Wanajf msaada wa matibabu unahitajika kwa kijana huyu

Mr EWA

JF-Expert Member
Mar 15, 2007
332
225
Heshima Kwenu wote!
Kwa imani niliyonayo humu ndiko kuna waungwana na wazalendo wengi zaidi,

Katika kupitia gazeti la mwananchi nimekutana na habari hii hapa chini na ikanigusa sana nikafikiria niwashirikishe na wenzangu pia na sina hakika kama kuna baadhi yetu ameileta huku na kama imefika naomba mniwie radhi kwa kuirudia. Naombeeni tumsaidie kijana huyu ndugu zangu ili aweze kupata matibabu.





Mtoto Abdulaziz hana sehemu ya haja kubwa Send to a friend
Saturday, 16 July 2011 18:56
0diggsdigg
* ANATOLEA SEHEMU YA TUMBO, ANAHITAJI MSAADA WA KUFANYIWA OPERESHENI KCMC
Na Julius Magodi
Abdulaziz Tumboni
Ni saa 4.00 asubuhi, ninafika katika nyumba ya familia ya Hassan Ali Kapela, ninapokelewa na mtoto mdogo wa kiume ambaye ananisalimia huku akiwa amejawa tabasamu usoni.

Ninamshika mkono na kukaribishwa na mwenyeji wangu, Mzee Kapela kuketi kwenye kiti nje ya nyumba hii iliyopo katika Kijiji cha Kiru Ndogo, Wilaya ya Babati mkoani Manyara. Hata hivyo, tabasamu hili la mtoto huyu baadaye ninagundua kuwa limeficha machungu na shida nyingi ambazo anazipata tangu azaliwe.

Mtoto huyu, Abdulaziz Abbas (2), alizaliwa akiwa hana sehemu ya kutolea haja kubwa. Anaishi vipi? Mama yake mzazi, Salma Sehho (26) anasimulia kuwa baada ya kujifungua Februari 26, 2009, hakujua kama mtoto wake hakuwa na sehemu ya kutolea haja kubwa.

Anasema hata Mkunga wa jadi aliyemsaidia kujifungua mtoto huyo, Ashura Seif naye hakujua tatizo hilo, hivyo alianza kumnyonyesha huku akiwa na furaha ya kupata mtoto huyo wa kiume. Salma anasema furaha yake iligeuka masikitiko kesho yake asubuhi baada ya mtoto kuanza kulia huku tumbo likiwa linaonekana kujaa. Wakati mtoto huyo akiendelea kulia kwa nguvu, Mkunga Ashura alimkagua kila sehemu ya mwili wa mtoto huyo ndipo alipogundua kuwa hana sehemu ya kutolea haja kubwa kabisa. "Kwa kweli nilichaganyikiwa baada ya kugundua kuwa mtoto wangu alikuwa hana sehemu ya kutolea haja kubwa kama ilivyo kwa watu wengine," anasema. Salma anasema baada ya kungudulika tatizo hilo, kwa msaada wa shemeji yake, Mzee Kapela, Februari 28 walimpeleka mtoto Hospitali ya Mission ya Dareda, iliyopo Wilaya ya Babati kupatiwa matibabu.

"Kwa hakika hatukuwa na matumiani kama mtoto huyo ataweza kupona kutokana na hali aliyokuwa nayo kwa wakati huo," anasimulia. Wakiwa katika hospitali hiyo, madaktari walipomchunguza waliamua kumpa huduma ya kwanza ambayo ni kumfanyia operesheni ya kutoboa utumbo sehemu ya tumbo lake ili aweze kujisiadia kwa muda. Baada ya kufanyiwa operesheni hiyo na kuwekewa sehemu ya muda ya kujisaidia mtoto alitulia, walilazwa katika hospitali hiyo kwa siku tatu. Hata hivyo, Salma anasema madaktari wa hospitali hiyo walimweleza kuwa mtoto huyo anatakiwa kupelekwa haraka Hospitali ya KCMC, iliyopo mjini Moshi kwa ajili ya kufanyiwa operesheni ili apatikane sehemu ya kutolea haja kubwa.

"Madaktari walituambia kwamba ingawa amepata huduma hii ya muda, ili aweze kuishi anatakiwa kufanyiwa operesheni haraka ya kutobolewa sehemu ya kujisaidia kwenye makalio," anasema. Walipoulizia gharama za operesheni hiyo katika hospitali KCMC kupitia baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo ya Dareda waliambiwa ni Sh 800,000. Hata hivyo, ushauri huu wa madaktari wa hospitali ya Dareda ulikuwa ni sawa na pilipili kwenye kidonda, hawakuwa na uwezo wa kumpeleka katika hospitali hiyo.

Gharama za matibabu walizotumia katika hospitali hiyo kiasi cha sh 350,000 ambazo shemeji yake Mzee Kapela alikopa kutoka kwa majirani, ndio uwezo wao ulipoishia. Ingawa walihangaika kutafuta msaada wa fedha kutoka kwa watu mbalimbali, lakini walishindwa kupata kiasi hicho, wakaamua kumkabidhi mwenyezi Mungu mtoto huyo aweze kumlinda. Hatua hiyo ya kumwachia mungu amlinde mtoto wake ilichangiwa zaidi na mama huyo kuwa mzazi peke yake, kwani baba wa mtoto huyo, Abbas Safari alifariki dunia akiwa bado mjamzito.

"Uwezo mdogo ndio ambao umemfanya mtoto wangu mpaka leo sijampeleka Hospitali ya KCMC, nitatoa wapi kiasi hicho wakati mimi mwenyewe niko peke yangu mzazi mwenzangu alifariki nikiwa na mimba," anasema Salma. Mtoto anaishije? Abdulaziz anaishi kwa kufungwa kipande cha kanga kuzunguka tumbo na kifua, ili kuzuia anapojisaidia haja kubwa kumwagika chini.

Kipande hicho cha kanga, hubadilishwa kila baada ya muda ili kumfanya asikae na kinyesi muda mrefu. "Tunamfunga kitambaa cha nguo ili kuzuia kinyesi kisidondoke ovyo chini, " anasema Salma na kuongeza kuwa pamoja na kumfunga kitambaa pia humvalisha shati kuhakikisha kuwa hakuna uchafu unaoweza kuingia katika sehemu anayopitisha haja kubwa.

Salma anaomba wasamaria wema wamsaidie kumpatia fedha za kugharimia matibabu yake katika Hospitali ya KCMC ili mtoto wake aweze kuishi maisha ya kawaida. "Sina uwezo, ninaishi kwa shemeji yangu, ninaomba wenye uwezo wanisaidie mtoto wangu afanyiwe operesheni ili aishi kama watoto wengine," anasema.

Kwa upande wake, Mzee Kapela ambaye ni shemeji yake na Salma anawaomba wasamaria wema kujitokeza kumsaidia mwanamke huyo ambaye hana uwezo. "Mimi kwa sasa nawalea Salma na mtoto wake,lakini hata mimi sina uwezo wowote wa kumsaidia kumpatia matibabu mtoto Abdulaziz," anasema Mzee huyo. Anayeguswa kumsaidia mtoto Abdulaziz anaweza kutumia namba 0788 535130 au 0655 304336 kwa mawasiliano.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom