Wanaokibeza, kukidhalilisha Kiswahili waadhibiwe ...UNASEMAJE?


Ustaadh

Ustaadh

JF-Expert Member
Joined
Oct 25, 2009
Messages
413
Likes
7
Points
0
Ustaadh

Ustaadh

JF-Expert Member
Joined Oct 25, 2009
413 7 0
HIVI karibuni Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) waliingia mkataba na kampuni ya udalali ya Majembe Auction Mart ili iwasaidie kusimamia biashara ya usafirishaji wa abiria jijini Dar es Salaam.

Sumatra waliona bila kutumia sheria na nguvu kazi, madereva na wamiliki wa daladala wangeendelea kupuuza na kuvunja sheria na hatimaye kuwaharibia utendaji wao wa kazi pamoja na suala zima la usafirishaji jijini Dar es Salaam.

Lakini nilijiuliza kwa nini Sumatra wameingia mkataba na Majembe wakati mamlaka hiyo ipo kisheria na hivyo nikadhani kuwa bila msaada huo wangewadhibiti hao wakorofi.

Nilidhani labda ni kwa sababu ya uchache wa watumishi katika Mamlaka hiyo. Au Sumatra walitumia usemi usemao, “Ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni”.

Hata hivyo nawapongeza kwa hatua hiyo, kwani tumeanza kuona matunda yake. Kutokana na mafanikio hayo nikaona kuwa kumbe Majembe wanafaa kutusaidia kazi.

Kwa nini tusiendelee kuwatumia? Kwa mtazamo wangu ninaona huenda hata Kiswahili kinahitaji Majembe Auction Mart ili kudhibiti, matumizi mabovu ya lugha ya Kiswahili yanayoendelea miongoni mwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili hapa nchini, wakiwemo wasomi.

Watanzania tumekuwa tukijivunia kuwa Kiswahili ni chetu kuliko Kenya na Uganda katika nchi za Afrika Mashariki. Kutokana na hilo, bila shaka sisi ni watumiaji wazuri wa lugha ya Kiswahili, wenye kuzungumza Kiswahili sanifu.

Hili sina hakika, huenda ni kweli au si kweli. Hata hivyo tulipaswa kuwa wazungumzaji wazuri wa lugha hii kwa kuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa, ni lugha rasmi, inatumika kufundishia katika Shule za Msingi na ni lugha ya mawasiliano katika shughuli zote za kila siku.

Pia Kiswahili ni utambulisho wa Mtanzania na ndiyo lugha iliyoleta umoja wa kitaifa hapa nchini. Nimejiuliza hivi pamoja na sifa zote hizo kwa nini tusiwe wazungumzaji wazuri wa lugha hii?

Cha kushangaza sisi ndiyo tumekuwa wa kwanza kukibeza Kiswahili, kukidharau na kukichafua katika uzungumzaji kuliko hata wenzetu ambao tunawaita wachanga katika lugha hii.

Je tuwatumie Majembe Auction Mart, ili watusaidie kuwakamata hawa wanaoendelea kukiharibu Kiswahili, kukibeza na kukidharau?

Kwa jinsi hali ilivyo, Kiswahili kinazidi kupigwa kumbo na kuendelea kudhalilishwa. Nadhani kuna haja ya kuwa na nguvu za ziada kukilinda na kukitetea hasa katika kipindi hiki cha utandawazi.

Sikatai kuwa Kiswahili kinaendelea kukua licha ya vikwazo vingi kinachopata.

Shida yangu ni jinsi Watanzania tunavyozidi kukidharau na kukikwaza Kiswahili; kinyume na wageni wa mataifa mbalimbali wanavyokithamini na kuona kuwa ni lugha inayokua na inafaa kulindwa na kukuzwa kwa manufaa ya wazungumzaji wake hapa Afrika Mashariki, kitovu ikiwa ni Tanzania.

“Hakika nabii hathaminiwi kwao”. Usemi huu unaweza kuhitimisha yale ninayoyafikiria kuhusiana na Lugha hii kwani kwa hakika Kiswahili hakithaminiwi hapa nchini.

Upo ushahidi wa kutosha unaoonesha kuwa Kiswahili si chochote kwa Watanzania; hatuoni umuhimu wa lugha hii kabisa, ingawa tunajua bila shaka kuwa kimetutoa tongotongo na kutufikisha hapa tulipo.

Hakuna lugha yoyote iliyotetea maslahi ya Taifa letu kama Kiswahili. Ni Kiswahili kilichotumika katika harakati za kudai uhuru na hatimaye kutuletea uhuru na umoja wa kitaifa ambao matokeo yake ni utulivu.

Utulivu na amani ndivyo vilivyotuwezesha wasomi kusoma, na kupata madigrii yanayotupa kiburi na kukidharau Kiswahili hivi leo.

Napenda kukiri kuwa si wote, lakini wapo watu wa namna hiyo na wengine ni viongozi tena wenye dhamana kubwa waliyopewa ama na Rais au wananchi.

Nilikwishasema kuwa upo ushahidi unaoonesha kuwa Watanzania bado hatujakithamini Kiswahili, zaidi sana tunaendelea kukibeza na kuona kuwa si kitu cha kushikamana nacho.

Kwa mfano, mpaka sasa ni miaka 49 tangu tupate uhuru, miaka 43 tangu Kiswahili kutangazwa kuwa lugha ya Taifa, lakini hadi sasa bado hatuna sera ya lugha inayoeleweka ili kukilinda Kiswahili na kuvipa nguvu vyombo na taasisi zinazosimamia maendeleo ya lugha hii ili kuwa na uwezo na udhibiti halisi wa matumizi mabovu ya lugha ya Kiswahili.

Vyombo na taasisi kama BAKITA, TATAKI bado havijapewa uwezo wa kutosha kisera katika kudhibiti matumizi ya lugha ya Kiswahili hapa nchini.

Kama ndivyo, nani atusaidie kazi hii? Katika kipindi chote hicho cha miaka 43 tangu Kiswahili kutangazwa kuwa ni lugha ya Taifa bado kuna ubishi na upinzani mkubwa miongoni mwa wasomi kuhusu lugha ya kufundishia.

Wapo wanaokubali Kiswahili kitumike kufundishia katika ngazi zote za elimu lakini bado wanapata upinzani kwa wale wanaokataa kuwa Kiswahili bado na kuwa hakifai, na hakijafikia kiwango cha lugha ya kufundishia. Hapa mimi huwa najiuliza ni lini basi Kiswahili kitafikia hatua hiyo?

Mimi ninaamini kuwa kitu chochote kikiwa katika matumizi, hukomaa na baadaye kinafikia ubora katika matumizi yake. Hivi bila kukitumia utajuaje ubora wake?

Je, lugha ya Kiswahili itafikia hatua ya kufundishia hivi hivi bila kutumika? Lugha hizi za “tutakuajiri lakini tunahitaji uzoefu wako wa muda fulani”, zimepitwa na wakati kwa sababu uzoefu huo nitaupata wapi kama hujaniajiri?

Hii ni dhana potofu kabisa. Huwezi kutaka kujua mtu alifanyaje kazi kama hujawahi kumpa kazi. Nadhani umefika wakati sasa, tuitumie lugha ya Kiswahili ili iimarike katika matumizi yote, hata ya sayansi na teknolojia yanayowatia hofu wasomi hawa.

Ushahidi mwingine unaonesha kuwa Watanzania hatuoni Kiswahili kama lulu ya Taifa, ni kuwa siku hizi kuna mfumuko wa wazazi kupeleka watoto wao kusoma nje ya nchi au ndani ya nchi wakitafuta Kiingereza katika shule hizo wanazoziita “English Medium”, hata kama shule hizo si bora na mitaala yake haiendani na mitaala na maadili ya Kitanzania.

Kinachotafutwa huko ni Kiingereza,mtoto akijua kuongea Kiingereza, hapo mzazi huridhika na kuona kuwa sasa mtoto wake kaenda shule. Hivi shule ni Kiingereza tu? Hivi mtoto huyo anajifunza maadili gani katika utamaduni wa watu.

Je, atakuwa mzalendo wa kweli? Ataifaa vipi nchi yake? Tujiulize Watanzania kinachotushinda sisi kujifunza Kiingereza ni nini? Mbona zipo nchi nyingi duniani zinazozungumza na kuthamini lugha zao na bado wanafahamu kuongea lugha nyingine za kimataifa. Kasumba yetu ni ya nini? Tatizo ni nini?

Je tunataka kujenga jamii ya namna gani? Jamii isiyofahamu lugha yake! Jamii inayofahamu lugha yake nusunusu na Kiingereza nusunusu. Narudia haya ni maswali ya kujiuliza.

Kwa mfano; ongezeko la shule za awali na msingi zinazofundisha Kiingereza ni kubwa na litakuwa tishio baada ya miaka kumi ijayo.

Mfano, hadi Julai 2009 kulingana na takwimu za Wizara ya Elimu, shule 15,257 zilikwishasajiliwa hapa nchini, tukiacha sekondari. Je ni watoto wangapi wanaofundishwa kuwa Kiswahili si lugha ya maana? Kiswahili ni lugha ya wasiosoma, Kiswahili ni lugha ya bibi na babu nyumbani.

Hili ni kweli, kwani katika mitaala yao, somo la Kiswahili halipo au limepewa umuhimu kidogo sana; ikiambatana na adhabu zinazotolewa kwa wale watakaozungumza Kiswahili. Hii ni hali ya kufifisha kabisa juhudi za kuiendeleza lugha ya Kiswahili miongoni mwa watoto na wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma katika shule hizo.

Je, tutajivuniaje utaifa na utamaduni wetu? Tunajenga taifa la namna gani? Hali hii ikiendelea, upo wakati ambapo Watanzania watahitaji kujifunza lugha ya Kiswahili nchini mwao kama wafanyavyo wageni. Kitu ambacho ni cha ajabu kabisa, na hii ni kuonesha jinsi ambavyo bado hatujajikomboa kifikira.

Sasa tufanyeje, tuwatumie Majembe watukamatie watu hawa? Yawezekana pia Majembe si watu muafaka wa kufanya kazi hii ya wenzetu wachache ambao wanakiuka umoja wetu wa kuiendeleza lugha yetu azizi ya Kiswahili, lakini naomba Watanzania wenzangu tusaidiane mawazo.

Hii ni kuonesha jinsi ambavyo hatuthamini lugha yetu ya Kiswahili na kung’ang’ania cha watu ambacho pia hatukiwezi.

Chanzo: http://www.habarileo.co.tz/uchambuzi/?n=5235
 

Forum statistics

Threads 1,250,853
Members 481,494
Posts 29,747,788