Wanafunzi wakutwa na majibu ndani ya chumba cha mtihani

Idimi

JF-Expert Member
Mar 18, 2007
15,055
10,596
Wanafunzi wakutwa na majibu ndani ya chumba cha mtihani
Na Abdalla Nsabi, Maswa

SAKATA la kuvuja kwa mitihani ya kidato cha pili inayoendelea kote nchini imeingaia hatua mpya baada ya baadhi ya wanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Binza mkoani Shinyanga kukutwa na majibu ya mitihani ya kemia na fizikia.

Hali hiyo iliwafanya wasimamizi wa mtihani huo katika kituohicho kuwanyanganya wanafunzi hao karatasi hizo na kisha kuzichana na kuwapatia karatasi zingine kwa ajili ya kufanyia mitihani hiyo.

Taarifa zinasema kuwa kuvuja kwa mitihani hiyo kulitokana na kufunguliwa katika maeneo ya ofisi za walimu wa shule hiyo bila kuwepo na ulinzi wowote wa kusimamia shughuli za ufunguaji huo.

Imeelezwa kuwa chanzo cha upatikanaji wa majibu ya masomo hayo ilitokana na mtihani ya masomo hayo kufunguliwa kinyemela na wasimamizi wa mitihani waliopangwa huku wakiwa na uhuru mkubwa baina yao hali iliyosababisha majibu ya mtihani huo kupatikana kwa njia ya fedha na undugu.

Mwanafunzi mmoja wa shule hiyo ambaye alikuwa ni mmoja kati ya waliokuwa wakifanya mtihani huo ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wenzake walipata majibu hayo kwa njia ya kuitwa ofisini mmoja baada ya mwingine na kutakiwa kurudi darasani na kutotoa siri ya kile walichopatiwa ofisini walikokuwa wameitwa na baadhi ya wasimamizi wa mtihani huo.

Alisema kuwa wakati wanafunzi hao wakirejea darasani walionekana kuwa na karatasi zilizokuwa zikionekana kuwa na majibu ya mitihani ya masomo hayo wakiwa wanayasoma kwa kuibia hadi hapo waliposhikwa nayo na mmoja wa wasimamizi ambaye inasemekana hakuhusishwa katika mpango huo toka awali.

"Ni kweli baadhi ya wanafunzi wenzetu waligundulika wakiwa na majibu ya mitihani ya masomo ya Kemia na Fizikia ambayo walipewa na baadhi ya wasimamizi waliokuwa wamewaita ofisini kwa minajili ya kupatiwa fedha na wengine wakipatiwa kutokana na kuwa na undugu na wasimamizi hao, ndipo baadaye waligunduliwa na msimamizi ambaye aliichukua karatasi hizo na kuzichana chana na kuwapa zingine mpya kuendelea nazo," alisema mwanafunzi huyo.

Ilibainishwa kuwa msimamizi huyo aliyegundua hujuma hizo aliwanyanganya wanafunzi hao karatasi za majibu na kisha kuzichana chana na kugawa karatasi zingine kwa wanafunzi hao na kuwaomba waendelee kufanya mitihani ya masomo hayo na kuweka ulinzi mkali akishirikiana na msimamizi mwenzake ambaye awakushirikishwa na wenzake katika mikakati yote iliyokuwa ikiendelea.

Alipoulizwa na waandishi wa habari waliotembelea shuleni hapo msimamizi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa madai siyo msemaji wa suala hilo alisema ni kweli aliichana mitihani hiyo kwa sababu ilikuwa tayari imejazwa majibu katika masomo hayo mawili yaliyofanyika kwa siku moja yote mawili.

Alisema hujuma hizo zilifanya na baadhi ya wasimamizi wenzake waliokuwa tayari wamepokea rushwa kutoka kwa wanafunzi hao na kisha kutolewa majibu hayo bila ya yeye kujua kutokana na kutengwa na wasimamizi hao wenzake.

Alizidi kudai kuwa wakati akigundua hali hiyo na kuyateketeza majibu hayo ya mitihani waliyopatiwa kwa kuyachana baadhi ya wenzake walianza kumlaumu wakimwomba aachene na hali hiyo kwa kuwa watamwezesha kwa lolote lile.

Mmoja wa watumishi wa idara ya elimu alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alikiri kuzisikia lakini alisema wao kama idara hawahusiki na uangalizi wa mitihani ya kidato cha pili ila waliahidi kulifuatilia suala hilo kwa ukaribu kwa kuwa linagusa idara yao na kuomba atafutwe mkaguzi mkuu wa shule wilaya kwa kuwa ndiye mwenye maamlaka hayo.

Akizungumzia hali hiyo msimamizi mkuu wa mitihani hiyo kutoka kanda ya magharibi, Bi Suzani Fedinandi alisema yeye si msemaji wa suala hilo na kuomba waandishi wawasiliane na msemaji mkuu wa kanda hiyo aliyepo mkoni Tabora, licha ya kupigiwa simu yake ya mkononi iliyonekana kutopatikana muda wote.

Lakini Bi Suzani alionekana kutokuwa na taarifa hizo na kuahidi kuzifuatilia shuleni hapo na kusema kuwa mitihani hiyo imemalizika jana katika shule hiyo.

Mitihani ya kidato cha pili imeonekana kuvuja katika baadhi ya shule za sekondari wilayani hapa ambapo shule nyingine inayoelezwa mtihani huo kuvuja ni shule ya wasichana ya Maswa iliyopo wilayani hapa.


Hivi huu usanii mpaka kwelye mitihani tunakuwa tunamkomoa nani?
Tuchmbe suala hili kwa undani.
 
Back
Top Bottom