Walisema: ‘Rais’ John Pombe Magufuli: Kula pombe, bangi uokoe taifa

Ufipa-Kinondoni

JF-Expert Member
Jan 3, 2012
4,582
2,783
MASIKINI Dk. John Pombe Joseph Magufuli; bahati [au balaa?] inaelekea kumwangukia, ya kuukwaa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mazingira magumu ya kuparanganyika kwa nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii. Mwanzo ndio utakaothibitisha au kuhalalisha atakavyomaliza Urais anaotarajia kuingia kwenye kinyang’anyiro, Oktoba 25, mwaka huu.

Tunasema ni bahati kwa sababu urais ni taasisi adhimu inayodhaniwa siku zote, kushikwa kwa mafanikio na wateule wa Mungu pekee. Je, haikusemwa na wahenga kinadharia, kwamba, “Watawala huchaguliwa na Mungu?”
Inaweza pia kuwa balaa inayomnyemelea kwa sababu atashika nchi iliyoghubikwa na changamoto lukuki, nchi isiyokuwa na dira, itikadi wala sera thabiti ya Maendeleo. Ni nchi iliyoachwa kujiendesha mithili ya ndege isiyo na rubani.

Tunamtupia pakacha la yote hayo kwa sababu tunaamini atashinda kinyang’anyiro cha nafasi hiyo; Umma wa Kitanzania unajua hilo, wakiwamo wa Vyama vya siasa vya Upinzani, kwamba Magufuli, japo ni mwenye chongo kwenye nchi ya vipofu na ukame wa Viongozi bora, yeye ni Mfalme.
Katika hali ya kuboronga kwenye usimamizi wa nchi kwa awamu zote tatu za mwisho; mawazo ya wananchi ni kwamba, Taifa linahitaji Kiongozi “kichaa” – mkali na mwenye msimamo aina ya Magufuli kuirudisha nchi “relini”, licha ya ukweli kwamba huenda sehemu kubwa ya Wabunge wa Chama chake wakapukutika kwa ghadhabu ya umma kama adhabu kwa Bunge na wao wenyewe kushindwa kuwajibika vyema kwa wananchi.

Lakini, ataanzaje na atamalizaje uongozi wake kwa nchi iliyolika kwa kutu ya kila maovu yenye kuangamiza Taifa: rushwa na ufisadi uliokithiri; kuporomoka kwa maadili ya uongozi na kijamii, kuyoyoma kwa uzalendo na umoja wa kitaifa; nchi kukosa dira na itikadi ya maendeleo, demokrasia duni na Taifa kuwekwa rehani kwa mtandao wa “Wawekezaji” wa kigeni wakishirikiana na mawakala wa ubeberu na ubepari wa kimataifa nchini?.

Ni maovu haya ambayo kutoweka kwake, wananchi wanaweka matumaini kwa Dakta Magufuli, wakiamini hivyo kutokana na weledi na umahiri wake wa kutenda kwa vitendo na tija, alioonesha bila kuyumba kama Waziri katika Serikali ya Muungano.

Tayari amekwishadokeza jinsi atakavyoanza na kuendelea, kama atapata nafasi ya kuchaguliwa. Amesema, atasimamia yote ya Waasisi wa Taifa letu – Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.
Huku akielewa vizingiti mbele yake, amebuni kauli mbiu ya kuchapa kazi na kuongoza inayokita kwa lugha yake ya Kisukuma, “Aliselema, Alija”, yaani, “Bandu bandu humaliza gogo”. Ni gogo au magogo yapi yaliyo njiani mwake?.
Lakini kuzungumzia uongozi bora mfano wa Mwalimu Nyerere ni kuzungumzia “Azimio la Arusha” ambalo amekufa akisema halina ubaya kiasi cha kuhitaji kufanyiwa marekebisho kwa maendeleo ya nchi. Maovu yanayolikabili Taifa leo yasingekuwa hivi chini ya Azimio la Arusha, lililotaka rasilimali za Taifa kuwa mikononi mwa wananchi na kwa Viongozi kuzingatia Maadili bora ya Uongozi; ambapo neno “Maendeleo” lilitafsiriwa kumaanisha “Maendeleo ya Watu, kwa ajili ya watu” na si maendeleo ya vitu.

Ataweza kurejesha Azimio la Arusha katikati ya ubepari uliokaba koo taifa kiuchumi, kiasi cha kupanuka bila udhibiti, kwa ufa kati ya [kikundi kidogo cha] matajiri na umma masikini, unaoendelea kufukarishwa na kikundi hicho?. Je, ataweza kudhibiti uporaji wa rasilimali/utajiri wa Taifa unaofanywa na kikundi hicho, kilichohakikishiwa ulaji bila hofu ya kuhojiwa?

Je, ataweza kurejesha heshima ya serikali na ya utumishi wa umma, kwa kuteua Wasaidizi na Watendaji waadilifu badala ya uozo atakaorithi kutoka kwa waliomtangulia? Atapataje ujasiri huo wakati amezungukwa na hao hao ambao wangependa kuona anakanyaga ganda la ndizi ateleze na kupiga mweleka, kisha wajidai kumwinua kwa “huruma”, awakumbatie kama wenye kumtakia mema wakati ni nyang’au kwenye mawindo?

Pia Dk. Magufuli amesema atafuata nyayo za marais Ali Hassan Mwinyi (Awamu ya pili), Benjamin William Mkapa (awamu ya tatu) na Rais anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete.

Atazungumziaje sera za uchumi za Rais Mwinyi [1985 – 1995] bila kuchokoza ghadhabu ya Mwalimu Nyerere aliyekasirishwa na tabia ya Rais huyo kutaka kuigeuza “Ikulu kuwa pango la Wanyang’anyi”, akatahadharisha mapema juu ya ubinafsishaji usiojali, na kwamba tusipokuwa makini, “mtabinafsisha hata Magereza”?.

Je, haikuwa enzi za utawala wa Mzee Mwinyi, mwaka 1992; pale Azimio la Arusha lilipopigwa ngwara na Azimio la Zanzibar, Wabunge na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa [NEC] ya CCM, wakabembea kwa furaha kwenye bustani ya watoto huko walikokutana Visiwani, kukaribisha “ulaji bila kunawa” wala hofu ya kuhojiwa, utamaduni unaitafuna nchi hadi leo?.

Awamu ya Rais Mwinyi haiwezi kukwepa lawama kwa kufuta dira ya maendeleo ya nchi [Azimio la Arusha] licha ya yeye kujitetea mara nyingi kwamba awamu yake haikuua Azimio hilo bali “tulilizimua”.

Ni Awamu hii iliyofungua milango kwa Wawekezaji upana wa bawaba ya mwisho na kutoa “Ruksa” kwa uporaji wa kila aina, kiasi cha Rais huyo kupachikwa jina “Mzee Ruksa”.

Awamu hii itakumbukwa kwa mabaya machache lakini makubwa kuliko mazuri mengi, yakiwemo kuwekwa kwa uchumi mikononi mwa wageni, kuibuka kwa matabaka ya kijamii kwa misingi ya kiuchumi na udini, kuyoyoma kwa [moyo wa] Uzalendo na maadili ya Taifa na kukomaa kwa ufisadi na kulindana. Ni kipindi cha nchi kugeuzwa “Shamba la Bibi”, kwa kila mwenye uwezo kupora kadri ya ukali wa meno yake.

Je, Dk. Magufuli atakuwa na ujasiri wa kufyeka msitu wa giza wa maovu yaliyotanda njiani, kumwezesha kushikana mikono na Mwalimu Nyerere ambaye amekufa akilalamikia mwenendo wa Serikali ya awamu ya pili?.
Dk. Magufuli ana shauku pia ya kuongozwa na uzoefu wa Awamu ya tatu, ya Rais Benjamin William Mkapa [1995 – 2005], iliyoingia madarakani kwa kishindo na mbwembwe kwa kauli mbiu ya “Uwazi na Ukweli”, kwa ahadi ya kutokomeza rushwa na ufisadi uliokithiri.

Kuonesha kwamba alikuwa tofauti na mtangulizi wake, haraka haraka aliunda Tume ya kubainisha mianya ya rushwa na jinsi ya kutokomeza janga hilo la kitaifa, chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba. Tume ikatoa taarifa yake nzuri na kukabidhi.

Tena, Mkapa akajiwekea utaratibu wa kulihutubia taifa kwa njia ya redio kila mwisho wa mwezi ili pengine kukidhi matakwa ya Katiba ya nchi [ibara 18 (2)] kwamba, “kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi”.
Na juu ya mikakati yote, aliteua Baraza la Mawaziri aliowapa jina “Askari wa Miavuli”, akiwaelezea kuwa na uwezo wa “kutua ardhini wakikimbia” [hiting the ground running] katika vita ya kuendeleza nchi.

Lakini wakati huo wote, mafisadi pangoni yalikuwa yakimpima kwa hatua za kuhesabu, na haikuchukua muda, Rais Mkapa hakuwa Mkapa yule tuliyeanza naye; tayari alikuwa amenaswa na kunasika kwenye ulimbo wa mafisadi na kupoteza dira.

Taarifa ya Tume ya Warioba ikatupwa “jalalani”, na taarifa za kila mwisho wa mwezi zikawa rojo rojo kupoteza lengo na hivyo kuzua kelele miongoni mwa umma ulioonekana kuelewa mengi ya nchi na kwa maisha ya wananchi kuliko viongozi walivyofikiri.

Na pale umma ulipopaza sauti dhidi ya upotoshaji wa mambo, alikuwa mkali kufikia kuwaita wananchi “wavivu wa kufikiri”, na wakati fulani mmoja wa askari wake wa miavuli, alidiriki kukandia akiwatukana wananchi akisema, “kuleni nyasi”.

Chini ya Awamu hii, zoezi la ubinafsishaji, usiojali lililoanzia Awamu ya pili, liliongeza kasi kwa Viwanda vyote nchini kubinafsishwa, kisha vikatelekezwa makusudi kuikosesha nchi uwezo wa kuongeza thamani mazao yake na kwa Taifa kufanywa tegemezi kwa kila bidhaa za Viwanda, kuanzia kiberiti hadi vipuri kutoka nje.

Ni Awamu hii ambayo, mbali na ubinafsishaji huo, ilijiuzia kwa bei ya chee, nyumba za Serikali kwa adha kubwa kwa utumishi Serikalini, wakati huo Mheshimiwa Magufuli akiwa Waziri mwenye dhamana ya nyumba hizo.
Awamu hii iliondoka madarakani katikati ya milipuko ya kashfa kubwa kubwa za ufisadi kama zile za uporaji wa mabilioni ya BOT [EPA], IPTL, TANESCO, TICTS, Ununuzi wa ndege mbovu ya Rais, kashfa ya Rada, Meremeta, Tangold, Deep Green, Mikataba mibovu ya madini, kuuzwa kwa Kilimanjaro Hotel, Hotel 77, Shirika la Simu nchini TTCL, Benki ya NBC na Kiwira Coal Mines, mgodi ambao Rais Mkapa anatuhumiwa kujiuzia kwa bei ya kutupa.

Kwa upande wa Benki ya NBC, ambayo ilikuwa Benki ya umma kubwa kuliko zote Afrika Mashariki, inaelezwa, iliuzwa kwa Makaburu wa Afrika Kusini kwa Sh. 15bn/= tu, wakalipa Sh. 12bn/= pekee ambazo hata hivyo hazikuonekana kupokelewa kwenye vitabu vya Serikali.

Inajulikana, Dk. Magufuli ni chaguo la Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa, ambaye ndiye aliyeokoa jahazi kwenye NEC mjini Dodoma wakati kambi ya Waziri Mkuu aliyepata kujiuzulu na ambaye alienguliwa katika kinyang’anyiro cha kuteuliwa, Edward Lowassa, iliposhinikiza kwa vitisho, huku maandamano mjini yakirindima kutaka kurejeshwa kwa jina lake ambapo ingekuwa hivyo, Lowassa angepeta kwa nguvu ya “ushirikina” wa kifedha na “rehani” kwa Taifa, aliomwaga kwa Viongozi wa Chama nchi nzima na kwa “kenge” wengine ndani na nje ya nchi, kiasi kwamba, Taifa na wananchi wangebebeshwa mzigo wa kulipia deni la Urais wa kununua.

Dk. Magufuli atahitaji ujasiri mkubwa, kwa kufunga roho na moyo kwa makufuli imara na kwa kuziba masikio, pale atakapotakiwa na mkuu wake huyo wa zamani, kutoa fadhila kwa kumfichia “maovu” hayo ya kale. Na akikubali hilo, atakuwa amefungua njia ya kifo kwetu, kuelekea “golgota”.

Kwa haya, Dk. Magufuli ana lipi la kuiga kutoka Awamu hii, kama tu ilivyo kwa Awamu iliyotangulia? Awamu ya Nne, ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ilianza kwa mbwembwe na kauli mbiu, “Ari Mpya, Nguvu Mpya, na Kasi Mpya”, kwa kifupi, “ANGUKA”. Awamu hii iliingia wakati rushwa na ufisadi vikiwa vimeshika kasi na kuota mizizi. Lakini hakueleza “Mpya” hizo tatu zilikuwa kwa mambo yapi na kwa kipindi gani.

Kilichositua Watanzania ni kuona Kiongozi wao kutositushwa na maovu haya ndani ya jamii, na kwa Chama Tawala – CCM kugeuka kichaka na kimbilio la wadhalimu, wakijipambanua na ufadhili kwa Chama, na wengine “kuteuliwa” kuwa Makamanda wa Vijana, na baadhi yao kuwania nafasi mbali mbali za uongozi kwa imani kwamba “ukivaa kijani huguswi”, hata kama wewe ni mchafu kama Nguruwe.

Kwa njia hii, ufisadi na hujuma kwa Taifa vikapata kiota ndani ya Chama na Serikali kwa kinga ya kutoguswa, maana ukigusa fisadi umegusa Chama na hivyo wewe ni adui wa Chama na Serikali.

Unatarajia, kwa mfano, katika mazingira hayo, wabunge watunge sheria bungeni zenye manufaa kwa wananchi ili wajimalize kimaslahi, wakati kufukarika kwa mwananchi ndiko kuneemeka kwao?.

Angalia: wakati fulani, Mwenyekiti wa Chama na Rais, Jakaya Kikwete, alitaka viongozi wachague moja kati ya siasa/uongozi wa umma na biashara kwa sababu “hawawezi kutumikia mabwana wawili” wakawapenda wote. Tena akafika mahali kuwataka Viongozi wenye tuhuma na kashfa za ufisadi na rushwa wajivue “gamba” kwa maana ya kuachia ngazi.

Lakini kwa kuwa alikuwa tayari mateka wa mafisadi na magwiji ya rushwa; yakamtazama kwa macho mekundu na kejeli, akanywea.
Baadhi ya kejeli hizo kwa Rais zilikuwa ni pamoja na, “Kama Rais anataka kutenganisha siasa na biashara aanze yeye”; na pia kwamba, “gamba limekatalia kiunoni, anayetaka [Rais] litoke, achukue shoka aling’oe tumuone na tuone”. Rais akanywea zaidi.

Awamu hii ilizalisha mafisadi wa kutupa, kuanzia ndani ya Chama, Bunge, utumishi wa umma hadi Ikulu kwenyewe, kama ilivyothibitika kwenye kashfa za IPTL, Akaunti ya Escrow ya Tegeta na Meremeta”, na kwa Viongozi kuita mabilioni ya fedha wanazopora “vijisenti” au “fedha ya mboga”.
Haiingii akilini, kwa Serikali kumtia korokoroni mwananchi masikini asiye na uhakika wa mlo wa siku, kwa kushindwa kuchangia maabara kwa shule za Kata, wakati akiona utajiri wa nchi ambao ungefanya kazi hiyo, ukiporwa bila hofu na Mapakashume wachache.

Inawezekana Rais Kikwete anakerwa na haya, lakini kwa kuwa ni mateke afanyeje?. Anaishia kulalama, kama vile kusema, “moyo unatamani [kukomesha ufisadi], lakini mwili [matendo] ni dhaifu”. Hapo tena, Dk. Magufuli ana kipi cha kuiga?.

Na hili ni dhahiri, kwamba katika Watiania wa CCM wote 42 wa Urais waliotoa sera zao japo kwa ufupi, hakuna hata mmoja ambaye, kwa nahau moja au nyingine, hakuikandia awamu hii kwa maovu tuliyoyaona hapo juu kuonesha kwamba hali ndani ya serikali anayorithi Dk. Magufuli, si shwari.
Ataingia Ikulu na kuongoza serikali kwa kupokelewa na mabwana “Vijisenti” wale wale wenye fungate ya ndoa na ufisadi mkubwa na ubepari wa Kimataifa anaopashwa kuupiga vita kwa moto mkali wa enzi za uhuru. Je, anao ujasiri huo kuweza kuokoa Taifa kwenda “golgota”?.

Hapa Dk. Magufuli anatakiwa kumsoma na kumuelewa vyema Mwanafalsafa, Niccolo Machiavelli, katika kitabu chake kiitwacho “The Prince” au “Mtawala wa Kiume”, anavyotahadharisha akisema: “Na yeyote awaye mrithi wa Serikali iliyopita yenye maovu, asipoyaharibu masalia ya uovu huo, yeye mwenyewe ataharibiwa nayo, kwani siku zote [masalia] huwa na tabia ya uasi kutafuta raha na matanuzi ya kale hata baada ya kupita muda mrefu…..”.

Machiavelli anaona njia pekee ya kuepuka “uasi” huo ni kwa mtawala mpya kuwa katili kidogo, anasema: “Na kwa Watawala wote, ni vigumu kwa mtawala mpya kuepuka tuhuma za ukatili inapokuwa muhimu kuliepushia Taifa maovu …...ukatili waweza kutumiwa vizuri [benevolent despotism] ikiwa ni kwa manufaa ya nchi na raia wake kuweza kuondokana na maovu kwa njia ya ukatili…...”.

Tunafahamu Dakta John Pombe Magufuli anayo sifa ya “ukatili” unaotakiwa kwa mtawala yeyote; lakini kwa hali mbaya ya sasa tulimo, ya uvunjifu wa maadili, uwajibikaji duni na kwa nchi kukosa dira ya maendeleo, itampasa kunywa “pombe” kwa kuchanganya na “bangi” kidogo kupata ujasiri wa kutosha kukabiliana na “magogo” njiani kuthibitisha kauli mbiu yake ya “Aliselema…….Alija”. Bila hivyo, itakuwa mambo yale yale, kwa mdundo na “mdundiko” ule ule.

Chanzo: Raia Mwema
 
Mwandishi du! ulikuwa umetulia. Jpm Asinywe pombe wala bangi tunaamini He can
 
Back
Top Bottom