Wapinzani waibuka

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,045
Wapinzani waibuka

na Mustafa Leu, Arusha
Tanzania daima

VYAMA vya upinzani vimeitaka serikali kuzitoa hadharani taarifa za ripoti ya tume iliyoongozwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Robert Mboma na kamati iliyoongozwa na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Lawrence Masha, zilizohusu sekta ya madini, ili wananchi waelewe kilichopendekezwa na kamati hizo.
Hayo yameelezwa juzi mjini hapa na mwanaharakati Tundu Lissu, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa NMC, ulioitishwa na umoja wa vyama vinne vya upinzani nchini, kuhusu uamuzi wa serikali wa kuunda tume ya kuchunguza na kupitia upya mikataba ya madini.

Lissu alisema kuwa, anashangaa kuona serikali imeunda tume nyingine kupitia mikataba ya madini wakati ripoti za tume mbili za Jenerali Mboma na Kamati ya Masha hazijafanyiwa kazi na wananchi hawajui nini kilipendekezwa nao.

Lissu alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa zilizovuja, tume hizo zilipendekeza mambo mengi yanayolenga kuifanya sekta ya madini iwasaidie zaidi wazawa, lakini inashangaza kuwa ripoti hizo hazijawekwa hadharani na badala yake zinaundwa tume na kamati nyingine kuangalia suala hilohilo ambalo lilishaangaliwa.

Alisema kuwa anashangaa kuona wafanyakazi nchini wanatozwa kodi katika mishahara yao, lakini wawekezaji wakubwa katika madini wanapewa misamaha ya kodi na kusema kuwa huo ni unyanyasaji.

"Tunahitaji tupate viongozi wasafi wasiokuwa na dosari ili hatimaye tujikomboe na hali hiyo, hili litawezekana kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika chaguzi mbalimbali pamoja na kulinda kura zao kwa gharama yeyote ile," alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, akihutubia katika mkutano huo, alisema waliokomba mabilioni ya fedha toka Benki Kuu hawajashughulikiwa na serikali na badala yake wanakamatwa wajawazito kwa kutochangia miradi ya maendeleo na wanajifungulia kwenye ofisi za watendaji.

"Huu ni ukatili wa hali ya juu unaofanywa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi," alisema.

Kuhusu hoja ya mzee Peter Kisumo, ambaye ni kada wa siku nyingi wa CCM aliyenukuliwa akisema hivi karibuni kuwa CHADEMA imeiba sera ya mikataba ya madini kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete, Dk. Slaa alisema kuna uwezekano mkubwa mzee huyo alikurupuka.

"Nchi hii imefikishwa hapa na wao… sijui haijui katiba ya jamhuri au anafanya makusudi ili azidi kujipendekeza. Hawa wazee ndio walioifikisha Tanzania hapa ilipo… waache kujikomba kwa serikali," alisema.

Aliitaka serikali kuiweka hadharani taarifa ya ukaguzi ya Benki Kuu ili wananchi wajue nini kilichomo ndani yake badala ya kuendelea na ubabaishaji usiokuwa na mwisho.

Alisema kuwa kila mbunge amepewa kitabu cha matumizi ya fedha za BoT, hivyo akawataka kuwasomea wananchi kilichomo katika kitabu hicho, na kama hawako tayari kutekeleza hilo wananchi wawahoji ili waeleze kilichoandikwa.

Naye Mwenyekiti wa TLP, Augostine Mrema, alisema kuwa iwapo CCM wanazuia upinzani kwenda Ikulu kwa mlango mkubwa wa mbele, wao watapitia dirishani.

Alisema kuwa yeye aliteseka na upinzani na amekuwa akijiuliza kwa muda mrefu atamwachia nani nchi, lakini sasa anashukuru amepata warithi baada ya kuibuka kwa vijana mahiri katika kambi hiyo.
 
Back
Top Bottom