Wanasheria 50 wa serikali wazuiliwa kupata uwakili

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
207,580
2,000
Wanasheria 50 wa serikali wazuiliwa kupata uwakili
Monday, 20 December 2010 20:28

James Magi
SERIKALI imewawekea pingamizi wanasheria takribani 50 waliokuwa wameomba kusajiliwa kuwa mawakili wa kujitegemea, baada ya kufaulu usaili mbele ya Baraza la Elimu ya Sheria, Mwananchi limebaini.

Wanasheria waliowekewa pingamizi na serikali ni wale ambao ni watumishi wa umma wanaofanya shughuli za kisheria chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na wale walioko katika mashirika, taasisi na wakala mbalimbali wa serikali.

Kutokana na pingamizi hilo la serikali, wanasheria hao ambao walikuwa ni miongoni mwa waombaji 387 wa nafasi hiyo, katika sherehe za 42 za usajili wa mawakili wapya zilizofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salamwamekwama kupata uwakili.

Akizungumza mara baada ya kuwakabidhi vyeti vyao waombaji wengine, Jaji Mkuu Agustino Ramadhani alisema waombaji hao 50 wameamua kuwaacha kwa kuwa kuna taratibu ambazo bado hazijakamilika na kwamba zitakapokamilika nao watakabidhiwa vyeti hivyo.

Lakini habari zilizolifikia Mwananchi na kuthibitishwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG) George Masaju zilieleza kuwa waombaji hao wametemwa baada ya kuwekewa pingamizi na serikali.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake muda mfupi baada ya sherehe hizo kumalizika, Masaju alilithibitishia Mwananchi kuwawekea pingamizi waombaji hao akisema kuwa ni kwa sababu walikiuka sheria Namba 4 ya mwaka 2005 ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Masaju alisema kwa kujibu wa sheria hiyo na Kanuni zake za mwaka 2006, wakili wa serikali, Ofisa wa Sheria au mtumishi yeyote anayefanya shughuli za kisheria katika shirika, taasisi au wakala wa serikali, ni kinyume cha sheria kuwa wakili wa kujitegemea.

Alisema kitendo walichokifanya waombaji hao ambao ni watumishi wa umma ni ukiukwaji wa sheria hiyo na kanuni zake na kwamba ndio maana serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ndio inaratibu na kusimamia taratibu na maadili yao iliwawekea pingamizi hilo.

“Hawa ni watumishi wa umma, lakini walikuwa wameomba kuwa mawakili wa kujitemea nafasi ambayo ingewawezesha kwenda mahakamani kuwawakilisha watu na kuwatoza ada, hili sheria hii imelizuia,”alisema Masaju na kuongeza; huku akisoma kifungu cha 8 (2) cha Kanuni hizo.

Akielezea athari za wakili wa serikali au ofisa sheria katika shirikia , taasisi au kampuni ya umma wa serikali, Masaju alisema itawapa nafasi kutumia nafasi yao katika utumishi wa umma kutekeleza majukumu yao binafisi, jambo ambalo linaleta mgongano wa maslahi.

Kwa upande wake Rais wa Chama Cha Wanasheria nchini (TLS), Felix Kibodya alisema katika utaratibu wa ajira hilo ni suala lisilowezekana na kwamba wanachotakiwa kufanya waombaji hao ni kujiuzulu kwanza utumishi wao serikalini.

Awali waombaji hao walifika katika eneo la sherehe za kuwasajili na kukabidhiwa vyeti vya kukubaliwa kuwa mawakili wa kujitegemea, wakiwa ndani ya majoho yao ya uwakili huku wakiwa wameambatana na ndugu, jamaa na marafiki zao kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo.

Hata hivyo bila kutarajia walijikuta wakitemwa na kuondolewa katika orodha hiyo katika dakika za mwisho na kubakia kuwa washuhudiaji tu wa waombaji wenzao.

Kufuatia pingamizi hilo uongozi wa mahakama uliazimika kufanya kikao cha dharura baada ya kuwasili katika eneo la sherehe, ili kuweka mambo sawa, kabla ya kuendelea na utaratibu wa utoaji vyeti kwa waombaji wengine.

Hata hivyo jana waombaji hao waliowekewa pingamizi walifika Mahakama Kuu kujua hatma yao.

Msajili wa Mahakama Kuu Ignasi Kitusi hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo kwa kuwa alikuwa kwenye kikao Mahakama ya Rufani.
Lakaini habari ambazo Mwananchi lilizipata kutoka kwa ofisa mmoja mahakamani hapo zilieleza kuwa waombaji hao waliambiwa warudi siku nyingine(ambayo hakuitaja) kwa ajili kulipatia ufumbuzi suala lao.


Jumla ya mawakili wapya 337 walisajiliwa na kukabidhiwa vyeti vya uwakili, idadi ambayo ilielezewa na Jaji Ramadhani, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Felix Kibodya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ni ya kihistoria kwa mawakili wengi kiasi hicho kusajiliwa mara moja.

Kwa mujibu wa Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania Ignas Kitusi, mawakili hao wapya wamefanya idadi ya wakili wote nchini kufikia 1660.

Hata hivyo Jaji Ramadhani pamoja na Kibodya walisema idadi hiyo bado ni ndogo sana kulinganisha na nchi nyingine jirani kama Kenya na Uganda.

Jaji Mkuu alisema kuwa kuna mikoa mingine hadi sasa haina wakili hata mmoja wa kuwatetea wananchi, jambo ambalo alisema ni aibu katika kipindi cha miaka 49 ya Uhuru.

Hata hivyo Jaji Ramadhani alisema kwa sasa kuna orodha ya waombaji 1130 ambao wanasubiri kusajiliwa, na akawaomba wale waliotuma maombi yao miaka ya nyuma na hawajaitwa wawasiliane na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu haraka.

Akitoa uwiano wa mawakili nchini kulinganisha na nchi jirani Kibodya alisema nchini Kenya kuna mawakili takribani 7,000 ambapo wakili mmoja huwakilisha wananchi 6,000, Uganda wakili mmoja kwa wananchi 3,500 wakati Tanzania wakili mmoja huwakilisha wananchi 36,000.

Miongoni mwa wanasheria waliosajiliwa jana ni pamoja na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu (Kitengo cha Mahakama ya Kazi), Ernest Mwipopo.

Wengine ni Padre wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dodoma, Isidor Qaya, na aliyewahi kuwa mrembo wa Tanzania namba mbili (Miss Tanzania) 2003 Mbiki Msumi, ambaye sasa ni mfanyakazi katika kitivo cha sheria cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
 

Nyani Ngabu

Platinum Member
May 15, 2006
88,755
2,000
Kwanza, huo usaili mbele ya Baraza la Elimu ya Sheria unafanyika kwa kutumia lugha gani?

Pili, hao wanasheria wa serikali waliozuiwa kupata uwakili wa kujitegemea, aidha ni vilaza wasioijua sheria ya nchi kuhusiana na hilo ikoje au sheria yenyewe ndiyo haieleweki. Nasema ni vilaza kwa sababu mgongano wa kimaslahi hapo upo bayana kabisa. Jiuzulu nafasi yako serikalini halafu ndo uingie kwenye private practice. What is not clear about that?

Sielewi hata kilichowafanya watume hayo maombi kabla hata hawajajiuzulu nafasi zao serikalini na kwenye hayo mashirika mengine ya umma. Kudhihirisha ukilaza wao hiyo taarifa inasema kuwa hao waombaji walifika hadi eneo la sherehe na kukabidhiwa hati zao za uwakili wa kujitegemea. Ukilaza na utovu wa umakini umedhihirishwa pia na wanaohusika na usajili wa hao mawakili wapya. Kwa nini hawakugundua hilo kabla ya siku hiyo? Jibu ni kwamba hawafanyi kazi yao sawasawa. Walitakiwa ku cross check na ku double check sifa za kila mwombaji na kuhakikisha kuwa kila mwombaji ametimiza sifa zote zinazotakiwa. Kilichotokea ni usumbufu kwa pande zote mbili kwa sababu ya uzembe.

Halafu sijui nimesoma vibaya au vipi lakini Tanzania nzima ina mawakili 1660? Hii ni idadi ndogo sana na inatia aibu. Kwa nini idadi iwe ndogo hivi? Ni kwamba watu hawavutiwi na hii fani au? It's a shame and it's pathetic.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom