Wapambanaji wasambaratishwa

Josh Michael

JF-Expert Member
Jun 12, 2009
2,523
77
Msekwa asema chanzo cha mgogoro ni Richmond

na Mwandishi Wetu



HATIMAYE lile kundi la wabunge wapambanaji wa vita dhidi ya ufisadi, limesambaratishwa na kuondoa tofauti zilizolitikisa Bunge kwa zaidi ya miaka miwili sasa, Tanzania Daima Jumatano imebaini.
Kusambaratika kwa kundi hilo lililojipatia umaarufu mkubwa kumetokana na mkakati maalum uliosukwa wakati wa kikao cha 18 cha Bunge na vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vilivyomalizika mjini Dodoma juzi.
Kundi hilo linaongozwa na Spika Samuel Sitta. Pia yumo Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, Lucas Selelii (Nzega), Christopher ole Sendeka (Simanjiro), Fred Mpendazoe (Kishapu), Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), James Lembeli (Kahama), William Shelukindo (Bumbuli) na Aloyce Kimaro (Vunjo).
Wiki iliyopita, mkakati huo ulifanikiwa kuwazima wapambanaji hao na kuamua kunyamazia ripoti isiyoridhisha ya jinsi serikali ilivyotekeleza maazimio 21 kati ya 23 ya Bunge kuhusu kashfa ya Richmond.
Sitta baada ya kupata taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini na maelezo ya serikali, alitangaza kufunga mjadala wa Richmond bila kujali kwamba serikali imegoma kumwajibisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyestaafu, John Mwanyika na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini. Jukumu la kuwawajibisha lilikuwa mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete.
Upole wa ghafla wa wapambanaji hao, pia ulionekana ndani ya vikao vya NEC vilivyomalizika jana mjini Dodoma kwa sababu zile zile za kudhibitiwa.
Awali kabla ya kuanza kwa vikao vya NEC, wapambanaji hao waliipania ripoti ya kamati iliyoundwa na NEC na kuongozwa na Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, iliyokuwa ikichunguza chanzo na kutafuta suluhu ya mgogoro baina ya wabunge wa CCM.
Wajumbe wengine katika kamati hiyo ambayo imeongezewa muda kuendelea na usuluhishi ni pamoja na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, Bara, Pius Msekwa na aliyekuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahaman Kinana.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka mjini Dodoma, vilisema kuwa baada ya ripoti kusomwa na Msekwa, wabunge wapambanaji hawakujitokeza kwa ujasiri kama kawaida yao kutaka waliokichafua chama watoswe na badala yake waliungana na kuwa wamoja.
"NEC haikuwa na matatizo kabisa, hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kupigilia msumari wa kuipongeza ripoti hiyo, wabunge wote waliikubali japo wapo waliojaribu kutaka kuendeleza mjadala na kujikuta hawaungwi mkono," alisema mmoja wa wajumbe wa NEC.
Kwa mujibu wa habari hizo, Mbunge wa Ukonga, Makongoro Mahanga baada ya kusomwa kwa ripoti ya Kamati ya Mwinyi, aliitaka NEC imsafishe Edward Lowassa kwa madai kuwa alionewa kama ilivyowahi kutokea kwa Mzee Mwinyi alipoamua kujiuzulu nafasi yake ya uwaziri.
Hata hivyo, kauli ya Mahanga ilibezwa na Mzee Mwinyi mwenyewe aliyesema kuwa yeye hakusafishwa na NEC wala chombo chochote.
Baadhi ya wabunge wapambanaji hao waliozungumza na Tanzania Daima Jumatano, walisema ubutu wao safari hii ulilenga kumnusuru Rais Kikwete asipigiwe kura ya kutokuwa na imani naye, na vile vile kujenga mazingira ya kuwasuluhisha Sitta na Lowassa katika kikao cha NEC.
Mbunge wa Vunjo, Kimaro, aliliambia Tanzania Daima Jumatano kuwa serikali imetekeleza maazimio 21 ya Bunge na hakuna sababu tena ya wabunge kuendelea kulumbana kwa jambo ambalo limezungumzwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
"Mimi nadhani kama wabunge tumefanya kazi kubwa na hayo yaliyobaki bado yako chini ya rais, lakini pia tunaangalia wakati huu si wa kuendelea kulumbana, tunapaswa kuwa wamoja ili tuweze kushinda uchaguzi mkuu ujao," alisema Kimaro.
Hata hivyo, baadhi ya vyanzo vya habari vilidai kikao hicho kimerejesha umoja na mshikamano miongoni mwa wanaCCM kueleka uchaguzi mkuu, ingawa kutosuluhishana kwa Lowassa na Sitta kunaweza kuendeleza mgawanyiko utakaokiyumbisha chama kueleka uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma kuhusiana na ripoti ya Kamati ya Mwinyi, Msekwa alisema kamati yao imebaini kuwa chanzo cha mgawanyiko huo ni mgogoro binafsi kati ya Lowassa na Sitta na ulikolezwa zaidi na kashfa ya Richmond.
Alisema vigogo hao waliwagawa wabunge katika makundi mawili, moja likijiita wapambanaji na wengine wakiitwa mafisadi licha ya juhudi zao kukataa kuitwa jina hilo.
"Kamati imebaini kwamba vinara wa mgogoro huo ni Spika wa Bunge Samuel Sitta na Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa. Sitta na kundi lake waliliita kundi la Lowassa mafisadi na kutaka waadhibiwe, huku Lowassa na kundi lake wakipinga kuitwa hivyo," alisema.
Alisema mgogoro huo ulikuwa mkubwa wakati wa mjadala wa Richmond ambapo wabunge wa kundi la Sitta, walikuwa wakichangia kwa kuwataja wale wa kundi la Lowassa kwa kuwaita mafisadi.
"Mjadala wa Richmond bungeni kwa kweli ndiyo kiini cha mgogoro wote uliojitokeza maana kabla ya hapo hakukuwa na kasoro baina ya makundi yoyote ya wabunge wa CCM," alisema.
Msekwa alisema taarifa ya Richmond ndiyo iliyozaa msamiati wa ufisadi ambao tafsiri yake ni rushwa, hivyo kusababisha mgawanyiko uliojitokeza kupitia mijadala ya bungeni.
Alisema wabunge wenyewe walipohojiwa na Kamati ya Mwinyi walikiri kuwa kila kundi linafanya jitihada ili kuhakikisha linawaondoa wenzao madarakani kupitia wagombea ambao walikuwa wakiandaliwa na kila kundi.
"Tuliambiwa kuwa kila kundi lina watu wao wanaowasapoti na kuwatuma wakagombee kwa mahasimu wao ili waweze kuwaondoa madarakani na hili ndilo hasa liliongeza matatizo zaidi kwani hakuna mtu anayependa kuondolewa madarakani.
"Baada ya kubaini kuwepo kwa hali hiyo, tuliamua kukutana na vinara wa makundi hayo kwa lengo la kuongea nao ili kupata suluhu baada ya kukutana na wabunge wote wa CCM kwa lengo la kubaini wahusika wa makundi hayo mawili.
"Kazi ya kuzungumza na vinara wa makundi yote, imekamilika, hivyo tumeongezewa muda ili tuweze kuyaweka makundi hayo katika meza moja na kutafuta suluhu ya kudumu na kuhakikisha tunapoingia kwenye uchaguzi tunakuwa wamoja," alisema Msekwa.
Alibainisha kuwa hakuna hatua zozote zitakazochukuliwa na CCM dhidi ya mwanachama yeyote kutokana na tuhuma ambazo hazijathibitika katika vyombo vya dola.
"Unajua hapa tusichanganye mambo, vitu vingine ni vya ndani ya chama na siwezi kuvisema. Lakini hatuwezi kumuwajibisha mwanachama anayetuhumiwa tu wakati mahakama zipo, kama mtu ataonekana ana makosa atafungwa na hawezi kuwa kiongozi tena," alisema Msekwa.
Kwa mujibu wa Msekwa, kazi ya kamati hiyo inatarajia kukamilika Machi mwaka huu na hatarajii kuwapo kwa kundi litakalokiuka maridhiano hayo. Msekwa alisema kuwepo kwa makundi hayo mawili hakuwezi kukigawa chama hicho kwani kinao wanachama wengi ambao hawajui kama ipo migogoro ya aina yoyote na wamekuwa wakishangaa kuona kupitia vikao vya Bunge ambavyo hurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari. "Tuna wanachama takribani milioni 4.6 kwa nchi nzima kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2008, hivi viongozi hawa wachache wanawezaje kuwapasua wanachama wote hawa? Jambo hili si kweli na kwanza haliwezekani. Linazungumzwa na watu wachache wasiopenda maendeleo ya chama," alibainisha katibu huyo wa Kamati ya Mwinyi.


h.sep3.gif


 
'Sanaa na wasanii' tu!
Ni usanii mtupu hapa na pia hapa naona kama vile udanganyifu kwa Taifa letu na pia mimi nadiriki kusema kuwa CCM waje na waseme kuwa hakuna fisadi hata mmoja na hata hawa wapiganaji watakosa cha kusema na neno fisadi sio lao ni la CHADEMA
 
Back
Top Bottom