Wanawake mmepata mtu wa kuwasemea na kuwainua, sasa achaneni na ajenda za pesa mboga, njooni na ajenda muhimu!

Mwadilifu Mdhulumiwa

JF-Expert Member
Jul 22, 2021
418
630
Kheri kwenu kina mama wote!

Niende moja kwa moja kwenye mada.

Natumaini sote tunatambua Rais na kiongozi wan chi yetu kwa sasa ni Mwanamke, kama jinsi alivyojipambanua mara baada ta kula kiapo kuwa Yeye ndiye Rais wa JMT ambaye kimaumbile ni mwanamke, nasi tulimpokea na tunaendelea kumuunga mkono.

Hata hivyo katika kipindi chote hiki Rais wetu amejikita sana kwenye mada ya haki za wanawake, Haki sawa kati sawa kati ya mwanaume na mwanaume, mwanamke kuaminiwa na kupewa fursa na majukumu sawa na mwanamke.

Katika siku ya demokrasia duniani, rais alienda mbali na kuwataka wanawake wa Tz kuhakikisha wanaweka Rais wa kwanza mwanamke madarakani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2025. Hapa Rais aliweka wazi mpango wake wa kugombea tena mwaka 2025 au kusimamisha mgombea mwanamke kwa uchaguzi huo, huku akiwasihi pia wanawake kuchangamkia fursa hizo za uongozi nchini.

Kwa ufupi haya yote yameamsha aina flani ya kampeni inayoitwa usawa wa kijinsia.

Lakini kwa upande mwingine tunaona mwitikio wa wanawake umekuwa na tafsiri tofauti, kuna wengine wameona ndio fursa ya kuanzisha kiburi na maugomvi na waume zao majumbani kwao, kuna wengine wameona ndio muda wa kuvurumisha kampeni ya taulo za kike nchi nzima, kuna wengine wameona ndio muda wa kufanya kila aina ya mipango kupata teuzi za uongozi, kuna wengine wameacha shughuli na biashara zao muhimu sasa wamejiingiza kwenye siasa, na mambo mengine meengi ambayo hata hivyo hayawezi kuwajengea msingi imara utakaowahakikishia hizo haki zao kuendelea kuwepo hata siku asipokuwepo rais mwanamke pale Ikulu.

Najaribu kuwafananisha wanawake na kisa cha Mzungu na Mwafrika nilichowahi kusimuliwa na babu yangu mmoja wa kufikia huko miaka ya nyuma, sasa ni marehemu R.I.P, Babu! …..Katika kisa kile Babu alinieleza alivokuwa akimsifu Mwalimu Nyerere na hata kusema Nyerere hakustahili kuzaliwa Afrika kwakuwa ana akili kama ya wazungu! Katika kisa hicho Babu alieleza sababu ya sisi wafrika kuwa nyuma kimaendeleo ukilinganisha na wazungu ambao walishapiga hatua mbali toka miaka mingi sana!

Akisimulia kisa hicho alisema chanzo cha umaskini wa sisi wafrika ni tangu asili ya kuumbwa kwetu akieleza kuwa Mungu alipomuumba Mzungu na Mwafrika aliweka vitu viwili mbele yao, vitu hivyo ni gari (kuashiria utajiri) na Ngoma (kuashiria umaskini), na kisha akawaweka Mzungu na Mwanafrika umbali wa mita 100 kutoka vilipo, akawaambia wakimbilie kila mmoja atakachowahi ndicho chake!......Looh! Mwafrika alitoka nduki ya uhakika na kumuacha Mzungu mbali, lakini cha ajabu alipofika pale akachagua ngoma na kurukia juu yake, akaanza kuipiga na kucheza! Mzungu alipofika kwa raha zake akaingia kwenye gari alipoanza kuitoa ndipo Mwafrika akabaki na butwaa, lakini uchaguzi ukabakia kwa kila mmoja kuwa hivyo!

Japo kisa hiki ni cha kufikirika lakini kinatufundisha ukweli kuwa wakati mwingine unaweza kuwa unabakia kuwa nyuma kimaendeleo si kwasababu hujiwezi bali ni kwasababu unahangaika na vitu vidogo!

Hapa ndipo nataka kuwashtua wanawake mmeshapata Rais mwanamke, kwa experience yake anayajua madhila na shida zote mnazopitia katika jamii. Hata zile shida asizozijuwa pengine kutokana na tofauti ya mazingira na mapito alikopita yeye, bado ni rahisi kumuelesha kwa lugha na sentesi fupi kabisa na mkaelewana!

Hivyo basi hii ni fursa muhimu kwenu kujipanga mtoke na ajenda muhimu zitakazo wahakikishia kile mlichokuwa mkikihangaikia kwa miaka nenda rudi.

Hatuwezi kuuondoa mfumo dume uliopo nchini kwetu kama hatutaweza kutengeneza katiba mpya inayolazimisha kuuondosha mfumo . Mwelezeni Mh. Rais na mwanamke mwenzenu kwamba ubovu wa katiba ya sasa ndio chanzo cha kuwafikisha hapa mlipo. Mpeni ukweli huu kuwa hakuna jambo litakalompatia heshima kubwa katika historia na ramani ya Tanzania na dunia nzima kama kuliachia Taifa lake katiba mpya!

Rais mwenyewe ameshakiri kuwa bado hamjapata Rais mwanamke , kwakuwa aliyeko Ikulu sasa ni kwa kudra za Mungu! Sasa pazeni sauti hili jambo liwe takwa la kikatiba, Kwamba kila baada ya muhula wa miaka 10, kuwe na mbadilishano wa wa uongozi kati ya mwanamke na mwanaume, kuanzia ngazi ya mtaa,kata, jimbo hadi kiti cha urais! Iwe hivyo pia kwenye kamati za bunge, Bodi za wakurugenzi katika taasisi na mashirika ya umma, muundo mahakama, muundo wa wizara, baraza la mawaziri nchini kote iwe hivyo.

Bila kusahau suala la Elimu kwa wanawake, kuna wanawake wengi walikatisha masomo kutokana na ujauzito na sasa walishaonja maisha wakagonga mwamba, wamebakia mtaani wanaungua na maisha! Mwombeni Mh Rais na mwanamke mwenzenu awarudishe shuleni, kuwepo na mpango wa kuwapa elimu bila kujali umri na wapate uwezeshaji wa mitaji ili wajiajiri na shughuli halali chini ya mazingira wezeshi na sio kuwapa muda na amri waondoke tu wanakofanyia shughuli zao za kuuza miili pale uwanja wa fisi na vijiwe vingine nchini kote!

Acheni utamaduni wa kwenda tu kujumuika na kucheza nae ngoma kwenye makongamano huku mkiwa mmeshona vitenge na kujifunga vibwebwe, mkionyesha furaha kubwa wakati hamuongei chochote ilihali mna matatizo lukuki!

Ongeeni na Mwanamke mwenzenu aziamrishe halmashauri kote nchini ziongeze fungu la uwezeshaji mitaji kwa wakina mama katika mfumo mzuri usio na urasimu kama hivi sasa, kuna halmashauri hazitowi mikopo kwa vikundi vyakina mama na hakuna sababu za msingi, eti wamepeleka hela kwenye miradi ya mwenge, huku ni kuchezea maisha ya wakina mama!

Pazeni sauti kukataa utaratibu uliopo sasa halmashauri nyingi katika utoaji wa hiyo mikopo sio rafiki, ubadilishwe mwanamama yeyote aruhusiwe personaly kwenda kuomba mkopo halmashauri na sio lazima mpaka wajiunge kikundi kuna wakina mama wengine hawapo serious na maisha ya utafutaji, hawa wanawakwamisha wenye utayari. Pia hata wakati wa urejeshaji wa mikopo kuna wengine wanaleta usumbufu na hivyo kuwagharimu wenzao.

Akina mama mna ushawishi mkubwa sana ndani ya jamii, mkiwezesha mabadiliko ya katiba haya yote yatakuja yenyewe, acheni kuwasikiliza wanaotoa sababu nyepesi eti takwa la katiba sio takwa la wananchi ni takwa la wanasiasa!

Hii kauli si ya kweli hata chembe, ni uoga wa wanasiasa wanaoamini kuwa katiba ikiwekwa vizuri ulaji wao usio na maslahi kwa taifa letu utakatwa! Ubovu wa katiba ya sasa unagusa makundi yote tangu wanawake, watoto wenu, waume zenu, baba na mama zenu wastaafu na vizazi vingine vinavyokuja.

Hivyo kwa nguvu ya kina mama tunaweza kupata katiba mpya sababu akina mama ni jeshi kubwa kama mnavyojiita, sasa onyesheni hili kwa vitendo tupate katiba mpya! Kumbukeni mama ndiye mzazi wa jamii nzima, ni huyohuyo ndiye mlezi na kiongozi wa jamii aliyoizaa, sasa isaidieni jamii mliyoizaa iishi katika misingi na maadili mema, hili litawezekana chini ya matumizi ya katiba bora inayokwenda na wakati na kukidhi mahitaji ya jamii nzima kwa haki na usawa!

ANGALIZO: Akina mama pamoja na kuendesha kampeni hii mliyoianzisha, nawasihi msigombane na akina wanaume, mkumbuke kuwa mfanikishaji wa mipango yoyote ya mwanamke ni mwanaume! Hivyo endeleni kuwaheshimu na kushikamana nao huku mkiwatumia wao kufanikisha mipango hiyo!
 
Back
Top Bottom