Wananchi wagoma kupokea mradi wadai una harufu ya ufisadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wananchi wagoma kupokea mradi wadai una harufu ya ufisadi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Sep 5, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Sep 5, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,813
  Likes Received: 83,194
  Trophy Points: 280
  Wananchi wagoma kupokea mradi wadai una harufu ya ufisadi
  Na Daniel Mjema, Hai
  Mwananchi

  WAKAZI wa Kijiji cha Mtakuja, jana walimweka kiti moto Mbunge wa Jimbo la Hai,Fuya Kimbita kuhusiana na mradi wa maji wakidai kuwa kuna harufu ya ufisadi kama ilivyotokea kwa kampuni ya kufua umeme ya Richmond.

  Tuhuma nzito zilitolewa na wananchi katika mkutano huo huku wakishangazwa na shinikizo la kutakiwa kupokea mradi huo wakati utafiti wa kimaabara umeonyesha kuwa maji hayo ya kisima ni hatari kwa afya za binadamu.

  Mwenyekiti wa Kitongoji cha Upareni, Bakari Saidi, alishangazwa na hatua ya kulazimishwa kupokea mradi huo na kusema kuwa shinikizo hilo lina mkono wa mtu nyuma yake kwa sababu si la kawaida.

  “Mimi nashangaa maji yanakuwa kama kampeni ya Urais, ulituahidi majisafi na salama sio haya ya kisima cha Mjapani ambacho hata wao waliacha kukitumia kwa sababu maji yake si salama,” alidai Saidi.

  Ernest Mweupe alimweleza Mbunge huyo waziwazi kuwa kamwe hawatakunywa maji hayo kwa sababu kilijengwa mahsusi mwaka 1989 kwa ajili ya kupatikana maji ya kilimo cha umwagiliaji na maji ya mifugo na si binadamu.

  Mwananchi huyo alipasua jipu pale alipomweleza Mbunge huyo kuwa kama hawezi kuwapatia majisafi na salama kutoka mradi wa Losaa-Kia basi mwaka 2010 atapatikana Mbunge atakayewatimizia hilo .

  Alisema mwaka 2006 waliambiwa zimepatikana Sh300 Milioni wachague mradi na walichagua mradi wa majisafi na salama kutokea Losaa-Kia, lakini wanashangazwa kushinikizwa kutumia maji ya kisima hicho.

  Mhudumu wa Afya kijijini hapo, Teddy Mweupe, alisema utafiti uliofanywa na mtalaamu toka Marekani kwa kushirikiana na wataalamu wa Tanzania umethibitisha kuwa maji hayo yanapindisha miguu ya watoto na kuharibu meno.

  Akijibu tuhuma hizo,Kimbita alisema mradi huo utasimama ili kuruhusu wataalamu washauri wafanye utatafiti upya kuhusu ubora wa maji hayo ya kisima yanayolalamikiwa.

  “Kama maji yataonekana kuwa yanafaa au hayafai kwa matumizi ya binadamu mtaambiwa, lakini yanataka yaongezewe kitu cha kitaalamu ili yafae kwa matumizi ya binadamu, pia mtaambiwa baada ya utafiti,” alisema Kimbita.

  Mbunge huyo alisema endapo itabainika kuwa hayafai kabisa itabidi lijengwe tenki na maji yachukuliwe mradi wa Losaa-Kia, lakini kwa masharti kuwa maji hayo yatatumika tu kwa ajili ya kunywa na si kwa matumizi mengine.

  Hata hivyo baadhi ya wananchi walipaza sauti wakisema hawaoni sababu ya kufanyika kwa utafiti upya wakati ripoti ya utafiti wa awali ipo na kutaka mjadala wa maji ya kisima ufungwe kwa sababu hayafai kwa matumizi ya binadamu.

  Mbunge huyo alilazimika kusimama tena na kuwaomba wawape ushirikiano wataalamu hao na kwamba mradi mpya wa majisafi na salama utatekelezwa kuanzia Januari mwakani kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB).
   
Loading...