Wapinzani wamjibu Kikwete

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Posted Date::10/12/2007
Wapinzani wamjibu Kikwete
* Wasema hajajibu hoja yao ya ufisadi

* Wasema hawajakamata wala kumhukumu mtu

* Wamtaka aunde tume huru ya kuchunguza

Na Muhibu Said
Mwananchi

VYAMA vya siasa vilivyo kwenye ushirikiano, vimemtaka Rais Jakaya Kikwete kuiachia tume huru kazi ya kuwasafisha vigogo wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi badala ya kuchukua msimamo mkali kujibu hoja hiyo.

Ushirikiano huo unaoundwa na vyama vya CUF, Chadema, TLP na NCCR-Mageuzi, umesema umekwishatekeleza jukumu lao la kuwatuhumu vigogo hao, hivyo anachotakiwa kukifanya Rais Kikwete ni kutumia busara kuunda tume hiyo ili ukweli juu ya tuhuma hizo ujulikane, badala ya kuwalamu waliotoa tuhuma hizo.

"Tume ndiyo iwaoshe na wala asijaribu kuchukua msimamo mkali katika hoja zinazohitaji matumizi ya busara," vilisema vyama hivyo kupitia tamko lao lililosomwa na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema kwa niaba ya wenyeviti wenzake wa vyama hivyo, katika mkutano wao na waandishi wa habari, uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam jana.

Tamko hilo limetolewa na vyama hivyo, siku moja baada ya Rais kikwete kukaririwa na vyombo vya habari jana akionya tabia ya kutuhumiana kwa ufisadi, aliyodai kuwa imejengeka kwa baadhi ya wanasiasa ambao wanajifanya dola ya kupeleleza, kukamata, kuendesha mashtaka na kutoa hukumu bila kuwepo watuhumiwa.

Rais Kikwete aliyasema hayo Jumanne wiki hii katika hafla ya uchangiaji wa ujenzi wa hosteli ya Kanisa la Kiinjili la Kiluthei Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mkoani Arusha, iliyofanyika katika Hoteli ya Kibo Palace, ambako alialikwa na Mkuu wa Dayosisi hiyo, Askofu Thomas Laiser.

Alisema utaratibu huo wa kutuhumiana utawatisha wananchi Mbali na kujenga chuki miongoni mwa jamii na kwamba hali hiyo haiendani na taratibu za kuendesha nchi kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria.

Rais Kikwete alisema tabia ya kumpeleleza mtu, kumkamata na kumsomea mashtaka na kumhukumu bila kumpa nafasi ya kutetea, haimtendei haki mtuhumiwa ambaye naye ana haki ya msingi kulindwa mbele ya sheria.

Katika tamko lao la jana, vilisema wao wametoa tuhuma na si kukamata wa kuhukumu kama Rais Kikwete alivyosema kwa sababu hawana uwezo wa kufanya hivyo.

"Mtuhumiwa hukamatwa na polisi na kuwekwa rumande, huchunguzwa, hushitakiwa, huhukumiwa na kupewa adhabu. Je, kwa waliotajwa ni nani amewekwa rumande ya wapinzani? Je, ni nani amesimamishwa kwenye ofisi za upinzani (kama vyumba vya mahakama)," alisema na kuhoji Mrema na kuongeza:

"Sisi tunasema tumewatuhumu baadhi ya viongozi wa serikali yake hatujamhukumu yeye kwenda jela na kulipa hasara waliyoisababishia taifa, isipokuwa tunamtaka rais aunde tume huru ya kuchunguza tuhuma hizo na ukweli ujulikane".

Mrema alisema walifikia hatua ya kuwataja vigogo hao hadharani baada ya Bunge kukataa hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto kutaka liunde kamati teule ya kuchunguza uhalali wa mkataba wa mradi wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi, na kisha kuamua kumsimamisha kuhudhuria vikao hadi Januari, mwakani.

Alisema sababu nyingine ni barua iliyosomwa na Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Willibrod Slaa, Agosti 18, mwaka huu, katika viwanja vya Jangwani, ikimtaka Waziri Mkuu afanye kila linalowezekana kupinga na kuficha ukweli juu ya tuhuma hizo zilizotaka kupelekwa bungeni na mbunge huyo.

"Katika mkutano huo rais alitumiwa taarifa kuwa achukue hatua dhidi ya tuhuma hizo," alidai Mrema.

Oktoba 7, mwaka vyama hivyo vilitangaza msimamo wao wa kupinga hatua ya serikali kuamua kuchunguza tuhuma hizo na kutishia kutangaza mgogoro wa kitaifa utakaohusisha maandamano na migomo nchi nzima, kuanzia Novemba, mwaka huu, kama Rais Kikwete hatakubali kuunda tume kufanya uchunguzi huo.

katika tamko lao vilipinga uchunguzi wa tuhuma hizo kufanywa na serikali kwa kuwa wengi wa watuhumiwa ni viongozi wake, hivyo hawana imani kama serikali inaweza kufanya uadilifu na kutoa ripoti ya kuridhisha kuhusu uchunguzi huo.

Mbali na hayo, vyama hivyo pia vilimtaka Rais Kikwete kuitisha kongamano la kitaifa kwa kuvihusisha vyama vya siasa, taasisi za kidini, wasomi, wanasheria na kuunda tume huru ya kuchunguza tuhuma zote.

Tuhuma hizo zilitangazwa na Dk Slaa kwa kushirikiana na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu walipohutubia mkutano wa hadhara, katika viwanja vya Mwembe Yanga, jijini Dar es Salaam Septemba 15, mwaka huu.

Kutokana na hatua hiyo, watu mbalimbali, wakiwamo wasomi, wanasheria, waandishi wa habari, viongozi wa dini, mabalozi wa nchi mbalimbali waliitaka serikali kutoa tamko linaloeleweka na la wazi kuhusu tuhuma hizo.

Kutokana na shinikizo hilo, Ijumaa wiki iliyopita, serikali kupitia Waziri Benard Membe ilitangaza uamuzi wake wa kuchunguza tuhuma hizo na kuonya kwamba, itawachukulia hatua za kisheria au kuwawajibisha watakaopatikana na hatia.

Serikali pia ilitangaza kuchunguza tuhuma za kuwapo mazingira ya rushwa katika utiaji saini mkataba wa Buzwagi, uliosababisha Zitto, kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge, baada ya kuwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu suala hilo.

Tayari viongozi sita, wameshatoa taarifa kwa vyombo vya habari dhidi ya tuhuma za ufisadi zilizoelekezwa kwao na Dk Slaa, huku baadhi ya watuhumiwa wakikanusha kuhusika kabisa, wengine wakizipuuza na wengine wakitangaza azma ya kumshtaki mahakamani mbunge huyo.

Baadhi ya viongozi waliojibu tuhuma hizo kwa kukana na kutishia kumshtaki Dk Slaa pamoja na Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini (CCM) na mwanasheria mkongwe, Nimrod Mkono, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Patrick Rutabanzibwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Septemba 24, mwaka huu, Waziri Karamagi alimpa Dk Slaa na Lissu wamwombe radhi na kumlipa Sh10 bilioni zikiwa ni fidia ya kuchafuliwa jina kwa kuhusishwa na ufisadi.

Hata hivyo, Dk Slaa na Lissu, walisema hawani nia ya kuomba radhi wala kulipa kiasi hicho cha fedha kwa maelezo kuwa tuhuma walizozitoa dhidi ya viongozi hao zina ushahidi.

Naye Jackson Odoyo anaripoti kuwa baadhi ya wananchi wamesema kuwa tamko la alilolitoa Rais Kikwete juzi akiwa Arusha limeacha maswali mengi badala ya kuwapa mwanga juu ya tuhuma za ufisadi zinazowakabili baadhi ya vigogo wake.

Wakizungumza na Mwananchi jana jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kauli ya rais kwamba kuchukua hatua bila uthibitisho na kwamba tuhuma hizo zitaipeleka nchi pabaya ni za kuwatetea mawaziri wake wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Joyce Lyapembile Mkazi wa Ubungo Kibangu alisema maelezo ya rais yatawapa kiburi waliotuhumiwa .

George Joseph mkazi wa Mabibo External alisema kauli yake iko wazi na inawalinda mawaziri wake ambao ndio watuhumiwa wa ufisadi.
 
Back
Top Bottom