Wanafunzi wa Sekondari Mpaka Chuo Kikuu: Pata Vitabu vya Masomo Mbalimbali Hapa

MADA YA TANO: USIMULIZI
Usimulizi ni jumla ya maelezo yanayotolewa na mtu au watu wengi kuhusu tukio fulani. Katika mada hii utajifunza juu ya taratibu za usimulizi wa matukio kupitia njia kuu mbili za masimulizi, yaani kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi. Pia utaweza kujifunza juu ya mbinu mbalimbali za usimulizi.
Usimulizi wa Hadithi
Usimulizi hufanyika kwa njia kuu mbili yaani kwa njia ya maandishi na kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Kila njia hutegemea namna msimuliaji anavyoweza kuwasiliana na msikilizaji. Ikiwa msimuliaji na msikilizaji hawakukaribiana, njia ambayo itatumika ni ile ya maandishi. Kwa mfano kama utahitaji kumweleza mtu aliyembali kuhusu tukio fulani la kusisimua utalazimika kutumia maandishi, yaani utatumia njia ya kumwandikia barua.
Lakini kama unamsimulia mtu ambaye yupo karibu nawe, utatumia njia ya mazungumzo ya ana kwa ana.
Usimulizi wa Habari
Taratibu za Usimulizi wa Matukio
Usimulizi wa matukio dhamira yake ni kumweleza mtu au watu tukio ambalo wao hawakulishuhudia. Hivyo katika usimulizi msimuliaji hutakiwa kutoa maelezo muhimu ambayo yatawawezesha watu hao kulielewa tukio linalosimuliwa sawasawa na huyo anayeshuhudia.
Mambo muhimu ya kutaja katika usimulizi wa matukio ni pamoja na haya yafuatayo:
  1. Aina ya tukio – msimuliaji atatakiwa kubainisha katika maelezo yake aina ya tukio. Kwa mfano, kama ni harusi, ubatizo, ajali ya barabarani au mkutano.
  2. Mahali pa tukio – ili msimuliaji aweze kuielewa habari inayosimuliwa, ni lazima kumwelewesha ni mahali gani tukio hilo limetokea. Kwa mfano, kama ni mjini inafaa kutaja hata jina la mtaa.
  3. Wakati – katika usimulizi ni muhimu pia kutaja muda ambao tukio limetendeka kama ni asubuhi, mchana au jioni bila kusahau kutaja muda halisi yaani ilikuwa saa ngapi.
  4. Wahusika wa tukio – ni muhimu kutaja tukio limehusisha watu gani, wingi wao, jinsia yao, umri wao n.k.
  5. Chanzo cha tukio – kila tukio lina chanzo chake hivyo ni muhimu kutajwa katika usimulizi.
  6. Athari za tukio – athari za tukio nazo ni sharti zibainishwe. Kama ni ajali, je watu wangapi wameumia; wangapi wamepoteza maisha n.k.
  7. Hatima ya tukio – msimuliaji katika usimulizi wake ni lazima abainishe baada ya tukio kutokea na kushughulikiwa hatima yake ilikuwaje. Kwa mfano, kama tukio ni ajali ya barabarani hatima yake inaweza kuwa majeruhi kupelekwa hospitalini na dereva aliyehusika kukamatwa.
Kwa hiyo misingi hii ya usimulizi hufanya usimulizi wa tukio kuwa na sehemu kuu tatu:
  • Utangulizi – sehemu hii huwa na maelezo tu ya utangulizi ambayo hulenga kuvuta hisia na umakini wa msikilizaji au wasikilizaji. Kwa kawaida utangulizi wa tukio huwa ni maneno machache kiasi yasiyozidi aya moja.
  • Kiini – kiini cha usimulizi huelezea tukio halisi kuanzia chanzo chake, wahusika, muda, mahali na athari za tukio.
  • Mwisho – mwisho wa usimulizi ni matokeo yanayoonyesha matokeo ya mwisho ya tukio linalohusika, wakati mwingine matukio haya yanaweza kuambatana na maelezo ya msimuliaji kuhusu mtazamo au maoni yake binafsi juu ya tukio ambalo amesimulia.
Mbinu za usimulizi
Ili habari inayosimuliwa ipate kueleweka vizuri, sharti msimuliaji ajue mbinu za kusimulia katika hali inayovuta hisia za msikilizaji wake.
Baadhi ya mbinu hizo ni uigizi, utumizi wa lugha fasaha inayozingatia lafudhi sahihi ya Kiswahili.
Kwa upande wa uigizi msimuliaji atatakiwa kuigiza mambo muhimu yanayohusiana na tukio ambalo anasimulia. Nayo ni kama vile milio, sauti na matendo.
Kwa upande wa usimulizi ambao unafanyika kwa njia ya maandishi, sharti usimulizi huo uwe na kichwa cha habari. Kichwa cha habari kinatakiwa kuandikwa kwa maneno yasiyozidi matano, yaliyoandikwa kwa herufi kubwa.
Kwa vile usimulizi wa tukio huwa unahusu tukio lililopita, maelezo yake mengi huwa katika wakati uliopita.
 
MADA YA SITA: UANDISHI WA INSHA
Uandishi Wa Insha

Uandishi ni kitendo cha kupangilia maneno katika maandishi. Mada hii inazungumzia uandishi wa insha za wasifu kwa umahususi wake. Kabla ya kuanza uandishi utajifunza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika uandishi wa insha kwa ujumla. Utaelewa muundo wa insha na mwisho utajifunza juu ya dhana ya insha ya wasifu na namna inavyoandikwa na mwisho kabisa utaangalia mfano wa insha ya wasifu.
Insha za Wasifu
Insha ya wasifu ni ile ya kutoa maelezo juu ya jinsi mtu au kitu kilivyo, tabia, vitendo na mandhari (sura ya mahali jinsi panavyoonekana).
Mambo muhimu katika insha ya wasifu ni: sura, rangi, umbo, vipimo, tabia, na kadhalika. Insha hizi zinaweza kuongelea kitu chochote kile, inaweza kuwa ni mnyama, mtu, Shule, nchi na kadhalika.
Hatua za Uandishi wa Insha
Kabla ya kuanza kuandika insha, ni muhimu sana uamue unataka kuandika juu ya nini. Inafaa uchague ile mada iliyo rahisi kwako kuweza kujieleza kikamilifu na kwa urahisi.
Kama unaandika insha za kufanyia mazoezi ni heri uchague mada zenye habari ambazo unazielewa. Iwapo hulijui au hulielewi jambo, ufanye uchunguzi kwanza. Ukisha kupata habari muhimu ndipo baadaye uandike insha yako kulingana na jinsi unavyoijua na jinsi unavyoikumbuka habari inayohusika.
Katika mtihani ni muhimu uyasome maagizo kwa makini. Kwa mfano, maagizo yanaweza kuwa: Chagua mojawapo ya habari zifuatazo kisha uandike insha isiyopungua kurasa mbili za karatasi za majibu.
Au:
Chagua mojawapo ya habari hizi kisha uandike insha ya maneno yasiyopungua 400.
Ni heri uandike insha nzuri ya kiwango kinachotakiwa kuliko ndefu (zaidi ya maneno 400) ambayo haitakuwa na mambo muhimu hadi mwisho, na pengine yenye makosa na uchafu mwingi kupindukia. Ni muhimu ikumbukwe jinsi insha ilivyo ndefu, hasa katika mtihani, ndivyo idadi ya makosa inavyozidi kuongezeka.
Muundo wa Insha
Katika uandishi wa insha, muundo wake unakuwa na vitu vifuatavyo:
  1. Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya n.k
  2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako.
  3. Kiini cha insha; katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.
  4. Hitimisho; hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichohadiliwa katika insha.
Hebu soma mfano ufuatao wa insha ya wasifu:
Mfano 1
SHULE YANGU
Shule yangu inaitwa Shule ya Sekondari ya Mwananchi. Ni shule ya zamani iliyoanzishwa siku ya Ijumaa, tarehe 5 Agosti 1966 na Mheshimiwa Donna Matembele, aliyekuwa diwani wa kata ya Masuba.
Shule hii ambayo ni maarufu sana ipo katika Tarafa ya Mkunazini. Imejengwa katika uwanja wa hekta kumi na mbili. Ina madarasa kumi na mawili ya vidato vinne vya mikondo mitatu kila kimoja. Ina wanafunzi mia tano na wanne badala ya idadi halali ya wanafunzi mia nne themanini. Ni shule inayopendwa sana.
Wanafunzi wa kike ni mia mbili na watatu na wa kiume ni mia tatu na mmoja. Walimu ni thelathini na mmoja. Jamii hii inapendana sana. Wanafunzi wana imani kubwa sana na walimu wao. Walimu huwahimiza wawe wanafanya bidii katika kazi na masomo kwa ujumla.
Wanafunzi hukadiria ugumu wa mazoezi wapewayo. Yale wayaonayo kuwa ni rahisi wao hujifanyia. Yale magumu kidogo hushughulikia kwa pamoja kwa kusaidiana wenyewe kwa wenyewe. Walimu hushirikishwa tu wakati wa mazoezi tata.
Shule ya Sekondari ya Mwananchi ni ya kuvutia sana. Ina miti mingi sana ya matunda. Ina maua ya aina aina. Kutokana na nidhamu na uwajibikaji matunda hukomaa ndipo yatumiwe kwa mpango wakati wa chakula.
Heshima imethaminiwa mno na wanafunzi. Wanaheshimiana na kuwaheshimu walimu wao. Kwao heshima ni utiifu na uzingativu. Kutii na kuzingatia mambo waambiwayo na walimu ndicho kipimo cha heshima.
Katika shule yangu wanafunzi tuko kama paka. Paka hamtumi mtu nyama lakini atunukiwapo kipande hawezi kumruhusu yeyote kukigusa. Nasi tutunukiwapo nafasi yoyote ya kusoma hatumruhusu mtu yeyote kutupokonya nafasi hiyo.
Wanafunzi wa shule wana sare zao za kuvutia wazivaazo kiungwana kabisa. Sare hizo ni sweta ya bluu, shati au blauzi ya samawati, tai ya rangi ya damu ya mzee, suruali ndefu au sketi ya kijani kibichi, viatu vyeusi vya soli ndogo na visigino vifupi.
Katika shule yetu kuna uhusianao mwema baina ya walimu, wazazi, Chama cha Wazazi na Walimu (CHAWAWA) na Baraza la Shule. Kamati ya CHAWAWA na Baraza la Shule huanzisha miradi na kuitekeleza haraka kutokana na wazazi kuiunga mkono.
Kwa muda mrefu sasa matokeo ya mitihani yamekuwa ya kuridhisha kabisa. Na si hayo peke yake. Wanafunzi washirikipo katika michezo ya mpira, ya riadha na matamasha ya muziki takribani mara zote huibuka washindi.
Kwa ufupi shule yangu ni ya mafanikio mengi.
Mambo muhimu ya kuzingtiwa katika insha hii ya wasifu:
  • KICHWA (Shule yangu).
  • MAELEZO KAMILI yenye:
  • JINA la shule
  • HISTORIA ya shule
  • MAZINGIRA ya shule
  • IDADI ya wanafunzi na walimu
  • HALI ya wanafunzi
  • MAFANIKIO ya shule.
  • HITIMISHO lenye sifa ya jumla.
Insha za Kisanaa na zisizo za Kisanaa
Tofautisha insha za kisanaa na zisizo za kisanaa
Zoezi 1
Tofautisha insha za kisanaa na zisizo za kisanaa
 
MADA YA SABA: UANDISHI WA BARUA
Uandishi Wa Barua

Barua za kirafiki ambazo pia huitwa za kidugu huandikwa baina ya watu wa undugu au jamii moja. Katika mada hii utaweza kujifunza muundo wa uandishi wa barua ya kirafiki na jinsi ya kuandika barua ya kirafiki. Utaweza kutofautisha kati ya barua ya kirafiki na ile isiyokuwa ya kirafiki.
Barua za Kirafiki
Iwapo ni katika ndugu barua za kirafiki zaweza kuwa kwa watu kama: baba, mama, shangazi, mume, mke, mtoto, na kadhalika. Katika jamii waandikiwao barua za kirafiki ni kama jirani, rafiki, mpenzi, mwalimu, mwanafunzi, daktari, mgonjwa, na kadhalika.
Muundo wa Barua za Kirafiki
Mambo muhimu ya kuzingatia katika uandishi wa barua za kirafiki:
  • ANWANI kamili ya mwandishi, katika herufi hukaa juu upande wa kulia mwa karatasi.
  • TAREHE, chini ya anwani.
  • MTAJO wa heshima kwa anayeandikiwa, kama vile, mpendwa, mpenzi, na kadhalika, huandikwa kushoto, baada ya tarehe.
  • UTANGULIZI wa barua yenyewe ambao kwa desturi huwa ni salamu.
  • BARUA YENYEWE ambayo ndiyo kiini cha waraka.
  • SALAMU za kumalizia, pengine kwa jamaa na jamii.
  • HITIMISHO, katika aya, maalumu ambayo huwa, kwa mfano: ‘Ni mimi baba yako akupendaye,’ na kadhalika.
  • SAHIHI ambayo si sharti wala muhimu sana.
  • JINA au MAJINA ya mwandishi, mwishoni.
Tazama mfano wa barua ya kirafiki:
Mfano 1

MUSOMA FISH PACK
S.L.P 4546
MUSOMA
23/5/2013
Mwanangu Nyamchele,
Ninafuraha kukujulisha kuwa nimepokea barua yako. Mambo yote uliyoyaeleza nimeyaelewa barabara. Huku nyumbani sote tu wazima na ni matumaini yetu kwamba afya yako ni nzuri.

Tabia ya kulalamikia chakula ni mbaya. Tabia kama hii ikikomaa husababisha ulafi. Kumbuka hukwenda shuleni kula kama nguruwe. Huko shuleni nimekupeleka ili usome kwa bidii na ujifunze mengi. Usitamani kustarehe na kufikiria maakuli na anasa zingine za ulimwengu huu. Ondoa fikira za chakula akilini mwako na uache uzembe, eboo!

Hebu nikuonye kuhusu kuwapima na kuwachagua walimu. Walimu katika shule hiyo ni wabobezi na ndio maana nikakupeleka hapo. Wanajua mnayostahili kufundishwa. Huna ruhusa ya kusema eti walimu wengine ni wakali na hufundisha haraka haraka sana. Wewe unahitaji kutega sikio na kutii. Ukiwa makini na uwe na imani utayaelewa mambo unayofundishwa. Usisahau kuwa mchagua jembe si mkulima.

Mambo makubwa unayostahili kuyatilia bidii ni masomo yako. Muda wa miaka minne ni mfupi sana. Uonyeshe adabu njema kila wakati. Uwaonyeshe walimu wako taadhima na uwatii daima dawamu.
Jambo lililo kubwa katika shughuli yoyote ni uvumilivu. Ukivumilia utavuna matunda mabivu. Sitachoka kukusisitizia, ‘Ukilima pantosha, utavuna pankwisha.’ Fanya kila jitihada utimize mambo mengi iwezekanavyo kuanzia leo lakini usipapie chochote. Ndo ndo ndo hujaza ndoo.

Mungu akubariki. Umwombe akusaidie katika kila jambo. Ujiepushe na maovu yoyote yale. Ukiwa na jambo usiwe na hofu kutuarifu mara moja. Mama yako amekusalimu sana. Amenikumbusha nikupashe hakuna refu lisilo na ncha.
Kwaheri kwa sasa.
Ni mimi, baba yako akupendaye,
Magafu Malima
 

KIDATO CHA PILI​


MADA YA KWANZA: UUNDAJI WA MANENO
Uundaji wa maneno ni ujenzi au uzalishaji au utengenezaji wa maneno mapya. Uundaji wa maneno mapya husaidia kuongeza msamiati katika lugha ili kukidhi mahitaji ya mawasiliano. Uundaji wa maneno mapya husababishwa na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni na maendeleo ya kisayansi yanayotokea katika jamii. Kwa mfano tunayo maneno mapya, kama vile ufisadi, uwekezaji, ukeketaji, ujasiriamali na mengine mengi kutokana na mabadiliko ya kijamii.
Kutumia Uambishaji
Kubainisha Mofimu katika Maneno
Uambishaji wa maneno ni kitendo cha kupata maneno kwa kubandika Mofimu kwenye kiini cha neno, uambishaji kutokea kabla ya kiini cha neno au mzizi wa neno. Mfano kiini pig- unaweza kuunda maneno kama inapiga, anayepiga, mpigaji, amepigika nk.
Mofimu zinazobadilika kwenye kiini cha neno huitwa Viambishi.
Katika lugha ya Kiswahili viambishi hutokea kabla na baada ya kiini cha neno.
Mfano
Wanapendana = Wa-na-pendan-a kiini cha neno ni-pend-.
Mofimu zilizobadilisha baada ya kiini –an-na-a viambishi vinavyotokea kabla ya kiini cha neno huitwa viambisha awali au tangulizi. Viambisha vinavyotokea baada ya kiini cha neno huitwa viambishi tamati au fuatishi.
Example 1
Angalia mifano ifuatayo:
NenoViambisha AwaliKiini ViambishaTamati
Unapendeleau-na--pendael-e-a
Waliongozanawa-li--ongoz-an-a
Analimaa-na--lim--a
anayeiimbishaa-na-ye-imb--ish-a
Dhima za Mofimu
Bainisha dhima za mofimu
Baadhi ya dhima za uambishaji ni kama ifuatavyo:
  1. Kuonyesha upatanisho wa usanifu maana ya maneno yanayozalishwa kutofautiana katika msingi wa kusanifu tu, lakini uhusiano wa maneno hayo hutokana na kiini au mzizi wake uleule.Mfano;Fundisha kiini chake ni fund. Unaweza kuzalisha maneno mengine kwa kutumia mzizi/kiini kilichopo kama vile fundishana, mafundisho, mfundishaji, fundishwa, fundishana.
  2. Uambishaji huonyesha nafsi
  3. Uambashaji huonyesha njeo (muda)
  4. Uambishaji huonyesha urejeshi
  5. Uambishaji huonyesha ukanushi
  6. Uambishaji huonyesha hali mbalimbali za kitenzi
Vitenzi vikiambishwa huweza kujenga/kuunda/kuzalisha vitenzi vingine au nomino.
Example 2
Mfano

VitenziKiiniNominoVitenzi
Cheza-chez-Mchezaji, mchezowanacheza/atamchezea
Piga-pig-Mpigaji, Mpiganajiwatanipiga, aliyempiga/wanaompiga
Uambishaji hutumika kuzalisha viwakilishi na vielezi.
Neno (Kiwakilishi)KiiniKielezi
Huyu, HuyoHuHumu, humo
Wangu, wako,wakewa
Hii, hizo, hikihi
Viambishi awali vina dhima ya kudokeza nafsi, njia, idadi urejeshi na ukanushi.Mfano: Hawakulima
  • Ha-, kiambishi cha ukanushi
  • Ku-, kiambishi njeo/wakati
Viambishi tamati vina dhima mbalimbali hudokeza hali ya utendekaji, ukamilishaji au kimalizio cha neno na kauli za matendo kama vile kutendwa, kutendewa,kutendeka nk.
Dhima:Ukanusho, kutendeana, agizo na mtendwa, ukamilisho, usababishi.
Mfano 3
NenoViambishi Tamati
Anapiga-a
Wanapigana-an
Asipigwe-w
Amempigisha-ish-
Viambishi tamati vina dhima ya kutambulishwa mapema/nomino zilizoundwa kutokana na vitenzi.
NenoKiiniViambishi Tamati
Pigapig--o
Mchezochez--o
Mtembezitembe--z-i
Mfiwa-fi--us-a
Kutumia Mnyumbuliko
Mazingira yanayosababisha Mahitaji ya Maneno Mapya
Elezea mazingira yanayosababisha mahitaji ya maneno mapya
Mnyumbulisho ni neno linalotokana na neno nyumbua. Kunyumbua kitu ni kuvuta, kuongeza urefu wa kitu hicho.
Kunyumbua katika lugha ya Kiswahili ni kuongeza vinyumbulishi katika katika kiini ili kupata msamiati mpya. Hivyo basi, mnyumbulisho ni njia mojawapo na inasaidia kuunda maneno kwa njia ya kunyumbulisha.
Viambishi vinapochukuliwa katika kiini cha neno, basi neno hilo huwa limenyumbulishwa. Kwa mfano neno lima kiini chake lim- huweza kunyumbulishwa na kupata maneno mengine mpya, kama lim-ishwa, lim-ia, lim-w-a.
Pia maneno ya mnyumbulisho yanaweza kuundwa kwa kuongeza viambishi kwenye shina, kwa mfano:
NenoKiini Shina Maneno ya Mnyumbuliko
ElekeaelekelekaElekeana, elekea, elekwa, elekesha
ShikishanashikshikishaShikishana, shikisha, shikishaneni
Kwa ujumla tunawaza kusema kuwa maneno ya kawaida hunyumbulika. Hivyo kiini/mzizi au shina moja huweza kuzalisha maneno mengine mengi ambayo yanatokana na msingi mmoja wa maana.
Dhima ya Uambishaji na Mnyambulikoa wa Maneno
Dhima ya uambishaji ni kuleta upatanisho wa kisarufi, kuonesha idadi na umoja na wingi katika ngeli za majina, kuonesha njeo na kuonesha urejeshi pamoja na hali mbalimbali kwa uambikaji wa viambishi kabla ya mzizi wa neno. Aidha dhima ya mnyambuliko ni kuonesha matokeo ya tendo na kuzalisha kauli mbalimbali kwa kupachika viambishi baada ya mzizi wa neno.
Kuunda Maneno mbalimbali kwa kutumia Mnyambuliko
Unda maneno mbalimbali kwa kutumia mnyambuliko
Uundaji wa maneno mbalimbali kwa kutumia mnyambuliko hufanyika kwa kupachika viambishi baada ya mzizi wa neno na hivyo kulifanya neno husika liweze kuonesha matokeo mbalimbali ya matendo pamoja na kuzalisha kauli mbalimbali za matendo.
Zoezi 1
Unda maneno mbalimbali kwa kutumia mnyambuliko
Kutumia Maneno ya Mnyambuliko katika Miktadha mablimbali
Tumia maneno ya mnyambuliko katika miktadha mablimbali
Maneno ya mnyambuliko hutumika katika miktadha mbalimbali ambapo miktadha hiyo hujitokeza katika kauli mbalimbali za vitenzi. Kauli hizo ni kauli ya kutenda, kauli ya kutendwa, kauli ya kutendewa, kauli ya kutendea, kauli ya kutendeka, kauli ya kutendesha, kauli ya kutendana, na kauli ya kutendama.
Zoezi 2
Tumia maneno ya mnyambuliko katika miktadha mbalimbali
 
MADA YA PILI: MATUMIZI YA LUGHA KATIKA MIKTADHA MBALI MBALI
Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika.
Rejesta
Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani na kadhalika.
Kuwasiliana kwa kutumia Rejesta
Rejesta za Mitaani

Haya ni mazungumzo yanayozungumzwa magengeni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe. Ni lugha ambayo huchipuka kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo. Mfano wa maneno yanayotumika sana mitaani ni kama vile “Mshikaji” (rafiki) Demu” (mwanamke) n.k. Kwa ujumla lugha ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha iliyojaa maneno ya mitaani ambayo yanaeleweka kwa wazungumzaji wenyewe.
Mazungumzo ya Kwenye Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali)
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na kanuni maalum zinazojitokeza katika mazingira haya. Kutokana na kutumiwa kwake kwa muda mrefu kwenye mazingira yale yale.
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
  • Maofisini au mahali popote pa kazi
  • Mahakamani
  • Hotelini
  • Hospitalini
  • Msikitini
  • Kanisani n.k
Mazungumzo ya mahotelini yana utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.
Nani wali kuku?
B: Mimi
Chai moja wapi?
B: Hapa
Katika mazungumzo haya A anapouliza “Nani wali kuku”, ana maana kuwa nani anahitaji kula wali na nyama ya kuku”. Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaaye “wali kuku”.
Kwa upande wa lugha ya mahakamani ni tofauti na lugha ya hotelini. Lugha ya mahakamani inasisitiza usahihi ili kuondoa migongano miongoni mwa wanaohusika.
Mfano 1
Mfano:
Wakili wa Utetezi: Nakuuliza jaribio la kutaka kupindua serikali litakuwa kosa la namna gani katika sheria za Tanzania?
Kamishna Msaidizi: (Baada ya kupewa kitabu cha sheria za Tanzania na kukisoma) Ni kosa la uhaini.
Wakili wa Utetezi: Ulichukua muda mrefu kufikia jibu hili. Washitakiwa wawili hawahusiani na makosa haya?
Kamishna Msaidizi: Sijui.
Kimsingi hii ni hali ya kawaida kabisa katika mahojiano ya mahakamani. Mara nyingi mahojiano katika mahakama hayaendi haraka sana. Kila mtu anayehusika – hakimu, mwendesha mashtaka, wakili, mdaiwa, shahidi, n.k. hujieleza kwa wazi wazi bila kujali urefu wa maelezo.
Rejesta Zinazohusu Watu
Rejesta zinazohusu watu ni yale mawasiliano yasiyo rasmi, ni yale maongezi ya kawaida ya kila siku au mazungumzo rasmi; kwa mfano mazungumzo kati ya:
  • Vijana wenye rika moja,
  • Wazee wenyewe,
  • Wanawake wenyewe,
  • Wanaume wenyewe,
  • Mwalimu na mwanafunzi,
  • Meneja na wafanyakazi wake,
  • Mtu na mpenzi wake, n.k.
Mazungumzo miongoni mwa marafiki wa rika moja huzungumza lugha ambayo wao wenyewe wanaielewa na sio rahisi kwa mtu wa rika lingine kuielewa lugha hiyo.
Mfano 2
Mfano:
'Basi, Master jana wikiendi ilikuwa kibaridi sana. Basi nilizamia infoo kwenye zinga la mnuso huko saiti za upanga. Nilifika getini nikakuta baunsa kanyuti chedro likisubiri kumtoa noma kila mzamiaji. Alikuwa mnoko kishenzi. Akatema mkwara mbuzi, nikajibu kwa mkwaradume....akabloo mimi ndani’.
Maana ya Maneno
  • Wikiendi – Mwisho wa wiki
  • Kibaridi –tulivu
  • Kuzamia infoo – Kuingia mahali bila kualikwa
  • Zinga la Mnuso –sherehe kubwa
  • Saiti –sehemu
  • Baunsa limenyuti chedro – Ni mlinzi wa mlangoni ametulia pembeni
  • Noma – Hatari
  • Mnoko kishenzi – kinaa sana
  • Mkwara mbuzi – Vitisho dhaifu (Sani, Toleo Na 49).
Mtu asomapo maelezo hayo, mara moja unaona jinsi vijana hawa wa rika moja waishio mjini wanavyozungumza Kiswahili. Si rahisi kwa mzungumzaji wa Kiswahili sanifu kuielewa kirahisi lugha hiyo.
Dhima za Rejesta
Katika kipengele cha utambulisho wa kijamii tunaangalia namna aina ya lugha ya mazungumzo inavyoweza kujidhihirisha miongoni mwa watumiaji wake au kuwatambulisha na kuwatofautisha wanajamii husika. Pia katika utambaulisho wa kijamii tunaangalia vile ambavyo mtu hutambulika katika jamii kulingana na namna anavyoongea kulingana na hadhi, tabaka, na jinsi ambavyo mtu huyo anavyoweza kusababisha mshikamano au mwachano katika mazungumzo. Kwa mfano jamii itamtambua mwanajamii kuwa ni msomi kulingana na mtindo wa lugha ya mazungumzo anaoutumia, au ni mtu wa mtaani kulingana na lugha anayotumia.
Rejesta, ina nafasi kubwa sana katika maendeleo ya kiuchumi kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Hii ni kutokana na kwamba, madhumuni makuu ya mawasiliano katika biashara ni kuwavutia wateja na kuwafanya kuamini kuwa bidhaa ama huduma wanazouziwa ni za kiwango cha juu na ni thamani bora kwa pesa zao. Hivyo lugha ya biashara (rejesta), kwa kawaida ni lugha ya kutangaza uzuri wa bidhaa au huduma, huwa na sentensi au vifungu vifupi, mfano “Okoa mapesa chungu mbovu” pia huwa na lugha ya kupumbaza na kuaminisha, mfano “Kunywa XYZ kufumba na kufumbua afya yako itakurudia”.
Pia rejesta inasaidia sana kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji katika masuala mbalimbali ya kibiashara na hata katika huduma mbalimbali za kijamii. Mfano hospitalini “mbili mara tatu”, hotelini “kuku wali tafadhali”, sokoni “kata nusu” na maeneo mengine.
Baadhi ya rejesta hutumika kupunguza idadi ya maneno hivyo kufanya mazungumzo yawe mafupi na yanayoeleweka kwa urahisi mfano rejesta za hotelini kama vile:- Muuzaji: wapi ng’ombe? Mteja: hapa Muuzaji: wapi chai chapati? Mteja: hapa.
Pia katika kutolea elimu ya dini kanisani na msikitini rejesta ina nafasi kubwa katika kujenga maadili.
Vilevile rejesta ina nafasi ya kupamba mazungumzo, wazungumzaji wengi wanapozungumza hapa na pale hupenda kutumia maneno tofautitofauti ili kufanya mazungumzo yawe ya kuvutia. Mfano mazungumzo miongoni mwa vijana:
Kijana 1: Niaje? Nakuona umechili
Kijana 2: mzuka jembe. Kama kawa… kama dawa!
MISIMU
Kuwasiliana kwa Kutumia Misimu
Misimu ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. misimu inayodumu huweza kuingia katika methali, nahau au misemo ya lugha ya jamii hiyo.
Chanzo cha misimu
  • Misimu huzuka kulingana na mabadiliko ya kihistoria yanayoikumba jamii husika katika nyakati mbalimbali.
  • Misimu huzuka kutokana na haja ya watu kuelezea hisia zoa juu ya matukio mbalimbali yaliyotokea katika vipindi fulani kwa mfano, njaa, mafuriko, vita n.k.
Aina za misimu
  1. Misimu ya pekee. Hii ni misimu ambayo huelezea mahusiano ya kikundi kimoja kutoka katika utamaduni mmoja, na hujulikana miongoni mwao pekee.
  2. Misimu ya kitarafa. Misimu hii hujulikana na watu wengi katikia eneo kubwa, yaweza kuwa ni kata, wilaya au tarafa.
  3. Misimu zagao. Ni misimu iliyoenea nchi nzima au pengine kuvuka mipaka ya nchi, misimu hii husikika redioni, magazetini na hata kwenye vitabu. Msimu uliokita mizizi sana huweza kusanifishwa na kuwa msamiati rasmi.
Sifa za misimu
  • Huzuka na kutoweka kufuatana na mabadiliko ya jamii
  • Ni lugha isiyo sanifu
  • Ina chuki
  • Ni lugha ya mafumbo
  • Ina maana nyingi
Dhima ya misimu
  • Hutumika kupamba lugha
  • Hutumika kukuza lugha
  • Hutumika kutunza historia ya jamii fulani
  • Hutumika kuibua hisia mbalimbali za wazungumzaji
  • Hufurahisha na kuchekesha
Lugha ya Kimazungumzo na ya Kimaandishi
Sifa ya Lugha ya Kimazungumzo
Lugha ya mazugumzo ni maongezi ya watu wawili au zaidi bila kutumia maandishi. Lugha ya mazungumzo ambayo ndiyo lugha kongwe zaidi ya lugha ya maandishi ina dhima kubwa ya kufanikisha mawasiliano miongoni mwa watu au kikundi fulani. Lugha hii ya mazungumzo ilianza punde tu binadamu alipoanza kukabiliana na mazingira yake, hivyo kimsingi lugha ya mazungumzo ndiyo nguzo kuu ya kufanikisha shughuli zote za kibinadamu kutokana na nafasi yake kimatumizi.
Faida ya lugha ya mazungumzo
  • Mzungumzaji anaweza kukaa ana kwa ana na msikilizaji, hivyo hukuza uhusiano.
  • Mzungumzaji anaweza kutumia ishara za mwili katika kusisitiza maelezo yake.
  • Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kuuliza au kuulizwa maswali.
  • Mzungumzaji anaweza kuonesha hisia zake kwa kulia, kupaza sauti, kupunguza sauti, kuonyesha furaha huzuni au hasira.
  • Mzungumzaji anaweza kuuliza maswali, kuona hisia za mzungumzaji kwa kusikiliza lugha zinazotolewa na kuangalia ishara za mwili zinazotumika.
  • Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kufuta usemi wake, kuongezea jambo au kutoa maelezo ya ziada.
  • Mzungumzaji anaweza kubadilisha lugha yake kulingana na mazingira aliyomo.
  • Mzungumzaji anao uhuru wa kutumia lugha ya mitaani, misimu kulingana na muktadha.
Matatizo ya lugha ya mazungumzo
  • Maelezo lazima yahifadhiwe kichwani, hivyo kama mtu hana kumbukumbu, taarifa zilizotolewa hupotea na kusahaulika.
  • Mtumiaji wa lugha ya mazungumzo anaweza kurudiarudia vipengele fulani na hivyo kuichosha hadhira.
  • Ujumbe unaweza usieleweka kama unatolewa kwenye kelele nyingi
Lugha ya maandishi
Hii ni lugha inayowasilishwa kwa njia ya maandishi. Lugha ya maandishi huzihusiha pande mbili, mwandishi na msomaji. Lugha ya maandishi sharti iwe fasaha ili msomaji anaposoma maandishi hayo, apate kuelewa kila kitu, yaani asibaki akijiuliza maswali.
Lugha ya maandishi huambatana na alama za uakifishaaji, hii husaidia maandishi kusomeka vizuri na kueleweka kwa urahisi
Ubora wa lugha ya maandishi
  • Lugha ya maandishi huwawezesha watu walio mbali kuwasiliana.
  • Lugha ya maandishi hustawisha sarufi ya lugha na misingi yake, kwa sababu mwandishi anahakikisha kwamba anazingatia vizuri kanuni za kisarufi ili msomaji wake aweze kumwelewa.
  • Ili kuhakikisha maelezo yake yanaeleweka mwandishi analazimika kuandika kwa uwazi na kwa kuzingatia kanuni na miiko yote ya uandishi.
Udhaifu wa lugha ya maandishi
  • Lugha hii hutumiwa na wale tu wanaojua kusoma na kuandika.
  • Lugha ya maandishi haina msisimko uletwao na lafudhi na matamshi.
  • Msomaji hukosa vidokezo vingi ambavyo katika lugha ya mazungumzo huchangia katika mawasiliano.
  • Lugha ya maandshi inamnyima mwandishi nafasi ya kupima welewa wa msomaji kwa kuwa hamwoni.
Dhima ya lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi
Lugha ya mazungumzo na lugha ya maandshi zote zina umuhimu wa pekee katika maisha ya kila siku kwa sababu ndizo zinzaowezesha watu kuwasiliana kwa namna mbalimbali.
Umuhimu wa lugha ya maandshi pia hutokana na dhima yake kwa watu. Maandishi yanaweza kuhifadhiwa na kusambazwa kwa watu wengi hata walio mbali. Maandishi yanahifadhi kumbukumbu na kwa muda mrefu. Kwa hali hii, watu wa vizazi vingine wanaweza kusoma na kujua mambo yaliyofanyika karne nyingi zilizopita.
Tofauti kati ya lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi
  1. Lugha ya mazungumzo huwezesha mawasiliano ya ana kwa ana lakini lugha ya maandishi haiwezeshi mawasiliano ya ana kwa ana.
  2. Lugha ya mazungumzo haihitaji maandalizi wakati lugha ya maandishi huhitaji maandalizi. Mwandishi atalazimika kupata muda wa kuandika pamoja na kuandaa vifaa kama vile kalamu, karatasi n.k
  3. Lugha ya mazungumzo hailazimiki kuzingatia kanuni za kisarufi, lakini lugha ya maandshi hutakiwa kuzingatia kanuni za kisarufi.
Tofauti nyingine kati ya lugha ya maandishi na lugha ya mazungumzo huweza kuonyeshwa katika jedwali lifuatalo.
Kipengele Mazungumzo Maandishi
Muktadha
  1. Wahusika huonana
  2. Viungo vya mwili hutumika
  3. Maandalizi na matumizi hufanyika wakati mmoja
  1. Wahusika hawaonani
  2. Viungo vya mwili havitumiki
  3. Maandalizi hufanyika kabla ya matumizi
MadaHazina uzito mkubwaHuelekea kuwa na uzito mkubwa.
Mpangilio wa mada na mawazoHautabiriki. Unaelekea kutokuwa na mtiririko.Hutabirika. Huelekea kuwa na mtiririko.
Mjadala wa madaHauelekei kuwa na kina. Hazichujwi kwa uaangalifu.Unaelekea kuwa na kina. Huchujwa.
Dhima ya matumizi ya lugha
Dhima kuu ya lugha ni kupashana habari, ujuzi na maarifa mbalimbali. Vilevile lugha husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu. Uhusiano huo unaweza kuwa wa kijamii, kielimu, kibiashara, kihuduma, kisiasa, kiuchumi n.k. Kwa hiyo, kujua jinsi ya kuitumia lugha kama inavyotakiwa, kunasaidia kufikisha vizuri ujumbe unaotakiwa bila kuupotosha. Vilevile kunasaidia kuepuka migongano, hasa ya kijamii kwa kuwa utakuwa umetumia lugha kwa mujibu wa mila na desturi za jamii inayohusika.
Mambo ya kuzingatia katika matumizi ya lugha
  1. Mada inayozungumziwa: Mada za mazungumzo zipo nyingi. Kuna mada za kijamii, kwa mafano ndoa, unyago, mapenzi, kifo, matanga, burudani, muziki n.k. Kuna mada za kibiashara kwa mfano bidhaa, kodi, vibali, fedha, hasara, faida n.k. Kwa hiyo, ili mazungumzo yaweze kwenda vizuri, wazungumzaji wanatakiwa kuzingatia mada husika.
  2. Muktadha wa mazungumzo: Mazungumzo yanaweza kuathiriwa na miktadha tofauti. Kwa mfano kuna miktadha ya kidini, kiganga, huzuni, sherehe, kisiasa, kielimu, kibiashara n.k. Mazungumzo yanaweza kufanyika mjini, kijijini, ugenini, shuleni, dukani, hotelini n.k
  3. Malengo ya mazungumzo hayo: Malengo ya mazungumzo nayo yanaathiri matumizi ya lugha. Kwa mfano, lengo linaweza kutoa taarifa, kuhoji, kukejeli, kutia moyo n.k. Sasa jinsi lugha itakavyotumika katika kutoa taarifa ni tofauti na itakavyotumika katika kutia moyo au kukejeli.
  4. Uhusiano uliopo baina ya wazungumzaji: Matumizi ya lugha huweza kuathiriwa pia na mahusiano ya wazungumzaji. Kuna mazungumzo baina ya watoto, wanafunzi, wazee, viongozi, marafiki n.k. Upo uhusiano wa daktari na mgonjwa, mwalimu na mwanafunzi, mnunuzi na muuzaji. Kwa hiyo mazingira baina ya pande hizi mbili yatategemea uhusiano wao, kwa hiyo kaida za uhusiano huu utapaswa kuzingatiwa. Kwa hiyo, kwa kuzingatia mambo haya manne, itawafanya wazungumzaji wawe makini katika uteuzi wa maneno, miundo, mifano na kina cha ufafanuzi wa maelezo au habari inayozungumzwa.
Dhima ya Lugha ya Kimazungumzo na ya Kimaandishi
Lugha ya kimazungumzo na ya kimaandishi zina dhima kuu ya kupasha habari, ujuzi, na maarifa mbalimbali, husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu, kufikisha ujumbe unaotakiwa vizuri bila kupotosha, kufundishia ujuzi, kuchochea maendeleo, kuhifadhi historia ya jamii na kueleza mawazo au hisia za watu.
Lugha ya Kimazungumzo na ya Kimaandishi katika Miktadha Sahihi
Tumia lugha ya kimazungumzo na ya kimaandishi katika miktadha sahihi
Matumizi ya lugha ya kimazungumzo na ya kimaandishi katika muktadha sahihi huongozwa na mambo yafuatayo, ambayo ni mada inayozungumzwa, muktadha au mahali mazungumzo hayo yanapofanyika, malengo ya mazungumzo hayo na uhusiano uliopo kati ya wazungumzaji.
Zoezi 1.
Tumia lugha ya kimazungumzo na ya kimaandishi katika miktadha sahihi.
Matamshi na Lafudhi ya Kiswahili
Matamshi ni namna ambavyo mtu anatamka neno au jinsi mtu anavyozungumza lugha. Unaposema fulani ana matamshi mazuri ya Kiswahili utakuwa unamaanisha anazungumza Kiswahili fasaha.
Neno moja linaweza kuzungumzwa/kutamkwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali kutokana na sababu mbali mbali, sababu hizo ni pamoja na eneo la kijiografia anakotoka huyo mtu, kabila lake, kundi lake la kijamii mfano msanii au mwanasiasa, na elimu aliyonayo. Hizi zote zinaweza zikawa ni sababu za kufanya watu watofautiane katika matamshi.
Lafudhi Mbalimbali za Kiswahili
Dhana ya matamshi huhusisha
  • Sauti za lugha husika
  • Mkazo
  • Kiimbo
Sauti za lugha ya Kiswahili
Sauti za lugha ya Kiswahili hujumuisha irabu na konsonanti, ambazo kwa ujumla huunda sauti 24, irabu tano na konsonanti 19 (konsonanti x na q hazipo katika matamshi ya kiswahili). Sauti za Kiswahili hutamkwa kama zilivyoandikwa, kwa mfano maneno “data” au “dengue” wewe unayatamkaje? Wengi huyatamka kama yalivyo hata kama wakiwa wanazungumza kiingereza, hii ni kwa sababu maneno ya Kiswahili hutamkwa kama yalivyoandikwa.
Kwa hiyo unapotamka maneno ya Kiswahili ni sharti uzingatie sauti asilia za lugha ya Kiswahili. Kuna watu huwa wanaandika hivi “xaxa”, hii huwa unaitamkaje? Au “ucjal” huwa unaitamkaje? Kwa kufuata matamshi asilia ya Kiswahili “ucjal” itatamkwa “uchijal” sijui itakuwa ina maana gani sasa. Na pengine umekuwa ukitumia maandishi ya namna hii hata kwenye insha zako ukidhani upo sahihi au ni kwa mazoea tu, sasa kwa kuwa umejua matamshi sahihi ya Kiswahili ni yapi, utajifunza kuyatumia kwa usahihi katika maandishi rasmi na yasiyo rasmi.
Mkazo
Katika lugha ya Kiswahili kuna namna ya kutamka maneno ili kuleta maana mbali mbali, kwa mfano neno “barabara” litaleta maana husika kulingana na jinsi lilivyotamkwa. Hivyo, mkazo ni pale silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.
Kwa mfano:ba’bu, maya’i, rama’ni (mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba'ra (njia).
Baadhi ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine. Kwa mfano: bara'bara (sawa sawa), Alha’misi
Kiimbo
Ni utaratibu maalum wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza katika utamkaji wa lugha fulani.
Katika utaratibu wa utamkaji, dhana ya Kiimbo huandamana pia na dhanna ya kidatu ( yaani , kiwango cha juu, cha chini au cha kati cha sauti katika usemaj), Kwa hivyo ni muhimu hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu. Wakati kiimbo kina maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha, kidatu kina maana ya kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati au kuwa chini.
Aina za viimbo
  • Kiimbo cha maelezo: Kiimbo cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida msemaji wa lugha akiwa kwenye kidatu chochote kile mawimbi sauti ya usemaji wake yanakuwa takriban katika mstari ulionyooka. Mfano, Mwalimu anafundisha.
  • Kiimbo cha maulizo: Kiimbo cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango tofauti vya kidatu kutegemeana na aina ya swali linaloulizwa. Mfano, mwalimu anafundisha?
  • Kiimbo cha amri: kiimbo cha amri hakitofautiyani sana na kiimbo cha maulizo. Kiimbo cha amri, mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo katika kiimbo cha maelezo. Mfano, njoo hapa!
Lafudhi ya Kiswahili
Lafudhi ni matamshi ya msemaji wa lugha fulani ambayo yanatokana na athari za kimazingira. Mazingira hayo yanaweza kuwa eneo atokalo mtu, mahali alikosomea, kiwango chake cha elimu, tabaka lake la kijamii na kadhalika.
Lugha ya Kiswahili ni lugha ya pili kwa watumiaji wengi wa afrika mashariki, kwa hiyo hii inafanya kuwatambua wazungumzaji wa Kiswahili kulingana na makabila yao au maeneo wanakotoka. Kwa mfano, kwa hapa Tanzania tunaweza kuwatambua watu wa mwanza kwa lafudhi yao, watu wa mtwara kwa lafudhi yao, watu wa pemba kwa lafudhi yao au watu wa Musoma kwa lafudhi yao.
Mfano 3.
Mifano
  1. Usiniretee maswara ya ubaguzi wa kikabira hapa (Wakuria)
  2. Amemupiga mutoto ya watu juu amemuibia mfaranga makumi mawili (Wakongo)
  3. Ukikaa nchale, ukichimama nchale (Wamakonde)
  4. Wewe unakamuaga mang’ombe tu moja kwa moja (Wasukuma)
  5. Mbona unakuwa kinganganizi, nilishakwambia sikupendi lakini wewe bado unaningangania tu! (Wahaya)
Utata katika Mawasiliano
Utata ni hali ya neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja. Kwa hiyo tungo tata ni tungo ambayo inaweza kuwa na maana zaidi ya moja.
Sababu za Utata
Utata katika tungo hutokea kwa sababu zifuatazo:
  1. Neno kuwa na maana zaidi ya moja, kwa mfano neno mbuzi, kata n.k.
  2. Kutozingatia taratibu za uandishi, Mfano; Tulimkuta Nyammy na rafiki yake, Mazala vs Tulimkuta Nyammy na rafiki yake Mazala. Katika sentensi hizi alama (,) ndio huleta tofauti, sentensi ya kwanza inamaana kulikuwa na watu wawili Nyammy na rafiki yake aitwaye Mazala na sentensi ya pili isiyo na alama (,) inamaanisha kulikuwa na watu wawili Nyammy na mtu mwingine ambaye ni rafiki yake Mazala
  3. Kutumia maneno bila kuzingatia muktadha wa matumizi ya maneno hayo.
  4. Utamkaji wa maneno. Wakati mwingine utata unaweza kujitokeza katika matamshi tu, ili hali katika maandishi utata hauonekani. Kwa mfano; Mimina wewe, katika maandishi linaweza kuandikwa mimi na wewe, na hivyo kuondoa utata.
  5. Mjengo wa maneno. Utata huu huzuka katika vitenzi kama pigia. Chanzo cha utata katika kitenzi hiki ni kiambishi –i-. Kiambishi hiki kinaweza kumaanisha: kwa ajili ya…, kwa sababu ya.., kwa kutumia chombo fulani.., au mahali fulani.
Mfano 4
Mfano:
  • Alimpigia ukorofi wake (kwa sababu ya)
  • Alimpigia kiatu (kifaa)
  • Alimpigia ndani (mahali)
Mfano 5
Mifano ya utata katika tungo
  1. Patience amemwandikia Lilian barua: Sentensi hii huweza kuwa na maana kuwa Patience ameandika barua kwenda kwa Lilian au Patience ameandika barua kwa niaba ya Lilian
  2. Umefanikiwa kununua mbuzi? Sentensi hii huweza kumaanisha ununuzi wa mbuzi mnyama au mbuzi kifaa cha kukunia nazi.
  3. Alimkuta amelala kwenye nyumba ya wageni: Sentensi hii huweza kumaanisha, nyumba ya mtu lakini inatumika kwa ajili ya wageni kwa malipo au ni nyumba inayomilikiwa na watu ambao ni wageni katika eneo lile.
  4. Attu ametumwa na Aritamba: Sentensi hii inaweza kueleweka kumaanisha, Aritamba amemtuma Attu au Attu na Aritamba wametumwa wote kwa pamoja
 
MADA YA TATU: UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Fasihi simulizi kama zilivyo kazi nyingine za fasihi andishi hufanyiwa uhakiki. Uhakiki huu huzingatia vipengele vya fani na maudhui ili kubainisha usanaa wa kazi husika pamoja na kile ilichokusudia kufikishwa kwa hadhira.
Uhakiki wa Ushairi
Mashairi kama kazi nyingine za kifasihi huhakikiwa kwa kutumia vigezo sawa na vinavyotumika katika kazi nyingine za kifasihi. Vigezo hivyo ni kwa kuzingatia vipengele vyake viwili yaani fani na maudhui.
Vipengele vya Fani na Maudhui katika Kuhakiki Ushairi
Elezea vipengele vya fani na maudhui katika kuhakiki ushairi
Vipengele vya fani
Uhakiki wa fani za ushairi ni uchambuzi wa kina na kuziweka wazi mbinu za kisanaa alizotumia mshairi katika kutunga kazi yake. Vipengele muhimu vya kuhakiki katika fani ya ushairi ni kama vifuatavyo:
Mtindo
Jambo la kuonyesha hapa ni kwamba iwapo shairi ni la kimapokeo ama ni la kisasa.
Muundo
Katika kuhakiki muundo wa shairi mhakiki inatakiwa aweke wazi mambo yafutayo:
  1. Idadi ya beti
  2. Idadi ya mistari na aina ya vibwagizo
  3. Idadi ya vipande
  4. Idadi ya mizani
  5. Aina na mpangilio wa vina
Wahusika
Ikiwa shairi limehusisha wahusika ni vema pia mhakiki awabainishe
Matumizi ya lugha
Katika kipengele hiki mhakiki huchunguza:
  1. Mpangilio wa maneno. Mf. Wengi wari badala ya wari wengi
  2. Matumizi ya : Mazida – kurefusha neno mfano, kiwembe badala ya wembe; Ikisari – kufupisha neno mfano siombe badala ya usiombe; Tabdila – kubadilisha mwendelezo wa neno mfano kujitanuwa badala ya kujitanua.
  3. Matumizi ya methali, misemo na nahau
  4. Matumizi ya lugha ya picha
  5. Matumizi ya tamathali za semi kama vile takriri, sitiari n.k
  6. Mbinu nyingine za kisanaa
Mhakiki anapochunguza vipengele vya fani, jambo muhimu la kuzingatia ni jinsi vipengele hivyo vinavyosaidia kuwasilisha maudhui.
Vipengele vya maudhui
Ili kuhakiki na kupata maudhui ya shairi inatakiwa kulisoma shairi kwa kulielewa zaidi. Baada ya kupata picha fulani kuhusu shairi na kutafakari maana za maneno muhimu, itatubidi tuelewe vipengele vya maudhui, ambavyo ni dhamira, mtazamo, msimamo, falsafa ya mwandishi, ujumbe na maadili, migogoro na muktadha.
Uhakiki wa Maigizo
Igizo huhakikiwa kwa namna lilivyo katika maumbo yake yote mawili yaani fani na maudhui.
Vipengele vya Fani na Maudhui katika Kuhakiki Maigizo
Elezea vipengele vya fani na maudhui katika kuhakiki maigizo
Fani
Uhakiki wa fani katika maigizo unajihusisha na ufundi uliotumiwa. Ufundi huu unajumuisha mambo kadhaa kama ifuatavyo:
Mtindo
Mtindo ni sura ya maigizo inayojitokeza kupitia mpangilio wa maneno na vitendo. Inabidi mhakiki achunguze kama kazi ni:
  1. Mchezo wa jukwaani – wenye mpangilio wa mazungumzo baina ya watu na matendo yao.
  2. Majigambo
  3. Vichekesho – mpangilio wa maneno yanayowasilisha ujumbe kwa kuchekesha.
  4. Mazungumzo – maongezi ya kujibizana baina ya watu.
  5. Ngonjera – mpangilio wa tungo za kishairi ambapo watu wawili au makundi mawili hukinzana.
  6. Miviga – sherehe za kitamaduni kama vile matambiko
Pamoja na haya, mtindo hutegemea lengo la maigizo ambalo laweza kuwa kuelimisha, kukejeli, kuburudisha, kuonya, kukosoa na kadhalika.
Mandhari
Mazingira ya kutendea ni kipengele muhimu cha fani. Mhakiki hana budi kujiuliza iwapo utendaji unadhihirisha wakati au mahali halisi. Jambo hili huweza kutekelezwa kupitia vifaa, maleba, maneno n.k.
Wahusika
Maswali ya mhakiki kuuliza ni:
  • Wamejitokeza kikamilifu?
  • Wanaaminika?
Matumizi ya lugha
Vigezo anavyotumia mhakiki kuchunguza lugha ni:
  • Kama usemaji ni wa kisanaa, yaani unatumia picha, tamathali za semi, methali, nahau n.k.
  • Kama lugha imetumika vile inavyotumiwa katika jamii. Mfano: kiimbo, mkazo, miguno, vihisishi n.k.
  • Matumizi ya maneno ya ajabu kama yale yanayotumiwa na waganga.
Maleba na vifaa
Hivi huakisi mandhari na husaidia kuzua mukatadha. Kwa hiyo ni muhimu kuchunguza kama vimetumiwa ipasavyo.
Matumizi ya ala
Matumizi ya ala kama ngoma, baragumu, au sauti zingine ili kuamsha hisia za hadhira ni jambo muhimu kuchunguza.
Mbinu nyingine
Mhakiki anapaswa pia kuchunguza matumizi ya nyimbo, uchezaji ngoma, usimulizi na mbinu nyingine katika kuibua hisia za watazamaji.
Maudhui
Kwa upande wa maudhui, mhakiki wa maudhui hutakiwa kuchunguza vipengele vyote vya kimaudhui ambavyo ni dhamira, migogoro, maadili, mtazamo na msimamo wa fanani pamoja na ujumbe bila kusahau kipengele cha falsafa. Yote hayo kwa pamoja ndiyo humsaidia mhakiki kubaini ukinzani wa igizo na maisha halisi ya jamii ambayo huwa ndiyo hadhira ya igizo hilo.
 
MADA YA NNE: UHIFADHI WA KAZI YA FASIHI SIMULIZI
Ili kitu kidumu ni lazima kihifadhiwe; fasihi simulizi kama sanaa kutokana na umuhimu wake katika jamii nayo huhufadhiwa kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho. Katika mada hii utaweza kujifunza umuhimu wa fasihi simulizi katika jamii. Utajifunza njia mbalimbali zitumikazo katika uhifadhi wa fasihi simulizi pia utaweza kubainisha ubora na udhaifu wa kila njia.
Njia za kuhifadhi Fasihi Simulizi
Kuhifadhi Fasihi Simulizi
Bainisha njia za kuhifadhi fasihi simulizi
Umuhimu wa kazi za fasihi simulizi
Ingawa kila utanzu wa fasihi una umuhimu wake, kwa pamoja tanzu zake zote zina umuhimu mkubwa katika jamii.
Kwaza fasihi hutumika kama chombo cha kuwaelimisha watu. Kupitia fasihi andishi na fasihi simulizi, watu hupata maarifa ya kutambua mambo maovu na namna ya kuyakwepa. Licha ya haya, wanajamii hujifunza njia za kujitawala, kuzalisha mali na kuishi kwa misingi ya haki, usawa na demokrasia.
Pili, fasihi ni nyenzo ya kutoa mafunzo kuhusu mambo kama vile historia, dini, siasa, jiografia na tiba. Kwa hiyo watu hujifahamisha juu ya maumbile na asili yake, mazingira, utawala, uchumi, sheria n.k.
Aidha fasihi huwapa watu mazoezi na kuimarisha uwezo wao wa kuzungumza kwa ufasaha, kuimba nyimbo kwa ufundi, kuigiza mambo kwa ustadi, kucheza ngoma kwa umahiri, kughani mashairi kwa mvuto na kusimulia matukio kwa mtindo ufaao.
Fasihi hufahamisha, huhifadhi na hurithisha mambo kuhusu utamaduni kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mambo hayo ni pamoja na mila, desturi, falsafa, imani na itikadi. Pia hudumisha maarifa ya kijadi kama vile tiba, sayansi ya kilimo, uhifadhi wa mazingira na sayansi ya utabiri wa hali ya hewa.
Umuhimu mwingine wa fasihi unatokana na kutumika kwake kama chombo cha kuburudisha na kupumbaza. Watu wanaposoma kazi mbalimbali za fasihi hupata, msisimko wa kimwili na kiakili. Kadhalika fasihi hugusa hisia za watu na kuwafanya wafurahi au wahuzunike.
Istoshe fasihi hudumisha na kukuza lugha. Watu hupanua msamiati wao na miundo ya lugha kupitia kazi zake. Hivyo fasihi inakuwa kama hazina ya maneno na dafina ya kanuni za kisarufi.
Kutokana na umuhimu huu ndio maana fasihi huhifadhiwa ili isipotee. Na uhifadhi huu hufanyika kwa njia mabalimbali.
Ubora na Udhaifu wa kila Njia ya Kuhifadhi kazi za Fasihi Simulizi
Elezea ubora na udhaifu wa kila njia ya kuhifadhi kazi za fasihi simulizi
Fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa kwa njia zifuatazo:
Kichwani
Hii ndio njia ambayo imekuwa ikitumiwa kuhifadhi kazi za fasihi tangu kale na inaendelea kutumika hadi leo. Kwa kutumia njia hii kazi ya msanii hukaa kwenye ubongo wa msanii, naye huweza kuiwasilisha kazi hiyo, wakati wowote bila gharama yoyote.
Ubora wake
  • Uwasilishaji wa kazi hiyo unaweza kufanyika wakati wowote bila kuhitaji kufanyika maandalizi yoyote, hususani ya kiufundi.
  • Hakuna gharama yoyote wakati wa uwasilishaji wa kazi ya fashi. Msanii hahitaji kugharimia kitu chochote ili waweze kuitoa kichwani, ni uamzi wake tu, anaweza kuimba papo kwa papo.
  • Kazi ya fasihi iliyohifadhiwa kichwani ni hai. Hii ni kwa sababu msanii anakuwa ana kwa ana na hadhira yake. Kutokana na matumizi ya mbinu tofauti za kisanaa kama vile kucheza, kubadili sauti, miondoko na mengineyo mengi, kazi yake inapata uhalisia zaidi mbele ya hadhira.
Udhaifu wake
  • Uwezekano wa kazi kupotea au kuharibika hasa katika fani ni mkubwa. Kwa mfano msanii anapokuwa amefariki dunia kazi anayokuwa ameihifadhi kichwani nayo hupotea. Ndio maana katika baadhi ya jamii kazi za kifasihi zimepotea. Hii ni kwa sababu wasanii wanapoondoka duniani hondoka na fani hizo.
  • Kazi inapohifadhiwa kichwani ni rahisi kubadilika. Hii inatokea pale ambapo msanii anasahau baadhi ya maneno kutokana na umri wake au sababu nyinginezo
Njia ya maandishi
Maandishi ni njia moja wapo inayotumika kuhifadhia kazi za fasihi. Njia hii imeanza kutumika baada ya watu kujua kusoma na kuandika. Uhifadhi wa kazi za fasihi kwa njia hii hupitia njia mbili kubwa. Hatua ya kwanza ni kubuni kisa au wazo; na hatua ya pili ni kuliweka wazo hilo katika maandishi. Kazi za fasihi simulizi zinazoweza kuhifadhiwa katika maandishi ni hadithi, nyimbo, mashairi, ngonjera, majigambo n.k
Ubora wake
  • Kazi iliyohifadhiwa inaweza kudumu kwa muda mrefu
  • Kazi iliyohifadhiwa inaweza kufikia hadhira hata ya mbali na aliko msanii.
  • Kazi iliyohifadhiwa katika maandshi haipotezi fani yake na maudhui yake bali huendelea kuwa katika asili yake ya awali hadi msanii atakapoamua kuibadilisha.
Udhaifu wake
  • Hii njia ni kwa ajili ya watu wachache tu wanaojua kusoma na kuandika.
  • Wasanii wanaoweza kutumia njia hii ni wale tu wanaojua kusoma na kuandika.
  • Ni aghali sana kuhifadhi kazi za kifasihi kwa njia ya maandishi. Msanii atalazimika kununua vifaa vinavyohitajika katika maandishi ambavyo ni kalamu, karatasi, meza. Kwa hiyo ni aghali.
  • Uwasilishaji wake si hai kwani hakuna kuonana ana kwa ana kati ya hadhira na fanani. Kwa hiyo msomaji hawezi pata vionjo vya msanii hivyo itambidi ajibunie yeye mwenyewe.
  • Wahusika pia hawawezi kuonekana, endapo ni igizo mabalo limehifadhiwa katika maandishi, hivyo ubora wa kazi ya msanii huchujuka.
Njia ya vinasasauti
Vinasasauti ni miongoni mwa vyombo vinavyotumika kuhifadhi kazi za fasihi simulizi. Hii ni njia iliyoendelea kuliko ile ya maandishi.
Ubora wake
  • Kazi ya msanii huweza kuwafikia watu hata walio mbali na alipo mtunzi.
  • Ikihifadhiwa katika vinasasauti kama vile tepurekoda au CD ubora wake huwa haupotei wala kuharibika endapo vifaa hivyo vitatunzwa vizuri.
  • Sauti ya mtunzi unaiskia moja kwa moja
  • Unaweza kusikia vionjo vya msanii
Udhaifu wake
  • Njia hii ni aghali kutumia, kununua vinasasauti ni gharama.
  • Uwasilishaji wake si hai, ingawa unaweza sikia sauti ya msanii au wahusika lakini hahawezi kuonekana.
  • Kazi yoyote ya kifasihi inapohifadhiwa katika vinasasauti, kwa mfano nyimbo, huwa ni mali ya msanii husika, mtu yeyote haruhusiwi kuitumia kama mali yake binafsi bila kuruhusiwa na msanii.
Njia ya kompyuta
Njia hii imeanza kutumika katika miaka ya hivi karibuni baada ya watu kuanza kujua na mna ya kutumia kompyuta.
Ubora wake
  • Njia hii ni ya uhakika zaidi kwa vile shuguli za kisanaa zinazohusika huhifadhiwa katika kompyuta na hutolewa pale zinapokuwa zinahitajika.
Udhaifu
  • Msanii au wasanii wanohusika hawawasiliani na hadhira papo kwa papo. Hivyo hadhira hukosa kuuliza maswali katika vipengele vinavyotatiza.
  • Ili kuhifadhi kazi ya fasihi kwa kutumia njia hii ni sharti msanii awe anajua kutumia kompyuta.
  • Pia ni aghali sana, kuzingatia kwamba kununua komputa ni gharama kubwa.
Njia ya kanda za video
Msanii huweza kutumia kanda ya video kuhifadhi kazi yake.
Ubora wake
  • Kwanza wasnii na vifaa wanavyotumia huonekana
  • Sauti zao na milio ya ala wanazotumia husikika na pia huonekana kwa hadhira. Hii angalau huipa uhai kazi ya msanii mbele ya hadhira.
  • Huweza kudumu kwa muda mrefu endapo kanda ya video iliyotumika kuhifadhi kazi ya msanii itatunzwa vizuri.
Udhaifu wake
  • Uhifadhi wa njia hii ni aghali, msanii atahitajika kununua, kanda ya video, kumlipa mpiga picha na mzalishaji pia.
  • Watu wanoweza kunufaika na njia hii ni wacheche mno na wengi wao ni wale wenye uwezo wa kumiliki televisheni ambao kimsingi hupatikana maeneo ya mijini.
  • Ingawaje hadhira wanaweza kumwona msanii lakini hawawezi kuwasiliana nae ana kwa ana, hivyo kukosa kuuliza swali pindi wanapohitaji kufanya hivyo.
Umuhimu wa kuhifadhi kazi za Fasihi Simulizi
Faida ya Kuhifadhi Fasihi Simulizi
Elezea faida ya kuhifadhi fasihi simulizi
Njia zote za uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi zina umuhimu mkubwa katika ukuzaji na uendelezaji wa utamaduni katika jamii. Kama ambavyo tumekwishaona, kazi za fasihi simulizi huelimisha, huburudisha, hurithisha maarifa, maadili, pia ni vielelezo vya utamaduni wetu wa asiili. Kwa ajili hiyo ni muhimu kuzihifadhi kazi hizo zisiharibike wala kupotea ili ziendelee kutumika kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Ni muhimu ziendelee kuwepo ili kuhifadhi utamaduni wetu na huku vikitumika kama vivutio vya watalii.
Kazi za fasihi simulizi kwa upande mwingine ni sehemu ya ajira. Kwa mfano, shughuli mabalimbali za kisanaa kama vile ngoma, maigizo na utunzi wa vitabu, vinawapatia vipato baadhi ya wasanii. Hivyo ni muhimu zihifadhiwe.
Kazi za fasihi simulizi pia ni kichocheo cha umoja na maelewano miongoni mwa jamii. Yote hayo kwa ujumla wake yanabainisha kuwepo na haja ya kuendelea kuzikusanya, kuzifanyia kazi, kuziendeleza, na kuzihifadhi kazi za fasihi simulizi.
 
MADA YA TANO: UTUNGAJI WA KAZI ZA KIFASIHI
Kazi za fasihi simulizi hazikutokea tu, zilitungwa. Mtu fulani alikaa na akatunga kazi fulani ambayo inajulikana katika jamii. Katika mada hii utajifunza kanuni mbalimbli zinazohusika na utunzi wa kazi za fasihi simulizi. Pia utapata fursa ya kujifunza jinsi ya kutunga kazi mbalimbali za fasihi simulizi kama vile ngonjera, methali , nahau, vitendawili na kazi nyingine. Utajifunza pia kanuni zinazoongoza utunzi wa kila kazi ya fasihi simulizi.
Mashairi
Kanuni za Utungaji wa Mashairi
Fafanua kanuni za utungaji wa mashairi
Uandishi wa kubuni unamtaka mtunzi atumie milango yake ya fahamu kinagaubaga. Kuna milango ya fahamu mitano ambayo ni pamoja na: kuona, kunusa, kusikia, kuhisi, na kuonja.
  • Kuona: je, mhusika unayemfikiria kichwani mwako unamwonaje? Umbo lake ni la kuvutia au kuchusha? Je, macho yake yakoje – je ni ya golori au la? Ni makubwa au madogo? Je, ni mlemavu wa macho?
  • Kunusa: pua zako zinakufanya usikie harufu gani? Je, ni harufu mbaya au nzuri? Je, ni uvundo au marashi? Je, mhusika wako ananuka kikwapa au uturi? Je, ananuka mdomo?
  • Kuhisi: je, unapokaa karibu naye unajihisi nini? Je, unapata mhemko wowote au huhisi chochote? Je, akikupapasa mwilini mwako unajisikia nini? Akikugusa bega unajisikia nini?
  • Kuonja: je, ukiweka kitu hicho mdomoni unaonjaje – ni chungu au tamu? Je, ina pilipili au masala? Je, kuna chumvi au sukari? Je, kitu hicho kina ukakasi au uchachu?
  • Kusikia: je, sauti unayoisikia ikoje? Inamtoa nyoka pangoni? Inakufanya ukose usingizi? Je, ni sauti nzuri au mbaya? Ni nyororo au nzito? Kama ni sauti ya muziki – je, iko chini au juu (kelele)?
Uzoefu wa Mwandishi
Uzoefu ni hali ya kukaa au kujishughulisha na jambo au kitu kwa muda mrefu. Mwandishi ana uzoefu (uzoevu) wa kukabiliana na maisha kwa kiasi gani? Je, ni matatizo gani ambayo umekutana nayo katika maisha yako? Je, ni mafanikio gani umekutana nayo katika maisha yako? Kwa mfano, katika ajali ya MV Spice (2011) kuna baadhi ya watu waliokolewa na magodoro ya Tanzania? Magodoro haya yana nailoni na je kama yasingekuwa na nailoni? Uzoevu/uzoefu wako ukoje?
Uchunguzi/utafiti
Uchunguzi unapaswa ufanywe na mwandishi ili aweze kuandika jambo au tukio bila kuongopa. Kwa kufanya udanganyifu, mwandishi atapoteza imani yake kwa wasomaji wa kazi zake.
Uchunguzi ili ufahamu au ujue mtu, mnyama, mdudu na kadhalika – anatembeaje, anakulaje, analalaje, anaishije, anachekaje, analiaje, anazaaje, anahusianaje na wenzane na mazingira yake? Haya ni maswali muhimu katika kumwezesha mtunzi kufanya utafiti wa kina ili ajue kitu anachotaka kukiandika akiandikaje na akiwasilishaje ili aweze kuikamata hadhira yake.
Mwandishi baada ya kuzingatia mambo haya sasa anaweza kuanza kutunga kazi yake. Hapa sisi tutajikita zaidi katika utunzi wa mashairi. Kabala hatujaenda katika hatua ya utunzi ni muhimu kujua dhana ya shairi kwa ujumla wake, na baada ya hapo tutakuwa tumekwisha pata maarifa yakutosha juu ya mashairi ambayo yatatuwezesha kutunga mashairi.
Dhana ya shairi
Shairi ni kipande cha maandishi kilichopangwa kwa utaratibu katika mistari. Sauti za silabi hufanana zikiwa kati au mwisho mwa mstari. Maandishi hayo yakisomwa huleta ujumbe na hisia fulani ya kimaisha.
Mpango wa maneno ya shairi, ambao huweza kuimbwa hutoa picha wazi, maana halisi na burudani ya kimuziki. Nyimbo nyingi za makabila zimepangiliwa kishairi ijapokuwa hazikuandikwa.
Mashairi yana umbo ambalo huonekana kwa mpangilio wa sauti na idadi ya maneno katika mistari. Umbo hili hutofautisha shairi na tenzi. Kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kufahamika kuhusu shairi, nayo ni:
  1. Beti – Kifungu kimoja cha shairi ambacho kina uzani sawa.
  2. Vina – Ni mwisho wa mistari ambayo huwa na silabi zenye sauti ileile mwishoni mwa sentensi.
  3. Mizani – Ni idadi zilizo sawa za silabi katika kila mstari, ubeti hadi ubeti.
  4. Kituo – Huu ni mstari wa mwisho wa ubeti. Kuna vituo vya aina tatu:Kituo cha bahari – ni mstari unaotoka mwanzo hadi mwisho bila kubadilika katika kila ubeti;Kituo cha kimalizio – ni kituo ambacho mstari wa mwisho maneno yake hubadilika ubeti hadi ubeti;Kituo nusu bahari – ni mstari wa mwisho ambao maneno yake nusu hubadilika na nusu hubaki kama ulivyo ubeti hadi ubeti.
Katika mashairi (ya kimapokeo), kila mstari lazima uwe umekamilika na ubeti uwe na maana kamili.
Vipengele vya fani katika mashairi
Vipengele vya fani katika shairi ni pamoja na:
  • Jina / anwani
  • Mandhari
  • Wahusika
  • Muundo –tathnia, tathlitha, tarbia, tathamisa, sabilia n.k
  • Mtindo – pindu, msisitizo, beti kubadilishana vina, kurudiwa kipande kizima cha mstari wa mwisho kikiwa ni chanzo cha ubeti unaofuatia.
Vipengele vya Maudhui kati mashairi
  • Vipengele vya maudhui ni pamoja na: migogoro, ujumbe, falsafa, msimamo, mtazamo, na dhamira za mwandishi.
  • Matumizi ya ushairi ni pamoja na: kuomboleza, kubembeleza, kuliwaza, kufundisha, kuburudisha, kukosoa, na kadharika.
Baada ya hapa sasa unaweza kuanza kutunga shairi lako la kwanza.
Kuigiza Ngonjera
Igiza ngonjera
Katika kuigiza ngonjera muigizaji hana budi kuzingatia fani yenye kanuni zifuatazo; mtindo wa mashairi ya kimapokeo, muundo wa mashairi ya kimapokeo wenye mizani, vina, vipande, mishororo na beti, kuteua mandhari kutegemeana na mada, kuwepo kwa wahusika wawili au zaidi au makundi mawili au zaidi na matumizi ya lugha ya kishairi.
Maigizo
Kanuni za Utungaji wa Maigizo
Elezea kanuni za utungaji wa maigizo
Maigizo ni tendo la kuiga sura, tabia, matendo na mazungumzo ya watu au viumbe wengine yaani kuiga jinsi walivyoumbwa, wanavyotembea, wanavyovaa, wanavyosema n.k
Kanuni na hatua za kutunga maigizo
  1. Kuchagua wazo, tendo, visa au tukio la kuigizwa:Ni lazima jambo hilo liwe na uzito, umuhimu au athari fulani katika jamii. Matukio hubainika kutokana na utafiti. Matukio yanayoweza kuwa kiini cha kutungiwa maigizo ni kama vile matumizi mabaya ya simu za mkononi, mitindo ya mavazi, madhara ya uganga wa kienyeji, madhara ya UKIMWI n.k.
  2. Kuchagua muktadha au mahali pa kutendeka kwa jambo:Muktadha waweza kuwa ofisini, shuleni, kijijini, mjini, barabarani, kwenye daladala n.k
  3. Kuamua mtindo wa kuwasilisha jambo la kuigizwa:Hapa mtunzi anaweza kutumia fumbo, vichekesho, historia, tanzia n.k. Inashauriwa mtunzi kuchanganya mbinu ili kuongeza mvuto.
  4. Kupanga hoja kuu zinazojenga maudhui ya igizo:Maudhui hujikita katika migogoro au mivutano. Suluhisho la mivutano hupatikana pale migogoro inapofikia kilele. Kwa mfano jamabazi sugu anapokamatwa.
  5. Kuweka mpangilio wa maonyesho:Maonyesho hujumuisha vitendo na hoja zinazokamilisha sehemu inayobeba aina moja au zaidi ya maudhui. Sehemu kadhaa nazo hukaa zikajenga kitendo ambacho hubeba jambo mojawapo muhimu. Katika migawanyo hii yapasa mtunzi atunge kauli na vitendo vinavyoandamana navyo.
  6. Kubuni wahusika na kuweka aina au idadi yao kulingana na matukio:Mtunzi anashauriwa kutumia wahusika wanaohitilafiana. Kwa mfano wazee, vijana, wanawake, wanaume, wanene, wafupi n.k. Mtunzi akishawateua anaweza kuwatungia kauli na zamu za matendo katika sehemu mbalimbali.
  7. Ni muhimu pia kwa mtunzi kuwaumba wahusika wake na kuamua maleba yao:Uamuzi huu yapasa ufanywe kwa kuzingatia mazingira. Kwa mfano siku hizi sio lazima wahusika wazee kuvaa ngozi, kutumia mkongojo na kuvuta mtemba.
  8. Urefu wa maigizo ni suala la kuamliwa kutegemea tukio
  9. Kutunga maelezo kuhusu mandhari:Maumbile ya wahusika na vitendo vyao, ni muhimu kuelezwa katika mabano.
  10. Kuandika maigizo na kuhariri:Ni muhimu kutumia lugha ya kimazungumzo inayovutia, yenye kuleta taharuki na yenye utamu unaoeleza maadili kwa mnato.
 
MADA YA SITA: UANDISHI
Insha za Hoja

Insha za hoja ni insha zinazoelezea jambo fulani katika hali ya kujenga hoja ambazo zinatetea msimamo fulani alionao mwandishi wa insha hiyo juu ya jambo analolizungumzia. Hoja ni maelezo bayana yanayotolewa na mwandishi kutetea msimamo wake.
Katika uandishi wa insha za aina hii, mwandishi hutakiwa kuonesha ni jambo gani ambalo analiunga mkono na ni lipi ambalo hakubaliani nalo.
Ili hoja zote zipate kueleweka ni sharti zipangwe katika mtiririko wa mawazo ulio sahihi kiasi kwamba mtu aisomapo anapata kuelewa ni mada gani mwandishi anaijadili na ana msimamo gani kuhusu mada hiyo.
Muundo wa Insha za Hoja
Elezea muundo wa insha za hoja
Katika uandishi wa insha, muundo wake unakuwa na vitu vifuatavyo:
  1. Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya n.k
  2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako.
  3. Kiini cha insha;katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.
  4. Hitimisho; hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichohadiliwa katika insha.
Barua Rasmi
Dhima ya Barua Rasmi
Elezea dhima ya barua rasmi
Barua rasmi ni barua zinazohusu mambo rasmi ya kiofisi. Dhima za barua rasmi ni kutoa taarifa, kuomba kazi au huduma, kuagiza vitu na kutoa mwaliko kwa mfano kwa kiongozi fulani wa nchi, kutoa malalamiko na kuweka kumbukumbu au marejeo.
Muundo wa Barua Rasmi
Elezea muundo wa barua rasmi
Barua rasmi au barua ya kiofisi/kibiashara huzingatia mtindo rasmi wa barua. Kwa kawaida huwa na sehemu zifuatazo:
  1. Anwani ya mwaandishi -huwekwa juu kabisa na huwa katika upande wa kulia wa karatasi.
  2. Tarehe ya barua hiyo- tarehe huandikwa chini ya anwani ya mwandishi
  3. Anuwani ya mpokeaji- Anwani ya anayeandikiwa huwa katika upande wa kushoto wa karatasi, na huwekwa msitari mmoja chini ya tarehe.
  4. Salamu- Chini ya anwani ya mpokeaji, barua huanza kwa kumrejelea mpokeaji kama bwana au bi. Ni makosa kumsalimia mpokeaji wa barua rasmi au kumwuliza hali yake.Ndugu Bwana Meshaki, => taja jina lake ikiwa mnajuana na unayemwandikia. Kwa Bw/Bi, => Ikiwa humjui mpokeaji wa barua, tumia bw/bi
  5. Mada- Kichwa cha barua rasmi huja pindi tu baada ya salamu. Hutangulizwa na maneno kama vile YAH:(yahusu). Ni sharti kichwa kiandikwe kwa herufi kubwa na kipigiwe mstari. Kichwa kinapaswa kuwa kifupi na kinachoelezea mada ya barua kiukamilifu.
  6. Utangulizi– Hukaa chini kidogo ya mada ya barua. Haya ni maelezo mafupi yasiyozidi aya moja ambayo huelezea kusudi kuu la barua kama kidokezo.
  7. Ujumbe- Ujumbe wa barua rasmi lazima uwe mfupi na unaotumia lugha rasmi.
  8. Tamati– mwandishi humalizia kwa maneno ya hitimisho kama vile: Wako mwaminifu, [jina], Sahihi
Simu
Dhima ya Simu ya Maandishi
Elezea dhima ya simu ya maandishi
Simu za maandishi ni aina ya barua fupi ambazo husafirishwa kwa haraka sana kuliko barua za kawaida.
Simu hizo huandikwa kwenye fomu maalumu ambazo hutolewa na shirika la posta. Simu za maandishi hujulikana kama telegram.
Kwa kawaida simu za maandishi hutumika kutuma ujumbe wa dharura. Kuandika simu za maandishi ni njia ya haraka ya kufikisha ujumbe kwa sababu, baada ya kuandika simu yako ujumbe humfikia huyo unayemtumia katika muda usiozidi siku tatu.
Gharama za simu za maandishi hutozwa kulingana na idadi ya maneno yaliyotumika. Kwa hiyo ujumbe unaotumwa huandikwa kwa maneno machache ili kuepuka kutozwa gharama kubwa.
Example 1
Mfano wa simu ya maandishi:
MUSA KINGAMBE SLP 5299 DSM
NJOO HARAKA
DADA MGONJWA LINGIDO
Kuandika Simu za Maandishi kwa Kuzingatia Muundo na Taratibu za Uandishi
Andika simu za maandishi kwa kuzingatia muundo na taratibu za uandishi
Muundo wa kuandika simu za maandishi una mambo yafuatayo ya kuzingatia ambayo ni anwani ya mpelekewa taarifa, ujumbe na jina la mwandishi au mtuma simu. Mambo mengine ya kuzingatia ni kuandika maneno yote kwa herufi kubwa ili kurahisisha usomaji na kuandika simu ya maandishi katika karatasi maalumu ambayo hutolewa na posta.
Activity 1
Andika simu za maandishi kwa kuzingatia muundo na taratibu za uandishi
Kadi za Mialiko
Kadi za mialiko ni aina ya karatasi ngumu zinazopeleka taarifa fupi za kumwomba mtu ahudhurie katika sherehe fulani kama vile harusi, ubatizo mahafali n.k
Muundo wa Kadi ya Mialiko
Fafanua muundo wa kadi ya mialiko
Mambo muhimu yanayotakiwa kuonyeshwa katika kadi ya mwaliko:
  1. Jina la mwandishi au mwalikaji
  2. Jina la mwalikwa, ni muhimu kuandika cheo chake kama vile: Profesa, Bi., Bw. Bw&Bi n.k
  3. Lengo la mwaliko
  4. Mahali pa kufanyika shughuli
  5. Tarehe ya mwaliko
  6. Wakati wa shughuli
  7. Jina na anwani ya mtu atakayepelekewa majibu.
Mialiko huweza kuandikwa kwa namna mbili yaani kama barua au kadi. Jina la mwalikwa katika kadi ya mwaliko hutakiwa kuanza na maneno ya heshima kama vile Bwana….Bi…..au Ndugu…ikiwa waalikwa ni mume na mke kadi itaanza na Bwana na Bibi.
Example 2
Mfano wa Kadi ya Mwaliko
Familia ya Manyama na Joseph
Wanapenda kukualika/kuwaalika Profesa/Dkt/Shekhe/Padri/Bi/Bw/Bw&Bi……… kwenye harusi ya kijana wao mpendwa Benny Joseph itakayofanyika huko Kiabakari katika ukumbi wa simba siku ya Jumapili tarehe 9/12/2016 sasa 8.00 mchana hadi saa 3.00 usiku
Kufika kwako ndio mafanikio ya sherehe hii.
Majibu kwa (wasiofika tu)
Emmanuel Joseph
Simu: 0786 67 54 62
Uandishi wa Dayalojia
Dhana ya Dayolojia
Elezea dhana ya dayolojia
Dayalojia ni mazungumzo au majibizano baina ya watu wawili au zaidi wanaozungumza kwa kupokezana. Kama zilivyo kazi nyingine za utunagaji, dayalojia inaweza kuwasilishwa kwa nijia ya mazungumzo au maandishi.
Katika kutunga dayalojia mtunzi hana budi kujifanya kama mhusika katika dayalojia hiyo. Kwanza anapaswa kutafakari kwa makini mada anayokusudia kuandikia dayalojia, kutayarisha na kupanga mawazo kimantiki na kwa mtiririko na kufikiria wahusika na kuwapangia majukumu kulingana na matendo yao. Kwa mfano kama mhusika ni mkulima, lugha anayopewa, vifaa anavyosemekana kuvitumia na mandhari aliyomo ni lazima vifanane na hali ya mkulima halisi.
Mambo ya kuzingatia katika dayalojia ni pamoja na haya yafuatayo:
  1. Kutoa maelezo ya ufafanuzi katika mabano ili kumfahamisha
  2. Kuwa na mazungumzo ya mkato na yasiyozidiana sana kati ya wahusika. Mhusika mmoja asitawale mazungumzo kupita wengine.
  3. Kutumia vihisishi ili kufanya dayalojia iwe ya kusisimua
  4. Pawepo mwingiliano wa mazungumzo ya wahusika na kudakia maneno ili dayalojia iwe na uhalisia.
Example 3
Mfano wa dayalojia
Wambura:(Anaonekana mwenye furaha,anamwita rafiki yake, Anna)Wow, Anna! Tumekutana tena, siamini macho yangu! (wanakumbatiana wote wakiwa na nyuso za furaha).
Anna:(Anatabasamu huku ameshikilia mkono wa kulia wa Wambura, anaonesha shauku kuu)Wambura! Bado unanikumbuka? Nina furaha sana kwa kweli, ni muda mrefu sana.
Wambura:(Anachekelea)Aaaah, nahisi kama naota Neema, siamini kama nimekutana na wee leo hii ni muda mrefu sana, nimefurahi kwa kweli.
Anna:(Anachekelea)
Wambura:Mbona wachekelea tu….
 
MADA YA SABA: USIMULIAJI WA MATUKIO
Usimuliaji wa Matukio
Njia za Usimulizi wa Matukio
Fafanua njia za usimulizi wa matukio
Usimulizi hufanyika kwa njia kuu mbili yaani kwa njia ya maandishi na kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Kila njia hutegemea kwa namna msimuliaji anavyoweza kuwasiliana na msikilizaji. Ikiwa msimuliaji na msikilizaji hawakukaribiana, njia ambayo itatumika ni ile ya maandishi. Kwa mfano kama utahitaji kumweleza mtu aliyembali kuhusu tukio fulani la kusisimua utalazimika kutumia maandishi, yaani utatumia njia ya kumwandikia barua.
Lakini kama unamsimulia mtu ambaye yupo karibu nawe, utatumia njia ya mazungumzo ya ana kwa ana.
Taratibu za usimulizi wa matukio
Usimulizi wa matukio dhamira yake ni kumweleza mtu au watu tukio ambalo wao hawakulishuhudia. Hivyo katika usimulizi msimuliaji hutakiwa kutoa maelezo muhimu ambayo yatawawezesha watu hao kulielewa tukio linalosimuliwa sawasawa na huyo anayeshuhudia.
Mambo muhimu ya kutaja katika usimulizi wa matukio ni pamoja na haya yafuatayo:
  1. Aina ya tukio – msimuliaji atatakiwa kubainisha katika maelezo yake aina ya tukio. Kwa mfano, kama ni harusi, ubatizo, ajali ya barabarani au mkutano.
  2. Mahali pa tukio – ili msimuliaji aweze kuielewa habari inayosimuliwa, ni lazima kumwelewesha ni mahali gani tukio hilo limetokea. Kwa mfano, kama ni mjini inafaa kutaja hata jina la mtaa.
  3. Wakati – katika usimulizi ni muhimu pia kutaja muda ambao tukio limetendeka kama ni asubuhi, mchana au jioni bila kusahau kutaja muda halisi yaani ilikuwa saa ngapi.
  4. Wahusika wa tukio – ni muhimu kutaja tukio limehusisha watu gani, wingi wao, jinsia yao, umri wao n.k.
  5. Chanzo cha tukio – kila tukio lina chanzo chake hivyo ni muhimu kutajwa katika usimulizi.
  6. Athari za tukio – athari za tukio nazo ni sharti zibainishwe. Kama ni ajali, je watu wangapi wameumia; wangapi wamepoteza maisha n.k.
  7. Hatima ya tukio – msimuliaji katika usimulizi wake ni lazima abainishe baada ya tukio kutokea na kushughulikiwa hatima yake ilikuwaje. Kwa mfano, kama tukio ni ajali ya barabarani hatima yake inaweza kuwa majeruhi kupelekwa hospitalini na dereva aliyehusika kukamatwa.
Kwa hiyo misingi hii ya usimulizi hufanya usimulizi wa tukio kuwa na sehemu kuu tatu:
  • Utangulizi – sehemu hii huwa na maelezo tu ya utangulizi ambayo hulenga kuvuta hisia na umakini wa msikilizaji au wasikilizaji. Kwa kawaida utangulizi wa tukio huwa ni maneno machache kiasi yasiyozodi aya moja.
  • Kiini – kiini cha usimulizi huelezea tukio halisi kuanzia chanzo chake, wahusika, muda, mahali na athari za tukio.
  • Mwisho – mwisho wa usimulizi ni matokeo yanayoonyesha matokeo ya mwisho ya tukio linalohusika, wakati mwingine matukio haya yanaweza kuambatana na maelezo ya msimuliaji kuhusu mtazamo au maoni yake binafsi juu ya tukio ambalo amesimulia.
Mbinu za usimulizi
Ili habari inayosimuliwa ipate kueleweka vizuri, sharti msimuliaji ajue mbinu za kusimulia katika hali inayovuta hisia za msikilizaji wake.
Baadhi ya mbinu hizo ni uigizi, utumizi wa lugha fasaha inayozingatia lafudhi sahihi ya Kiswahili.
Kwa upande wa uigizi msimuliaji atatakiwa kuigiza mambo muhimu yanayohusiana na tukio ambalo anasimulia. Nayo ni kama vile milio, sauti na matendo.
Kwa upande wa usimulizi ambao unafanyika kwa njia ya maandishi, sharti usimulizi huo uwe na kichwa cha habari. Kichwa cha habari kinatakiwa kuandikwa kwa maneno yasiyozidi matano, yaliyoandikwa kwa herufi kubwa.
Kwa vile usimulizi wa tukio huwa unahusu tukio lililopita, maelezo yake mengi huwa katika wakati uliopita.
 
MADA YA NANE: UFAHAMU
Ufahamu ni dhana inayorejelea kujua na kulielewa jambo kwa usahihi na kuweza kulielezea upya kwa usahihi bila kupoteza maana yake ya msingi. Ufahamu wa mtu waweza kupimwa katika kusikiliza jambo au katika kusoma.
Ufahamu wa Kusikiliza
Ufahamu wa kusikiliza ni zaidi ya kusikiliza tu kile kilichosemwa; badala yake ni uwezo wa mtu kuelewa maana ya maneno anayoyasikia na kuweza kuhusiana nayo kwa namna fulani. Kwa mfano mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake mwenyewe.
Kujibu Maswali ya Ufahamu kutokana na Habari uliyoisikiliza
Jibu maswali ya ufahamu kutokana na habari uliyoisikiliza
Ufahamu wa kusikiliza unahusisha michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa. Michakato hii inahusisha:
  • Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa
  • Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza
  • Kuelewa sintaksia (muundo wa maneno) ya sentensi kwa namna zinavyowasilishwa.
Katika ufahamu wa kusikiliza, msikilizaji hana budi kuzingatia mambo yafutayo:
  1. Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili kuweza kusikia kila anachokisema.
  2. Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo msemaji anaongeza jambo jipya, anatofautisha, anafafanua au anahitimisha hoja.
  3. Msomaji anatakiwa kuandika baadhi ya mambo anayoona kuwa ni ya muhimu ili kumasidia kukumbuka hapo baadae.
  4. Kuwa makini na ishara mbambali za mwili kama vile kurusha mikono, kutingisha kichwa, kutingisha mabega au hata kupepesa macho. Ishara hizi huwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kupata maana katika mazungumzo.
Kufupisha kwa Mdomo Habari uliyoisikiliza
Fupisha kwa mdomo habari uliyoisikiliza
Ili kuweza kufupisha kwa mdomo habari uliyoisikiliza yapo mambo ya kuzingatia. Mambo hayo ni kubaini mawazo makuu yanayopaswa yajitokeze katika habari iliyofupishwa, kupanga maelezo kwa usahihi katika usemaji, kuzingatia kichwa cha habari ambacho kinapaswa kihusiane na ufupisho na wazo kuu na mwisho ni kusema ufupisho kwa ufasaha na kwa lugha ambayo ni nzuri.
Activity 1
Fupisha kwa mdomo habari uliyoisikiliza
Ufahamu wa Kusoma
Ufahamu wa kusoma ni ule mtu anaoupata kwa njia ya kusoma makala, kifungu cha habari, kitabu au gazeti.
Kusoma kwa Sauti kwa kuzingatia Lafudhi ya Kiswahili
Soma kwa sauti kwa kuzingatia lafudhi ya kiswahili
Kuna vipengele viwili vinavyounda mchakato wa ufahamu wa kusoma:
  • Uelewa wa msamiati na
  • Uelewa wa matini
Ili kuilelewa habari/matini ni lazima msomaji awe na uwezo wa kuelewa msamiati uliotumika katika matini hiyo. Endapo maneno yaliyotumika hayataeleweka vilevile matini yote hataeleweka.
Katika ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
  1. Kubaini mawazo makuu; msomaji anaposoma habari fulani au kitabu inatakiwa ajiulize, Je, kinachoongelewa hapa ni nini? Ni jambo gani hasa analolizungumzia mwandishi? Msomaji akiwa na maswali haya akilini mwake basi itakuwa rahisi kwake kuielewa habari hiyo.
  2. Kuzingatia alama za uakifishi; msomaji ni lazima azingatie alama za uakifishi, kwa kufanya hivyo itamsaidia kuelewa ujumbe wa habari hiyo na endapo hatazingatia alama za uakifishaji anaweza kupotosha maana ya mwandishi.
  3. Kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali; habari nyingine huwa zina maneno ya kisanaa hivyo ni muhimu msomaji kubaini maana ya maneno hayo katika muktadha wa habari hiyo, hii itamsaidia kuelewa vyema maana ya mwandishi.
  4. Vilevile msomaji anatakiwa kumakinikia kile anachokisoma, kila kipengele anachokisoma inampasa akielewe vizuri.
Kwa kuzingatia haya yote msomaji atakuwa na uelewa mzuri juu ya habari aliyoisoma na pia anaweza kufupisha habari hiyo aliyoisoma.
Kujibu Maswali kutokana na Habari uliyoisoma
Jibu maswali kutokana na habari uliyoisoma
Ili kujibu maswali yanayotokana na habari uliyoisoma inatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo; kubaini mawazo makuu, kuzingatia alama za uandishi, kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali na kutilia maanani vidokezo vya maana. Aidha mawazo yanapaswa kuelekezwa katika jambo linalosomwa, kujiuliza maswali kadri unavyosoma na kuandika ufupisho.
Kufupisha Habari uliyoisoma
Fupisha habari uliyoisoma
Ili kuandika ufupisho mzuri wa habari uliyosoma yapaswa kuzingatia yafuatayo: kuisoma habari uliyopewa zaidi ya mara moja, kubainisha mawazo makuu, kuandika ufupisho kwa lugha fasaha na yenye mtirirko mzuri wa hoja, kuhesabu idadi ya maneno na kuhakikisha haizidi idadi inayotakiwa na kupitia habari ya mwanzo na kisha ufupisho ili kuona kama taarifa muhimu haijaachwa au kusahaulika.
Kusoma kwa Burudani
Huu ni usomaji ambao lengo lake kuu huwa ni kujiburudisha tu. Katika usomaji wa aina hii, msomaji hujisomea zaidi magazeti, majarida na vitabu tofauti na vile vinavyotumika darasani.
Wakati mwingine sio lazima msomaji awe na vitabu vyote ambavyo anahitaji kuvisoma au magazeti na majarida. Inapotokea hivyo, msomaji anaweza kwenda maktaba kuazima kitabu nachokihitaji.
Ingawa lengo la msomaji huwa ni kujiburudisha tu, lakini pia hujiongezea maarifa. Hii ni kwa sababu, magazeti, majarida na vitabu sambamba na kutuamia lugha sanifu huelezea mambo mabalimbali yanayoihusu jamii.
Mambo ya Kuzingatia katika Ufahamu wa Kusikiliza
Mambo ya kuzingatia katika usomaji kwa burudani
Msomaji kutokana na kusoma vitabu na majarida mbalimbali hujiongezea kiwango cha welewa wa lugha na mambo mengine ya kijamaii yanayojadiliwa humo.
Ni jambo zuri kwa msomaji kujijengea tabia ya kujipima ili aweze kuelewa kiwango cha maarifa aliyopata katika kujisomea. Kujipima huku kunaweza kufanywa kwa kujiundia utaratibu w kuweka kumbukumbu ya vitu au makala zilizosomwa na kufanya ufupisho wa kila makala.
Utaratibu unaopendekezwa katika kujipima na kujiwekea kumbukumbu ya usomaji wa burudani ni kama ufuatao:
  1. Tarehe...
  2. Jina la kitabu/makala/gazeti....
  3. Mchapishaji......
  4. Mwaka/tarehe ya uchapishaji.....
  5. Ufupisho wa habari(yasizidi maneno 20)
  6. Fundisho/ujumbe mkuu ni.....
  7. Jambo lililokuvutia sana......
  8. Maoni kwa ujumla kama yapo....
Matumizi ya Kamusi
Kamusi ni kitabu cha marejeo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani na kupangwa katika utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo wasomaji wanaweza kuelewa. Au kamusi ni orodha ya maneno yaliyo katika karatasi au nakala tepe yaliyopangwa kialfabeti na kutolewa maana pamoja na maelezo mengine na kuhifadhiwa katika kitabu, santuri, simu, tarakilishi au katika mfumo wowote wa kielekroniki.
Jinsi ya Kutumia Kamusi
Elezea jinsi ya kutumia kamusi
Maneno yanayoingizwa katika kamusi hupangwa kwa utaratibu wa alfabeti. Maneno yanayoanza na herufia, yote huwekwa chini ya herufiA. Maneno yanayoanza na herufi fulani nayo hupangwa katika utaratibu wa alfabeti kwa kuzingatia herufi ya pili, ya tatu, nne au tano ya neno kama mfano hapa chini unavyoonyesha.
Mfano:ja, jabali, jabiri, jadhibika, jadi.
Maneno yote yanaanza na herufi [j]. herufi ya pili kwa maneno yote ni [a]. herufi ya tatu ni na [d]. Kwa kuwa hutangulia [d] katika mpangilio wa alfabeti maneno yenye kabla ya yale yenye [d]. Kwa kuwa maneno yenye herufi ni mawili itabidi tutazame herufi ya nne ya hya maneno ili tuchague litakaloorodheshwa mwanzo. Neno ‘jabali’ litaorodhewshwa kabla ya ‘jabiri’ kwa kuwa [a] (herufi ya nne) ya ‘jabali’ hutangulia ya ‘jabiri’ ambayo pia ni herufi ya nne. Kisha tunatazama maneno yenye [d] kama herufi ya tatu. Hapa tunaangalia pia herufi ya nne ili kubaini neno litakaloandikwa mwanzo kati ya ‘jadhibika’ na ‘jadi’. Kwa kuwa [h] hutangulia basi ‘jadhibika’ huorodheshwa mwanzo ndipo lifuatiwe na ‘jadi’.
Kwa hiyo hivi ndivyo unavyopaswa kutafuta neno kwenye kamusi. Nenda kwenye herufi ya neno ulalotafuta alafu litafute kwa kufuata mlolongo huo huo wa herufi ya kwanza kuorodheshwa.
Neno linaloorodheshwa kwenye kamusi ili lifafanuliwe linaitwakidahizo.Kidahizo huandikiwa maelezo ya kukifafanua. Maelezo haya ni matamshi ya kidahizo, maana ya kidahizo, kategoria ya kisarufi, sentensi ya mfano wa matumizi ya kidahizo n.k. Kidahizo pamoja na maelezo yake ndio huitwakitomeocha kamusi.
Kutafuta maana unayoitaka
Neno linaweza kuwa na maana moja au zaidi ya moja. Maana inapokuwa moja mtumiaji kamusi hana tatizo kwani hiyo ndiyo atakayoipata na kuichukua. Lakini neno linapokuwa na maana zaidi ya moja, mtumiaji kamusi hutatizika asijue ni ipi aichague. Ili kupata maana inayosadifu itafaa mtumiaji kamusi kutafuta maana ambayo inahusiana na muktadha wa neno linalotafutwa.
Example 1
Mfano: kifungonm vi-
  • kitu cha kufungia
  • kitu kinachotumiwa kufungia vazi kama vile shati, gauni, suruali n.k
  • adhabu ya mtu kuwekwa jela kwa muda fulani
Iwapo mtumiaji aliona neno ‘kifungo’ kwa muktadha wa: “Juma alihukumiwa kifungo cha miaka kumi baada ya kupatikana na hatia ya kubaka….” Maana ya mukatadha huu itakuwa ni ile maana ya 3 kwa sababu ndiyo yenye kuhusiana na muktadha ambapo neno kifungo limetumika na wala sio maana ya 1 wala ya 2.
 
Uhakiki wa kazi za fasihi simulizi

Uchambuzi wa riwaya ya JOKA LA MDIMU
 

Attachments

  • UCHAMBUZI WA JOKA LA MDIMU.pdf
    305.1 KB · Views: 103
Ngoswe penzi kitovu cha uzembe
 

Attachments

  • UHAKIKI-WA-NGOSWE.pdf
    656 KB · Views: 113
TAKADINI
 

Attachments

  • TAKADINI UHAKIKI (MPELLA EDUCATION BLOG).pdf
    323.3 KB · Views: 104
Back
Top Bottom