Wanatutawala badala ya kutuongoza

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Wanatutawala badala ya kutuongoza

Padri Privatus Karugendo Disemba 17, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

KWENYE Raia Mwema, (toleo lililopita ukurasa wa kwanza) kulikuwa na habari iliyosema: Mpasuko wa Kitaifa, Ufisadi Mkubwa – Kanisa lashituka: Askofu Kilaini asema nchi inahitaji maombi isiangamie.

Kuyumba kwa mshikamano wa kitaifa kutokana na kuibuka kwa mgawanyiko katika jamii, ufisadi na mauaji ya watu wasio na hatia ni miongoni mwa mambo yaliyolishitua Kanisa Katoliki nchini na sasa limeamua kufanya ibada maalumu nchi nzima kumuomba Mungu ainusuru nchi isidizi kuangamia…”

Habari hii inaendelea kuelezea yale aliyoyasema Askofu Kilaini: “Tumeanza misa maalumu kila mahali kuliombea taifa, viongozi na wananchi wetu. Tunamuomba Mungu tuwe na amani, atuepushe na mpasuko wa kidini na kikabila ambayo imeanza kuikumba nchi yetu… Tumesikia sasa kuna mambo mazito kama haya ya ufisadi mkubwa wa kutisha wa mabilioni ya fedha na tunaambiwa kuwa kuna mabilioni mengine hayajatajwa. Pia hivi sasa kuna haya mauaji ya binadamu wenzetu maalbino kwa kuwa kuna watu wanatafuta viungo vyao kupata utajiri. Hatuna silaha ya kukabiliana na matatizo haya ndiyo maana sasa tunamuomba Mungu”.

Maelezo ya Askofu Kilaini, na ya maaskofu wengine wanayoyatoa kwenye matukio mbali mbali juu ya kuyumba kwa maadili katika taifa yanaonyesha wazi kwamba kwa njia moja ama nyingine Kanisa limeshindwa kuingiza ushawishi wake ndani ya jamii.

Maana kati ya mafisadi na wala rushwa kuna waumini wazuri wa Kanisa Katoliki, hata baadhi ya wale wanaoendesha mauaji ya maalbino ni wakatoliki. Lakini pia ndoa nyingi za wakatoliki zimesambaratika na maadili ya watoto hayana msimamo wala mfumo. Kanisa limeshindwa kuhubiri na kuyaishi mafundisho ya Yesu Kristu. Nafikiri hili ndilo jambo la kujadiliwa. Sala ni muhimu na kila binadamu anahimizwa kusali kwa muumba wake. Hivyo Askofu Kilaini, anaposema kwamba Kanisa linaanzisha ibada za kuliombea taifa, ni kitu kinachoeleweka.

Lakini hoja nzito inayojitokeza hapa ni kwamba kusali bila kubadilisha mazingira na mifumo ni kutaka kulazimisha miujiza isiyowezekana. Ni sawa na kukata miti ovyo, kuchoma moto na kisha kuendesha ibada na sala ya kuomba mvua. Ni miujiza isiyowezekana!

Haiwezekani rushwa na ufisadi vikatokomea kwa sala na ibada, bila kutibu chanzo cha yote haya. Hatukufika hapa tulipo kwa bahati mbaya. Kuna sababu, kuna historia, kuna chimbuko. Bila kushughulikia chimbuko, ni sawa na kumeza dawa za kutuliza maumivu bila kuutibu ugonjwa wenyewe.

Kwa mpango wake wa kuumba Mungu, alitupatia kila kitu. Alitupatia akili, utashi na uwezo wa kuyatiisha mazingira yanayotuzunguka. Kinachohitajika ni mifumo mizuri, uongozi bora na imani inayochimbuka ndani ya jamii yenyewe. Hii ni sala kamili isiyohitaji hata nyumba ya ibada!

Kama viongozi wa Kanisa wenyewe wameanza kuona kwamba Kanisa linashindwa kuingiza ushawishi ndani ya jamii, kuna haja ya kuwa na mjadala. Tukae chini na kujadili kwa uhuru. Ni viruri ikieleweka kwa waumini wote na Watanzania wote kwa ujumla kwamba tunapojadili mambo ya ubinadamu wetu, mambo ya imani yetu, mambo ya taifa, hatuhitaji ruhusa ya mtu yeyote yule.

Hatuhitaji ruhusa ya Askofu wala ruhusa ya Baba Mtakatifu. Tunatumia uhuru wa watoto wa Mungu! Binadamu wote ni sawa! Hakuna binadamu bora kuliko mwingine. Ulaya, Marekani na kwingineko duniani jambo hili liko wazi, giza limebaki Afrika! Ni lazima kutoka gizani na kutembea ndani ya nuru ya Muumba wetu. Hivyo kwa mjadala wa maisha ya binadamu, kila mtu ana haki sawa. Pia ndani ya taifa la Tanzania, sote tuna haki sawa. Hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine. Hivyo tunapojadili mambo ya kitaifa ni lazima tuyajadili bila woga na kwa uhuru wote.

Hivyo ninaandika makala hii kwa uhuru wote na ninawashawishi waumini na Watanzania wote kukubali kuingia ndani ya mjadala huu. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kutuzuia kufikiri na kuandika. Wanaweza kutufukuza, wanaweza kutufungia, lakini hawawezi kutuondolea imani yetu. Imani yetu, ndicho kiburi chetu. Wa kuipima imani hii, ni Mungu peke yake! Enzi za kuendesha kanisa kwa siri kubwa, umepitwa na wakati. Enzi za Roma, kuwasikiliza maaskofu peke yao zimepitwa na wakati. Kanisa ni la waumini wote!

Ingawa bado kuna mambo mengi ndani ya Kanisa na hasa Kanisa la Afrika, yanaendeshwa kwa siri, ni wakati sasa wa kushinikiza kuondolewa kwa siri hizi. Yesu mwenyewe, alisisitiza Uwazi ndani ya mfumo aliouanzisha:

“ Basi, msiwaogope watu hao. Hakuna cho chote kilichofunikwa ambacho hakitafunuliwa, wala kilichofichwa ambacho hakitafichuliwa. Ninalowaambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong’onezwa, litangazeni kwa sauti kuu…” (Matayo 10:26-27)”.

Kama huo ndio ulikuwa msimamo ya Yesu, inakuwa vipi Kanisa, na hasa Kanisa Katoliki, linaendeshwa kwa mfumo wa siri? Leo, niombe niandike mawazo jumla, Lakini makala zinazofuata nitatoa mifano ya “Usiri” ndani ya Kanisa Katoliki. Nitatoa mifano hai, ili itusaidie kupiga hatua. Nitafanya hivyo, kwa vile ninalipenda Kanisa na ningependa ushawishi wake upenyeze maana Ujumbe wa Yesu Kristu ni wa binadamu wote.

Hivyo basi hoja yangu kwanza ndani ya mjadala huu wa kwanini ushawishi wa Kanisa unakwama kupenyeza ndani ya jamii yetu, ni kwamba viongozi wetu wa Kanisa wanatutawala badala ya kutuongoza. Pia hapa leo nitaongelea kwa ujumla, ila makala zinazofuata, nitatoa mifano na majina ya viongozi wa Kanisa wanaotutawala badala ya kutuongoza.

Yesu Kristu, alikuwa kiongozi na wala hakuwa mtawala. Yeye alionyesha njia na yeye alikuwa njia yenyewe. Alitaka wale wanaopenda kumfuata, wabebe misalaba yao na kumfuata. Hakuwatawala wafuasi wake, bali aliwaongoza: “ Mimi ni njia, ukweli na uzima…”( Yohana14: 5-6).

Yesu Kristu, alionyesha wazi kwamba kiongozi, mbali ya kuwa ni njia, ni mtu anayeonyesha njia sahihi ya kupita, kiongozi pia ni mtumishi. Si mtawala wala mtu wa kutukuzwa, bali ni mtumishi wa wote: “Hapo mama ya wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake huku akimwomba kitu…..Ahidi kwamba hawa wanangu watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utawala wako. Yesu, akajibu, Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi? Wakajibu Tunaweza. Yesu akawaambia, Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia na kushoto kwangu, si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu. Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia wale ndugu wawili. Hivyo Yesu akawaita , akawaambia, ‘ Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa nguvu na wakuu hao huwamiliki watu wao. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila yeyote anayetaka kuwa mkubwa kati yenu sharti awe mtumishi wa wote; na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu. Jinsi hiyo hiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwakomboa watu wengi” (Matayo 20: 20-28).

Kama huo hapo juu ndiyo mfumo wa Yesu wa Nazareti, mfumo wa kiongozi kuwa mtumishi, haiwezekani ukawa sawa na mfumo wa leo ambamo viongozi wetu ni watawala. Ambamo viongozi wetu si watumishi. Sina haja ya kuelezea zaidi, maana ni mtu gani anayeweza kuamini kwamba maaskofu wetu ni watumishi wetu? Hata mwonekano wao ni wa kitawala, mavazi yao, kofia, fimbo hadi pete ni ishara ya utawala wa Wafalme wa Kale kule Ulaya.

Hawa ni watawala kama watawala wa mataifa, hivyo ni vigumu kwao kuupenyeza ushawishi wa Yesu Kristu wa Nazareti. Hivyo kama tunataka mabadiliko, si kuanzisha ibada na sala, bali ni kuufuata mfumo wa Yesu. Ni viongozi kukubali kuongoza badala ya kutawala.

Katika mfumo wa Yesu Kristu wa Nazareti, kiongozi ni njia, ni mtumishi na ni mwanga na chumvi:
“Ninyi ni kama chumvi kwa dunia! Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na kitu gain? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni mwanga wa Ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa chungu, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” ( Matayo 5:13-16).

Kwa vile viongozi wetu wa kanisa wameshindwa kuonyesha njia, wameshinwa kuwa watumishi, wameshindwa kuwa chumvi na mwanga, wakawa kama watawala wengine wa dunia hii, ndiyo maana wameshindwa kupambana na mambo mengine ya dunia hii. Wameshindwa kupambana na chuki, uonevu, ubaguzi na unyanyasaji. Ndiyo maana, pamoja na makanisa kusambaa nchi nzima, bado kuna rushwa, ufisadi na mauaji ya maalbino.

Kuna ushahidi wa kutosha kwamba kuna baadhi ya maaskofu wanaotunza chuki rohoni mwao zaidi ya miaka 10. Maaskofu kama hawa wanaotunza chuki, hawawezi kuwa na nguvu za kupambana na maovu ya dunia hii. Pia kuna ushahidi wa kutosha kwamba baadhi ya maaskofu wanatoa adhabu zinazokwenda kinyume na haki za binadamu. Katika hali ya kawaida, kila mfungwa, hata kama ni jambazi sugu au ameua, akiwa kifungoni anapatiwa mahitaji muhimu ya binadamu. Anapata malazi, chakula na matibabu. Lakini maaskofu, wakimhukumu mtu kifungo hawampatiii chakula, malazi na matibabu, na mbaya zaidi hawampatii hata chakula cha kiroho.

Mtu anatelekezwa na kunyimwa haki za msingi za binadamu. Ni ukatili hata kuzidi ule wa watawala wa Mataifa. Mtu mwenye ukatili wa aina hii, hawezi kupenyeza ushawishi wa kuondoa ukatili ndani ya jamii.

Maaskofu wetu, wanapenda sana kuishambulia serikali, wanayaona sana mapungufu ya serikali. Wanaviona vibanzi ndani ya macho ya watu wengine, wakati wao pia wana vibanzi ndani ya macho yao. Wakitaka waeleweke, wakitaka kupenyeza ushawishi wao ndani ya jamii yetu, ni bora wakayasafisha macho yao kwanza kabla ya wengine.

Hivyo basi kama tunataka ushawishi wa Kanisa, upenyeze ndani ya jamii. Kama tunataka ujumbe wa Yesu Kristu, wa haki, wema na huruma, uyaongoze maisha ya Watanzania, ni lazima tuwashinikize viongozi wetu wa Kanisa waachane na utawala. Tuwashinikize ili watuongoze, tuwashinikize ili wawe watumishi, tuwashinikize wawe chumvi na mwanga wa Taifa. Ibada na sala haziwezi kutusaidia kama mifumo mibovu haibadilishwi.
 
Viongozi wetu wengi si viongozi wazuri kwani hata wengine wameshindwa kuongoza familia zao. I accordingly agree with you kwamba wanatutawala. Kuongoza is out of their practice ingenuinely.
 
Back
Top Bottom