Wanasiasa watoe mwongozo mashindano haya

Paparazi Muwazi

JF-Expert Member
Dec 23, 2007
310
79
TANGU mashindano ya urembo yarudishwe nchini mwaka 1994, tumepata warembo "bomba" waliojumisha warembo wa Tanzania (Miss Tanzania) 14 ambao ni Aina Maeda (1994), Emile Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basilla Mwanukuzi (1998), Hoyce Temu (1999) na Jacqueline Ntuyabaliwe (2000).
Baadaye walifuata Happiness Magesse (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame (2003), Faraja Kota (2004), Nancy Sumari (2005), Wema Sepetu (2006) na Richa Adhia (2007).
Nimesema hao 14 wamejumuisha tu idadi ya wasichana "bomba" waliopatikana kwa miaka hiyo 14 kwa sababu zaidi ya hao waliovikwa taji, walikuwepo wengine ambao hawakuvikwa taji lakini yeyote kati ya hao waliokosa angeweza kuvikwa taji hilo.
Kwa hiyo, kwa kipindi hicho, wasichana "bomba" waliopatikana si hao 14 tu na wala si 42 kwa maana ya washindi wa juu watatu bali ni wengi zaidi yao kwani yeyote kati ya washiriki angeweza kuwa mshindi.
Mfano mmoja ni Miss Ocean Sandals Kanda ya Ziwa 2004, Eunice Andrew ambaye mwaka huo hakuambulia taji lolote katika mashindano ya Miss Tanzania lakini ni binti anayetisha kwa uzuri!
Katika mara zote 14 tulizoshiriki mashindano ya urembo wa dunia, kubwa la kujivunia tulilowahi kupata ni mrembo wetu wa mwaka 2005, Nancy Sumari, kushinda taji la Miss World Africa, yaani mrembo wa dunia kwa kanda ya Afrika.
Zaidi ya mafanikio hayo, tumekuwa washiriki tu. Kwa upande mmoja, hii inatokana na ukweli kwamba mashindano ya urembo wa dunia ni ya dunia nzima na hivyo ushindi wake ni kama bahati nasibu au kamari fulani hivi.
Lakini mashindano hayo yana mataji mengi. Itoshe basi tupate lolote bila kuwazia mafanikio ya mwafrika mwenzetu Agbani Darego wa Nigeria aliyetwaa taji la Miss World mwaka 2001 nchini Afrika Kusini, nchi yetu ilipowakilishwa na Happiness Magesse.
Sababu za kutofanikiwa kwetu katika mashindano hayo ni nyingi, mojawapo ikiwa hiyo ya kuwapo kwa washiriki wengi.
Kwa upande mwingine, tegemeo letu la kufanya vizuri katika mashindano hayo ni sawa sawa na halipo kutokana na hulka ya baadhi ya dada zetu wenye maumbo ya "umiss" ya unafiki, dharau, mabezo, kujikweza na kujiona bora kuliko wengine iliyoanza kujengwa tangu mwaka 1994, mashindano ya urembo yalipoasisiwa tena baada ya kusimamishwa na serikali mwaka 1967.
Baada ya uasisi mpya wa mashindano hayo na jamii kujulishwa kwamba kigezo cha msingi cha kushiriki mashindano hayo ni urefu na wembamba wa msichana, mara moja wengi wa wasichana wa maumbo hayo wakajiona thamani yao imepanda juu ghafla na kujiona hawako daraja moja na watu wengine, hasa kina dada wenzao waliojazia!
Hapo ndipo dharau, mabezo, kujikweza na kujiona bora kulipoanza. Ni katika kipindi hicho ndipo baadhi ya dada zetu walipoamua kujikondesha mpaka kubaki mifupa na kuonekana kama wanaumwa ugonjwa gani sijui, lengo likiwa nao waonekane "mamiss".
Shukrani kwa aliyetufumbua macho kwamba kukondeana na urefu wa kupitiliza ni vitu vinavyoweza kumkoseshea ushindi mshiriki wa mashindano ya urembo.
Vinginevyo dada zetu wangeendelea kujiharibu kwa kujikondesha kupita kiasi.
Kutokana na baadhi ya wenye maumbo ya "umiss" kujenga hali ya kujiona bora, mtu aliyekuwa na thamani kwao ni yule tu mwenye kitu fulani kama aliyetoka kwenye familia bora, anayemiliki mali ya thamani hasa gari la bei ya kusisimua, mwenye madaraka makubwa mahali fulani, mwenye pesa nyingi bila kujali anaipataje pesa hiyo, pamoja na mwenye umaarufu wowote ule.
Nje ya hao, si mtu kamili kwao! Hata tabasamu linaloonekana sana jukwaani wakati wa mashindano ya urembo, ni nadra sana kuonwa nje ya mashindano hayo mitaani na watu wasio na moja ya sifa hizo!
Kwa kusema ukweli, wengi wa wenye maumbo ya "umiss" si watu wa tabasamu katika maisha yao ya kawaida.
Unafiki wa wengi wao katika mashindano ya urembo uko katika kueleza dhamira ya kuwasaidia watoto yatima, watoto wa mitaani na watu mbali mbali wenye matatizo ya kijamii kama watashinda taji wakati katika maisha yao ya kawaida watu hao ni kama uchafu kwao kutokana na hali zao duni za kimaisha!
Hili wala halihitaji maelezo marefu. Kama mtu wa hali ya kawaida anayejimudu kimaisha "asiye wa hadhi" ya "mamiss" hawa wachache anatemwa mate, itakuwaje kwa mtoto wa mitaani?
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba kama vigezo vyetu vikuu vya mtu kushinda mashindano ya urembo ni wembamba na urefu wake pamoja na kujieleza vizuri kwa Kiingereza, basi tusitarajie kufanya vizuri hata siku moja kwenye mashindano ya dunia ya urembo.
Zaidi ya sifa hizo, ni vizuri kungekuwa kunafanyika uchunguzi mahsusi wa washiriki (vetting) ili washiriki wa mashindano yetu ya urembo wawe wale tu wanaofahamika kutowanyanyapaa wengine katika jumuiya wanazokuwamo kwa misingi ya hali zao kimaisha, afya zao, uwezo wao na nafasi zao katika jamii.
Ni lazima washiriki hao wawe wale tu wasio na dharau, wasiojikweza na kujiona bora zaidi ya wengine na walio waadilifu kwa kiwango cha kutosha.
Ni wazi, vingi kati ya vigezo hivi vinapatikana kwa kina dada waliojazia jazia. Wengi wao ni wacheshi, ni watu wa kujichanganya, wasio na dharau na kujikweza hata wakiwa wazuri namna gani na hata wakiwa na uwezo mkubwa vipi kimaisha.
Kutokana na wengi wao kuwa waadilifu, si kawaida sana kukuta wanaingia kwenye kashfa za mapenzi kwa kupora waume wa watu wenye hali nzuri kimaisha, jambo ambalo kwa baadhi ya "mamiss" wetu ni la kusikika hapa na pale.
Kuwa na wawakilishi wenye uhasama na jamii na wasio waadilifu katika mashindano yetu ya urembo kunatuathiri katika hali zifuatazo:
Kwanza, wakifuatiliwa maisha wanayoishi na washiriki wenzao kambini, huonekana hawana mwenendo unaokubalika kwa sababu tabia ya mtu haiwezi kubadilika ndani ya siku chache tangu alipopata nafasi ya uwakilishi. Akiwa ni wa tabia mbaya, atabaki kuwa hivyo.
Pili, atakapotakiwa aeleze ataifanyia nini jamii yake, hutoa maelezo ambayo, wenye kuelewa mambo, huyaona ni ya kisanii tu na hivyo kumpunguzia alama za ushindi.
Hii hutokea kwa sababu "miss" wetu huyo anakosa uzoefu wa kuishi kwa kuchanganyika kwenye jamii katika maisha yake halisi na jamii yake.
Hivyo, anapojieleza kwamba ataitumikia vizuri jamii, anaonekana kujieleza kwa kubabaika kwani hayo si maisha aliyo na uzoefu nayo.
Tatu, linapokuja suala la kumpigia kura akiwa mashindanoni, hapigiwi kura za kutosha kwa sababu, kwa upande mmoja wanaomfahamu huchukia nyodo zake na hivyo kuogopa kumsaidia ashinde ili asije akawanyima raha kwa nyodo zitakazokuwa za juu zaidi.
Kwa upande mwingine, hata wale wasiomfahamu, huacha kumpigia kura kwa madai ya jumlajumla kwamba "mamiss wanaringa".
Inabidi dhana hiyo ya jumlajumla ifutwe kwa kurekebisha utaratibu wa kuwapata warembo wetu kama ilivyoshauriwa.
Hapa, naomba kufafanua mambo matatu. Kwanza, makala hii haikulenga kuwashambulia "mamiss" wote bali baadhi yao wanaosababisha jamii iamini wote ndivyo walivyo.
Pili, inapotajwa "miss" au "mamiss", haimaanishi tu yule aliyewahi au wale waliowahi kushiriki mashindano ya urembo kwa ngazi yoyote ile bali wasichana wengi wa maumbo ya "umiss", hata wasiowahi kushiriki popote. Tena hao ndiyo wenye nyodo zaidi.
Jambo la tatu ni kubainisha kwamba kuna akina dada waliopata umaarufu au walioongeza umaarufu kupitia fani hii ya urembo lakini leo hii wamekuwa mfano wa kuigwa na jamii katika nyanja fulani fulani za maisha hata kama wana dosari zozote zinazofahamika, ikizingatiwa kuwa wao ni binadamu.
Naomba niwataje wachache. Yupo Lucy Kihwele wa Multi Choice (T) LTD ambaye wakati akishiriki mashindano ya urembo ya mwanzo mwanzo baada ya kuasisiwa tena alijulikana kama Tabasamu Ngongoseke.
Mwingine ni Stella Magaka, Miss Temeke 1996 wa Stella Promotions inayoandaa mashindano ya kutafuta mrembo wa mkoa wa Shinyanga.
Vilevile yumo Hoyce Temu, mwenye moyo wa dhati wa kusaidia wenye matatizo mbalimbali ya kijamii hadi leo ingawa alikuwa Miss Tanzania takriban miaka tisa iliyopita.
Yumo pia Jacqueline Ntuyabaliwe a.k.a K-Lynn asiyebagua wa kushirikiana naye kwenye nyimbo zake sasa akiwa mwanamuziki maarufu.
Vile vile yumo Dotto Nusurupia, mwenye heshima kwa kila mtu bila kujali mafanikio yake ya kuwa Miss Tanzania namba mbili mwaka 2003, tabia aliyo nayo pia dada mzuri sana Lilian Kusekwa, Miss Tanzania namba tatu wa mwaka 2000,anayeandaa mashindano ya warembo wa wilaya za Bariadi na Meatu mkoani Shinyanga mwaka huu.
Yumo pia Jokate Mwegelo anayekubalika na wanajamii wa hali tofauti za maisha kwa uadilifu wake. Mwingine ni Zuwena Omari Mustapha, Miss Ruvuma na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini 2003 anayejishughulisha na biashara ya nguo Ilala, Dar es Salaam kwa sasa.
Kwa waliowahi kuwa warembo wa Tanzania kwa miaka ya karibuni, Faraja Kotta na Nancy Sumari wamekuwa mfano mzuri wa kuiga kwa jinsi walivyoendelea kuishi kiuadilifu hata baada ya kuwa maarufu.
Hao ni wachache kati ya wengi wenye mienendo inayokubalika na jamii miongoni mwa warembo wetu maarufu. Hakuna yeyote kati yao aliyekwenda China na kuishi kwa muda mfupi wa maisha yake kisha akarudi hapa na kusema kuwa Kiswahili kinamshinda kwa sababu ya kujua zaidi kichina, kama alivyowahi kufanya mrembo mmoja maarufu, Mtanzania mwenzetu na Mswahili mwenzetu!
Tukitaka tufanikiwe kwenye mashindano ya kimataifa ya urembo,"vetting" ya warembo wetu ni muhimu ili tupate wawakilishi waadilifu na tufute dhana ya "mamiss wanaringa" ili kura zao zitoshe.
Pamoja na yote, natoa rai kwa Watanzania wenzangu kwamba ukijitokeza utaratibu wa kupiga kura kumpata mshindi wa mashindano ya urembo wa dunia, tupige kura nyingi kwa Mtanzania mwenzetu bila kujali kuwapo kwa sababu ndogo ndogo zinazohusiana na tabia yake.
Tufanye kama tulivyofanya kwa Richard wa Big Brother Africa 2 kwa kuujali zaidi Utanzania wetu.
Kamati ya Miss Tanzania nayo kama taasisi, ifanye juhudi kubwa ya kutoa matangazo ya kutosha kwenye vyombo vya habari kuhamasisha upigaji kura. Wasimuachie mwakilishi majukumu ya aina hiyo.
Ilisikitisha sana tuliposikia mwakilishi wetu Richa Adhia kwenda mashindanoni bila DVD ya muhimu kwa ushiriki mashindanoni! Kamati ya Miss Tanzania ingejali majukumu yake, hilo lisingetokea.
Kwa upande mwingine, ni vizuri warembo wetu wakatafakari uzito wa malalamiko dhidi yao na wakajipima wenyewe na kufikia uamuzi wa kubadili tabia ili wawe watu wanaoijali jamii yao kwa dhati ili kuwa warembo kikweli na si kisanii.

0713 297085
Barua pepe: ibramka2002@yahoo.com
 
Hivi hii nayo ni siasa, naomba moderator uipeleke inakostahili. Kuna mambo mengi ya muhimu sana yanayoigusa jamii yetu, sidhani kama mashindano ya miss TZ yanachukua uzito huo. Haya ni mawazo yangu.
 
Back
Top Bottom