Wapinzani watoa wosia kwa wake zao,wawasihi wananchi kuendeleza uasi mtakatifu.

BroJay4

JF-Expert Member
Aug 27, 2007
236
16
JK awaamsha wapinzani
na Mobini SaryaSIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa kauli akijibu tuhuma zilizotolewa na viongozi wa upinzani dhidi ya viongozi kadhaa wa serikali, wapinzani hao nao wamejibu na kusema kauli ya Kikwete inalenga kupotosha kile ambacho wao wamekisema.
Wakizungumza katika ofisi za Tanzania Labour Party (TLP), viongozi hao walisema kuwa, kauli ya Kikwete imeonyesha kuwa analenga kuwachonganisha wapinzani na wananchi ili yeye na serikali yake wapate nafasi ya kujivua kashfa zinazowakabili.

Aidha, viongozi hao wanaounda ushirikiano wa vyama vinne vya TLP, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF, wakiongozwa na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, walimshangaa Rais Kikwete kwenda kujibu tuhuma hizo kwa viongozi wa dini, mahali ambako alijua hawezi kuulizwa maswali.

Walihoji ametumia kigezo gani kuwaona wao kama wapelelezi ambao wanatuhumu na kuhukumu bila kuwapa watuhumiwa nafasi ya kujitetea.

Katika tamko lao la kujibu kauli ya Rais Kikwete lililosomwa na Mrema mbele ya waandishi wa habari, wapinzani walitoa sababu nne zinazoonyesha jinsi majibu ya rais ambavyo hayakutosheleza kujibu hoja zao za ufisadi.

Kwanza, walirejea kikao cha Bunge la Bajeti ya 2007/08 ambapo Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto (CHADEMA), kwa niaba ya kambi ya upinzani, alitoa hoja binafsi ya kutaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza uhalali wa mkataba wa Buzwagi lakini hilo halikutekelezwa, baadala yake alisimamishwa.

Aidha, walisema kuwa, Agosti 18 mwaka huu katika mkutano wao wa hadhara Jangwani jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisoma barua inayoaminika kutoka Idara ya Usalama wa Taifa iliyokuwa ikionyesha kuwa, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alikuwa akitakiwa kutumia kila njia inayowezekana, kuficha ukweli juu ya tuhuma za ufisadi alizotaka kuziwasilisha bungeni.

Pia walisema kuwa, kabla ya kufikia hatua ya kuyataja hadharani majina ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni mafisadi baada ya jitihada zao za kutaka kuonana na Rais Kikwete walizungumza suala hilo bila ya kusikilizwa.

Walisema kuwa walimwandikia barua Rais Kikwete kuhusiana na suala hilo lakini hadi leo hawajajibiwa.

Walibainisha kuwa aidha barua hiyo ( ambayo walitoa nakala yake kwa waandishi), yenye kumbukumbu namba UWU/DSM/002/2007/02, iliandikwa Agosti 24 mwaka huu kwenda kwa Rais Kikwete, wakiomba kukutana naye ili wazungumzie mchakato wa ujenzi wa demokrasia ya kweli, katiba inayokidhi mazingira ya sasa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi pamoja na ufisadi nchini.

“Katika barua hiyo tulimtahadharisha kuwa kama hatachukua hatua, tutawataja watuhumiwa hadharani na kuwashitaki kwa wananchi watuhumiwa hao,” walisema na kubainisha kuwa tayari wameshayaanza mapambano hayo na waliapa kuendelea nayo bila kurudi nyuma kwani wamekwisha andika wosia kwa wake zao.

Baada ya kutoa sababu hizo, wapinzani hao walianza kuchambua matamshi ya Rais Kikwete na kueleza kuwa mtuhumiwa hukamatwa na polisi na kuwekwa rumande kisha huchunguzwa na kupewa hukumu inayoambana na adhabu.

Mrema alihoji: “Kama ndivyo hivyo, je, kwa mafisadi waliotajwa (akitaja majina) ni nani ambaye amekamatwa na wapinzani kisha kuwekwa rumande?”

Aidha, alihoji ni nani amesimamishwa kwenye ofisi ya upinzani kama vyumba vya mahakama au ni nani amehukumiwa kwa ufisadi na kupigwa viboko kisha kupelekwa jela?

“Sisi tunasema tumemtuhumu yeye na baadhi ya viongozi wa Serikali yake, hatujamhukumu yeye kwenda jela na kulipa hasara waliyolisababishia taifa, isipokuwa tunamtaka Rais Kikwete aunde tume huru ya kuchunguza na ukweli ujulikane, tume ndiyo imuoshe yeye na watu wake na wala asijaribu kuchukua msimamo mkali katika hoja zinazohitaji matumizi ya busara,” linasema tamko hilo.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Juma Duni Haji, alisema kuwa kazi ya wapinzani ni kukosoa pale wanapoona hapajaenda sawa, wala hawafanyi kazi ya kuhukumu aliyowapa na kusisitiza kuwa, ufisadi nchini haujaanza leo, kwani hata yeye mwenyewe rais amewahi kusema kuwa, anawafahamu wala rushwa na akawapa muda wa kujirekebisha, ingawa ameshindwa kuwachukulia hatua hadi leo.

Duni alitolea mfano habari iliyoandikwa na gazeti moja linalotoka mara moja kwa wiki likimkariri Waziri wa Maliasili, Profesa Jumanne Maghembe akisema wizara yake imelemewa na mafisadi, akahoji kwa nini Serikali isiwashughulikie, wakati Profesa Maghembe aliwahi kusema bungeni kuwa majina yao amempa Rais Kikwete.

Naye Mkurugenzi wa Fedha wa CHADEMA, Anthony Komu, alisema Kikwete amewasikitisha, kwani hawakutegemea kama angetoa matamshi kama hayo na kulifikisha suala hilo kanisani.

Komu alisema kabla ya suala hili kufikia hapo lilipo sasa lilianzia bungeni ambako jitihada za makusudi zilifanywa kulikwamisha na ndipo walipotoka nalo nje wakampa Rais Kikwete siku 30 awe amelifanyia kazi, mambo ambayo yote hayakufanyiwa kazi.

Alisema kuwa, hawajawataja mafisadi kama nchi au BoT, bali wamemtaja mtu mmoja mmoja na ni vema Rais Kikwete akawaacha watuhumiwa wajitetee wenyewe.

Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Polisya Mwaiseje, alisema haya yote yasingetokea kama Kikwete angetumia vema jukwaa la majadiliamo lililoanzishwa mwaka 2005.

Akifunga mkutano huo, Mrema alisema kuwa hawatakubali rais kwenda nje kuwahamasisha waporaji wa maliasili za nchi kwa madai kuwa ni wawekezaji na kusisitiza kuwa, watawahimiza wananchi kuendelea na uasi mtakatifu.


Source:Tanzania Daima.


Pambana na Ruswa,pambana na ufisadi,pambana na JK,EL,RA,Karamagi,pambana na mafisadi,pambana na CCM.Mungu Ibariki Tanzania.
 
“Katika barua hiyo tulimtahadharisha kuwa kama hatachukua hatua, tutawataja watuhumiwa hadharani na kuwashitaki kwa wananchi watuhumiwa hao,” walisema na kubainisha kuwa tayari wameshayaanza mapambano hayo na waliapa kuendelea nayo bila kurudi nyuma kwani wamekwisha andika wosia kwa wake zao

Desperate measures from desperate people..... poor them
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom