengi walikuwa wameshajiunga kwenye mifuko ya hifadhi ya Jamii ambayo inaruhusu Fao la Kujitoa kabla ya kutungwa kwa sharia mpya. Matarajio na mateemeo yetu kisheria ilipaswa watu walioajiliwa kuanzia Julai 2019 ndiyo waende kwa sharia mpya ambayo nayo haikuwa rafiki kwa mfanyakazi. Cha kushangaza ambayo naamini kisheria ni kinyume, wote hasa tuliokuwa kwenye ajira kabla ya Mabadiliko ya sharia za Hifadhi ya Jamii tunalindwa na ilitakiwa sharia iendelee kama ilivyokuwa. Huu ulikuwa ni mkataba uliomvutia mchangiaji kujiunga na mfuko Fulani akijua baada ya mkataba wake wa miaka kadhaa ukisha, atachukua fedha zake na kwenda kujishughulisha. Lakini imekuwa ni kinyume ambapo sharia zimeanza kufanya Kazi kabla hazijatungwa, nikiwa na maana ya kuwa kwamba sharia zimerudi nyuma kusimamia mambo ambayo yalikuwepo yakisimamiwa na sharia zingine. Tunaomba kwa mamlaka yako turudishiwe haki hizi zilizokuwepo kwa mujibu wa sharia na uhalali wa mabadililiko ambayo nayo si rafiki uwe wa misingi ya kisheria.

Jambo jingine la muhimu ni miradi na uwekezaji unaofanywa na mifuko ya hifadhi ya Jamii. Mheshimiwa rais, tunatambua mifuko yetu imewekeza kwenye miradi mingi ikiwemo ya majengo ya makazi na biashara, viwanda na madaraja. Ni Jambo jema kuwekeza ili kuizalisha fedha inayochangwa ili iweze kutimiza lengo la kuhifadhi Jamii. Hatuna hakika kama wadau wakubwa wa uchangiaji juu ya tija ya miradi ya mifuko na hasa baadhi inayohusisha nyumba za makazi. Tunatambua Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilianzisha miradi ya nyumba za makazi kwa ajili ya kuuza. Jambo la Msingi kujiuliza ni kama mifuko ilijenga nyumba za kulenga wanachama wake au soko jingine tofauti. Nayasema haya hasa kwa kuangalia bei ya nyumba zenyewe kama zinaendana na uwezo wa wanachama wao na kama zinauzika hata kwa soko la jumla. Hata miradi ya majengo ya biashara inatakiwa ianze kutuonesha kwa uwazi kama ina mwelekea wa kulipa thamani ya uwekezaji uliofanywa ili kuendelea kulinda fedha za wachangiaji. Tunakubaliana na uwekezaji wa mifuko ya hifadhi ya Jamii lakini uwe unalinda na kukuza thamani ya fedha za wachangiaji wa mifuko.

Mheshimiwa rais, tunayo kero nyingine ambayo inazalishwa na uunganishwaji wa mifuko ambayo ni uhamaji na kurudi kwenye sekta husika. Watumishi wengi kama nilivyosema awali walikuwa na hiari ya kuchagua mfuko wowote kulingana na mambao yaliyowavutia. Kwa hali hii wapo waliokuwa kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma hata kama wao hawakuwa watumishi wa umma na pia wapo wa umma waliokuwa NSSF. Mpaka sasa mifuko mingine yote imeshavunjwa na sasa ipo miwili wa sekta binafsi na ule wa watumishi wa umma. Taratibu za kuhama kurudi kwenye eneo husika limekwisha kufanyika bali changamoto ni Pesa Kuhamiswa kwenda kwenye mfuko husika. Hii inatupa mkanganyiko mkubwa na itakuwa usumbufu kwa wanaostaafu au Kumaliza mikataba yao. Tunaomba ufanyike mchakato wa Pesa za mhusika kuwa kwenye mfuko wake husika na au kwa wale sharia za mifuko yao zilikuwa zikiwaruhusu kujitoa, basi waruhusiwe kufanya hivyo na kuchukua fedha zao ili watusaidie kutengeneza ajira kwao na kwa wengine.

Mwisho Mheshimiwa rais, niombe utusaidie wafanyakazi kwa kuondoa kero za utendaji unaochelewesha mafao ya wastaafu au wale ambao wanakuwa wamemaliza mikataba yao ili waweze kupata huduma zao kwa wakati. Tunatambua watumishi wanafanya kazi na kuchangia kila mwezi na uchangiaji unafanywa kisheria. Tungetamani sana mifuko ya hifadhi ya Jamii isiwe kama Gereza na Maabusu, Ibadili taswira na kutoa huduma kama ambavyo utafika kwenye benki au kampuni za simu ukaona unathaminiwa kwa sababu ni mteja. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii itambue kwamba ipo na watu wanaajiriwa kwa sababu ya fedha zilizochangwa na waajiriwa ambao tungesema ni wabia wamiliki wa mali za mifuko yote. Pia kwa sababu nazungumzia mafao basi niombe kupitia hapa nilete nyongeza ya ombi la kuangalia kiinua mgongo kinachosemwa kwenye Sheria ya Mahusiano Kazini ya 2004. Mwajiriwa ulipwa mshahara wa siku sababa kwa kila mwaka aliofanya kazi na isizidi miaka kumi. Maoni yangu kwa sababu linaendana na mafao ndiyo maana naliunganisha kwamba sharia ile ipitiwe upwa na Kiinua mgongo angalau kiwe mshahara wa mwezi Mmoja kwa kila Mwaka ambao mwajiriwa amefanya kazi na iwe kwa miaka yote ya utumishi pasipo ukomo.

Kwa mara nyingine nikushukuru Mheshimiwa Rais, na ninayoimani kwamba niliyoyaandika ni ushauri wa uzoefu wa ambayo kama mwajiriwa nimeyaona na yawezekana na wengine wameyaona kama mimi au kwa namna nyingene. Na niseme huu ni mwanzo na nitaendelea kuleta ushauri wa mambo tofauti tofauti ya kijamii ambayo yote yatafanywa kwa lengo la kujenga ili kwa pamoja tuweze kuifanya Kazi Ikaendelea kwa hatua na mafanikio Makubwa.



Imeandikwa na;

Sunday Beebwa,

0787585860.
 

Attachments

  • KILIO CHA WAFANYAKAZI KWENYE HIFADHI YA JAMII.docx
    16.5 KB · Views: 15

Similar Discussions

Back
Top Bottom