Wanatuibia, kisha wanatukebehi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,825
287,849
Wanatuibia, kisha wanatukebehi

Evarist Chahali, Uskochi Mei 7, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo


NILIRUDI nyumbani kwa ziara ya masomo Oktoba 2005 wakati Taifa likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu.

Kwa hakika ulikuwa ni muda mwafaka sana kwani sehemu ya utafiti wangu inahusu ushiriki wa wananchi kwenye siasa, na haikuwa vigumu kumaizi kwamba Watanzania wengi wana mwamko mkubwa wa kisiasa.

Pamoja na jitihada za vyama vya upinzani kuelezea mapungufu ya CCM, ilionekana dhahiri kuwa mgombea wa chama hicho tawala, Jakaya Kikwete, alikuwa na sifa ya ziada kulinganisha na wagombea wengine: mvuto wa kisiasa. Yayumkinika kuhitimisha kwamba kilichompatia Kikwete ushindi mkubwa katika uchaguzi huo si ubora wa sera za CCM bali ni mvuto huo uliochanganyika na kauli zake zilizoashiria anatambua nini kinawasibu Watanzania wenzake, nini kifanyike kuwarejeshea matumaini na hatimaye kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya neema.

Hata hivyo, miongoni mwa mambo yaliyonipa hofu kuhusu CCM ni wingi wa ahadi zilizokuwa zinatolewa wakati wa kampeni na baada ya ushindi ambazo kwa hakika utekelezaji wake ungehitaji muda mrefu zaidi ya miaka mitano iliyokuwa ikiombewa ridhaa kwa wananchi.

Pamoja na wasiwasi huo, nilijaribu kujifariji kwamba iwapo utekelezaji wa ahadi hizo ungeanza mara baada ya CCM kurejea madarakani, basi kuna uwezekano wa angalau nusu yake kuwa zimetimia ifikapo mwaka 2010. Kwa bahati mbaya, hadi sasa nyingi ya ahadi hizo zimebaki kuwa ahadi tu kama wasemavyo Waingereza: a promise means nothing until delivered.

Tatizo la kwanza kabisa lililojenga picha kwamba utekelezaji wa falsafa ya kasi, ari na nguvu mpya ungepata wakati mgumu kutimia ni pale ilipotangazwa kabineti ya zaidi ya mawaziri na manaibu wao 60 huku ikijumuisha baadhi ya sura zinazosifika zaidi kwa ngebe, uzembe na ubabaishaji kuliko utumishi bora.

Ukubwa wa kabineti ulifanya baadhi ya wachambuzi wa siasa kuhoji ni namna gani Awamu ya Nne ingeweza kusimamia vizuri malengo yake, kwani japo wingi wa watu unaweza kurahisisha utekelezaji wa majukumu, unaweza pia kuwarahisishia wazembe kujificha kwenye msitu huo wa watu.

Kwa vile Watanzania wengi walikuwa na kiu ya maendeleo, ukubwa huo wa baraza haukuwasumbua sana hasa baada ya kuelezwa kwamba ili Tanzania ifike inakotaka, ni lazima kuwe na timu kubwa ya wawajibikaji wenye kuamini kuwa Maisha Bora kwa Kila Mtanzania si kaulimbiu tu ya kuingilia Ikulu bali jambo linalowezekana.

Ziara za Kikwete katika kila wizara kuwapa somo mawaziri wake, na semina elekezi huko Ngurdoto zilitoa ishara kwamba hatimaye Tanzania inaelekea kwenye neema. Hotuba zake kadhaa za zilimtambulisha kama mrithi halisi wa Julius Nyerere, kwani alizungumza lugha ya mtu mwenye uchungu na nchi yake, anayejua matatizo ya anaowaongoza na mwenye dhamira ya dhati kuwasaidia.

Japo kauli kwamba anawafahamu wala rushwa na anawapa muda wajirekebishe iliwafanya baadhi ya watu kuanza kuhisi kuwa huenda ni yaleyale ya Benjamin Mkapa kuunda Tume ya Warioba na kisha kukalia mapendekezo yake, wengi wetu tuliamini kuwa anatengeneza visheni ya namna fulani ambayo ingeweza kuwa ya mafanikio makubwa usoni.

Nimerudi tena nyumbani takriban miaka mitatu baadaye na kukuta mambo yakienda mrama. Kinachosikitisha zaidi, ile kaulimbiu ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania Yanawezekana ni kama imekwisha umuhimu wake: kwa walioibuni na kwa walioahidiwa.

Je ilikuwa "changa la macho" au utekelezaji wake umeshindikana? Kibaya zaidi, wahuni kadhaa wakaanza kugeuza mambo na kudai eti "maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezi kupatikana kwa kukaa vijiweni"! Haya ni matusi ya mchana kweupe kwa wakulima wanaopinda mgongo mashambani na kuishia kukopwa mazao yao na vyama vya kijambazi vya ushirika, au kwa akinamama wanaotembea maili kadhaa kusaka maji au wanafunzi wanaokaa chini shuleni kwa ukosefu wa madawati.

Binafsi naamini kwamba kauli ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania Yanawezekana ilikuwa kauli-thabiti kutoka kwa watu waliokuwa wakifahamu fika kwamba Tanzania si nchi ya kuwa masiini kiasi hiki wakati tuna utajiri mkubwa unaotafunwa na majambazi wachache huku wananchi wengi wakiwa hawana uhakika na mlo wao wa siku.

Tatizo kubwa zaidi linaloikabili Tanzania kwa sasa ni ufisadi, lakini ni dhahiri kwamba kasi ya kushughulikia tatizo hili ni ya kusuasua mno na ni vigumu kutarajia matokeo mazuri huko mbele hasa ikizingatiwa kwamba muda si mrefu wanasiasa wetu wataanza kuhangaika kutushawishi tuwarejeshe madarakani (kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010).

Itakuwa vigumu sana kwao kujihangaisha na vita dhidi ya ufisadi kwani wengi wa mafisadi ni haohao wanaotarajiwa kufadhili kampeni za wanasiasa hao, na kuwabana kwa namna yoyote ile itapelekea wagome kutoa ufadhili.

Kuna mambo yaliyo ndani ya uwezo wa viongozi wetu ambayo utekelezaji wake unahitaji dhamira tu. Kwa mfano, kuna jamaa mmoja anayefahamika takriban kila kona ya Dar es Salaam kuwa anatumia vijisenti vyake vya kifisadi kuwaambukiza ukimwi mabinti.

Mtumishi huyo wa taasisi moja nyeti ya fedha, anayesifika kwa kuhonga magari mekundu, amekwisha kutajwa hadi kwenye hotuba mkoani Tabora katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, na tuliambiwa kuwa maharamia wa aina hiyo wanaundiwa sheria ya kuwabana lakini hadi leo "anapeta" na sheria tuliyoahidiwa imeendelea kubaki ahadi tu.

Baradhuli huyu ana bahati sana kuzaliwa Tanzania kwani laiti angekuwa nchi za "wenye hasira" angekuwa amekwisha kwa kupigwa mawe kwa vile ni kiumbe hatari zaidi ya yule mtoto anayedaiwa kukutwa na kichwa cha binadamu pale Muhimbili.

Mafisadi wanafahamika, sheria na mamlaka za kuwabana zipo, hivyo hakuna haja ya kusubiri hadi vyombo vya habari viwaweke hadharani na waishie kujiuzulu tu badala ya kufukuzwa kazi au kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wengine baada ya kujiuzulu wanaandaa mapokezi ya kufuru kana kwamba wanatubeza sie waliotuibia. Wenye makosa hapo si hao wenye nyodo za fedha za kifisadi bali wale waliowapa uhuru wa kufanya hivyo, kwani laiti wangetupwa rumande wasingethubutu kutukebehi kiasi hicho.

Hivi CCM itazungumza nini mwaka 2010 kuwaaminisha Watanzania kwamba inachukia ufisadi na haina urafiki na mafisadi? Haiwezekani chama makini kitumie muda mwingi zaidi kujitetea (defensive) kuhusu ufisadi badala ya chenyewe kuwa mstari wa mbele katika mapambano (offensive).

Baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi bado wana nyadhifa za juu kwenye chama hicho na yaelekea hakuna mwenye ujasiri wa kuwaadhibu. Ni uoga wa kunyimwa fadhila au ushirika wa kiharamia (partnership in crime)? CCM wanaweza kuendeleza utoto wao wa kuchafuana kila kukicha lakini chondechonde wasituangamizie Taifa.

Atakayechukizwa na uchambuzi huu anapaswa si tu kuhojiwa kuhusu uzalendo wake bali ikiwezekana aripotiwe Idara ya Uhamiaji kuchunguzwa kama ni Mtanzania halisi, kwani yeyote aipendae kwa dhati Tanzania anapaswa kuguswa na mwenendo mbaya wa Taifa na ahoji wapi tunaelekea.

Hii ni mithili ya boti inayozongwa na mawimbi na sote tukiwa abiria ndani ya boti hiyo lazima tujiulize kama tutafika salama, kwani ikizama tutazama sote (isipokuwa wenzetu wenye vijisenti huko nje).
 

Atakayechukizwa na uchambuzi huu anapaswa si tu kuhojiwa kuhusu uzalendo wake bali ikiwezekana aripotiwe Idara ya Uhamiaji kuchunguzwa kama ni Mtanzania halisi, kwani yeyote aipendae kwa dhati Tanzania anapaswa kuguswa na mwenendo mbaya wa Taifa na ahoji wapi tunaelekea.
.

Ni uchambuzi mzuri, nami nashindwa kuelewa hasa hat hayo mabarabara yaliyojengwa kwa wingi nchini yanatupeleka wapi?

Pia, sisi tunaoguswa na hali hii tunafanya nini kuhakikisha kuwa wananchi wenzetu walioko vijijini wanapata uelewa huu??
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom