Walisema JK katumwa na Mungu wakalala sasa wameanza kuamka na kunena

Lunyungu

JF-Expert Member
Aug 7, 2006
8,873
1,894
Waraka mzito wa maaskofu kwa JK

na Kulwa Karedia
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

MAASKOFU wa makanisa kadhaa kupitia kile wanachokiita Ushirika wa Maaskofu Tanzania, wameandika waraka maalumu wenye ujumbe mkali na mzito kwa serikali, wakitaka kuchukuliwa kwa hatua kubwa ili kulinusuru taifa dhidi ya misukosuko linayokabiliana nayo.

Waraka huo wa maaskofu wanaofanya kazi chini ya uenyekiti wa mtu anayetajwa kuwa ni Askofu John Mwela, unaelezwa kuwa ni matokeo ya kikao cha pili cha kamati ya maaskofu hao kilichokutana Dodoma kwa siku nne kuanzia Mei 13 hadi 16 mwaka huu.

Kwa mujibu wa waraka huo wa maaskofu ambao Tanzania Daima imeusoma, pia kuchapwa katika baadhi ya magazeti jana, maaskofu hao wanaeleza kuguswa na matukio kadhaa wanayoyaelezea kuwa yaliyochangia kuliyumbisha taifa.

Miongoni mwa mambo yanayotajwa katika waraka huo wa kwanza wa aina yake, ni pamoja na ufisadi, mpasuko wa kisiasa Zanzibar, uwakilishi wa viti maalumu bungeni, migomo vyuoni na katika mashirika na tatizo la usafiri kwa wanafunzi wa mijini.

Wakirejea matukio ya siku za hivi karibuni, maaskofu hao wanasema kuwa yana sura nne, zikihusisha ubadhirifu wa fedha za Watanzania kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu (EPA), Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Richmond, na kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wengine kadhaa.

Mawaziri waliojiuzulu wanaotajwa katika waraka huo ni pamoja na Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi na Andrew Chenge.

Maaskofu hao wanabainisha kuwa mwelekeo wa mambo hapa nchini unaonyesha kuwa serikali inahitaji msaada mkubwa katika kuweka hali sawa.

Wanasema kuwa matukio hayo ya ufisadi yamesababisha Watanzania wagawanyike katika makundi manne, ambayo hata hivyo hawataji chanzo chao cha utafiti kilichowawezesha kufikia katika mpangilio wao huo.

Kwa mtazamo wao, kundi linaloongoza ni lile linalojumuisha watu wanaofikia asilimia 60, wanaochukizwa na kuumizwa na viongozi na watu wachache waliojilimbikizia mali.

Kundi la pili wanalolitaja ni la watu wanaofikia asilimia 25, ambao wao ni wale wanaolia na kutoa hukumu yao kwa kulalamika wakiiona serikali kuwa iliyoshindwa kuwajibika.

Aidha, walilitaja kundi la tatu (asilimia 14.75) kuwa ni lile la watu wasioona shida yoyote, kwa maana wao wana kila kitu, huku kundi la nne na la mwisho likijumuisha watu wachache (asilimia 0.25) wanaomlilia Mungu aliponye taifa la Tanzania.

Kutokana na mambo hayo, maaskofu hao wanatamka kujifunga kuisaidia serikali na hususan Rais Kikwete, katika maeneo kadhaa, kwa kutoa ushauri katika masuala ya ufisadi, mabadiliko yanayohitajika katika kuandaa uchumi wenye nguvu, pamoja na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Aidha, ushauri wao huo unahusisha pia jinsi ya kufikia muafaka kati ya CCM na CUF huko Zanzibar, na kugusia njia ya kushughulikia migomo katika vyuo vikuu, mashirika ya umma na makampuni binafsi, pamoja na serikalini kwenyewe.

Kwa upande mwingine, wakati serikali imekuwa ikifikiria kuongeza idadi ya viti vya wabunge maalumu hadi kufikia asilimia 50 mwaka 2010, kwa lengo la kukuza ushiriki wa wanawake katika hatua za maamuzi, maaskofu hao wamelitaka Bunge kufuta mara moja sera ya uwakilishi bungeni kupitia utaratibu wa viti maalumu.

Kamati hiyo imesema iwapo Bunge halitachukua hatua hiyo, basi kanisa nalo litaomba viti saba vya uwakilishi, wakivigawa vitatu kwenda kwa makanisa ya kiprotestanti yaliyo chini ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), viwili Kanisa Katoliki chini ya TEC, na makanisa ya kipentekoste yapate kimoja na kimoja kingine kiende kwa makanisa yanayojitegemea.

Tamko la kamati hiyo, lililosainiwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Askofu Mwela na Katibu wake, Godfred Lema, linasema hatua yao hiyo imelenga kuboresha uwiano wa uwakilishi bungeni, tofauti na hali ilivyo sasa.

Katika hayo yote, maaskofu hao wamesema kuwa wapo tayari kusimama kidete kumsaidia Rais Jakaya Kikwete kutafuta suluhisho dhidi viongozi mafisadi ndani ya serikali.

Maaskofu hao wanasema wamejitoa kupambana na ufisadi kwa sababu hali hiyo imefika katika hatua mbaya, ambayo rais anapaswa kusaidiwa haraka, ili kupunguza hatari ya mgawanyiko ndani ya jamii.

“Tumekubaliana kusimama na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume na serikali zao kutafuta suluhisho la matukio haya, kwa sababu tunajua nchi ni ya Watanzania wa dini na rangi zote, hivyo sote tunawajibika mbele za Mungu kuitunza,” inasomeka sehemu ya waraka huo.

Wanasema kuwa wakati umefika kwa makanisa kujiingiza katika vita dhidi ya ufisadi, kwa sababu baadhi ya watu wanaoendeleza vitendo hivyo wamo ndani ya makanisa hayo.

“Wengi wa watu hawa wanaoitwa mafisadi wako katika makanisa yetu, hivyo tutatumia nguvu kutoka kwa Mungu ili kuwaumbua na kuwaongoza, kuwa mabadiliko haya yanahitajika katika kuandaa uchumi wenye nguvu,” inasomeka taarifa hiyo.

Sambamba na vita dhidi ya ufisadi, waraka huo unasema maaskofu hao wamekubaliana pia kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Katika hili wanatoa ahadi ya kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ili kushauriana kwa pamoja, mambo yanayohusu umoja wa kitaifa na masilahi yake.

“Tutawaelekeza na kuwafundisha wale wanaowaongoza, umuhimu wa kutuunga mkono katika azima yetu. Tunaamini kwa kufanya hivi na kwa maelekezo haya sahihi ya Mungu, tutakuwa na umoja wa kitaifa, taifa lisilo na magonjwa kama vile malaria, ukimwi na vifo katika umri mdogo pamoja na kuondokana na umaskini na maisha duni,” inasomeka sehemu ya waraka huo.

Katika sehemu moja ya waraka huo, maaskofu hao wanaandika kuwa wanasubiri kuundwa kwa kamati ya kudumu ya maaskofu, baada ya kufanyika kwa vikao vya makanisa yaliyo chini ya CCT, TEC na PCT.
 
Mungu wetu ana mipango mingi isiyoweza kuonekana na binadamu lakini kwa faida ya binadamu, hili kwa kikwete kuwa chaguo la Mungu nadhani halikuwa katika mipango yake, bali kwa mipango ya S>>> wa mafisadi
 
Mwikimbi nimecheka sana .Ujue hata mafisadi yanasema Mungu wao ni mkubwa na Mungu wa washinda hoi hana nguvu .Kazi kweli kweli .Mimi hawa jamaa wamenipa furaha kudai Wabunge wa chee waondoke .Nakubaliana nao na mengine haya hapa maana ni wao walituletea ujinga huu .Je kwenye hili Kundi yule Askofu wa Lowasa yuko upande gani ?
 
Mtu aliyetumwa na Mungu haogopi mafisadi!! Siku zote atatawala kwa kuweka mbele maslahi ya nchi yake na wananchi waliomchagua.
 
Back
Top Bottom