Wanaougua presha hatarini kupoteza uwezo wa kufikiri, kumbukumbu

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,000
9,861
Watafiti nchini Tanzania wamebaini wagonjwa wanaougua shinikizo la damu la muda mrefu maarufu ‘blood pressure’ wapo hatarini kupata mabadiliko ya mfumo wa fahamu ikiwemo ubongo.

Matokeo ya utafiti huo uliochapishwa jana Jumatatu Novemba 9, 2021 na jarida la BMC Neurology la nchini Uingereza, yameonyesha kati ya watu 1,201 waliohusishwa asilimia 43.6 ambayo ni sawa na jumla ya wagonjwa 524 walikutwa na mabadiliko hasi ya mfumo wa fahamu ulioleta athari katika ubongo.

Miongoni mwa mabadiliko hasi yametajwa kusababisha kupungua kwa uwezo wa ubongo kufikiria, kuweza kuongea au kuwa na kauli sawasawa, kupungua kwa uwezo wa kumbukumbu na umakini.

Akizungumza kiongozi wa utafiti huo, Mkuu wa kitengo cha utafiti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dk Pedro Palangyo amesema utafiti huo ulilenga kuangalia mabadiliko ya kwenye mfumo wa fahamu na ubongo ambayo yanatokana na madhara ya shinikizo la damu la muda mrefu.

Alisema ugonjwa wa shinikizo la damu kwa muda mrefu umekuwa ukihusishwa na kuleta matokeo hasi katika ubongo wa mwanadamu na yamekuwa yakitokana na ukweli kwamba shinikizo huathiri mishipa inayopeleka damu kwenye ubongo na kutokana na athari hiyo wagonjwa wanaougua muda mrefu wameonekana kuathirika zaidi.

“Kwa wanaougua kwa muda mrefu uwezo wa ubongo wao unapungua kwa jinsi ambavyo wanazidi kukaa na presha na wale ambao kwa namna moja ama nyingine wameshindwa kuitibu au kuanza matibabu.

“Shinikizo la damu limehusishwa na kupunguza uwezo wa ubongo kufikiria, imepunguza uwezo pia wa mwanadamu kuweza kuongea au kuwa na kauli sawasawa, uwezo wa kuwa na kumbukumbu na umakini,” amesema.

Dk Pedro ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, amesema waliangalia mabadiliko yanayotokea katika ubongo na kwa namna gani wagonjwa wanapata matokeo hasi kupitia ugonjwa huu.

“Tulihusisha wagonjwa wa nje ambao wanahudhuria kliniki katika taasisi ya JKCI kuanzia Marchi 2020 hadi Februari mwaka huu. Kati ya tuliowahusisha wastani wa umri wao ilikuwa miaka 58, wanawake wakiwa wengi zaidi na zaidi ya robo tatu ya washiriki wote walikuwa na uzito mkubwa kuliko inavyopaswa kuwa,” amesema.

Amesema asilimia 17 walikuwa na kisukari, asilimia 8 kiharusi, asilimia 6 matatizo ya moyo na takribani asilimia 17 walikuwa na matatizo ya figo ya kudumu huku asilimia 54 wakiwa na upungufu wa damu na theluthi mbili walikuwa na kiwango kikubwa cha mafuta kwenye damu ‘choresto’.

Majibu ya utafiti
Dk Pedro amesema walitumia dodoso ambalo linatumika katika kupima uwezo wa ubongo ‘PCOG’ kwa kuwahoji wagonjwa 1,201 na kwa ujumla asilimia 43.6 ambayo ni sawa na jumla ya wagonjwa 524 walikutwa na mabadiliko hasi.
Amesema walienda mbele zaidi kwa kuangalia vitu gani vingine ambavyo vilihusishwa na upungufu wa uwezo wa ubongo kwa wahusika na waliona kuna vitu vinachangia hayo mabadiliko ikiwemo elimu.

“Waliokuwa na elimu ya msingi, au kwenda chini walikuwa na uwezekano mara tatu na nusu ya kupata athari ukilingansiha na waliosoma sekondari na elimu za juu. Waliostaafu wana ongezeko la asilimia 70 ya kuwa na hili tatizo ukilinganisha na waliokuwa wana shughuli za kila siku za kuwaongezea kipato.

“Lakini pia watu wengine ambao walikuwa wanaishi katika mazingira ya kijijini walikuwa na ongezeko pia la asilimia 80 la kuwa na upungufu huu ukilinganisha na wale waliokuwa wakiishi mijini,” amesema.

Dk Pedro amesema utafiti pia ulibaini wagonjwa waliokuwa na tatizo la figo la kudumu walikuwa na ongezeko la asilimia 70 ya kupata athari ukilinganisha na wagonjwa ambao figo zao zilikuwa bado vizuri.

“Utafiti huu umeonyesha asilimia kubwa kuliko wale walioripotiwa kuwa na shinikizo la damu walionekana wana uwezekano mkubwa wa kupata athari ukilinganisha na wenzao ambao walikuwa hawana presha.

“Tunashauri kwa kuwa karibu nusu ya wagonjwa wote wamepata athari kwenye ubongo, madaktari na watoa huduma wajitahidi sana kutoa huduma ili wagonjwa wao waweze kudhibiti ugonjwa wa shinikizo la damu vizuri na kuweza kuzuia au kupunguza uharaka wa mabadiliko ya presha kwenye ubongo wao.

“Pia madaktari kama sehemu ya matibabu yao kwa wagonjwa waweze kuwa wanaangalia hilo ili kuboresha afya ya wagonjwa,” amesema Dk Pedro.

Hata hivyo wataalamu hao wametahadharisha kuwa watu wanapaswa kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kujua na kuepuka madhara yatokanayo na ugonjwa huo.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa ni asilimia 10 pekee ya wenye shinikizo la damu nchini wanajua kuhusu hali zao.

Tatizo hilo linaonekana kuwa ni kubwa zaidi kwani katika Taasisi ya Moyo na Jakaya Kikwete (JKCI) pekee, takwimu zinaonyesha kati ya watu 10 wanaoanza matibabu ya moyo sita hukutwa na shinikizo la damu bila kujua.

Ripoti ya WHO inaonyesha kila kina mama wanne mmoja ana tatizo hilo na kila kina baba watano mmoja ana tatizo hilo na zaidi ya watu bilioni moja duniani (Tanzania ikiwemo) wanaugua shinikizo la damu.

Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya moyo, Peter Kisenge amesema kuna umuhimu wa watu kupima shinikizo lao la damu mara kwa mara ili kuondokana na madhara makubwa yanayosababishwa na ugonjwa huo.

“Duniani wanaojua kuhusu hali zao kwamba wana shinikizo la damu ni asilimia 50 pekee hapa kwetu ni asilimia 10, kwa JKCI pekee wagonjwa 10 tunaowaona wa mara ya kwanza sita wana shinikizo la damu na hawakutambua hali zao,” amesema.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom