Wanafunzi Sekondari ya Chidya `wapagawa`

Mtu wa Pwani

JF-Expert Member
Dec 26, 2006
4,190
671
Wanafunzi Sekondari ya Chidya `wapagawa`
na abdallah bakari, mtwara

WANAFUNZI wa Sekondari ya Wavulana Chidya, iliyopo Wilaya ya Masasi, mkoani hapa, wamechoma shule hiyo na kuharibu mali mbalimbali, zikiwamo za mkuu wa shule, kwa kile wanachodai kuchoshwa kunywa uji usio na sukari.

Tukio hilo lilitokea juzi, saa 2:30 usiku, baada ya baadhi ya wanafunzi shuleni hapo, kujikusanya na kuanza vurugu zilizosababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 34.

Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa wanafunzi hao licha ya kuchoma shule hiyo, pia walichoma gari la shule aina ya Isuzu, tani saba, zizi la ng’ombe, mbolea na dawa ya mimea mali ya mkuu wa shule hiyo, Gaitan Mwatenga. Pia wanafunzi hao wanadaiwa kuvunja na kusomba vitu vilivyokuwamo katika duka linalomilikiwa na mhasibu wa shule hiyo, Salum Napinda.

Habari hizo zinadai kuwa wanafunzi hao walichoma ofisi ya walimu na maktaba ya shule na kufanikiwa kuteketeza kila kilichokuwamo ndani yake.

Wanafunzi hao wanadaiwa kuvunja luninga ya shule pamoja na kinasa mawimbi chake (Satellite Dish) kabla ya vurugu na moto huo kuzimwa na wanakijiji, baada ya walimu kuomba msaada.

Kabla ya kufanya uovu huo, wanafunzi hao walifanya mkutano katika moja ya chumba cha darasa na baadaye walizima umeme shuleni hapo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Ephraim Mrema, wanafunzi hao walivunja stoo ya kuhifadhia vifaa vya shule hiyo na kuchukua mapanga na fyekeo na fagio ambazo walizitumia katika uharibifu huo.

Kamanda Mrema alisema polisi walipofika eneo la tukio walikuta vibutu vya fagio vilivyotumika kuchoma gari, ofisi, maktaba, na zizi la ng’ombe.

Alisema inadaiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo ni wanafunzi hao kunywa uji usio na sukari kuanzia Machi, 30 mwaka huu, hadi siku ya tukio. Hali ya wanafunzi kunywa ujio usio na sukari imeelezwa na walimu kuwa imetokana na ufinyu wa bajeti.

Mrema alisema tangu kutolewa kwa taarifa za uji kutokuwa na sukari, wanafunzi walianza kupungua katika foleni ya uji siku hadi siku, jambo ambalo lilianza kuwatia shaka walimu.

Hata hivyo, licha ya walimu hao kutilia shaka mwenendo wa wanafunzi wao, hawakutoa taarifa katika vyombo vya dola.

“Taarifa za kiupelelezi zinaonyesha kuwa hakukuwapo na mawasiliano mazuri kwa wanafunzi juu ya kuwapo kwa uji usio na sukari, walimu hawakuwa wazi kwa wanafunzi. Hata kama walitoa taarifa ni kwa wachache ambao nao hawakufikisha ujumbe kwa wenzao,” alisema Kamanda Mrema.

Kamanda alisema jeshi lake linawatuhumu wanafunzi watano, akiwamo Kiranja Mkuu wa shule hiyo, Hamidu Matema (18) ambaye ni wa kidato cha nne. Hata hivyo, Matema amefanikiwa kutoroka na hajulikani alipo. Wanafunzi wengine wanne wamekamatwa.

Aliwataja wanaotuhumiwa na ambao watafikishwa mahakamani wakati wowote kuwa ni Hamidu Haruna (18) wa kidato cha nne, Mwahamudu Issa (18) kidato cha tatu, na wengine wawili wa kidato cha pili ambao ni Shabani Ramadhani (18) na Ramadhani Bofu (18).

Katika vurugu hiyo, wanafunzi 20 walitajwa kuhusika na tukio hilo. Uchunguzi wa awali wa polisi uliwabaini watuhumiwa hao kuhusika moja kwa moja, hivyo watafikishwa mahakamani na wengine 15 watajadiliwa katika vikao vya Bodi ya Shule na kuadhibiwa.

Shule hiyo ya bweni iliyoko umbali wa kilomita 22 kutoka barabara kuu ya Mtwara kwenda Masasi, ni miongoni mwa shule kongwe nchini. Ilianzishwa mwaka 1923, ikiwa chini ya Kanisa la Anglikana. Kwa sasa inamilikiwa na Serikali, ikiwa na mafanikio ya kuridhisha kitaaluma. Mwaka jana, wanafunzi 47 walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano na hivyo shule hiyo kushika nafasi ya kwanza katika Mkoa wa Mtwara.

mtanzania
 
Wanafunzi wa miaka 18 wanafanya mambo haya kwa sababu ya uji usiokuwa na sukari!so sad. Hawa wanastahili adhabu watakayopewa.
 
Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa wanafunzi hao licha ya kuchoma shule hiyo, pia walichoma gari la shule aina ya Isuzu, tani saba, zizi la ng'ombe, mbolea na dawa ya mimea mali ya mkuu wa shule hiyo, Gaitan Mwatenga. Pia wanafunzi hao wanadaiwa kuvunja na kusomba vitu vilivyokuwamo katika duka linalomilikiwa na mhasibu wa shule hiyo, Salum Napinda.

Azimio la Zanziba kwenda mrama! Mwalimu Mkuu ana mifugo ambapo utakuta mazao anauzia shule, mhasibu wa shule ana duka ambamo pengine kuna sukari anauzia wanafunzi. Halafu karne hii tunanyweshana uji sekondari? Usio na sukari? Isije ikawa ndio chelewa iliyomvunja mgongo ngamia!
 
hivi tuangalie sosi, ujasiri huu hawa watoto wameutowa wa[i?

jee hii hali yetu ya kuzomea vuongozi wetu, migomo na kukejeli viongozi hachezi duru ktk kuharibu vijana wetu?


tanzania tunapoelekea tunalea taifa la vijana wasiojielewa na wasioweza kutumia busara ktk kutatua matatizo yao.

mfano wa haya yanatokea hapa wenye kutaka serikali zipinduliwe, sehemu zijitenge, viongozi wazomewe, mafisadi wanyan'ganywe mali zao kwa nguvu.

tuna kazi kama jamiii,

kuutaka uongofu bila ya kufata njia zake ni sawa na kulitaka jahazi litembee nchi kavu
 
Mimi natofautiana na Mtu wa Pwani. Naamini matatizo ni wale wanaoongoza kutowathamini wale walio chini yao. Hii ni katika nyanja zote za jamii kuanzia mzazi na mtoto wake. Matatizo mengi yangeepushwa kwa kuwa wazi na kuwashirikisha stakeholders wote kwenye maamuzi. Mashuleni, kuweka mapato na matumizi wazi kwa kila anayehusika. Hii hatufanyi bali tunapendelea usiri na ubabe. Mimi sifurahii vitendo vya hawa wanafunzi bali ninachoomba ni wakati tunawahukumu tujaribu kuangalia mazingira yaliyopo kwa upana zaidi. Wakati tunasoma sisi, kila mtu alijua nafasi yake na aliiheshimu hivyo. Wakati sasa umebadilika na lazima na sisi kama jamii tubadilike kama tunataka maendeleo ya kweli na kujiepusha na migogoro kama hii.
 
Hapa lawama ni ktk sehemu zote mbili.Wanafunzi huwa wanadanganyika sana wakiwa ktk makundi na yawezekana ata wenyewe hawakutegemea litakuwa ktk kiwango hiki lakini maadamu walilianza waache walinywe kwa adhabu wanazostahili.Ni mara ngapi mtu ukiwa nyumbani unakosa vile vitu muhimu na ayumkini uchome vitu vyote eti kwasababu ya sukari ya tshs500 ni ujinga unaohitaji adhabu kubwa tu na ikiwezekana ata kulipa gharama.
Kwa walimu/wafanyakazi kuwa na duka sioni tatizo kwani wanawapelekea huduma karibu wanafunzi.Kwawale ambao hawajafika Chidya ni kuwa maduka ni mpaka uende Ndanda ambako unatakiwa aidha utembee kwa muda usiopungua msaa matatu mpaka Ndanda na ktk miteremko mikali au utumie barabara mpaka Chigugu huku magari yenyewe si uhakika sana.
Kubwa zaidi kwa upande wa Utawala ni taarifa.Kama walikuwa na matatizo ya bajetiwanafunzi wangepewa taarifa.Hakutokuwa na sukari kwa muda huu lakini we promise kuanzia tareh fulani sukari itapatikana.Ushirikishwaji na kwa kuanzia unawachukua viongozi mnaongea nao na kisha unawahutubia wanafunzi kwa ujumla.
Tatizo nililonalo mimi ni uwezekano wa mtu kuwa amefanya kosa lakini asiweze kujulikana na baadhi ya hao walio tajwa maskini pengine hawakuhusika hivyo basi zoezi la kuwapata wahusika lifanyike kwa umakini mno ili kuondoa kuonea wanafunzi na kuacha baadhi ya watuhumiwa.

Nawasilisha.
 
Back
Top Bottom