Wameshindwa kuongoza, sasa wanashikana mashati! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wameshindwa kuongoza, sasa wanashikana mashati!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, Jul 22, 2009.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Jul 22, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Na. M. M. Mwanakijiji (Tanzania Daima)

  MIONGONI mwa hesabu rahisi kabisa kujifunza ni hesabu za seti. Ni miongoni mwa mambo ya msingi kabisa ambayo mtoto anajifunza katika kuhusisha mafungu mbalimbali ya vitu na idadi.

  Hata hivyo lengo kubwa la kujifunza hesabu za seti si kujua hasa idadi ya vitu bali kujua vitu vinahusiana vipi na kuweza kupima kipi kikubwa chenye kuhusisha vitu vingi zaidi. Hivyo, kama umesahau hesabu hizi usiwe na shaka nitakukumbusha kwa haraka haraka (hivyo usitimke!).
  Hesabu za seti zinahusu makundi ya vitu mbalimbali. Zinahusu kuhusisha kundi kubwa na makundi madogo madogo na kuona jinsi gani makundi madogo yanahusiana na kundi kubwa na jinsi gani yenyewe yanahusiana au kutohusiana.

  Kwa mfano, katika kundi kubwa (Seti kubwa) ya "Vyombo vya usafiri" vimo vyombo vyote vinavyotumiwa na wanadamu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ukiondoa miguu yao.Ndani ya hii seti kubwa kuna makundi madogomadogo (seti ndogo) za "vyombo vya majini", "vyombo vya anga" na vyombo vya "ardhini".

  Na seti hizo ndogo ndogo nazo zinaweza kugawanywa ndani yake na kukuta kwa mfano kwenye vyombo vya majini kuna "mitumbwi, ngalawa, merikebu, nyambizi" na kwenye vyombo vya ardhini kuna "pikipiki, treni, mabasi, magari madogo madogo, punda, ngamia n.k."

  Sasa mtu anaweza kuendelea kugawanya seti hizo ndogo ndogo hata kwa aina ya nishati inayotumika, watengenezaji, nchi vinakotoka vyombo hiyo n.k

  Lakini mwisho wa siku, vitu hivyo vyote hata uviweke kwenye seti ndogo kiasi gani bado vinabakia kuwa kwenye seti kubwa ya "vyombo vya usafiri."

  Sasa mtu ambaye ujuzi wake au uzoefu wake ni kutumia usafiri wa punda mnaweza kubishana milele ukijaribu kumfafanulia faida ya kusafiri na ngamia au ubora wa ngamia, kama vile mtu ambaye hajawahi kupanda ndege na amezoea mabasi, ukimuambia raha na uharaka wa kupanda ndege.

  Sasa, bila ya kuzama sana kwenye seti za vyombo vya usafiri, niseme kwamba tuna seti moja kubwa inaitwa "Watanzania". Seti hii inajumuisha watu wote ambao wana uraia wa Tanzania.

  Seti hii haingalii usomi, dini, rangi, kabila au kitu kingine chochote, yenyewe inaangalia kitu kimoja tu nacho ni "je wewe ni Mtanzania". Kama wewe ni Mtanzania basi umo ndani ya seti yetu. Hivyo, mtu yeyote ambaye ni Mtanzania anaingia kwenye seti hii bila hata ya kubisha hodi.
  Hata hivyo, seti yetu hii ndani yake yenyewe kuna seti nyingine ndogo ndogo ambazo hao Watanzania wamegawanyika ndani yake.
  Nitatumia seti ndogo tatu nazo ni "Makabila", "Imani/Dini" na "Vyama vya Siasa."

  Kwenye seti ndogo ya "Makabila" kuna seti ndogo za "Wakurya, Wanyiramba, Wamatengo n.k", na kwenye seti ndogo ya "Imani/Dini" ndani yake kuna "Waislamu, Wakristu, Wapagani, Wabudha n.k" hali kadhalika kwenye seti ndogo ya "Vyama vya Siasa" kuna "Wana CCM, Wana CHADEMA, Wana CUF, n.k."

  Wakati mwingine, utakuta mtu ni mwanachama wa seti hizo ndogo zote tatu, kwamba yuko kwenye kabila la Mnyaturu, ni Muislamu na vile vile ni mwanachama wa CHADEMA. Lakini bado ni Mtanzania (seti kubwa).
  Utakutana na mtu mwingine ambaye yuko ndani ya Ukristu lakini hajitambulishi na kabila moja la Tanzania, lakini bado ni Mtanzania (mfano mzungu aliyehamia toka Uingereza na kuupata uraia wa Tanzania.)
  Vile vile unaweza kukutana na mtu ambaye ni mwanachama wa chama siasa lakini haamini dini yoyote ile na tena yawezekana haamini hata uwepo wa Mungu. Huyu naye ni Mtanzania.

  Hivyo, sisi sote katika vijiseti vyetu vidogo vidogo tuna tofauti. Tena wakati mwingine tofauti hizo ni kubwa mno na zinaweza kusababisha hata watu watoane ngeu. Lakini tukijiangalia katika picha kubwa tunajikuta kuwa sisi ni Watanzania, SISI TUKO KWENYE SETI MOJA.

  Malumbano na migongano ya maneno ya hivi karibuni katika mjadala wa Kadhi, mjadala wa OIC, mjadala wa Ilani ya Wakatoliki (Waraka), na mijadala ya kisiasa Bungeni imenithibitishia kuwa sisi sote kwa namna tofauti tofauti tumepigwa upofu wa kutoona nje ya seti zetu.

  Hapa nazungumzia seti ndogo ya Dini/Imani. Karibu sisi sote tumejikuta tukigawanyika kwa misingi ya dini zetu na dini za wale tunaowaunga mkono katika mijadala hii.

  Waislamu wamejikuta wakiunganishwa pamoja kutetea Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga OIC. Wakristu wamejikuta wakijiunga pamoja kupinga Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga OIC.

  Na Wanasiasa wamefuata misingi ya dini zao kutetea Bungeni yale wanayokubaliana na imani zao; Wakristu wanaonekana kuunga mkono viongozi wao Wakristu, na Waislamu wanaonekana kuunga mkono yale viongozi wa Kiislamu wanataka. Kila mmoja hataki kutoka nje ya seti yake.

  Inasikitisha na inatisha.

  Inasikitisha kwa sababu inathibitisha kile nilichokisema miaka karibu miwili iliyopita; kwamba "wameshindwa kuongoza, sasa wanatuburuza."
  Ndio maana yangu ya kuwabambikia hawa tunaowaita viongozi kuwa ni "watawala wetu." Neno hilo nililitunga nikimaanisha kuwa hawa siyo viongozi tena, bali ni mabingwa wa kutawala na katika kututawala hivyo badala ya kutushawishi ili tukubaliane nao, wamebakia kutuburuza.

  Lakini sasa bahati mbaya, wakati wanatuburuza sisi wengine, wao wenyewe wamebakia kushikana mashati. Kwenda mbele hawendi, kurudi nyuma aibu, kukubali kushindwa hawawezi; imebakia kupigana mikwara.
  Inatisha kwa sababu kwa kadiri wanavyoendelea kushikana mashati kitakachofuatia, mmoja atampiga ngumi mwingine, na mara mwingine ataingilia kati akaambulia kisukusuku, matokeo yake wanapigana na wale Watanzania wenye kufuata seti zao ndogo ndogo watajipanga kuunga mkono upande mmoja au upande mwingine.

  Ninachosema ni kuwa, kiuzembe uzembe na kijinga kijinga, sisi wenyewe tunatengeneza mazingira ya kuleta machafuko ambayo kwa mtu yeyote mwenye akili timamu hayana A wala Z.

  Lakini hizi seti ziko vipi? Je mtu anaweza kutoka nje ya seti yake na kujaribu kuangalia kile kilichoko kwenye seti nyingine ili akielewe? Je, kwa vile wote tuko kwenye seti moja, tunaweza kukaa chini pamoja na kusema ni nini kilichobora kwa seti yetu nzima.

  Hadi hivi sasa sijaona kiongozi ambaye anafikiria nje ya seti yake. Wengine (kama kina Kingunge) wanajaribu kutokuwa na upande, lakini wanapofanya hivyo wanaonekana wamechagua upande! Hivyo wanaongeza kukorogana.
  Kikwete, amekaa pembeni anamtuma Pinda na kumuweka mahali pagumu; kabla hawajatulia, Membe naye anakuja na jambo jingine; wote wawili ni Wakatoliki wanatolea misimamo ya serikali masuala ya Waislamu.

  Waislamu wanajiuliza "kulikoni". Mufti na wenzake na wenyewe wanakuja juu wanataka kile ambacho wanaamini ni haki yao. Mohammed Said anasema Waislamu wameonewa; Mara Hizibu nyingine imeibuka inasema utawala bora ni dola ya Kiislamu; Kilaini naye anakuja na hoja zake na kabla hatujatulia, Mokiwa naye ndani na hatujavuta pumzi Khalifa Khamisi. Mtanzania wa kawaida anakodoa macho anajiuliza "kaugonjwa gani kamewakumba hawa?"

  Hebu tuziangalie hizi seti ndogo ndogo, tuangalie kama mtu ambaye yuko nje ya seti hizo:

  Wakatoliki/Wakristu
  Hawa ndugu zetu wamekuja na Ilani pamoja na mwongozo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010. Kwa mujibu wa utangulizi wa Ilani hiyo Wakatoliki wametoa mapendekezo yao kwani ni "muhimu kupendekeza vipaumbele vyetu kama jamii tukiwaambia viongozi wetu wajao yale ambayo tungependa yafanyike kwa ajili ya jamii yetu.

  Katika uchaguzi, hatupigi kura tu, tunapaswa kueleza makusudio yetu kwa yale tunayofikiri kuwa muhimu sana kwa Taifa."
  Ukisoma Ilani nzima utakutana na mambo mengi mazuri na ya kuvutia ambayo hata watu wa seti nyingine wakiyasoma (ukiondoa machache) wanaweza kuyakubali tu. Tatizo ni kuwa, Wakatoliki wametoa mapendekezo yao kutoka kati seti yao lakini wanataka yakubalike na watu wa seti nyingine pia! Wanaamini kuwa ni mambo mazuri kwa "jamii" lakini wakati huo huo wanapendekeza mambo mengine yasifanyike ambayo watu wa seti nyingine wanaona ni muhimu kwa jamii vile vile.

  Matokeo yake, wanawavutia watu wa seti moja (Wakristu wenzao) na wakati huo huo kuwatenga mbali watu wa seti nyingine (Waislamu).
  Kwa vile Ilani yao na Mwongozo wao vyote vimetoka katika mtazamo wa seti ya Wakatoliki/Wakristu hata kama kuna mazuri 1001, Waislamu wanajikuta siyo tu wametengwa lakini wanaonekana wamelengwa na nyaraka hizo. Hivyo, Waislamu wanakunja nyuso zao, seti yao inatishiwa.
  Wakatoliki wanasema hizi nyaraka zinawatishia mafisadi; wanadai kuwa mafisadi ndio wanaziogopa. Hawajali hisia na fikra za ndugu zao Waislamu. Wanapuuza madai ya Waislamu, wanayaona hayana msingi, hawako tayari kukaa chini kuyaelewa.

  Inanikumbusha matukio ya Mwembe Chai na yale ya Pemba. Jinsi dola ilivyotumia nguvu chini ya kiongozi Mkatoliki (Benjamin Mkapa) dhidi ya raia wasio na silaha kali.

  Nilitarajia viongozi wa Kanisa wangetoa msimamo mkali wakati ule, lakini kinyume chake walionekana kutoa baraka za vitendo vile. Hawakutaka kuungana na ndugu zao Waislamu kutaka uchunguzi huru ufanyike. Hawakufanya hivyo, kwa sababu watu walioshambuliwa si watu wa seti yao, na bahati mbaya kiongozi aliyeruhusu mambo hayo ni mtu wa seti yao!

  Sasa leo serikali ikiwa chini ya kiongozi Muislamu, Wakatoliki wanaonekana wana ujasiri wa kuzungumza sana na hata kuinyoshea kidole serikali. Sitashangaa muda si mrefu ujao majina ya viongozi wa kisiasa yataanza kutajwa hadharani kuwa hawafai. Fikra za seti zinadumishwa.

  Waislamu
  Ndugu zetu Waislamu nao wako kwenye seti yao. Katika seti hii kila mtu anachosema kinachogusa Waislamu bora afikilie mara mbili kwani vinginevyo atanyoshewa kidole kuwa ni "adui wa Uislamu." Hivyo imefikia mahali watu wanaamua kufunga vinywa vyao kwa sababu hata kama wanaujua ukweli au wanataka kuchangia jambo fulani lenye manufaa wanaogopa kunyoshewa kidole.

  Matokeo yake ndani ya seti hiyo hiyo kuna kugawanyika. Wapo wale wanaoounga mkono BAKWATA na wamsikiliza Mufti na pia wapo wale ambao ukiwatajia neno ‘BAKWATA' wanaona umewatajia kitu kutoka sayari nyingine. Kwa hilo kundi la pili, BAKWATA ni chombo cha serikali.

  Hivyo, wanaikataa kuwakilisha maslahi yao. Wakati huo huo, watu wa Bakwata wanajua kuwa wao wanawakilisha waislamu wengi zaidi nchini na hivyo wanazungumza kwa niaba ya waislamu wengi (japo si wote).
  Sasa, katika seti hii kuna watu ambao wao hakuna lolote ambalo serikali inaweza kufanya likawa zuri isipokuwa lenye maslahi kwa Waislamu kwanza. Na kama kuna kitu ambacho kimenishtua, ni pale kundi fulani lilipojitokeza na kudai kuwa kama Mahakama ya Kadhi haitaundwa, basi Waislamu wasiichague CCM mwaka 2010.

  Yaani, kati ya vitu vyote ambavyo vinaweza kusababisha watu wasiichague CCM, kwao suala la Mahakama ya Kadhi ndiyo msumari wa mwisho! Lakini vile vile wanaposikia Wakatoliki wamekuja na mwongozo wa kupiga kura na wao wanakuja juu kwanini Kanisa linaingilia siasa. Lakini hawakusimama kuwapinga watu wa seti yao waliposema Waislamu wasiichague CCM.

  Naweza kuendelea na kuchambua seti hizi na kuonyesha ni jinsi gani zimefungwa katika seti zao na matokeo yake sisi wengine tunaburuzwa tu.
  Ni mpaka pale viongozi wa Kiislamu na viongozi wa Kikristu na hata wasio na dini watakapotoka nje ya seti zao na kujiangalia kama watu wa seti moja kubwa (Watanzania) ndipo baadhi ya matatizo yanaweza kuonekana vizuri na masuluhisho yaliyo bora kwa wote yanaweza kupatikana.

  Kwa mtindo wa sasa, kila seti inasababisha matatizo yake na hivyo kusababisha matatizo kwa seti kubwa na suluhisho, yote yanatolewa yakiwa na misingi ya fikra za seti.

  Vipi nao Wapagani?
  Ukisikiliza mijadala ya kidini inayoendelea unaweza kuamini kabisa kuwa Tanzania ina Waislamu na Wakristu tu! Imefika mahali wanazungumza kana kwamba wanawakilisha Watanzania wote. Tena ukiangalia vizuri utagundua kuwa wote hawa wanajivunia dini za kigeni kila mmoja akitaka kujionyesha anaishika dini yake zaidi na imefika mahali, wanazungumza kana kwamba dini hizo zina haki miliki ya dini Tanzania.

  Sasa ni nani anatetea maslahi ya wale wanaoabudu mizimu na wenye imani za jadi? Je hawa imani zao ni za chini kulinganisha na za Wakristu na Waislamu na hivyo siyo Watanzania kamili?

  Je, hawa nao wana nafasi gani katika mijadala inayoendelea? Kwa mfano itakapoanzishwa mahakama ya Kadhi, je Mpagani au mtu asiye na imani ambaye ameoa Muislamu au Kuolewa na Muislamu ana haki gani?

  Je wale wasio na imani na wenyewe wachague viongozi wajao kwa misingi ipi au ni nani atakayetoa muongozo ukasikika? Ni kwa sababu hiyo sitaki kuamini kuwa serikali inawasikiliza Wakristu na Waislamu zaidi kana kwamba seti ya imani ina makundi hayo mawili tu!

  Hoja yangu kubwa ni kuwa, tujifunze kukaa pamoja kama watu wa seti moja. Tofauti zetu ziwe msingi wa sisi kukaa pamoja kuzungumza na kujaribu kutafuta utatuzi wa migogoro yetu.

  Tusijikite katika seti zetu hizi kiasi kwamba mtu mwingine wa seti nyingine akisema jambo, hata kama ni bora, basi tunalipinga alimradi hatutaki kuonekana tunamuunga mkono hata kama ukweli wa jambo hilo.
  Ndugu zangu, kama kichaa anakupigia kelele utoke barabarani kwa sababu kuna gari linakuja kwa kasi, utamdharau na hautaungalia upande anaoelekeza kwa sababu yeye ni kichaa? Kama adui yako akikuambia ‘angalia mwiba huo,' utaendelea kukanyaga na kuvumilia maumivu kwa sababu hukutaka kumsikiliza adui yako? Kufanya hivyo ni kujificha katika seti.

  Napendekeza kabla hatujazama katika ubovu wa seti zetu na kiburi cha seti zetu, tukae pamoja tuzungumze. Ningependa kweli kuona muongozo wa kuelekea uchaguzi mkuu unatolewa kwa pamoja na viongozi wote wa dini baada ya kukaa pamoja.

  Muongozo ambao utatufaa watu wa seti zote. Muongozo ambao kweli mafisadi wataogopa kwani hakuna mtu wa seti yao atakayesimama kuubeza kwa vile umetolewa na seti moja kubwa; ya WATANZANIA.

  mwanakijiji@jamiiforums.com
   
 2. Che Guevara

  Che Guevara JF-Expert Member

  #2
  Jul 22, 2009
  Joined: May 22, 2009
  Messages: 1,178
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 145
  Mkuu Mkjj umechokoza vizuri.

  Najua unafahamu kuwa aliyesema kuwa kama Mahakama ya Kadhi haitaundwa, basi waislamu wasiichague CCM mwaka 2010 ni Mufti wa waislamu, Sheikh Issa Shaaban bin Simba. Mzee Kingunge hapo hakusema kitu, alikaa kimyaaaa...

  Waraka wa maaskofu haukutaja majina ya vyama vya kupigiwa (au kutopigiwa) kura wala majina ya watu. Umetaja sifa tu za anayefaa na asiyefaa.

  Inasemekana kuwa Kingunge ni mpagani...

  Kingunge amesaidia kitu kimoja bila kujua. Kauli yake ya kupinga kwake Waraka akiwa Bungeni kumefanya watu wengi ambao bado walikuwa hawajausikia wala kuufahamu kuutafuta ili wauone na kuusoma ili wafahamu kilichomo ndani yake. Wengi wameuona na kuusoma, na wengine wanaendelea. This has become a part of civic education to the people.

  Kingunge amepagawa kwani alitaka Serikali ya CCM tu ndio iwe na monopoly ya "kuelimisha" wapiga kura purely for its own advantage.
   
  Last edited: Jul 23, 2009
 3. M

  Magezi JF-Expert Member

  #3
  Jul 22, 2009
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  Kama watanzania wote wakielewa ulichoandika hapa ambacho nimekiwekea rangi nyekundu, basi malumbano ya kidini yasinge kuwepo. Hongera Mwanakijiji kwa kutuelimisha
   
 4. B

  Bull JF-Expert Member

  #4
  Jul 22, 2009
  Joined: Nov 4, 2008
  Messages: 984
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Hivi CHADEMA waki-win election mwakani watakua kwenye set gani? wataleta mahakama au LA? nivizuri tuelewe msimamo wao kuliko kuwa mabubu!
   
 5. H

  Hofstede JF-Expert Member

  #5
  Jul 22, 2009
  Joined: Jul 15, 2007
  Messages: 3,584
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 0
  Duh! mkuu samahani, huenda memory chip imecorrupt. Ila ninachojua na kufahamu ni kuwa mauaji ya mwembechai yalitokea Ijumaa tarehe 13 February 1998. Sasa kama kipindi hicho rais bado alikuwa ni Mwinyi utakuwa upo sahihi. Ila ninachojua mimi Mkapa (Mkatoliki) alishika IKULU mwaka 1995 kwa asilimia 60% + hivi.

  Mwanakijiji uchambuzi wako umekaa vizuri unameoneka kuwa umetolewa na mtu aliye kwenye "Set kubwa" au "Universal set", japo kidoogo umekuwa attracted na ka-subset ka "ukristu". Maana umechambua sana uislam kuliko ukristu, umeacha DECI, kina Kakobe, Mapigano ya kule Arusha ya KKKT. Ila umeshindwa kumalizia subsets za siasa na vyama vya siasa na ukabila kama ulivyoanza. Any way labla itaendelea...
   
  Last edited: Jul 22, 2009
 6. Mtimti

  Mtimti JF-Expert Member

  #6
  Jul 22, 2009
  Joined: Feb 23, 2008
  Messages: 912
  Likes Received: 185
  Trophy Points: 60
  mzee mwanakijiji nakupa kumi zote,umeandika kitu ambacho hakifikiriki lakini kipo ndani ya ubongo na maisha yetu ya kila siku na ndicho kinachotusumbua na ndicho kitakochotupeleka pabaya(kuchukiana,kutoshirikiana kwenye shida na raha,vita vya wenyewe kwa wenyewe nk)kama viongozi wetu hawatokuwa na ujasiri wa kuzuia hili jambo.
   
 7. Mtimti

  Mtimti JF-Expert Member

  #7
  Jul 22, 2009
  Joined: Feb 23, 2008
  Messages: 912
  Likes Received: 185
  Trophy Points: 60
  ndg mbona umeng'ang'ania sana kujua msimamo wa chadema juu ya hili suala?maana naona thread nyingi tu lazima uulize hii kitu.
  ushauri;chadema wana ilani yao ya uchaguzi hivyo ni vizuri ukaitafuta na kuisoma kwani huo ni mwongozo wa mambo watakayoyafanya pindi wangekuwa madarakani
   
 8. Juma Contena

  Juma Contena JF-Expert Member

  #8
  Jul 22, 2009
  Joined: May 21, 2009
  Messages: 1,195
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 135
  mh, umeongolea yote especially hizo set, ambazo ni chanzo cha matatizo yasikoua na kichwa wala miguu. Cha muhimi ni hiyo seti kubwa ambayo ni Tanzania, na ambayo inatakiwa iwe aina dini yeyote au kuwafurahisha wengine basi ina amini miungu yote. point ni kwamba watu wajue kuheshimu set za wengine vinginevyo bwana god afungue mbingu siku moja na aseme ni dini gani au njia gani itumike kumfikia yeye.

  tatizo kubwa si viongozi wa dini, bali ni viongozi wa serikali kwa upande wangu
  mh.Kikwete awe rahisi wa mwisho tanznania kuchaguliwa kupitia urafiki wa zamu yetu ya kujisaidia imefiaka, kikwete we ndio nahodha wacha sisi tule kwa chini. wabunge wana play a big role kwenye kuchagua kiongozi wa taifa sasa umefikia wakati wa wao kufikiria ni yupi apewe kura ya urais kwenye uchaguzi. na wengi wajitokeze kugombania kiti hicho rather watuletee tu mtu from knowwhere.

  Hii biashara ya dini mi nadahani imeruhusiwa kupamba moto huko tanzania for fear of upsetting religious figure viongozi wanasahau kwamba tanzania aina dini au ni ya dini zote. kwa fikra hizi mi nadhani ilikuwa ni jukumu la serikali kupiga vita miistari hii ya kufikiria kwa namna yeyote hile ataikibidi........

  kitu au naweza kusema tatizo lingine linalojitokeza ni jinsi gani inaonesha viongozi wetu wasivyo fahamu watu wao, na what role they have to play in that whole set. lilikua ni jukumula wabunge wote na viongozi wote wa sheria kukemea including the police and the judiaciary kukemea mambo ya dini after all part off their swearing include kuheshimu na kulinda katiba ya watanzania ambayo aina dini sasa leo iweje hawa watu wafike hapo walipo na baadhi ya wabunge wathubutu hata kuwa tetea wana haki gani katika macho ya set kubwa ambayo aina dini au ni ya dini zote. iweje mmoja ajione yeye apewe special treatment i think viongozi wetu wa serikali have nurtured those ideas for long enough, something has to be done. we do not elect them for their small sets but the whole set, so they should start to think for the benefit of the greater whole and those religious ideas should remain as believes only.
   
 9. Che Guevara

  Che Guevara JF-Expert Member

  #9
  Jul 22, 2009
  Joined: May 22, 2009
  Messages: 1,178
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 145
  yalitokea Ijumaa tarehe 13 February 1998.

  Ebwana mkuu Hofstede, poa... Thanks.
   
 10. Alwatan

  Alwatan JF-Expert Member

  #10
  Jul 22, 2009
  Joined: May 19, 2009
  Messages: 409
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 33
  Hili neno mkuu... hoja bora ni ile inayoweza kujisimamia yenyewe, na hii ni mfano.
   
 11. M

  Mwafrika JF-Expert Member

  #11
  Jul 22, 2009
  Joined: Nov 20, 2006
  Messages: 5,490
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  KIkwete anajua kuwa nchi imemshinda kuongoza na sasa ameamua kutumia udini kuwagawa watanzania. Hebu mtanzania jiulize swali moja, kwa nini Game Theory na wadini wenzake hapa wanangagania (msisitizo kwenye ng bila ') sana kuwa CHADEMA itoe tamko kuhusu mahakama ya kadhi wakati ambapo Kikwete (aliyeapa kuiheshimu na kuilinda katiba ya JMT) amekaa kimya?

  Kikwete anahusika kwa njia moja au nyingine katika mambo haya na wanaomfahamu hawashangai kuwa amekaa kimya kabisa (huku akienda nchi za nje) kama vile hakuna kinachoendelea.
   
 12. F

  Felister JF-Expert Member

  #12
  Jul 22, 2009
  Joined: Aug 5, 2008
  Messages: 377
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 0
  Mwanakijiji thanks a lot for the gud analysis Mungu akubariki. Jambo moja la kuzingatia katika kuondoa mawazo/hisia hasi katika makundi yetu ya kijamii ya kitanzania ni muhimu kwa viongozi wa dini kuheshimu utaifa wa Tanzania kwamba serikali yetu haina dini ila watu wake wana dini. Pindi kiongozi yeyote yule wa dini anapovuka mipaka yake bila maridhiano ya wenzake katika mambo yanayohusu taifa; hilo ni kosa hata tulipake rangi ipi bado litabaki kosa na hasa kwa wakristo tunaoongozwa na amri kuu mbili ya upendo. Mtizamo wangu ni kuwa nikosa kwa viongozi wa Rc kuruhusu waraka huo hasa kwakuzingatia kuwa haukuwashirikisha watu wa makundi mengine katika uandaaji kwani hilo jambo linahusu taifa na si kundi fulani la jamii hata kama yaliyomo ni mazuri lakini ubaya mmoja tu ni kuwa taasisi inayoisimamia ni ya kundi moja la wanajamii na uwezekano wa kuingiza mionjo ya kiimani ni mkubwa. Kama hao viongozi wange mainstream agenda ya uchaguzi ndani ya mahubiri yao hapo wangekuwa sahihi tatizo langu kwao nikuandaa waraka kama vile vyama vya siasa vinavyofanya, sasa hapo ndo tunapo changanya mambo na hapo ndo wengi wanapoona viongozi hawakufikiria hisia ya makundi mengine.

  Well inaweza ikawa hawakukusudia na kwavile makundi mengine yamelalamika basi kwa kuongozwa na upendo wafikirie otherwise. Kama ulivyotoa wito ni bora sasa viongozi wa makundi hayo wakakaa pamoja na kuona jinsi ambavyo kwa pamoja wanaweza saidia elimu hiyo kwa raia wote wa Tanzania bila kujali itikadi ama imani zao lengo likiwa kupata viongozi wanaokubalika kitaifa. Kwa hakika kazi hii ilipaswa kuwa ya serikali lakini maadamu serikali yetu pengine haina resources za kutosha basi viongozi wa dini watumie hekima na busara katika kutekeleza hilo jukumu.
   
 13. Madela Wa- Madilu

  Madela Wa- Madilu JF-Expert Member

  #13
  Jul 22, 2009
  Joined: Mar 24, 2007
  Messages: 3,074
  Likes Received: 35
  Trophy Points: 135
  Tumeingia kiwi cha akili.
  Kiwi cha macho aghalabu hutoweka katika muda mfupi.
  Kiwi cha akili hutanda kivuli chake na kufunika mazuri na mabaya kwa pamoja kwa muda mrefu na athari zake hujitokeza tena na tena.

  Konda wa DD haoni abiria wake katika sura zao huwaona katika thamani yao kwa kiwango cha nauli. Ndiyo maana huja juu sana aonapo dent kakalia siti kwani thamani ya denti ni kiduchu, denti huonyesha sura ya Sh50 au 100 tu.

  Mwenye Hoteli huona wateja wake katika sura ya sahani za pilau wali chapati na vikombe vya chai.

  Mbunge naye huwaona wananchi awawakirishao katika sura ya karatasi ya kupigia kura, ndiyo maana akirudi jimboni na kuulizwa ahadi na watu wa jimboni kwake, mbunge huyu hushika tama na kujiuliza tangu lini kura zikadai ahadi? Akili mwake mbunge hakuna watu kuna kura (makaratasi yasiyo na thamani).

  Sijui na maaskofu wanatuona ni kondoo na mbuzi??

  Majaji nao sijui watuonaje?

  Askari polisi je?

  Watu wa TRA?

  Viongozi wa serikali yetu huenda wanajiona ni Warithi wa damu wa nchi Tanzania!! Sijui.

  Mzee MMK, ni kama vile akili zetu wote zinashinda kule kwenye 6Th dimension ambako hakuna siri. Mawazo yote yako wazi kwa kila afikae huko.
  Umesema mawazo yangu sina cha kuongezea.
   
 14. Haki.tupu

  Haki.tupu JF-Expert Member

  #14
  Jul 22, 2009
  Joined: Apr 25, 2008
  Messages: 254
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Madela, you made my day! Ingawa nawe siku hizi huonekani sana hapa jamvini.
   
 15. H

  Haki JF-Expert Member

  #15
  Jul 23, 2009
  Joined: Jan 14, 2009
  Messages: 356
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kwangu mimi seti kubwa ni dini ninayoamini. Utanzania umeanzia miaka ya karibuni tu; lakini dini yangu ilikuwepo kabla Tanzania. Wazungu ndiyo waliyosababisha tuwe Tanganyika halafu Nyerere akaanzisha Tanzania. Wazungu walisababisha tuungane mikoa yote na hayakuwa mawazo yetu. Pili: Huu muungano wa Jamhuri na Zanzibar haukuwa na ridhaa ya Wananchi bali ni mawazo ya mtu mmoja. Nitasherehekea Umoja pale tu nitakaposhirikishwa kwenye kura za kweli.
   
 16. K

  Kidatu JF-Expert Member

  #16
  Jul 23, 2009
  Joined: Jun 11, 2008
  Messages: 1,491
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 135
  Mzee MMJ,
  Asante kwa uchambuzi wa kina katika hili.
  Lakini kwa upande wangu nilikuwa na mtazamo ufuatao:-

  Tumekuwa na set zote ulizozitaja (set kubwa na ndogo) kwa muda mrefu na katika awamu zote za utawala hapa Tanzania. Tatizo ninalo liona hapa ni kwamba katika awamu hii ya utawala Watanzania wamegawanywa katika makundi makubwa mawili :- matajiri na masikini bila kujali dini, na mbaya zaidi masikini ni wengi mno. Ila kitu kizuri watanzania wameanza kupata mwamko na kutambua nini chanzo cha tatizo lao, ila wanashindwa kuwa na kauli ya pamoja katika kupinga jambo hilo. Na walio nacho wanatumia uwezo wao kipesa kuzidi kuwavuruga na kuwatisha masikini ili kuvunja mshikamano wao dhidi ya mapambano haya. Malumbano yote tuliyokuwa nayo kwa sasa hapa nchini chanzo chake ni ufisadi. Kila dini inatoa kauli yake kuhusu hili suala na kuleta mkorogano. Inachotakiwa kufanywa ili kumaliza malumbano haya na kurudisha Utanzania wetu ni kwamba viongozi wa dini zote wakae pamoja na kutoa kauli moja kuhusu hili suala kwa lengo la kumsaidia Mtanzania.
   
 17. PJ

  PJ JF-Expert Member

  #17
  Jul 23, 2009
  Joined: Oct 10, 2007
  Messages: 297
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
   
 18. Safari_ni_Safari

  Safari_ni_Safari JF-Expert Member

  #18
  Jul 23, 2009
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 22,470
  Likes Received: 5,850
  Trophy Points: 280
  Mwembechai jamani ilukwa 1997 na 1999.je alhaji mwinyi alikuwa madarakani?
   
 19. Safari_ni_Safari

  Safari_ni_Safari JF-Expert Member

  #19
  Jul 23, 2009
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 22,470
  Likes Received: 5,850
  Trophy Points: 280
  Mwembechai jamani ilikuwa 1997 na 1999.Je alhaji mwinyi alikuwa madarakani?
   
 20. Ncha

  Ncha JF-Expert Member

  #20
  Jul 23, 2009
  Joined: Jul 8, 2008
  Messages: 254
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  MMkj bigup!!

  Viongozi wa hizo set wangekuwa wote wako na mtizamo moja na hakuna anayetaka kuonelana bora zaidi ya mwingine naamini wangeshirikishan na waraka utoke kama waraka wa dini zote.

  hapo sidhani kama haya yote yangekuwapo malumbano. pia matokeo yake yangekuwa mazuri mno na jamii yote ingeelimika kiujumla na ktk mtizamo mmoja wa kuwa na TZ mpya yenye neema.

  Utengano, kutoaminiana na kutaka kuonekana bora zaidi kunafanya hata mawazo mazuri ya baadhi ya viongozi wa set fulani yasichukuliwe kwa uzito unaostahili na wadau wengine.

  UMOJA ni muhimu sana kwa TZ mpya yenye matumaini
   
Loading...