Wananchi wa Hai tunamhitaji DC Kiongozi, sio Mtawala

MMASSY

JF-Expert Member
Jan 13, 2011
290
193
Nimemsikia Rais wetu mama Samia akitueleza vijana kuwa mkeka wa wakuu wa wilaya uko mbioni kutolewa na ameeleza wazi dhamira yake ya kuwaamini vijana.

Nikiwa kama mwenyeji wa wilaya ya Hai kijiji cha mbatakero kitongoji cha mlimafaru, naamini kabisa ninayo haki kama walivyonayo wengine ya kushauri aina ya DC anayetakiwa wilayani hapa kwa sasa ukizingatia tumetoka katika utawakaba DC kijana, korofi, Keurig na asiyeambilika.

Wilaya hii kwa kipindi chote cha miaka ya Sabaya, imepitia kipindi cha kuzoea matumizi mabaya ya miguvu isiyo ya lazima.Kwa bahati mbaya sana, wakazi wa eneo hili kuanzia Machame hadi tambarare ya longoi, kikavu na hata masama, haina watu wenye asili ya ukorofi hivyo hawakustahili kuwa na DC mkorofi kiasi kile.

Wilaya hii Ina Wachaga wa Machame ambao wako Machame, Masama na maeneo mengine, wakibosho waliohamia miaka ya 1970, Wapare walioko maeneo mengi ya tambarare, wamasai ambao wanakuja Hai kulisha mifugo yao na kuondoka wakati wa kilimo. Kwa upande mwingine, wilaya ya Hai ina watu wa kabila zote ambao kama ilivyo maeneo mengine, huna kwa ajili ya harakati za kimaisha ambao wengi wako maeneo ya Boma, Kwa Sadala, Kia na maeneo ya huduma kama kanisani, misikitini, shuleni, hospitalini n.k. Lakini wenyeji kabisa ni hao niliotaja mwanzo.

Wilaya ya Hai ina dini zote zilizoko nchini kama yalivyo maeneo mengine,na ni moja ya sehemu ambazo dini hizi zimekuwa zikiunganisha watu zaidi. Mfano eneo la kwa sadala ukitazama kanisa la KKKT na msikiti vipo sehemu moja na yanatazamana kama mtu na jirani yake. Wananchi wanasaidiana kiimani.Ikiyokea Muislamu anaabudu au anafunga utakuta Mkristu anamsaidia futari jioni. Kukiwa na shughuli za sherehe, mazishi n.k hutojua ni yupi wa dini ipi, watu wanaoendana, wanashirikiana na wanaheshimiana. Maeneo ya Maili sita so ajabu kukuta kipindi cha Eid wakristu wanasaidiana na Waislamu kupamba msikiti na kufanya usafi. Binafsi nikiri Hai hasa eneo la Maili sita ndiko nimeona msikiti ukipambwa mithili ya kanisa wakati wa Eid.

Baada ya maelezo hayo,naomba sasa nichangie ni aina gani ya DC anayehitajika Hai kwa sasa. Na ninatoa mchango huu bila kuingilia maamuzi ya Rais sababu yeye ndiye kikatiba mwenye mamlaka ya kumteua mtanzania yeyote kuwa mkuu wa wilaya kama atakidhi vigezo vyake Rais.

Hai inamuhitaji DC mwenye kurudisha upendo,ushirikiano na ustaarabu. Kama nilichoeleza hapo juu,wilaya ya Hai ina makabila yote ya Tanzania.Ina watu wa dini zote na Ina vyama vyote vya siasa vilivyo hapa nchini. Hai ndiko anatokea kiongozi wa chama Kikuu cha upinzani chini CHADEMA. Kwa bahati mbaya, Sabaya alijiona kuwa amekuja Hai kupambana na Mbowe na Chadema yake.Ukifuatilia nyendo zake utagundua maovu yote aliyokuwa anayafanya kisingizio kikubwa ilikuwa ni kuua upinzani. Ni kweli kuwa kazi mojawapo isiyo rasmi sana ya mkuu wa wilaya ni kuimarisha chama chake, lakini sio kwa kufaranisha watu. Hai imekuwa kitovu cha ustaarabu kwa muda mrefu.

Viongozi wa vyama tofauti, dini tofauti wamekuwa wakikaa pamoja, wakipingana kwa hoja na sio mabavu.Ukitazama uchaguzi wa mwaka jana kwa mara ya kwanza kuna vijana waliotobolewa misumari miguuni kama Yesu,wapo waliowekewa matambara mdomoni, wakatekwa watu, wakaogopeshwa kama kwamba ndio uchaguzi wa kwanza kufanyika Hai. Mbunge wa sasa Saashisha na Mbowe ni ndugu wa familia kabisa.Lakini Sabaya alivuka mipaka,akatumia nguvu kubwa isiyo na ulazima kuumiza watu.

Watu waliopendana kwa muda mrefu,ambao ni ndugu unakuja Hai unaanza kuwafarakanisha,unatumia mabavu kama vile wewe ndiwe uliyeileta CCM wa kwanza Hai? Wakati unafanya hivyo, yupo Mwenyekiti wa CCM Mkoa ambaye ana maelewano mazuri na vyama vingine, yupo Mwenyekiti wa CCM wilaya ambaye ana maelewano mazuri kabisa na vyama vingine. Sishabikii Chadema Wala upinzani Hapana, hoja yangu ni kuwa, mkuu wa wilaya anayetakiwa Hai ni mtu mwenye uwezo wa kuponya majeraha, mwenye akihubiri amani, upendo na mshikamano. Rangi za vyama isiwe ndio kigezo cha DC kiutawala Hai. Mbowe angeweza kushindwa katika uchaguzi kama alivyowahi kushindwa huko nyuma. Lakini kutumia nguvu na kuwaumiza watu ili Mbowe ashindwe kumeacha maswali mengi kila Kona. Ukikaa na viongozi waCCM hawakukubaliana na namna nguvu ilivyotumika kuumiza watu kwenye uchaguzi.Wao wanaelewa namna ya kudeal na upinzani zaidi.

Pili, Hai inamuhitaji DC mbunifu,sio wa maagizo. Huko nyuma ndugu yetu Antony mtaka alikuwa DC Hai.Legacy aliyoiacha inamfuata kokote aliko. Hadi leo tunamkumbuka. Hakuwahi kuwagawia wananchi fedha Wala kuwatishia ili wampende. Aliwasaidia watu,akaishi nao kwa upendo,akawa kiongozi na sio mtawala. Wilaya ya Hai ina watu wanajitu mno,ukifuatilia historia ya Machame ambao ndio wakazi wa asili wa eneo hili kulikuwa na desturi kuwa binti hawezi kuolewa kwako kama huna "kabati ya mbeho" yaani friji, na kama kwenye familia yenu hakuna Stout haingemuwa rahisi kupata mke.

Tafsiri yake ni kwamba Hai ina watu wenye asili ya utafutaji. Kinachotakuwa ni DC atakayeweza kuwatafutia masoko wamachane wauze maziwa kama wale kina mama kule Kalali waliokuwa wa kwanza Afrika mashariki kuuza maziwa kwa ATM, anatakuwa DC atakayetafuta soko kwa ajili ya vijana wa Rundugai, mbatakero na Ngosero ambao wanakesha shambani kulima Mazao mbalimbali, anahitajika DC mbunifu atakayesaidia masoko kama Masama, Sadala, Maili sita kuongeza mapato na kujenga masoko zaidi ili Ari ya vijana isijeisha.

Anahitajika DC mwenye uwezo wa kumaliza tofauti za wakulima na wafugaji maeneo ya tambarare ambako mara nyingi wamasai huvamia na kulisha Mazao ya wakulima na kusababisha taharuki na uvunjifu wa amani.Hai tunahitaji DC mbunifu wa ajira.Wako vijana wengi tumemaliza vyuo na tuna ari ya kujiajiri, wako wenzetu ambao hawana elimu ya darasani lakini wana maarifa.Anahitajika DC kijana mwenye uwezo wa kushauriana na vijana wenzake na kuja na suluhisho la ajira kwa vijana wa Hai.

Pia wilaya ya Hai inahitaji DC mpenda maendeleo. Sehemu kubwa ya wilaya ya Hai ni Mashamba,kuanzia Machame hadi kimashuku, katiza longoi hadi TPC na masama hadi uswaa kote ni maeneo potential kwa kilimo. Ardhi ya Hai haihitaji mbolea ya ruzuku ya serikali ili tuvune. Kinachohitajika maeneo mengi ya tambarare ni maji tu basi. Sabaya amekuwa DC wa kwenda kula bata Arusha, kukimbizana na dada zetu wanaosoma vyuo, akasahau kuwa, angesaidia upatikanaji wa maji kama Yale waliokuja kuchimba watu wa Arusha na kuyapeleka huko(AUWSA)wananchi tungelima misimu mitatu kwa mwaka. Tunahitaji DC atakayeona aibu kuitwa DC wa Hai wakati maji ya mto Kikavu na weruweru yanakatisha katikati ya wilaya yake yanatirirka huku walio pembeni wakikosa maji hata ya kumwagilia mboga. Sabaya angefanya juhudi za kupandisha tu maji na kutengeneza mifereji Leo angekuwa na watu wengi sana wa kumuombea msamaha.

Kule ukanda wa juu(Machame na Masama) kuna ndizi nzuri na zinazoweza kuuzwa kokote duniani.Mandhari ya ukanda wa juu,Kati na chini wilayani hai unafaa kwa kuliko cha parachichi ambazo ni deal sana duniani kwa sasa.Pamekosekana viongozi wabunifu kuwaunganisha vijana na PASS na wadau wengine wachanhamkie fursa hiyo. Angepatikana DC mwenye utimamu akaonana na waziri wa Kilimo tayari wananchi wangesaidika. Wakati wa kampeni kule Rombo tulimsikia Prof. Mkenda alivyolisemea hiki kwa facts. Yawezekana Mlenda anatamani hili lifanyiwe Kazi,lakini viongozi wa wilaya zetu hawa wako tayari kuacha kukalia viti vyenye kuwavmburidisha washuke shambani? Wako tayari kushuka kwenye mashangingi na kuingia site? Wataacha lini kukodi mabaunsa wa kuwalinda? Watathubutu kuwa rafiki za wananchi kama walivyokuwa akina mtaka?

Wilaya ya Hai inahitaji chief organizer,yaani mtu wa kuyaweka makundi kadhaa ya wananchi pamoja.Vijana wawe kwenye vikundi waweze kuwezeshwa.Mama Samia kasema wazi inakuwa ngumu vijana kusaidika sababu hawana ushirikiano.Binafsi najionea huruma na kumwonea mama huruma pia. Nani awaunganishe vijana?Hai inamuhitaji DC mwenye kipaji hicho.Kikichokosekana hapa ni elimu na skills za kuorganise tu. Hii wilaya wanatoka matajiri wakubwa nchi hii. Tunavyoona mabasi ya mikoani huko kuanzia Machame Safari, Lim sijui, sijui Ulomi wa Panone na Dar lux wote hawa ni matajiri wa machame. Tunapoona akina Nsilo Swai, akina Mengi, Mbowe n.k hawa wote ni kutoka Hai na wana moyo wa utoaji kama wakiwa na uhakika fedha zao hazitapotea kizembe. Hatumhitaji DC aina ya Sabaya atakayekuja kuwaomba Rushwa ili wakikataa awabamkizikie kesi za kuhujumu mataruma ya meli Wala kuwavamia majumbani na mabaunsa kuwanyang'anya pesa. Hai anatakuwa DC mwenye uelewa sana wa namna ya kuwatumia matajiri kwa maslahi ya wengi.

Hai ni wilaya inayofaa sana kwa uwekezaji. Ukianzia kule karibia TPC, mijengweni, Kimashuku, longoi, Kikavu, ukakatisha Rundugai hadi Kia ukageuja kuja bomang'onbe kuelekea Nronga, Kalali, mferejini na ukaenda hadi Lyamungo ukageukia Narumu yote ni maeneo yanayofaa kuwekeza viwanda, Mashamba na watu wakapata ajira. Hai haihitaji DC kama Byakanwa aliyevamia Mashamba ya familia ya akina Mbowe na kuikatakata na kuharibu miundombinu, Wala haihitaji akina Sabaya wa kuwavuruga wawekezaji wenye Protea Hotels na weruweru Lodge Hapana. Yaani anahitajika DC anayekusanya sio kutapanya. Mashamba mengi hai hayalimwi kutokana na kukosekana maji tu, ipo mito mikubwa ambayo ukipata viongozi wenye maono hakuna wilaya utakuta hii hapa kaskazini kwa kuzalisha mbogamboga na matunda.

Mwisho lakini sio kwa umuhimu,Hai inahitaji DC mwenye kujali huduma za kijamii kwa ujumla wake.Serikali imejitahidi kujenga shule maeneo mengi lakini bado zipo changamoto za umbali. Fikiria kutoka kijiji changu mimi cha Mabatakero,mwanafunzi akifaulu shule ya msingi anatembea km 18 kufuata shule ya kata. MwanafunI huyo alikuwa akitembea km 6 kila siku kufuata shule ya msingi. Hakuna wa kulaumu hapa.maeneo mengi ya wilaya ya Hai ni Mashamba makubwa ambayo watu huja kulima na kuondoka. Kaya za maeneo ya tambarare ni chache na ziko dispersed. Anahitajika DC mjanja wa kushirikisha wananchi,baraza la madiwani na matajiri wa Hai wajenge mabweni tu basi.

Wanaanchi hatutashindwa kuchangia gharama na hata chakula cha wanetu.Tukishindwa sisi ambao hatuna mapesa basi tunahitaji DC mwenye kuelewana na matajiri wa Hai na wawekezaji watusaidie.Naziomba sana mamlaka za nchi hii zisituletee DC wa kuwapiga mkwara walimu, sijui usipofaulisha nakuweka ndani, hapo tutarudi kule kwa Sabaya mbaya. Sielekezi mamlaka ni nani wa kutuletea Hai, Wala sijipigii debe Wala kumpigia debe yeyote. Ninatoa maoni yangu kama mwananchi mwenyeji kabisa na mwenye kuijua japo kwa kiasi wilaya yangu,lakini kama kijana aliyesomea uongozi, siasa na Utawala wa watu.

Napendekeza kuomba, kukesha nikiomba dua ili wilaya ya Hai ipate kiongozi mwenye maono,anayeweza kututoa alikokuwa ametutumbukiza Sabaya. Tunatamani kuona nuru iangazayo,tuendelee kupendana achilia mbali tofauti zetu, kipindi cha kampeni na wakati mwingine chama kishinde kwa hoja, mikakati na wananchi wabaki salama ili Mbowe aendelee na mambo yake bila kuumizwa watu, matajiri na walalahoi kama sisi tuendelee kuishi kwa kutegemeana na kuchukuliana kama ilivyo kawaida yetu.

Nausubiria mkeka kwa hamu.

Jerome Mmassy

Mbatakero- Hai

0623141643
 
Mtaletewa, msiwe na hofu! Na akianza maupuuzi yake kama ya huyo mliyemsema anaondolewa mzobe mzobe! Mama hadi muda huu kaonesha hana ushkaji kwenye teuzi zake, Ukimzingua anakuzingua (Ref. Chalamila, Sabaya, Kakoko, DED Temeke, jamaa wa DART na wengineo wengi). Na ukimletea uchawa, mapambio na kujipendekeza ndiyo unaharibu kabisa.
 
Hivi ndivyo UDC Unavyotafutwa.

Ndugu Jerome Mmassy kuna wilaya haina mchanganyiko wa makabila Tanzania?

Kuna wilaya ina watu wakorofi?
 
Nikiletwa mimi, mchakamchaka wake mtausikilizia. Mtachapa kazi mpaka muhame Wilaya! Inaoneka ninyi ni wapiga porojo sana mtafikiri ni ninyi tu ndio mna DC. Subiri nije!!
 
Namba kwaajili ya vetting, kama Mama ataona ikimpendeza, amjumuishe kwenye mkeka.
Sitegemei vetting Wala nini,maandiko yangu yote huweka namba za simu na naruhusu maoni ya simu,sms n.k..
 
Hivi ndivyo UDC Unavyotafutwa.

Ndugu Jerome Mmassy kuna wilaya haina mchanganyiko wa makabila Tanzania?

Kuna wilaya ina watu wakorofi?
Unaruhusiwa kukosoa kwa kuonyesha uelekeo tofauti.Lakini nakukosoa,huwa siandiki kutafuta huo unayosema ni udc.Nina haki ya kuandika maoni yangu kutokana na ninavyofahamu wilaya yangu hii.Wewe pia ukiandika kuhusu ya kwako utakuwa umetusaidia sana.Unavyosikia mkoa Maalum wa kipolisi au kanda Maalum huwa unahisi unaalum wake unatokana na nini?
 
Nikiletwa mimi, mchakamchaka wake mtausikilizia. Mtachapa kazi mpaka muhame Wilaya! Inaoneka ninyi ni wapiga porojo sana mtafikiri ni ninyi tu ndio mna DC. Subiri nije!!
Karibu sana.Sisi ni wachapa kazi kuliko unavyodhania.Sio ajabu wewe ndio utaukimbia ukuu wenyewe wa wilaya.Nadhani kule kwenu wanahitaji pia juhudi zako za mchakamchaka.Ha haaa
 
Back
Top Bottom