Wapinzani waibua tena suala la BoT

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,886
Wapinzani waibua tena suala la BoT
Stella Nyemenohi, Dodoma
Daily News; Tuesday,June 17, 2008 @00:01

Sakata la ujenzi wa majengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) limeibuliwa tena bungeni na kambi ya upinzani wakitaka waelezwe thamani halisi ya ujenzi wake, wakidai kuwa matumizi yake yalisababisha mfumuko wa bei.

Sambamba na kuhoji juu ya majengo hayo (Twin Towers), kambi hiyo ya upinzani imetaka pia kupata maelezo ya kina kama BoT iliendelea kuwekeza katika kampuni ya Mwananchi Gold Mine na kiasi cha mapato yaliyopatikana hadi sasa na kuelezwa rasmi juu ya umiliki wa Kampuni ya Meremeta.

Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed alitoa hoja hizo jana kupitia hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2008/09. Akizungumzia kuhusu majengo ya BoT, Hamad alisema kwa taarifa ya benki hiyo, gharama za ujenzi imeshazidi wastani wa Sh bilioni 600 wakati mjenzi hajakabidhi rasmi majengo pamoja na kwamba lilifunguliwa mwaka 2005 na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

“Kuna wasiwasi kuwa matumizi haya pia yalisababisha mfumuko wa bei. Tunataka maelezo. Pia tunamtaka atupatie taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Benki Kuu tuweze kulinganisha na taarifa tulizo nazo,” alisema Hamad ambaye ni Mbunge wa Wawi (CUF).

Kuhusu uwekezaji wa BoT katika Mwananchi Gold Mine wa dola za Marekani 5,512,398.55 hadi Juni 30, 2006, kiongozi huyo wa upinzani alisema, “tunataka serikali itupatie maelezo ya kina ambayo tunatumaini yatakuwa tofauti na ya mwaka jana, yatakuwa si majibu ya kisiasa.”

Kwa upande wa Meremeta Gold, kambi hiyo inataka kupata taarifa ya kina kuhusu tathmini iliyofanywa na BoT juu ya mradi huo, pamoja na kupatiwa taarifa rasmi ya umiliki wake sasa. Kwa mujibu wa Mohamed katika kikao cha bajeti cha mwaka 2006/07, Bunge lilielezwa kuwa Meremeta ilikuwa chini ya uongozi wa Time Mining ya Afrika Kusini na kudhaminiwa na BoT kwa Dola za Marekani milioni 100.

Ilielezwa kuwa BoT ilikuwa ikifanya tathmini kwa kuwa mgodi ulikuwa katika hatari ya kufilisika. Hotuba hiyo ya upinzani pia iligusia ukiukwaji wa utaratibu wa kumpata mzabuni wa kuchunguza mauzo ya dhahabu unaofanywa na Kampuni ya Alex Stuart Asseyers na kusema walitarajia serikali ingesema kiasi cha mapato kilichopatikana kutokana na taarifa ya kampuni hiyo, baada ya serikali kuilipa kiasi ambacho si chini ya Dola za Marekani milioni 65.

Katika hatua nyingine, wapinzani wameitaka serikali kuwasilisha bungeni ripoti ya Kamati ya Madini iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete ya kupitia mikataba ya madini, kufahamu ni namna gani mapendekezo yaliyomo yamezingatiwa katika bajeti mpya.Kamati iliundwa Novemba mwaka jana na kukabidhi ripoti yake mwezi uliopita.

Akiainisha vyanzo vya mapato vinavyopaswa kuzingatiwa katika bajeti, kiongozi huyo wa upinzani alisema kuna taarifa kuwa serikali imepoteza zaidi ya Sh bilioni 883 katika miaka 10 kutokana na sheria mbaya ya kodi ya mapato katika sekta ya madini iliyotungwa mwaka 1997. Kambi hiyo ya upinzani ilipendekeza kuwa msamaha wa ushuru wa bidhaa kwenye mafuta kwa kampuni za madini katika migodi mikubwa na kati ufutwe.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom