Wanasiasa wa Chama Tawala watafurahi zaidi msipojiandikisha na kupiga kura! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wanasiasa wa Chama Tawala watafurahi zaidi msipojiandikisha na kupiga kura!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mchokonozi, May 18, 2010.

 1. M

  Mchokonozi Member

  #1
  May 18, 2010
  Joined: Nov 17, 2009
  Messages: 15
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nimekuwa nikifanya tathmini kuhusu mfumo wa kisiasa uliopo nchini hapa, hususan sheria zinazohusu masuala ya chaguzi za kisiasa, kuanzia ngazi za serikali za mitaa, hadi ubunge na urais, na nimebaini mambo ambayo yamedhihirisha kwamba, demokrasia iliyopo nchini mwetu ni “kiini macho”. Kimsingi, mfumo uliopo hautoi nafasi kwa chama chochote kingine kushika hatamu, hata kwa miaka ishirini ijayo, kutokana na ukweli kwamba, Katiba, ambayo ndiyo sheria mama, ni mbovu na inastahili kuundwa upya kwani inawanyima Watanzania haki zao za msingi za kuwachagua viongozi wanaowataka, na wao kushiriki kikamilifu katika ngazi zote za kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuchaguliwa kushika madaraka ya uongozi.

  Kwenye utafiti wangu, nimegundua kwamba Tanzania inatumia mfumo wa “simple majority”, ambao unaweka mazingira ya kukiwezesha Chama Tawala kuendelea kuhodhi madaraka kwenye chombo cha kutunga sheria na kufanya maamuzi makuu, yaani Ubunge na Urais, mambo ambayo, kimsingi, hayawatendei haki wananchi.


  Ndani ya mfumo huu wa “simple majority”, panapotokea kuwapo kwa mgombea mmoja asiye na upinzani, kwenye nafasi yoyote ile ya uongozi wa kuchaguliwa, kuanzia serikali za mitaa, ubunge na urais, hata kama mgombea huyo hatapata kura hata moja, atahesabika kuwa ameshinda, KWA KUWA HAKUWA NA MPINZANI. Hii ndiyo maana halisi ya dhana ya “simple majority”.


  Kutokana na mazingira haya kuwapo nchini, viongozi wa Chama Tawala wameimarisha zaidi ufanisi wa dhana hii, kupitia Sheria ya Matumizi ya Uchaguzi, ili kuhakikisha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatumika ipasavyo kuwabana na kuwaengua wagombea wengi ipasavyo watakaojitokeza kupitia vyama vya kambi ya upinzani, kutokana na sheria hiyo kuweka mazingira ya kuiwezesha kufanya hivyo bila usumbufu.


  Kwanza kabisa, mojawapo ya kanuni mpya zilizopitishwa na kutangazwa hivi karibuni ni ile ya kupunguza muda wa kutoa majibu kwa Tume panapotokea kuenguliwa kwa mgombea, kutoka muda wa saa 48 hadi saa 24. Kwanza, muda huo wa saa 48 haukuwa unatosha kufanya hivyo, kwani kutokana na miundombinu kuwa duni kwenye sehemu nyingi hapa nchini, ilikuwa vigumu kwa viongozi wa vyama vya upinzani kujipanga, kuunda kamati, kufanya uchunguzi na kupeleka majibu ya utetezi kwa Tume ya Uchaguzi, ili kuhakikisha kwamba mgombea aliyeenguliwa anarejeshwa kwenye kampeni na kuweza kuchaguliwa. Muda huo wa saa 48 haukutosha. Lakini Tume hii, ambayo inafanya kazi kwa matakwa ya Rais aliyepo madarakani, ambaye ni wa Chama Tawala, imeona kwamba muda huo wa saa 48, ambao awali haukutosha, sasa upunguzwe zaidi kufikia saa 24, jambo ambalo litazidi kuviweka vyama vya upinzani kwenye wakati mgumu wakati wa kampeni na Uchaguzi Mkuu wa 2010.


  Kutokana na Sheria ya Matumizi ya Uchaguzi kuweka mazingira kwa Sheria ya Uchaguzi kuwezesha kuwapo kwa mazingira ya kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani kupitia majungu, kwani mtu yeyote yule atakeyetoa taarifa kwa Msajili wa Vyama, TAKUKURU au Msimamizi wa Uchaguzi kwenye Kata na Jimbo kuhusu kuwapo kwa mazingira ya ukiukwaji wa Sheria ya Matumizi ya Uchaguzi, tuhuma hizo zikiwa zimewalenga wagombea wa upinzani, mtu huyo hatapaswa kutambuliwa na mgombea aliyetuhumiwa au viongozi wa chama chake. Kimsingi, kipengele hiki cha Sheria hiyo tata kinakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri, kwani, ni haki ya kila mtuhumiwa – wa kosa lolote lile – kumtambua anayemtuhumu kukiuka sheria, pia kupata nafasi kikamilifu kujitetea.


  Kufungu hicho kilichowekwa na kupitishwa kwenye Sheria hiyo iliyopitishwa kwa mbwembwe na Rais Kikwete mapema mwaka huu kinaashiria wazi wazi kuwapo kwa mazingira ya ukiukwaji wa Katiba, kutokana na ukweli kwamba, hata kama yatakuwapo mazingira ya ukiukwaji wa Sheria hiyo kwa wagombea wa Chama Tawala, taarifa zitakazotolewa kwa Msajili wa Vyama, TAKUKURU au Msimamizi wa Uchaguzi wa Kata au Jimbo, hazitafanyiwa kazi, kwani vyombo hivi daima vimekuwa vikifanya kazi kwa manufaa ya Chama Tawala. Haiyumkini vyombo hivi, leo, kubadilika na kuanza kukipinga Chama Tawala, ambacho ndicho kimeviunda ili kuwezesha kuendelea kuwapo kwake madarakani.


  Jambo hili litaleta uhasama mkubwa miongoni mwa wananchi, kwani zipo ishara tosha kwamba, katika sehemu nyingi hapa nchini, wananchi wamekichoka Chama Tawala, na hawatakuwa tayari kuwaona wagombea wanaotaka kuwapigia kura kuwachagua kuwa viongozi wao kuenguliwa kinyemela kupitia sheria kandamizi. Upo uwezekano kutokea machafuko kama yaliyotokea nchini Kenya wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, machafuko ambayo sio tu kwamba yalisababisha mauaji ya maelfu ya watu, bali pia uharibifu wa mali, miundombinu na hasara kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo.


  Panapofuka moshi pana moto, na asiyesikia la mkuu huvunjika guu. “Mkuu” haswa wa nchi hii ni “mwananchi” mwenyewe, ambaye inaonekana dhahiri kwamba, mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu hatakuwa tayari kupokonywa haki yake ya kuchagua kiongozi anayemtaka, na tayari ameonesha dhahiri kutokuwa na woga wa kuhakikisha hapotezi haki yake hiyo. Ishara mojawapo ya “moshi” huo ni msimamo wa wafanyakazi kupitia shirikisho, TUCTA, ambao kwa mara ya kwanza waliamua kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani – Mei Mosi – bila kuwaalika viongozi wa nchi kuwa wageni rasmi, kama ilivyokuwa desturi miaka ya nyuma. Ishara nyingine ni kuendelea kuwapo kwa mgogoro unaotishia kufanyika kwa mgomo wa nchi nzima, hatima ya mgogoro huu ikisubiriwa kujulikana baada ya siku 21 kuanzia tarehe 8 Mei 2010, baada ya kikao cha majadiliano baina ya Serikali na TUCTA kilichofanyika mjini Morogoro kutopata muafaka baina ya pande mbili hizo.


  Ishara nyingi ziko kwamba wananchi wamechoka, ninyi wote mnazifahamu.


  Sasa nihitimishe kwa kusema kwa nini viongozi wa Chama Tawala watafurahi zaidi msipojiandikisha kupiga kura.


  Jambo hili ni kweli kabisa, kwani, msipojiandikisha kupiga kura mtakuwa mnawapa faida wagombea wa Chama Tawala, kwani wanatambua kwamba “kususa” kwenu kunawapunguzia kura za “hapana”, kura ambazo mnaweza kuzipiga iwapo mtajiandikisha. Kupitia mfumo wa “simple majority”, hata wakipata kura chache za “ndiyo” na chache zaidi za “hapana”, wagombea wa Chama Tawala watapita na kuwa washindi. Kura ambazo zingeweza kupelekwa kwenye upinzani zitakosekana kwa kuwa ninyi ndugu zangu mnafikiria kwamba chama pekee ni Chama Tawala. Hamjatambua kwamba upo uwezekano wa kuwapata viongozi wengine ambao si wa Chama Tawala. Hiki ndicho kiini cha matatizo yetu, kwani bado wengi wetu hawawatambui viongozi wa vyama kama vile CHADEMA, NCCR-Mageuzi, TLP, UDP, CUF na DP, vyama ambavyo vingeweza kuleta mabadiliko nchini iwapo vingepewa nafasi hiyo, ingawa siamini kwamba baadhi ya vyama hivi vina uwezo huo. Hayo ni maoni yangu, lakini, hatuwezi kusema kwamba “hawataweza” iwapo hatujawapa nafasi.


  Ndio, yapo mazingira ya kuweza kuwaengua wagombea wa upinzani kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kupitia sheria kandamizi, lakini sidhani kama Chama Tawala kitaweza kuwaengua wagombea wote bila kuhatarisha amani hapa nchini, kwani kufanya hivyo ni kukaribisha upotevu wa amani, jambo ambalo nina hakika hata Chama Tawala chenyewe hakitaki litokee.


  Kwa hiyo, ndugu zangu, shime, kwa wale mliopo Dar es Salaam, msikose kujiandikisha Mei 22 na 23, 2010, pamoja na kuhakiki kadi zenu za kupiga kura, ili mkaeneze elimu hii ya uraia – ambayo ni jukumu langu kuitoa kwenu kama mwanaharakati – na kuwawezesha Watanzania wenzenu kufanya maamuzi sahihi. Wengi wetu bado tuna upofu, wa kuamini kwamba wagombea kutoka vyama vya upinzani – ambavyo mimi naviita vyama mbadala – ni wasaliti na wahaini, kwa kuwa tu sio wanachama wa Chama Tawala. Lakini tunasahau kwamba, hata kwa nchi iliyojengeka katika demokrasia kwa karne kadhaa, Marekani, mazingira ya upinzani wa kisiasa kati ya vyama vikuu viwili, Democratic na Republican, yapo, na watu wanaishi vizuri bila kuhasimiana, tena kwa kuchaguana na kupokezana madaraka. Wapo wanachama wa Republican Party ambao hawakumpigia kura mgombea wa urais wa chama chao wakati wa uchaguzi mkuu wa 2008, na wapo pia wanachama wa Democratic Party ambao hawakumpigia kura mgombea wa urais wa chama chao wakati huo, lakini uchaguzi ulikamilika bila kutokea matatizo yoyote yale.


  Kama Marekani wanaweza kuendesha kampeni na kuchaguana, pasi na kumwaga damu, iweje sisi ambao tu wachanga kwenye demokrasia tunahasimiana kutokana na tofauti zetu, hususan wale waliopo kwenye Chama Tawala wakiamini kwamba nchi hii ni MALI yao, milele na milele, na mwingine yeyote hastahili kuiongoza, kwa hali yoyote ile?


  Tubadilike, tuoneshe ukomavu wa kisiasa, kwani tofauti zetu hizi – za kung’ang’ania madaraka – zitatufikisha pabaya. Tusisahau yaliyotokea nchini Kenya miaka michache iliyopita, kwani, ukiona mwenzio ananyolewa, nawe tia maji kichwani!


  Shime, mkajiandikishe, shime mkapige kura, shime mkawachague viongozi mnaowataka, sio wa Chama Tawala pekee, kwani Chama Tawala hakina HAKI ya kuitawala Tanzania milele. Hata hao kwenye vyama vya upinzani ni Watanzania pia, nao wana haki ya kuchaguliwa kuiongoza nchi yao. Tuwe waungwana, vita ni hatari, tusiichezee nchi yetu hii.


  Wasalaam,  >>> Mchokonozi wa Kuchokonoa!  P.S. Mimi ni Mtanzania mpenda amani, mzalendo halisi. Si mwanachama wa chama chochote cha siasa wala sina nia ya kujiunga na chama chochote cha siasa, lakini ninaipenda nchi yangu na nitailinda na kuitetea kwa nguvu zangu zote. Daima nitakuwa mkweli, uongo na unafiki kwangu ni mwiko!
   
 2. Ruge Opinion

  Ruge Opinion JF-Expert Member

  #2
  May 19, 2010
  Joined: Mar 22, 2006
  Messages: 1,696
  Likes Received: 306
  Trophy Points: 180
  Change in this country will not be brought by the ballot box. The odds are heavily loaded against that. The only remaining option is people's power. like what is happening in thailand or what happened in ukraine, georgia, etc.
   
 3. Abunwasi

  Abunwasi JF-Expert Member

  #3
  May 20, 2010
  Joined: Jun 25, 2009
  Messages: 3,166
  Likes Received: 1,064
  Trophy Points: 280
  Ingekuwa enzi mzee JKN kwa kauli yako hiyo tu ilitosha kuwekwa detentionkwa kutumia "subversive act" Lakini kutokana na kupanuka kwa demokrasi hivi sasa you can speak your heart out bila ya kuwa na wasiwasi.
  Hii inaonyesha jinsi tulivyoendelea katika kuheshimu haki za binadamu katika kujieleza.
  LONG LIVE TANZANIA
   
Loading...