Wamiliki wa mabasi walalamikia gharama za usafirishaji wa abiria kuongezeka. Waiomba Serikali kupitia upya sheria ya usafiri

miss zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
3,008
2,000
CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kimesema kuna umuhimu kwa serikali kupitia upya na kushirikisha wadau kikamilifu kuhusu kanuni za sheria ya usafiri, ili kuondoa tozo zitakazoongeza gharama za uendeshaji kwa usafirishaji wa abiria.


Kwa mfumo mpya, kwa sasa tiketi za usafiri zitakatwa kielektroniki kwa abiria wote, jambo ambalo litaondoa usumbufu na udanganyifu kwa wasafiri.

TABOA ilitoa malalamiko hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao baina yake na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).

Kaimu Katibu Mkuu wa TABOA, Joseph John, alisema ni vyema mamlaka hizo zikafuatilia kwa kina na kufafanua tozo ya asilimia mbili ya gharama za uendeshaji wa mfumo ulioletwa kwao na LATRA.

Alisema TABOA iliwasilisha kwa wazabuni waliokuwa tayari kufanya kazi hiyo kwa tozo ya asilimia 0.7 ya gharama ya tiketi, lakini hawakukubalika na sasa kumejitokeza mzigo wa uendeshaji.

Jingine ni malipo kupitia T-Pesa ambapo mmliki wa basi atalazimika kuweka kiasi cha fedha kwenye mashine ya kukatia tiketi (POS), ili amkatie abiria tiketi.

Kwa mujibu wa John, ni vyema mamlaka zikafafanua jinsi zilivyojipanga kufanya uwiano wa kisheria katika kuendesha mfumo huo ili isifike wakati wasafirishaji wakatozwa faini mara mbili kwa kosa moja.

“Kwa taswira ya haraka tunazo mamlaka mbili na kila moja ina majukumu tofauti ya kisheria. TRA itamtaka mmiliki kuhakikisha anatoa risiti halikadhalika LATRA inamtaka mmiliki kutoa tiketi, hivyo tutakuwa na risiti na tiketi, ni vema tuwe na hoja zenye nguvu ili kuzishauri mamlaka kuzingatia haya,” alisema John.

Jambo jingine lililolalamikiwa na TABOA ni tozo ya asilimia 0.5 ya mauzo ya tiketi inayotozwa na LATRA kupitia mfumo huo, na kwamba wanaona si sahihi kwa kuwa mamlaka hiyo haitoi huduma yoyote kwao na jukumu lake la msingi ni udhibiti.

Aidha, TABOA ililalamika kutoshirikishwa kwenye mchakato wa kupata mzabuni atakayeendesha mfumo wa ukatishaji tiketi pamoja na kuzuia leseni za mabasi kama hawatajiunga na mfumo huo, na kwamba ni vyema kukawa na maelewano ya wadau.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu, wasafirishaji hao walilazimika kwa kauli moja kutomtambua mzabuni wa mfumo aliyetafutwa na LATRA bila ushiriki kikamilifu wa wadau.

Pia waliazimia mashine za kutolea risiti za EFD ziruhusiwe kutumika kukatishia tiketi ukiwa mwafaka wa jambo hilo hautapatikana na kuitaka LATRA kujitoa kwenye uendeshaji wa mfumo wa ukatishaji tiketi hizo na kazi hiyo iwe chini ya TRA.

Walitaka kusogezwa mbele muda wa kuanza kutumia mfumo mpya wa kielektroniki, ili kutoa nafasi ya kuelimisha watumiaji na wananchi kwa ujumla.

Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa LATRA, Johansen Kahatano, alikubaliana na baadhi ya hoja za wadau hao ikiwamo kuongeza muda ili kuruhusu kutolewa kwa elimu zaidi.

“Tutatafuta nafasi kukutana na uongozi wenu ili tuone jinsi gani tunaweza kulifanya hili, tunawahakikishia kila mmoja tutamfikia. Kuhusu suala la kuzuia leseni kwa wasiojiunga na mfumo huu pia litasogezwe mbele,” alisisitiza Kahatano.

Kuhusu tozo ya asilimia 0.5, alisema ni takwa la kisheria lililowekwa na Sheria ya Mamalaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini ya mwaka 2019, ambalo ni lazima litekelezwe.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom