Wapinzani wamtimua DCI Manumba Dar

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,009
Wapinzani wamtimua DCI Manumba Dar

na Tamali Vullu
Tanzania Daima

MKURUNGEZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, jana alikutana na adha za kisiasa pale viongozi wa vyama vya siasa, hasa vya upinzani, walipomtimua katika mkutano wao ulioitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa.
Uamuzi wa kumtimua DCI katika mkutano huo ulifikiwa baada ya majadiliano yaliyotawaliwa na jazba, ambayo wakati fulani yalielekea kuzua vurugu, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa DCI hakupaswa kuhudhuria kikao hicho kilichowahusu wanasiasa.

Katika majadiliano hayo, wanasiasa waliokuwa wakipinga uwepo wa DCI katika mkutano huo, walimlaumu Tendwa kwa kuwaletea barua za mwaliko ambazo hazikueleza kuwa kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi nchini, angekuwapo katika mkutano wao.

Viongozi hao walisema kuwa, kitendo hicho cha Tendwa, kilionyesha dharau kwao, na kuhoji katika mkutano huo DCI alikuwa amekwenda kupeleleza kitu gani.

Kabla ya kufikia uamuzi huo, Tendwa alisema Manumba ni mmoja wa wadau katika masuala hayo na pia katika utendaji wake wa kazi anasimamia kazi za vyama vya siasa.

Hata hivyo, hilo lilipingwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), aliyesema kuwa, Sheria Namba 5 ya vyama vingi vya siasa, haijaeleza kuwa DCI naye ni mmoja wa watu wanaopaswa kuhudhuria mikutano ya kisiasa.

Alisema katika hali ya kawaida, Tendwa alipaswa kuwaarifu awali uwepo wa DCI na si kuwashitukiza kama alivyofanya.

“Kabla ya kumuita kwanza angepaswa kuomba ridhaa ya viongozi wa vyama vya siasa, yeye (DCI) si kiongozi wa chama cha siasa. Tukiacha hali hii, siku nyingine itaendelea… huku ni kutu-ambush (kutuvamia),” alisema Zitto.

Hata hivyo, Tendwa alisema utaratibu huo upo ndani ya Bunge na katika sheria zilizopo ofisini kwake hakuna kitu kama hicho na kueleza kuwa kwa kitendo hicho si kuwadharau.

“Tukizungumzia uwazi ndio huu, labda kama una hofu fulani. Ingekuwa hoja kama DCI angewaita ninyi ofisini kwake, lakini hapa ni mahali huru,” alisema Tendwa.

Alipoona kuwa kuna hatari kikao hicho kikavunjika kutokana na mabishano makali yaliyojitokeza, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, aliwashauri wajumbe walisamehe hilo ili kikao hicho kiendelee.

“Mimi sioni sababu kumwambia DCI aondoke, kwani hali ya sasa ya kisiasa inamuhusu… hakuna mtu aliyeitwa kukamatwa, kila mtu awe huru. Yeye ni mtendaji, anapaswa kusikiliza, kwa nini Tendwa kila siku awe posta?” alihoji Cheyo.

Hali hiyo ilimfanya Tendwa kuingilia kati kuwataka washiriki wafikie mahali wakubaliane ili kikao hicho kianze kufanyika.

Mwaiseje Polisya wa NCCR-Mageuzi, alishauri kikao hicho kitii maagizo ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ambaye alieleza masuala kama hayo yajadiliwe kwenye Baraza la Taifa la Majadiliano. “Lazima tuheshimu taratibu na sisi ni watu muhimu, tulipaswa kufahamishwa tangu awali,” alisema huku baadhi ya washiriki wakishangilia kwa kupiga makofi.

Mwanasiasa mwingine, alisema wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, serikali ilikuwa ikishutumiwa kwa kukumbatia rushwa na kwamba watu walikuwa wakizungumza hadharani, lakini katika kipindi hiki watu wanatishiwa.

“….sasa tunapoanza kuzungumza tunaitiwa DCI… DCI atuache tuzungumze siasa, lazima tupate uhuru wa kuwaambia viongozi wetu makosa yao. Kama DCI anaona kuna mtu ametenda kosa amwite ofisini kwake,” alisema.

Akionyesha kushangazwa kwake na tukio hilo, James Mapalala, alisema kuwa katika maisha yake hajawahi kuona DCI akihudhuria mikutano ya wanasiasa katika nchi yoyote duniani na kuhoji DCI amekwenda kupeleleza kitu gani katika kikao hicho.

Hata hivyo, alisema kama kulikuwapo na ulazima wa DCI kuhudhuria kikao hicho, ingekuwa vema wangetaarifiwa mapema, lakini kwa hali hiyo, Tendwa amekiuka mipaka yake ya kazi.

“Tendwa umekwenda nje ya madaraka yako, kutuitia polisi… watu hawataweza kuzungumza wanayotaka,” alisema.

Emmanuel Makaidi alisema yeye aliwahi kuwa mtendaji serikalini na kwamba hajawahi kuona hata siku moja mtendaji akachanganywa na mwanasiasa.

“Tukimuuliza masuala ya kisiasa ni kama kumuonea. Atashindwa kujibu. Tumuombe atuache tuzungumze. Viongozi wa siasa wana hofu DCI hapa kafuata nini? Hapa hakuna criminal (jinai),” alisema Makaidi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Jahazi Asilia, John Mswanyama, alisema watu wameanza kuhisi harufu fulani na kusema kwa kuwa kama serikali ingetaka kutuma mwakilishi kwenye kikao hicho, ingemtuma waziri mwenye dhamana ya siasa.

“…..mambo kama haya ndiyo maana watu wanazomewa. Wapinzani wamezunguka karibu nchi nzima hakuna mtu aliyezomewa wala kuku kukanyagwa,” alisema.

Aidha, Profesa Leonard Shayo, aliwashauri washiriki wenzake kumwacha DCI, kwani wakimuondoa wanaweza kukosa kitu fulani ambacho amekuja nacho.

“…jamani tusikilize atakayozungumza, lakini si kukataa kabisa. Tutakosa kitu fulani,” alisihi.

Baadaye, Tendwa alikiri kufanya kosa la kimenejimenti kwa kutowataarifu uwepo wa DCI katika kikao hicho, lakini alisisitiza kuwa DCI ni mmoja wa wadau katika vyama vya siasa na hilo lipo katika sheria.

Kitendo hicho kilipingwa na baadhi ya washiriki ambao walisikika wakisema kuwa iwapo waandishi wa habari wanafukuzwa kwa kuwa hawahusiki, naye DCI aondoke kwa kuwa hausiki.

“Tusichanganye vitu, kama kuzumgumza masuala ya siasa, waandishi wa habari hawahusiki, DCI naye hausiki, kwa sababu tunapoanza kuchanganya mambo hapa ndiyo vurugu zitakapoanza,” alisema Mapalala na kuongeza kuwa DCI aitwe kwa kufuata taratibu, kwa kuwa kikao hicho si mkutano wa hadhara.

Hatua hiyo, ilisababisha Cheyo kusimama na kuwataka viongozi wasiotaka kumsikiliza DCI watoke nje, na ndipo baadhi ya viongozi hao walianza kusimama na kutoka.

Makaidi alisimama na kuwasihi viongozi hao kurudi kwenye nafasi zao na kumwomba DCI awasalimie, ndipo aondoke.

DCI alisimama na kuwasalimia viongozi hao na kueleza kuwa anaheshimu maoni yao na kwamba siku nyingine ataitisha mkutano wa wanasiasa, wananchi na wadau wengine ili kujadili masuala mbalimbali.
 
Hivi tukiutaka ukweli kabisa Tendwa can he enlighten us , why DCI was there ?Anahusika na siasa zipi ?
 
Back
Top Bottom