Wananchi hawana imani na Bunge kwa kuwa wabunge hawajatimiza wajibu-Uchambuzi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,794
287,947
Posted Date::12/18/2007
Wananchi hawana imani na Bunge kwa kuwa wabunge hawajatimiza wajibu-Uchambuzi
Na Mathew Kwembe

INAWEZEKANA kitendo cha Bunge kumsimamisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini kilichangia wananchi kukosa imani nalo lakini sababu inayolikosesha umaarufu bunge hilo inajulikana.

Ukiacha siku ambayo Bunge hili lilifunguliwa kwa hotuba ya kihistoria ya Rais Jakaya Kikwete, Desemba 30, 2005, na sasa linakaribia miaka miwili, imani ya wananchi kwa Bunge hilo imeshuka.

Kwanza wananchi walilijenga imani kwa Bunge kwa kuzingatia kuwa lilikuwa linabeba dhamana kubwa ya kuwakilisha mawazo ya wananchi walio wengi, ni wazi kuwa waliwaamini wabunge wao na ndio maana wakawapa kura zao.

Sasa mwakilishi huyo wa wananchi ama kwa utashi wake au kwa ajili ya uwajibikaji wa pamoja wa Chama anapoamua kukaa kimya, ni wazi anamuangusha yule aliyempa dhamana ya kumwakilisha.

Katika kipindi cha miaka miwili ya uhai wa Bunge hili yapo mambo mengi yaliyojitokeza ambayo yameweza kusababisha Wapigakura kukosa imani na Bunge na watendaji wake.

Ingekuwa afadhali sana kama mambo mengi yanayosababisha wananchi kukosa imani na Bunge yangetokana na udhaifu wa kanuni zake, lakini mengi yanatokana na tatizo la kiitikadi linaloota mizizi.

Kwa kutazama jinsi mwenendo wa shughuli za Bunge ulivyo utaona kuwa kumekuwa na hali ya kusingizia udhaifu wa kanuni zilizopo katika kulinda maslahi ya itikadi za kichama zaidi.

Hali kama hiyo ndiyo inayopelekea hasira kwa wananchi dhidi ya wawakilishi wao.

Ukiacha suala la wabunge wa Chama Tawala, na wale wa upinzani kila mmoja kujali maslahi ya vyama vyao jambo lingine ni hali iliyopo ya kiutendaji ya wabunge wetu kuwa kama wafadhili kwa wananchi.

Kutokana na hali ya kipato kati ya wawakilishi na wanaowakilishwa kuwa kubwa imejitokeza dhana kuwa wawakilishi hawa huonekana kama wafadhili.

Wabunge huwaona Wapigakura wao kama kero kwa kuwa kila mara Wapigakura hulazimika kuwaeleza wabunge shida zao za kifamilia hasa zinazotokana na umasikini.

Katika hili utaona kuwa kumekuwa na hali ya kujengeka kwa chuki miongoni mwa Wapigakura na wabunge kwani kila mmoja anaona kuwa mwenzake ni kero.

Katika hali ya kawaida baadhi ya shughuli ambazo wananchi wanawalilia wabunge hazikupaswa kuendeshwa katika mtindo wa kusaidiana kindugu bali zilipaswa kufanywa kiserikali.

Wabunge wamesahau majukumu yao ya kuisimamia na kuikosoa Serikali badala yake wamekuwa wakizingatia zaidi kutatua matatizo ya wananchi kama vile kulipia karo watoto, na hela za chakula.

Mbali na fikra za aina hiyo ambazo ni majukumu wanayobeba kimakusudi kwa lengo la kulinda kitumbua chao hayana tija kwa maendeleo ya umma wa Tanzania ambao umewapa dhamana kubwa.

Hivi mbunge unapokuwa na majukumu ya kumsaidia mtu mmoja mmoja katika jimbo lako la uchaguzi, huoni kama unachofanya ni ubaguzi wa makusudi? Je wale Wapigakura walio mbali nawe watafaidika na nini?

Hali kama hiyo ndiyo inayopelekea baadhi ya wabunge kushindwa kwenda kwenye majimbo yao ya uchaguzi kwa wakati hadi wawe wamejiandaa kikamilifu kuwasaidia Wapigakura wao. Hiyo si sawa hata kidogo, kwani pamoja na kuwa Wapigakura wanataka maendeleo lakini wanachohitaji zaidi ni maendeleo ya jumla katika jimbo lao. Unapotaka kumsaidia mtu kuondokana na umasikini usimpe fedha bali mpe mshipi akavue.

Katika hali kama hii wabunge hawa wanawazoesha vibaya wananchi kutojituma zaidi kufanya kazi ili waweze kujimudu wenyewe kimaisha.

Katika mazingira hayo hayo ya kulinda kitumbua chao kwa ajili ya uchaguzi wao, wabunge wanashindwa kuwakemea wananchi wasiowajibika.

Zipo mila potofu kama ukeketaji kwa watoto wa kike, na baadhi ya maeneo yenye matatizo ya wafugaji na wakulima kung�ang�ania sehemu moja ya ardhi suluhisho halipatikani kwa sababu za kisiasa.

Wabunge na Bunge kama taasisi mnapaswa kusimama kidete kutafuta mbinu za kuiondoa nchi katika lindi la umasikini badala ya kufanya kazi ya ufadhili ambayo hamuwezi kusaidia kila mtu.

Maelfu ya vijana wanaomaliza shule wanakosa shughuli za kufanya kutokana na kukosa mwongozo utakaowavuta kubaki vijijini, na kama wabunge mlipaswa kutafuta mbinu za kuwavuta vijana hawa.

Kadhalika vijana wanaokaa mijini wasio na kazi nao wanapaswa kutengenezewa mwongozo mzuri wa kimaisha ambao utawawezesha kufanya shughuli zao halali badala ya kuishia kukaa vijiweni.

Kuhusu miundombinu hali nayo imekuwa ni ya kusikitisha mno, katika kipindi cha miaka miwili cha Bunge hili barabara zilizotengenezwa zinaweza kuwepo lakini chache mno.

Kwa hali hiyo utaona wazi kuwa wananchi wanazidi kupoteza imani na utendaji wa Bunge hili kwa kuwa mchango wake katika maisha yao ni mdogo.

Kwa ujumla uwajibikaji wa wabunge iwe mmoja mmoja, au kama taasisi kuna fursa kubwa kwa wananchi kuamua kama Bunge linastahili hadhi iliyonayo au la. Kama hali itaendelea hivi hivi ni wazi hadhi ya Bunge itazidi kuporomoka.

Uamuzi dhidi ya Mbunge Zitto Kabwe mbele ya macho ya Watanzania ilikuwa ni kama kutonesha kidonda cha machungu. Umeibua mengi!

Kama wabunge watazingatia kweli viapo vya kazi zao wakati wanaapa kwa Spika wa Bunge mbele ya macho ya Watanzania, lazima hadhi ya Bunge itarejea.

Mathew Kwembe ni Mwandishi wa Makala wa Gazeti la Mwananchi:mmethew@yahoo.com
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom