Wanafunzi Chuo Kikuu Tumaini wagoma

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,072
1,250
Wanafunzi wa vyuo vikuu vishiriki vya Tumaini Kampasi ya KCMC na Kampasi ya Masoka katika Manispaa ya Moshi, jana na juzi waliingia katika mgomo wa kutokuingia darasani ili kuushinikiza uongozi kutoa ufafanuzi kuhusu makato ya fedha zao kutoka katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB).
Katika Kampasi ya KCMC, wanafunzi hao juzi waligoma kuzungumza na uongozi wa chuo hicho kutokana na kile wanachodai ni kutokukubaliana na maelezo yao hivyo kuutaka uongozi huo kumwita mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Askofu Martin Shao.
Taarifa kutoka kwa mmoja kati ya viongozi wa serikali ya wanafunzi zinasema wameushinikiza uongozi kumwita Askofu Shao kumweleza kuhusu mabadiliko ya mwongozo wa chuo hicho hususani katika kipengele cha ada ya kitivo.
Mmoja wa viongozi wa wanafunzi alisema tatizo kubwa lililopo chuoni hapo ni kutokuelewana baina yao na uongozi wa chuo na kuongeza kuwa mambo yote yamewekwa bayana katika kitabu cha muongozo cha mwaka 2009/11 hivyo uongozi hauna budi kuwa wazi kwa wanafunzi.
Chanzo hicho cha habari kinabainisha kuwa kutokana na kutokuwapo kwa uwazi wa taarifa kuhusu fedha za mikopo zilizotumwa na HELSB ndicho chanzo cha migogoro hiyo.
“Tusingegoma ila ni kutokana na kufichwa kwa baadhi ya taarifa kutoka katika bodi ya mikopo ambazo zinakaliwa na uongozi wa chuo….sisi tunamtaka mwenyekiti wa bodi ili tumweleze matatizo yetu na siyo mkuu wa chuo wala mjumbe wa bodi,” alisema. Naye Mkuu wa chuo hicho Kampasi ya KCMC, Egbert Kessi, alithibitisha kuwapo kwa mgomo tangu Novemba 24 ambapo alisema walizungumza nao na kukubaliana kuwa Desemba Mosi watazungumza na kukubaliana kwa pamoja jambo ambalo lilimshangaza kutokana na maamuzi tofauti waliyoyachukua wanafunzi hao.
Alisema awali tatizo lilikuwa kwa wanafunzi wa mwaka wa tatu, lakini cha kushangaza mgomo huo jana ulikuwa ni wa chuo kizima jambo ambalo lilimlazimu Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mussa Samizi, na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lucas Ngh’oboko kuingilia kati bila mafanikio.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom