Wapambanaji watazamaji...

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,474
39,987
UAMUZI WA KUPAMBANA AU KUTAZAMA WAPAMBANAO!

Ni miaka karibu miwili na nusu imesalia hadi uchaguzi Mkuu wa 2010, uchaguzi ambao wengi wanausubiria kuona kama utaleta mabadiliko wanayoyatarajia. Uchaguzi huo na ule wa 2015 waweza kuwa ni uchaguzi muhimu zaidi tangu kupata Uhuru kwani kwa namna ya pekee, kundi jipya la wapiga kura waliozaliwa baada ya mfumo wa vyama vingi kurudishwa tena nchini watapiga kura kwa mara ya kwanza.

Kundi hili la vijana watakaokuwa wamefikisha miaka 18 wakati huo ambalo linakadiriwa kufikia milioni kama tano hivi laweza kuwa chanzo cha mabadiliko makubwa. Kama Rais Kikwete katika uchaguzi uliopita alipata kura milioni 9,123,952 kutoka makundi yote ya wapiga kura basi tunaweza kuona kuwa kundi hili la kizazi cha "M" (mageuzi) laweza kuwa ni tofauti kati ya mshindi na watakaoshindwa mwaka 2010. Ni kundi linalopiganiwa na vyama na wagombea.

Ukiondoa kundi la wapiga kura kuna mambo mengi ambayo yanaashiria kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa ni wa kuamua hasa mwelekeo wa Taifa kwani kwa namna ya pekee kizazi kilichochukua nchi baada ya Uhuru karibu chote kitakuwa kimefika muda wa kustaafu kutoka utumishi wa serikali kwa hiari na wachache watakuwa wamefikia muda wa kustaafu kwa lazima. Hivyo kuna kizazi kipya kabisa ambacho kitakuwa kimepanda ngazi katika sehemu nyingi sana za uongozi wetu.

Zaidi ya hayo basi kuna kila dalili pia kuwa mpangilio wa vyama vya kisiasa hautakuwa jinsi ulivyokuwa mwaka 2005 hasa baada ya sheria ya vyama vya kisiasa kupitishwa baadaye mwaka huu ambayo itarahisisha mambo mengi. Kuna uwezekano mkubwa kuwa mwishoni mwa mwaka huu au mapema mwakani vyama kadhaa vya kisiasa vitavunjika na kuunda chama kimoja cha kisiasa ambacho kitakuwa ni chama kikuu cha upinzani. Kama hilo litatokea basi kuna kila dalili ya chama tawala nacho kujipanga vizuri zaidi na hasa kufanya mabadiliko katika Katiba yake na hususan kwenye suala la uchaguzi wa viongozi wake na wagombea wake ili kufungua mlango wa kidemokrasia, uwazi, na nafasi sawa. Mtindo wake wa kura za maoni na maamuzi ya Kamati Kuu vinaweza kabisa kubadilishwa ili kuhakikisha chama hicho kinapata viongozi ambao kweli wananchi wanawataka na hivyo kutoa changamoto kwa vyama vya upinzani navyo kufikiri jinsi ya kujibu mkakati huo.

Hivyo basi kuna mengi ambayo yanaashiria kuwa muda si mrefu ujao motomoto wa uchaguzi utaanza kuwaka taratibu na watakuwa wapumbavu wale wasiojiandaa kwa mabadiliko yajayo kwani suala si kama yatatokea au hayatatokea bali ni kwa haraka gani yatatokea na athari zake kwa mtanzania zitakuwaje.

Kwanini naandika haya? Ndugu zangu, muda si mrefu kila mmoja wetu ataitwa na dhamira yake kufanya maamuzi; maamuzi ya kuchagua upande na kuchagua mwelekeo ambao anaona ni bora kwa Taifa na kwa ajili yake. Maamuzi hayo yatahitajika kufanywa mapema zaidi kuliko inavyodhaniwa.

Binafsi naamini kabisa kama mtu hajafanya uamuzi wa nini cha kufanya sasa basi mtu huyo anaweza kujikuta amechelewa na hivyo akajikuta ni "mpambanaji mtazamaji". Yaani, mtu ambaye hana athari yoyote isipokuwa ya kuangalia wengine wakipambana na yeye akibakia kama shabiki uwanjani kupiga kelele za kushangilia na miluzi ya kufurahia lakini kamwe hatoshiriki katika kinyang'anyiro cha mabadiliko yajayo.

Inasemwa kuwa katika mabadiliko kuna makundi makubwa matatu ya watu; wapo wale wanaoshiriki kuleta mabadiliko, kuna wale ambao wanakaa pembeni kuangalia wengine wakileta mabadiliko; na kuna wale ambao hata hawajui kama kuna mabadiliko!

Kundi la kwanza na la mwisho ni kama pande mbili zisizotazamana. Lakini kundi la katikati (la wale wanaoangalia wengine wakileta mabadiliko) ndilo kundi ambalo kwa hakika linaweza kuleta mabadiliko likiamua kuchagua upande. NI kundi ambalo likitaka linaweza kabisa kuijenga Tanzania linayoitaka endapo litaamua kuunganika na wale wa kundi la kwanza.

Kundi hili la katikati ndilo mara nyingi lina uwezo, nyenzo, na kila litanufaika zaidi na mabadiliko mazuri yatakayotokea kwenye jamii. Lakini, kwa kadiri linavyokaa pembeni kutazama na kushabikia; kwa kadiri linavyokaa kwenye mitandao na kuchangia hoja mbalimbali; kwa kadiri linavyokaa na kusoma makala na kufuatialia habari za kimataifa au siasa za nyumbani lakini likishindwa kuamua nani wa kumuunga mkono litaendelea kuwa butu na lisilo na athari zozote kwenye mabadiliko. Hili ni kundi ambalo naweza kusema ndiyo kiini cha mabadiliko.

Ni kundi hili ambalo naliandikia leo kuwa wakati umefika lianza kuunga mkono juhudi za wale wapambano ardhini au waliomstari wa mbele kuchochea mabadiliko ya kifikra. Kundi hili halina budi kufanya uamuzi wa kuunga mkono juhudi za wale wanaosimama kupambana ili wasijione wanafanya kazi bure na isiyo ya shukrani.

Kundi hili lazima liamue kuunga mkono juhudi za mtu mmoja mmoja, vikundi, taasisi, na vyombo mbalimbali ambavyo vinashikiri katika kuchachua jamii ili iweze kuamka na kusababisha mabadiliko yaliyobora kwa jamii hiyo.

Ninapoandika nasukumwa na kuangalia vitu kadhaa ambavyo watu wanaonekana kuvifurahia lakini hawako tayari kuviunga mkono au hawatoi mawazo ya jinsi ya kuviunga mkono. Nazungumzia mang'amuzi yangu binafsi.

Baada ya kukamatwa kwa Mac na Mike mapema mwaka huu kuna baadhi ya watu ambao waliposikia JF inahusishwa na Ughaidi waliamua kujificha na kukaa kimya kuona nini kitatokea; na wapo wale ambao walipoulizwa na jamaa au marafiki zao kuhusu JF waling'ana na kuhoji "Jambo what?" kana kwamba hawajawahi kuisikia. Lakini wapo wale waliposikia matatizo hayo walitoka mafichoni na kwa fahari wakajitokeza kuinga mkono JF wakati ule wa giza. Watu walijitokeza kwa namna moja au nyingine kuhakikisha kuwa JF inarudi hewani na inakuwa stronger than before.

Hilo limetokea hata kwangu na KLHN na jinsi ambavyo nilifika mahali nimekata tamaa baada ya kubeba mzigo wa kugharimia kila kitu na kushindwa hasa kufanya nilichotaka kufanya na kutaka kuweka manyanga chini kwani ni kujibebesha mzigo usio na shukrani. Wakajitokeza watu ambao waliniunga mkono na wakatoa resources zao kuwezesha yale tunayoyafanya sasa.

Katika yote mawili jambo moja kubwa nililoliona ni tabia ya watu kusubiri mgogoro, mkasa, au matatizo ndipo wawe tayari kutoa msaada au kuunga mkono lakini nje ya hapo ni hadi watu wapitishe bakuli la kuomba omba ili mambo yaende.

Ndugu zangu, kwa mwendo huo hatutaweza kufika isipokuwa kama vyombo vyetu hivi JF na KLHN na hata vingine vitakapoamua kulala kitanda kimoja na mafisadi na kujifunika mablanketi ya utajiri wao. Ni mara nyingi tunakabiliwa na ofa za ajabu (ajira na vinginevyo) ili tuwe sehemu ya vyombo "vyao" vya habari wakiahidi "uhuru" n.k Wapo wanaotoa ofa ambazo ni nzuri mfukoni na inaweza kutibu matatizo yote ya kiuendeshaji lakini wakiweka vipengele vidogo vya kiutawala na kiuhariri.

Wapo ambao wanatoa ofa "isiyo na masharti" lakini haileweki kama kutokuwa na masharti kuna maana kutokuwa na influence yoyote. Hili mara nyingi linatusumbua. Je mtu akija na kukuahidi ajira kwenye chombo chake na unajua jamaa ni fisadi au anataka kukubana baada ya kukuweka kibindoni unafanyaje?

Lakini wakati huo huo wapo wale ambao wanaamini kweli katika yale tunayoyafanya na wako tayari kweli kusaidia lakini hawa ni wachache na wanafanya hivyo kwa mapenzi yao wenyewe na hivyo siyo wa kuwaweka kwenye bajeti.

Vyombo vyetu hivi havina budi kuendeshwa na michango ya kujitolea ya mashabiki na wanachama wake. Lakini hili kwetu Wabongo ni gumu kweli. Hata kwenye gulobu maarufu kama ya Ndg. Michuzi hivi akiamua kuifanya watu walipie mnafikiri ni wangapi watakubali kulipia au wataanza kumkandia? Hata hapa JF tukiamua kuwa JF iwe ya malipo ni wangapi watakuwa tayari kulipia? Je KLHN inapofanya mahojiano ya kina na viongozi au watu mbalimbali ili kuyasikiliza lazima uwe mwanachama wa kulipia ni wangapi watakuwa tayari kufanya hivyo? Ukweli unaotokana na mang'amuzi yangu ni wachache sana watafanya hivyo.

Wengi wetu tumezoea vya bure na vya dezo na vile vyenye gharama tunaona kama jamaa watanufaika na fedha zetu au wanatafuta ulaji. Hatutaki kuamini kuwa kijana kama Mac anafanya kazi, anahitaji kwenda shule na anakaribia kuoa; kwamba maisha yake yana gharama. Hatutaki kufikiri kuwa behind the name "mwanakijiji" kuna mtu ambaye ana maisha yake ( the little that he has) na ana gharama ya maisha yake na anaweza kufanya vipi anayoyafanya?

Kuna watu kama Zitto ambaye wengi wanafurahia mchango wake na yale aliyoyafanya na wanaona kipaji chake na kwa namna fulani wanaona furaha kuwa na kijana kama huyo. Lakini ni wangapi wako tayari kumkatia cheki ya dola 50 na kusema "Mhe. Asante" kwa kazi yako, au kumuuliza anahitaji kitu gani katika kusaidia Jimbo lake la Kigoma Kaskazini? Of course, watu watasema "kwani wabunge wanalipwa kiasi gani, mbona wanapewa hela nyingi tu si azitumie hizo"? Hapo ni kumiss point. Gharama za Mbunge mmoja mara nyingi ni kubwa kuliko mapato yao hasa kama anataka kuwa mwadilifu. Lakini wale watazamaji wapambanaji watapiga makofi na kumpa "thank you" kwenye mtandao wakifikiri hilo linatosha.

Ndugu zangu, "pongezi" na maneno ya "shukrani" hayatoshi!! Kama kweli tunataka kuona mabadiliko ya kweli 2010 na kuweza kuteka mioyo ya Watanzania kuweza kuamini kuwa na wao wanastahili uongozi mzuri na Taifa la kisasa hatuna budi kuunga mkono juhudi za wale wanaoongoza mabadiliko hayo. Tusikae pembeni kuangalia wengine wakileta mabadiliko na kupiga makofi ya kushangilia!!

Nimejifunza kitu kimoja kutoka NPR (National Public Radio) kwa karibu miaka sita sasa nimekuwa mchangiaji wa kudumu wa radio yetu hapa Detroit (WDIV) ambayo iko Wayne State University. Nilianza kuchangia baada ya kuguswa na habari moja na nimekuwa msikilizaji wa vipindi vyao vya "All Things Considered", "Fresh Air", "Morning Edition" na "News and Notes".

Kila wakati wa Machipuko (Spring) wanakuwa na fundraising ya kusaidia vituo vyao na ni wachangiaji ambao ni wasikilizaji wanaoamua kuchangia kwa sababu wanathamini kile ambacho NPR inafanya na wanafanya hivyo aidha kuwa kutoa kiwango kimoja au kutoa kila mwezi. Wanafanya fundraising kama hiyo tena wakati wa Kipupwe(fall) na ndivyo ambavyo vituo vyao vingi vinaendeshwa; kwa michango ya wasikilizaji na mashabiki. Ni hiki kinachowezesha NPR kuwa na maripota wazuri na habari za kina kuliko vituo vya radio vya dakika mbili au tatu.

Kwanini wamarekani na watu wa magharibi wanasupport vitu wanavyovithamini? Ni mara ngapi umewahi kusikia michango ya kusaidia taasisi ya kansa, kituo fulani cha michezo n,k? Ni kitu gani kinawafanya waamini kuwa ni jambo bora kuunga mkono juhudi hizo? Si kwamba taasisi hizo hazina ufisadi au mapungufu (tunakumbuka jinsi Red Cross ilivyofanya baada ya September 11)na wengi tunajua jinsi michango ya Kimbunga cha Katrina ilivyokuwa abused. Lakini hayo yote hayakuzima roho ya kujitolea ya Wamarekani kwani hata ilipotokea Tsunami walikuwa pale tena na sitoshangaa licha na ugumu wa maisha kuna michango itaitishwa kusaidia Mynmar baada ya kimbunga hiki cha juzi.

Kwanini Watanzania hatuko tayari kusupport kwa mali na fedha vile tunavyovithamini au wale ambao tunaona wanafanya yale ambayo sisi wenyewe hatuna muda, uwezo au vipaji vya kufanya?

Juzi nilikuwa kwenye Kanisa moja muda mfupi kabla ya kwenda kumpokea Mhe. Zitto (Kanisa la Mchg. Keith Butler) na nikaona jinsi gani wenzetu wanachangia ujenzi wa kituo cha watoto cha kisasa zaidi. Je, sisi tunaweza kuchangia kujenga kitu fulani sisi wenyewe bila msaada kutoka kwa wafadhili au NGO?

Ninachosema ndugu zangu is very simple and straight forward. JF inapojiandaa kufanya mabadiliko makubwa itahitaji msaada na kuungwa mkono. Sisi wa KLHN tunapojaribu kujijenga na kutengeneza mtandao wa habari tunahitaji support ili tuwe wa kwanza kukuletea habari za kina pasipo gharama kubwa (yoyote) kwako. Lakini haya yote hayawezekani pasipo kuviunga mkono vyombo hivyo kwa michango yenu ya fedha.

Hatuwezi kufanikiwa kwani shughuli hizi kwa kweli zinataka moyo, na mara nyingi watu tunajikuta tuko pweke na kushindwa kuamua kama kweli kuna faida ya kufanya tunayoyafanya. Siwezi kushangaa ikitokea JF ikazimika watu watashtuka kwa muda tu lakini baada ya siku chache hawataimiss tena.

Ndugu zangu, tusimame kuunga mkono vile vitu tunavyovithamini badala ya kuvishabikia toka nje au kukaa pembeni. Mara nyingi hatuhitaji vitu vingi au kiasi kikubwa cha fedha kujiendesha kama NPR. Hatuhitaji mtu atoe mchango wa mamia ya dola, lakini kile kidogo kidogo kinachochangikwa kinasaidia kufanya mammbo mengi tu.

Mabadiliko yanayokuja ya mwaka 2010 ni ya lazima; lakini tusipoangalia yatakuwa siyo yale tuyatakayo na badala yake tutashangaa mbona haikuwa tulivyotaka. Tutafanya hivyo kwa sababu tutakuwa tumekubali watu wengine wafanya mabadiliko na sisi tubakie pembeni kama wapambanaji watazamaji. Binafsi, sitaki kuta mtazamaji au asiyejua nini kinatokea. Nimeamua kuwa sehemu ya mabadiliko hayo. Aidha kama mtu binafsi au kama taasisi ya KLHN.

Sina hofu sana ya kuizima KLH (nikishindwa kuiendesha) au kutokaa na kuandika makala kadhaa magazetini kwa sababu ya kuona ni kupoteza muda ambao ningeweza kushiriki kwenye mabadiliko na kuwassuport wanaoweza kufanya hivyo. Nadhani, kwa kadiri siku zinavyosogea uamuzi wa kuchagua upande ndivyo unavyokuwa wazi zaidi. Sijui mwenzangu kama unaona urgency niionayo.

Lakini vyovyote vile, tunaitwa kufanya uchaguzi wa kuwa sehemu ya mabadiliko ya kweli badala ya kuwa wachangiaji maandishi tu lakini inapokuja kutumia hazina na mali zetu tunagwaya na hatutaki kufanya hivyo.

Hata hivyo niseme wazi kuwa kuna wale wachache sana ambao kwa muda wote wa JF na KLHN kuwepo wamekuwa wakitoa support ya fedha, muda na mali zao. Hawa ni wale ambao majina yao yatakumbukwa katika umilele wa shukrani. Ni hawa ambao kila kukicha wanafikiria ni jinsi gani wataweza kusaidia vyombo hivi. Ingawa wao wana shughuli zao na bajeti zao, lakini katika kidogo walichonacho wanashikiri katika kuleta mabadiliko. Wengi tunafurahia vyombo hivi kwa sababu ya majasho ya watu hawa wachache ambao hawazidi kumi katika kundi la watu 5000!

Ni hawa ambao wanasimama kama vinara wa mabadiliko ya kweli na makamanda dhahiri wa mapambano ya kuiamsha Tanzania. Ni hawa ambao ni maamiri wa mabadiliko nchini na ambao kwa hakika mioyo yetu haina budi kuwashukuru. Ningependa kuwataja kwa majina lakini wao wanajijua na kwa hakika kutoka kwangu nawapa shukrani ya kweli na ya moyoni kwa kila mchango wao kutusaidia kufanikisha vyombo hivi.

Tukifikia hata kuwa na watu 100 tu ambao wanatupa support nawahakikisha matokeo yake 2010 yatakuwa ni ya kukumbukwa. Vinginevyo, tujue kabisa kupambana na watu wenye "vijisenti" tunajiandaa kuaibika. Tukumbuke kuwa sauti hizi za mabadiliko zitazimika siku moja, na zitakapozimika tusije kubakia na kumbukumbu ya "laiti ninge"

Tuungeni mkono!!

M. M. M.
 
Mwanakijiji,

Tuko pamoja Mkuu, umesomeka loud and clear na nachukua nafasi hii kuunga mkono hoja.....both kwa hali na mali!!
 
Ndugu Mwanakijiji

hayo unayosema ni ya kweli kabisa. Kwangu mimi binafsi ningefurahi kujua modes za operation na ni gharama kiasi gani JF inatumia katika kuendesha shughuli zake ili nijue nitasupport kiasi gani. Pili JF na KLH news inamilikiwa na watu wamoja (have same owners)?
 
Mwanakijiji... Well said!

Zaidi nisisitize kwa watanzania hasa wale mnaopitia hapa JF na KLH News; hatupo kwa maslahi ya watu flani. Ni kwa juhudi binafsi, maumivu makubwa tu, hatuko tayari kutumiwa hata siku moja japo mara nyingi hapa naona watu wakiandika maneno kadha wa kadha ili kuwakatisha tamaa. Wa kutumwa hawaishi!

Jitihada zetu haziishii JF pekee, tunaenda mbali zaidi... Mengi yaonekanayo kuibadili siasa ya Tanzania yanaanzia mbali... Ni vigumu kueleza hapa lakini ieleweke kuwa gharama zinazotukabili zinakuwa kubwa sana. Anachojaribu kukiainisha Mwanakijiji ni wazi kabisa kwa kila mpambanaji.

None is anti-gov't! I have to clear this out for God's sake.

Nimewahi kuwafahamisha wengi kuwa pamoja na gharama za vitisho, mikwara, kebehi, kuishiwa kifedha (wakati mwingine) na muda tunaoutumia bado tunaweza kuhimili mikikimikiki tunayokumbana nayo.

Napenda kuwashukuru wote ambao kwa namna moja ama nyingine wametuwezesha kuweza kufikia tulikofikia na kuwaomba kuendelea kuwa nasi bega kwa bega.

Mchango hata wa Tshs. 5,000 (ambao nina uhakika kila anayeweza kuingia online hapa JF anaweza kuuhimili) unaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa. Kuna ambao waliwahi kuniomba account za NBC, CRDB n.k kwa Tanzania nami nikawapa lakini ni wawili tu ambao walichangia Tshs 200,000 (shukrani zao niliwafikishia).

Pamoja tutafika... Naamini katika ushirikiano.

Invisible

BTW: Mwanakijiji had made a good point on the focus on Election 2010... Think of it!
 
kwa hiyo unamaanisha mchango uwe flat rate tshs 5000 au dola tano au Euro 5 au pound tano. Kwa mwezi, miezi mitatu, sita au mwaka mzima. Pia ningependekeza ile sehemu ya matangazo madogo madogo iwe inalipiwa na pia unaweza kuleta matangazo ya vyama mbalimbali vya siasa kuanzia CCM hadi CHAUSTA nao wakalipia pia. Hizo pesa lau zitakuwa ndogo lakini si haba zitasaidia mambo madogo madogo.

Vinginevyo inakuwa vigumu sana kuchanga kwa kadiri ya uwezo ikiwa hujui budget ni kiasi gani hasa kwa watu ambao tunadeal na mambo ya pesa ingawa kutoa ni moyo na si utajiri.
 
Na pia naomba nieleweke vizuri kabisa sina maana kusaidia vyombo hivi viwili tu, bali kila ambacho unaamini kina thamani kwako (value) basi kiunge mkono. Ni utamaduni huu wa kuunga mkono ndiyo kunafanya mambo fulani kuwezekana.

Nijibu swali la "mama" hapo juu, vyombo hivi viwili viko huru kutoka kingine lakini mahusiano yao ni symbiotic. Hata hivyo kikubwa zaidi ni JF ambayo ndiyo kama merikebu ibebayo kila mtu na KLH ni kama kangawala kaliko pembeni lakini nakenyewe kanapigwa kasikia kuelekea huko huko iliko merikebu na hakachelewi kusaidia Merikebu kubwa.

Gharama za kuendesha vyombo hivi na kulipia kila mwezi na gharama za mipango ya mbeleni ni tofauti sana na hata gharama za muda, vipaji, na nyenzo zinazotumika (kwa mfano invisible anapotumia umeme nyumbani kushughulikia JF, umeme huo anaulipia yeye kama matumizi ya nyumbani lakini faida ni kwa JF) je anarudishiwaje kiasi hicho.

Ndio maana napenda mtindo wa NPR kama mtu anaona kinachofanywa ni cha thamani basi changia kiasi chochote kile na mwingine atafanya hivyo na mwingine atafanya hivyo. Lengo si kuchangia gharama tu ya malipo ya kila mwezi lakini hata kusaidia maisha ya wale wanaochukua muda wao kufanya mambo haya.

Vinginevyo, kutakuwa na faida gani kwa Invisible atumie dola mie nne kulipia JF (alizochangiwa) halafu nyumbani shemeji yetu anaenda kuomba dola mia moja kwa wakwe za chakula?

Tunaposupport vyombo hivi tunawasupport na wale walioko nyuma yake.

Naomba tutambue jambo moja very critical; JF ina mission kubwa na pana zaidi kuliko KLHNews ilivyo sasa. KLHN ina lengo la kuleta habari muafaka wakati habari inapotokea na kuwa chombo huru kabisa cha habari kisichofungamana na wanasiasa au vyombo vya kisiasa.

JF kwa upande wake ina mission kubwa zaidi ambayo ni kuwa uwanja wa fikra, mawazo, maoni, na kichocheo cha mabadiliko ya fikra ambayo yana lengo la kuliamsha Taifa kuwa lile ambalo wengi wetu tunalitamania.

Ni tofauti, lakini lengo ni moja! Kuinua Tanzania na watu wake!
 
Samahani kama mtanielewa vinginevyo, lkn nasisitiza katika kuanzisha kitu sustainable, michango iwe kitu cha dharura. Kutapokuwa JF newsletter au tshirts nikanunua nadhani mchango wangu utakuwa worth than kuchanga pesa. Ni afadhali ninunue newsletter kwa 15000, kuliko kutoa mchango wa 5000. Meanwhile hiyo newsletter inaleta impact kubwa kwani yaweza kuwafikia watanzania zaidi kuliko jf online. Pia nasisitiza huduma ya matangazo ilipiwe. Au mwaonaje?
 
Michango ya wakati wa dharura ni ya wakati wa dharura, kwa hiyo unaweza kushauri kuwa JF iwe inafungwa na kufunguliwa kukitokea kashfa? Wakati ambako hakuna kashfa au hizo capital za kutengeneza tshirt na newsletter nani azitoe?

Wazo hilo ni zuri isipokuwa halizingatii ukweli kuwa ni lazima kuwa na sustainable source of income. Matangazo ya Intaneti ni mazuri kuangalia lakini ukitangaza kampuni ya SIMS hapa au FOMA au Colgatte ya Tanzania ni wangapi walioko nyumbani wanapitia kwenye mtandao kuona matangazo ya biashara ambayo tayari wanayaona kwenye Luninga, radio na magazeti?

Ukitegemea matangazo ya biashara pia inaweza kusaidia hasa haya ya internet kama Adsense na Adready. Lakini ni wangapi kati yetu wanabonyeza bonyeza haya matangazo wanayoyaona hapa au yanakuwa kero? Je tukiweka matangazo mbalimbali kwa wele wenye spidi ndogo ya internet na wanatumia vicafe itakuwaje kwao?

Ni katika kujaribu kufikiria maswali kama haya ndiyo maana wazo la watu kujitokea kuchangia au tuamue tu kuweka JF kuwa ni subscripiton service. Dola 10 kwa mwezi ndio una enjoy JF kusoma thread zozote na kuchangia. Kama unataka kuwa msomaji tu wa kawaida dola 5 kwa mwezi.
 
Na pia naomba nieleweke vizuri kabisa sina maana kusaidia vyombo hivi viwili tu, bali kila ambacho unaamini kina thamani kwako (value) basi kiunge mkono. Ni utamaduni huu wa kuunga mkono ndiyo kunafanya mambo fulani kuwezekana.

Nijibu swali la "mama" hapo juu, vyombo hivi viwili viko huru kutoka kingine lakini mahusiano yao ni symbiotic. Hata hivyo kikubwa zaidi ni JF ambayo ndiyo kama merikebu ibebayo kila mtu na KLH ni kama kangawala kaliko pembeni lakini nakenyewe kanapigwa kasikia kuelekea huko huko iliko merikebu na hakachelewi kusaidia Merikebu kubwa.

Gharama za kuendesha vyombo hivi na kulipia kila mwezi na gharama za mipango ya mbeleni ni tofauti sana na hata gharama za muda, vipaji, na nyenzo zinazotumika (kwa mfano invisible anapotumia umeme nyumbani kushughulikia JF, umeme huo anaulipia yeye kama matumizi ya nyumbani lakini faida ni kwa JF) je anarudishiwaje kiasi hicho.

Ndio maana napenda mtindo wa NPR kama mtu anaona kinachofanywa ni cha thamani basi changia kiasi chochote kile na mwingine atafanya hivyo na mwingine atafanya hivyo. Lengo si kuchangia gharama tu ya malipo ya kila mwezi lakini hata kusaidia maisha ya wale wanaochukua muda wao kufanya mambo haya.

Vinginevyo, kutakuwa na faida gani kwa Invisible atumie dola mie nne kulipia JF (alizochangiwa) halafu nyumbani shemeji yetu anaenda kuomba dola mia moja kwa wakwe za chakula?

Tunaposupport vyombo hivi tunawasupport na wale walioko nyuma yake.

Naomba tutambue jambo moja very critical; JF ina mission kubwa na pana zaidi kuliko KLHNews ilivyo sasa. KLHN ina lengo la kuleta habari muafaka wakati habari inapotokea na kuwa chombo huru kabisa cha habari kisichofungamana na wanasiasa au vyombo vya kisiasa.

JF kwa upande wake ina mission kubwa zaidi ambayo ni kuwa uwanja wa fikra, mawazo, maoni, na kichocheo cha mabadiliko ya fikra ambayo yana lengo la kuliamsha Taifa kuwa lile ambalo wengi wetu tunalitamania.

Ni tofauti, lakini lengo ni moja! Kuinua Tanzania na watu wake!

Mkuu mwanakijiji maoni yangu ni mengi ila naomba nianze na haya machache!

1)JF kama ilivyo nchi yetu...Iko kwenye defining moment! Na tunashukuru kuwa wewe unajaribu kutueleza ama kutuwekea wazi even though umetumia njia ya tofauti kulielezea hili swala.

Ni kivipi basi?
Tunajua kuwa JF is very powerfull in tems of its members na hits! Therefore it makes sense kuwa owners have to be benefited with all of the successes!

JF iko kwenye defining moment kwasababu imekuwa mwiba mbaya kwa mafisadi na pia mwanga na nuru kwa watanzania!

Ni wazi basi kutokana na hilo ndio maana JF imepitia misukosuko mingi ikiwa ni pamoja na kufungiwa kwa muda!

Ni wazi kama ulivyoweka wazi kuwa Mafisadi ni lazima watakuwa wamejaribu kuinunua JF kama walishindwa kuifunga kimabavu!

Pesa wanayo nyingi na uwezo wa kushindana nao hatuna!

Ni uzalendo pekee utakaoyoisimamisha JF na kuendelea kuwa chombo cha kihistoria kwenye siasa za nchi yetu!

JF pia hutumika kama zana ya kuelimishana!

2)Kutokana na hayo basi..Naunga mkono mjadala huu na mawazo ya namna ya kuhakikisha tunaendelea kuwa na uwanja huu huru na mpana wa kihistoria ambao umegeuka kuwa baraza la viongozi kukutana na wananchi wa aina zote na mara nyingi kujihusisha kwenye mijadala yenye kulenga kwenye mustakabali wa nchi yetu!

JF kuna vyama vyote, dini zote, watu wote, wanakijiji, madokta, walimu, wachungaji, masheikh, maprofessa, wabunge, wafanyabiashara etc etc! List ni kubwa!

Ila mara nyingi nimegundua kuwa nyingi za hits hapa ni za wageni na sio members!

Kuna wageni wengi zaidi ya members wanaotembelea JF!

JF ni chombo huru kama sikosei hivyo basi tuwa encourage pia wawe members!

Kama ilivyo kwa wachangiaji wengi..Bado naendela kutafakari mjadala huu na labda kujaribu kuja na mawazo mengi zaid ya namna ya kudeal na issue hii.

To be Continued....
 
Vinginevyo inakuwa vigumu sana kuchanga kwa kadiri ya uwezo ikiwa hujui budget ni kiasi gani hasa kwa watu ambao tunadeal na mambo ya pesa ingawa kutoa ni moyo na si utajiri.
Roughly JF ina-run kwa kitu kama $500 monthly... Ondoa muda wa Mods na gharama zao za uendeshaji. Kwa siku za awali ilikuwa gharama ndogo kwani ilikuwa na traffic ndogo. Kwa sasa hali ishakuwa tofauti na mwanzo... Rekodi za mwezi uliopita ni hits 7,320,628.

Mengine ngumu kueleza kwa sasa. Ila fikiria upande wa pili, hata KLHN inahitaji kuungwa mkono ili ifanikishe shughuli zake. JF na KLHN ni vyombo vyenye wamiliki tofauti kabisa japo wanajuana.
 
CAN I BUY JF? AND IF NOT THEN WHY?
 
Jmushi.. kwa jinsi unavyoona ni kwa kiasi gani unaweza kuinunua JF? ipe thamani halafu tuone hiyo ofa uliyonayo ikoje.
 
Michango ya wakati wa dharura ni ya wakati wa dharura, kwa hiyo unaweza kushauri kuwa JF iwe inafungwa na kufunguliwa kukitokea kashfa? Wakati ambako hakuna kashfa au hizo capital za kutengeneza tshirt na newsletter nani azitoe?

Wazo hilo ni zuri isipokuwa halizingatii ukweli kuwa ni lazima kuwa na sustainable source of income. Matangazo ya Intaneti ni mazuri kuangalia lakini ukitangaza kampuni ya SIMS hapa au FOMA au Colgatte ya Tanzania ni wangapi walioko nyumbani wanapitia kwenye mtandao kuona matangazo ya biashara ambayo tayari wanayaona kwenye Luninga, radio na magazeti?

Ukitegemea matangazo ya biashara pia inaweza kusaidia hasa haya ya internet kama Adsense na Adready. Lakini ni wangapi kati yetu wanabonyeza bonyeza haya matangazo wanayoyaona hapa au yanakuwa kero? Je tukiweka matangazo mbalimbali kwa wele wenye spidi ndogo ya internet na wanatumia vicafe itakuwaje kwao?

Ni katika kujaribu kufikiria maswali kama haya ndiyo maana wazo la watu kujitokea kuchangia au tuamue tu kuweka JF kuwa ni subscripiton service. Dola 10 kwa mwezi ndio una enjoy JF kusoma thread zozote na kuchangia. Kama unataka kuwa msomaji tu wa kawaida dola 5 kwa mwezi.

Ndugu mwanakijiji

nashukuru sana kwa maelezo yako. This is from experience, ukibase sana katika michango ndio mwanzo wa ngome kuvurugika. Utakubalije kupokea mchango from everyone, hapo ndipo utapopokea hata pesa za mafisadi na mwisho wa siku utajikuta uko kwenye chain au web ya ufisadi, it will be a shame. Thats why am skeptical about this kind of fundraising. Long term effects hazitakuwa kwa wachangaji bali kwa reputation ya JF as a whole.

Kujitegemea ndio njia pekee. Kufunga JF si suluhisho, na nadhani kazi ya JF sio kuibua kashfa tu ni kuelimisha pia. I can speak of myself how much I have learnt from JF, thanks to JF members. I was supposed to pay even a subscription fee!
 
Jmushi.. kwa jinsi unavyoona ni kwa kiasi gani unaweza kuinunua JF? ipe thamani halafu tuone hiyo ofa uliyonayo ikoje.
Thamani ya JF ni kubwa kuliko hata fedha kadhaa Mkuu!
Siwezi kutamka namba hapa halafu watu wa viwango vya juu wakanicheka!
Seriously JF should stay alive by any means!
Tatizo ni je tu dollar tuwili tutatu "tujisenti" Tunaweza kupambana na mafisadi kama issue itageuka kuwa simply the issue of survival and "MONEY?"
Hivi vile vijisenti vya Mh Chenge havitatosha kweli?

Roughly JF ina-run kwa kitu kama $500 monthly... Ondoa muda wa Mods na gharama zao za uendeshaji. Kwa siku za awali ilikuwa gharama ndogo kwani ilikuwa na traffic ndogo. Kwa sasa hali ishakuwa tofauti na mwanzo... Rekodi za mwezi uliopita ni hits 7,320,628.

Mengine ngumu kueleza kwa sasa. Ila fikiria upande wa pili, hata KLHN inahitaji kuungwa mkono ili ifanikishe shughuli zake. JF na KLHN ni vyombo vyenye wamiliki tofauti kabisa japo wanajuana.

lets say JF needs $1,500 per months: you need $18,000 per year divide by 5000 JF members is $4 per year! say this is the subscription fee.
 
Ndugu mwanakijiji

nashukuru sana kwa maelezo yako. This is from experience, ukibase sana katika michango ndio mwanzo wa ngome kuvurugika. Utakubalije kupokea mchango from everyone, hapo ndipo utapopokea hata pesa za mafisadi na mwisho wa siku utajikuta uko kwenye chain au web ya ufisadi, it will be a shame. Thats why am skeptical about this kind of fundraising. Long term effects hazitakuwa kwa wachangaji bali kwa reputation ya JF as a whole.

Kujitegemea ndio njia pekee. Kufunga JF si suluhisho, na nadhani kazi ya JF sio kuibua kashfa tu ni kuelimisha pia. I can speak of myself how much I have learnt from JF, thanks to JF members. I was supposed to pay even a suscription fee!
Kabla hawajaifunga mimi nataka niinunue!
Halafu naiita "JAMBO FREEDOM FORUMS" where we lift THE PEOPLE up!
Seriously Mods tuwasiliane!
 
Nafurahi kuwa JF ipo kuelimisha na wengi wanatambua hilo. Kadiri tunavyoishi ndivyo tujifunzavyo.

Kwa wale wenye nia ya kuichangia JF kwa njia yoyote incl KLH News wanaweza kuwasiliana nami via webmaster@jamboforums.com au wawasiliane na Mwanakijiji kwa njia anayoweza kuwapa. Wapo ambao hawajajisajili najua ambao kwao si rahisi kutuma Private Messages (PM) hivyo fursa ya barua pepe bado ipo. Your privacy is highly respected.
 
naweza pata jamboforums email account
 
Back
Top Bottom