waomba kukusanya mabilioni ya ufisadi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,825
287,845
Tusubiri tuone kama utasainiwa mkataba mwingine wa kifisadi wa kuwalipa haya makapmuni 80% ya wakachokusanya. Na si ajabu kuna makampuni ya waheshimiwa na 'takrima' itatembezwa kama kazi

11 waomba kukusanya mabilioni ya ufisadi
Shadrack Sagati
Daily News; Saturday,March 29, 2008 @00:01

KAMPUNI 11 za udalali zimeomba zipewe kazi ya kukusanya Sh bilioni 199 zilizochotwa serikalini na ‘wajanja’ kupitia Mpango wa Uagizaji wa Bidhaa Nje (CIS), lakini zikatumika kwa matumizi mengine bila kurudishwa.

Wizara ya Fedha na Uchumi inalazimika kutumia madalali kukusanya fedha hizo kutokana na watu waliochota fedha hizo kwa kisingizio cha kuagiza bidhaa nje kugoma kuzirudisha kama mkataba ulivyowataka kufanya.

Jana ilikuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha zabuni za kufanya kazi hiyo ya kukusanya mabilioni hayo ya fedha. Hadi kufikia saa nne jana, kampuni 11 ndizo zilikuwa zimewasilisha maombi ya zabuni hiyo.

Kampuni itakayopewa kazi hiyo italazimika kukusanya madeni hayo kutoka kwa watu na kampuni zipatazo 916 ambazo zilikopeshwa Yeni ya Japan Bilioni 16 (Sh bilioni 199). Watu hao wamegoma kurejesha fedha hizo, kitendo kinachotafsiriwa kuwa ni ufisadi dhidi ya fedha za umma.

Kampuni za udalali zilizoomba kufanya kazi hiyo ni Yono Auction Mart, Majengo Auction Mart, Rhino Auction Mart, Msolopa Investment Co Ltd, Bani Investment Ltd, Kitindi Co Ltd, GM Auction, Mpoki & Associates Advocates, Nakara Auction Mart, Aslyla Attorneys & TMK Enterprises na Rex Attorney.

Kila kampuni ambayo imeomba kufanya kazi hiyo imeambatanisha dhamana ya Sh milioni mbili na mapendekezo ya riba inayoombwa ilipwe kutokana na kiasi cha fedha itakachokusanya.

“Kwa zabuni hii inatakiwa kampuni moja tu ya kufanya kazi hiyo…kama itataka kushirikiana na kampuni nyingine inaruhusiwa, lakini Wizara inataka kazi ifanywe na kampuni moja tu,” alisema ofisa mmoja wa Sekretarieti ya Bodi ya Zabuni ya Wizara ya Fedha na Uchumi.

Baada ya kupokea zabuni hizo, Sekretarieti ya Bodi ya Zabuni ya Wizara hiyo itaanza kufanya mchanganuo kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kabla ya kupata kampuni sahihi ya kufanya kazi hiyo.

Wizara ya Fedha na Uchumi imeitisha zabuni hiyo huku tayari ikiwa imeshatishia kuwaanika hadharani na kuwachukulia hatua za kisheria watu waliochota fedha hizo kama hawatalipa deni hilo ndani ya miezi mitatu tangu tangazo hilo lianze kutoka kwenye vyombo vya habari.

Miongoni mwa wadaiwa hao wamo wafanyabiashara maarufu nchini, wanasiasa wakiwamo wabunge na baadhi ya maofisa wa serikali. Gazeti hili lina habari kuwa baadhi ya wadaiwa hao wengine walitumia kampuni bandia kujipatia fedha hizo, hali iliyosababisha kushindwa kuagiza bidhaa hizo kama ilivyotarajiwa na serikali. Mabilioni hayo yalichotwa kuanzia miaka ya 1980 mpaka mwaka 1993.

Fedha hizo zilitolewa na wahisani mbalimbali chini ya mpango huo wa CIS ili kuipa uwezo serikali wa kuimarisha uchumi wake, ikiwamo Japan ambayo imekuwa inatoa misaada mingi kwa Tanzania.

Lengo la wahisani kutoa fedha hizo ilikuwa kuzipatia taasisi, kampuni, viwanda na biashara mbalimbali uwezo wa kuagiza bidhaa na malighafi kutoka nje kwa kuwa wakati huo nchi ilikuwa na upungufu mkubwa wa fedha za kigeni.

Hata hivyo, wafanyabiashara wengi waliochukua fedha hizo ambazo zilitolewa kama mkopo wa masharti nafuu ambao hauna riba, walishindwa kuagiza bidhaa yoyote kutoka nje kama ilivyokusudiwa na serikali badala yake wakazitumia fedha hizo kwa manufaa binafsi.

Baadhi ya wafanyabiashara wamewahi kuchunguzwa na taasisi mbalimbali ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) juu ya namna walivyochota mabilioni hayo kwa njia ya uongo na kushindwa kuyarejesha serikalini.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom