X-PASTER
JF-Expert Member
- Feb 12, 2007
- 11,610
- 1,810
Wanafunzi Wa Sekondari Washindwa Kusoma Na Kuandika Sentensi Za Darasa La Kwanza!
Wanafunzi 14 wanaosoma katika Shule ya Sekondari Mgololo iliyoko Wilaya ya Mufindi, Iringa, wamebainika kuwa hawajui kusoma wala kuandika baada ya kutungiwa mtihani unaofanywa na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili wa Kiswahili wa kusoma na kuandika. Mtihani huo ulifanywa na wanafunzi wote wa shule hiyo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa shule hiyo, Jumanne Nyaulingo amemwandikia barua Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kulalamika kupelekewa wanafunzi ambao hawajui kusoma wala kuandika na akipendekeza warudishwe shule ya msingi.
Nyaulingo anasema alifikia hatua hiyo baada ya wanafunzi wa kidato cha pili kufanya mtihani na baadhi yao kuandika kwenye mitihani hiyo maneno yasiyosomeka, Yaani walichoandika ni kama Kilatini, hivyo tukashauriana kuwa yawezekana kuna wanafunzi ambao hawajui kusoma na kuandika na njia pekee ya kuwabaini ni kuwatungia mtihani rahisi unaofanywa na madarasa ya awali katika shule za msingi, alisema.
Wanafunzi hao wamegawanyika kaitka vidato mbalimbali kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne. Akasema kati ya hao 14, wanne ni wanafunzi wa kidato cha kwanza waliofaulu vizuri mitihani yao; lakini pia wazazi kwenda shuleni hapo kulalamika iweje watoto wao wafaulu wakati hawajui kusoma wala kuandika.
Nyaulingo alisema kutokana na hali hiyo, alipeleka malalamiko kwa DED na Mkuu wa wilaya kulalamikia hatua ya kupelekwa wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika, Nimepeleka majina ya wanafunzi 10 ambao wako kidato cha pili hadi cha nne ambao hawajui kusoma wala kuandika, lakini sijajibiwa barua yangu badala yake mtendaji wa kata ameelezwa suala hilo na DED amekuja shuleni hapo akanitaka nishauriane na walimu wa shule za msingi na shuleni hapo ili tuwasaidie wajue kusoma na kuandika. Mimi nimekataa kwa vile hapa shuleni sina walimu wenye ujuzi wa kumfundisha mtu ajue kusoma na kuandika, mimi naletewa walimu ambao ni wataalamu wa masomo ambao wana Stashahada na Shahada. Hiyo kazi ya kumfundisha mwanafunzi kusoma na kuandika inafanywa na walimu wa elimu ya awali, alisema mkuu huyo wa shule.
Alisema binafsi baada ya kubaini kuwapo kwa wanafunzi hao shuleni hapo, alipendekeza warudishwe shule ya msingi, lakini ikaonekana kuwa sera ya elimu hairuhusu mwanafunzi aliyehitimu shule ya msingi na kufaulu, haruhusiwi kurudi tena shule ya msingi, Hata kwenye mikutano ambayo tulifanya hapa na wazazi tulishauri warudi lakini ombi hilo limekataliwa na mamlaka husika, alisema Nyaulingo.
Kuhusu wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao walifaulu na wazazi wao wakaenda kulalamika shuleni hapo, alisema baada ya wanafunzi hao kufaulu wazazi wao walisita kuwapeleka shule na ndipo mtendaji wa kata akatishia kuwashtaki.
Alisema baada ya tishio hilo wazazi hao kila mmoja kwa wakati wake alienda na kijana wake shuleni hapo kulalamika kuwa analazimishwa ampeleke mtoto wake sekondari wakati anajua fika kuwa ataharibu fedha zake kwani mtoto wake hajui kusoma wala kuandika, Mtendaji aliwaambia awe anajua au hajui kusoma aliwataka watoto hao wawepo shuleni, lakini wazazi wakawa hawataki na baadaye waliwaleta nami nikataka kujiridhisha kwa kuwaandikia maneno ya darasa la kwanza ili wayasome lakini walishindwa, alisema.
Alimtaja mwanafunzi Happy Mwango aliyetoka shule ya Msingi Makungu ambaye alama zake za kufaulu ni 166 kati ya 250. Mwanafunzi huyo alishindwa kusoma sentensi zifuatazo Bibi anakula chakula. Mama analima bustani."
Mwanafunzi huyo alipelekwa shuleni hapo na mzazi wake Januari 3, mwaka huu. Mwanafunzi mwingine ni Rachael Mbilinyi aliyekuwa anasoma shule ya msingi Lugema.
Mtihani wa darasa la saba alifaulu kwa alama 106, lakini alishindwa kuandika maneno haya, "Shangazi, Popo" na pia alishindwa kusoma sentensi hii, "Babu ni mgonjwa sana."
Tilani Mbogela aliyetoka shule ya Msingi Makungu alishindwa kusoma sentensi, "Shangazi Ni mgonjwa," wakati Raymond Lukandema aliyetoka shule ya msingi Makungu na aliyefaulu mtihani wa darasa la saba kwa alama 144 naye alishindwa kusoma sentensi hiyo.
Chanzo: HabariLeo