Wanasiasa wameiteka Taifa Stars Misri, wasanii unafiki kama kawa!

Aaron Arsenal

JF-Expert Member
Jul 24, 2014
24,504
28,691
WANASIASA ndio zao! Kila kitu chenye kuvuta hisia za watu hukitumia kama mtaji wa kisiasa. Hata sasa, wanasiasa ni wengi Misri kiliko mashabiki kindakindaki wa mpira ambao liwake jua inyeshe mvua hawakosekani uwanjani.

Mashabiki wachache waliokuwemo Chamanzi siku Stars ilipotoa sare na Lesotho, wakawepo Uwanja wa Taifa dhidi ya Cape Verde ni muhimu zaidi kuliko waliojazana kwa mkumbo mechi ya mwisho dhidi ya Uganda ambayo ilikuwa na kelele nyingi, ikiwemo wanasiasa walioamua kuitumia kama ngazi ya kujikweza kisiasa.

Wanasiasa na wasanii hawakuwepo Chamanzi kipindi kigumu wachezaji wa Taifa Stars wakicheza kwa upweke na Lesotho. Waliposikia kuhusu uwezekano wa Stars kufuzu Fainali za Mataifa Afrika (Afcon) mwaka huu kama ingeifunga Uganda, basi wakatokeza kwa wingi. Wakaonesha uzalendo kweli.

Imempendeza Mungu Stars imefuzu Afcon baada ya miaka 39. Leo inaanza kampeni yake dhidi ya Senegal kwenye Uwanja wa Juni 30, Cairo. Mechi itaanza saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Juni 30 ni uwanja unaomilikiwa na Jeshi la Anga la Misri (EADF). Februari Mosi, 1968, aliyekuwa Rais wa Misri, Gamal Nasser, alitoa amri ya kuanzishwa kwa EADF, kisha Juni 30, 1968, kikosi cha EADF kilianzishwa rasmi. Uwanja huo unaitwa Juni 30 kuwakilisha siku rasmi ya kuanzishwa kwake.

Sasa, leo kwenye Uwanja wa Juni 30, Cairo, Misri, wale wazalendo wa kweli wenye kuipenda Stars kwa moyo wao wote, hawatakuwepo. Wanasiasa watang'ara sana. Watakaa kwenye viti kushangilia pamoja na chapombe kipenzi cha Watanzania, Pierre Liquid.

Watanzania walioipigania Taifa Stars nyakati ngumu, uwanja ukiwa na watu wachache, hawatakuwepo Juni 30 leo. Wanasiasa ambao waliikimbilia Taifa Stars kwa sababu iligeuka mkumbo kwa kila Mtanzania kuiunga mkoni ili ifuzu kwenda Afcon, watakuwa mstari wa mbele.

Stars isingefuzu Afcon kama isingepata sare dhidi ya Lesotho Chamanzi. Hata hivyo, waliojazana Uwanja wa Taifa kwenye mechi dhidi ya Uganda na kelele zao mitandaoni, wanajipongeza kuwa sehemu ya watu waliowatia nguvu Stars kufuzu Afcon.

Wabunge mbalimbali wamekuwa wakipost mitandaoni picha zao wakiwa kwenye mapiramid Misri. Kuonesha tayari wapo Misri kuipa nguvu Stars. Wengine hata majina ya wachezaji hawajui, ila wamepata nafasi na leo wapo Misri.

Wabunge walisafiri daraja la kwanza (business class) kwenda Misri. Wanakaa kwenye hoteli za hadhi ya juu. Gharama za kumsafirisha mbunge mmoja kumweka Misri, ingetosha kusafirisha Watanzania watano wazalendo wa kweli wenye kuupenda mpira.

Hata hivyo, kwa kuwa wanasiasa hupenda fursa za kujiuza, wapo Misri leo. Watanzania wanyonge wenye kupenda hasa mpira na ambao wamekuwa pamoja na Stars kipindi cha kupuuzwa na wengi, watatazama kwenye runinga leo, nyumbani na katika vibanda umiza.

Hao ndiyo wanasiasa, mwaka jana kwenye Kombe la Dunia Urusi, tuliwaona walivyochuana kwenye timu zao za Taifa. Vladimir Putin ghafla alikuwa shabiki wa soka na kupigia chapuo Timu ya Taifa ya Urusi, kama Macky Sall kwa Senegal auvAngela Merkel na Ujerumani yake.

Kiongozi Mkuu (Ayatollah) wa Iran, Ali Khamenei ungejuaje kama ni mtu wa soka? Alidhihirisha waziwazi uungaji mkono kwa Timu ya Taifa ya Iran. Dunia nzima ilivutiwa na bi mama, Rais wa Croatia, Kolinda Grabar-Kitarovic, aliyeweka kambi Urusi kuipigania timu yake.

Hatubishani kuwa wapo wanasiasa wanapenda sana mpira. Silvio Berlusconi ni mwanasiasa maarufu na Waziri Mkuu wa vipindi vinne nchini Italia. Berlusconi pia ni mmiliki wa klabu ya soka ya AC Milan.

Mwaka 2006 kwenye Fainali ya Kombe la Dunia ambayo Italia iliifunga Ufaransa katika Uwanja wa Olympiastadion, Berlin, Ujerumani, Berlusconi alitaka ajipake rangi ya Bendera ya Taifa ya Italia usoni na kushangilia na mashabiki wa kawaida, lakini alikataliwa na vyombo vya usalama kwa sababu za kiitifaki.

Vilevile, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni mtu wa mpira na hili lipo wazi. Ni kocha na kiukweli ushiriki wake katika masuala ya soka hautiliwi shaka. Majaliwa akienda Misri, kama kiongozi ni inawapa nguvu wachezaji, lakini tusikatae wengi wanakimbilia fursa ya kujipandisha kisiasa.

Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978, aliyekuwa dikteta wa Argentina, Jorge Videla, aliitumia michuano hiyo kuuonesha ulimwengu kuwa nchi hiyo ni tulivu na wananchi ni wamoja. Fainali hizo zilifanyika Argentina. Ni kama ambavyo Putin alivyoipamba michuano ya mwaka jana Urusi ili kuonesha kwamba nchi hiyo ina mazingira bora ya kiusalama na kisiasa.

Wanasiasa wamezifanya klabu za Real Madrid na Barcelona kuwa kiwakilishi cha harakati za siasa Hispania na vuguvugu la kujitenga Catalonia. Hata hapa, wanasiasa hutokeza sana Simba na Yanga nyakati za kujijenga kisiasa. Timu zikiwa hoi huwaoni. Zinapoimarika hutokeza kuchukua ujiko wa kisiasa.

Stars ilipoifunga Uganda mabao 3-0 na kufuzu Afcon 2019 Machi 24, mwaka huu, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole, aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter kuwa mabao matatu ambayo Stars walipata dhidi ya Uganda, yanagawanyika katika miradi mikubwa mitatu;

Mradi wa kwanza ni ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge), pili ni mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler's Gorge na tatu ni ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Mwisho wa ujumbe wake, Polepole alisema ushindi wa Stars unaendana na utekelezaji wa ilani ya CCM. Unajiuliza hivi Polepole alikuwa wapi kipindi Stars inacheza kinyonge dhidi ya Lesotho Chamanzi? Jibu lake ni hili; hao ndio wanasiasa na uchangamkiaji wa fursa.

Na ndio maana sasa hivi wameshaiteka Taifa Stars Misri. Imekuwa timu ya wabunge zaidi. Vigezo vya uwezo wa kifedha na upendeleo wa kimamlaka, umefanya wabunge waonekane ni wazalendo kwa Taifa Stars kwa sababu wapo Misri, kuliko wazalendo halisi ambao watajazana kwenye vibanda umiza leo.

Wasanii walikuwa mstari wa mbele kwenye mechi ya Taifa Stars dhidi ya Uganda. Walipost mitandaoni, walihamasisha watu kwenda uwanjani. Ukifuatilia nyuma yao kulikuwa na msukumo wa kufanya hivyo. Na baada ya kufuzu Afcon, walijishaua kweli na picha zao za uwanjani kuonesha na wao ni sehemu ya historia.

Leo Stars inacheza mechi ya kwanza Afcon, wasanii kimya. Hawaonekani kupost kuitakia heri nchi dhidi ya Senegal. Jinsi walivyopiga domo kuelekea mchezo na Uganda, unashangaa mpaka leo, hakuna msanii ameingia studio kutoa wimbo wa kuhamasisha ushindi kwa Taifa Stars Afcon.

Hao ndio wasanii na unafiki wao. Unaweza kudhani ni wazalendo kumbe ni pesa. Wangepewa pesa waimbe kuhusu Stars Afcon ungewapenda. Tungeshasikia nyimbo hata 10 sasa. Basi ndio hivyo, tuwapongeze wasanii kwa unafiki wao wa kujazana Taifa dhidi ya Uganda lakini wameshindwa kutoa wimbo wa kuihamasisha kwenye michuano ya Afcon.

Ndimi Luqman MALOTO
 
Kama timu ikifanyaga vizur wanasema ni juhudi za Serikali ya awamu ya tano basi hata ikifanya vibaya pia waseme vivyo hivyo....
 
22 Reactions
Reply
Back
Top Bottom